‘Wao Huzingatia Mazoezi Yao ya Kidini’
MWANAMKE mmoja kutoka Miami, Florida, Marekani, alipeleka barua ifuatayo kwa gazeti la habari la kwao: “Desemba tarehe 10 kibeti cha mwanangu kiliibwa kutoka mfukoni mwake akiwa kwenye soko la vitu vilivyotumiwa. Ndani mlikuwamo na leseni ya uendeshaji-gari, kadi ya Ruzuku ya Kijamii, n.k., na vilevile dola 260 za Kimarekani.
“Baada ya kuripoti kwa meneja kwamba kilikuwa kimepotea alirudi nyumbani. Mapema jioni alipokea simu kutoka kwa bibi mwenye kusema Kihispania ambaye, kupitia opareta wa simu akiwa mfasiri, alimwambia kwamba alikuwa amekipata kibeti chake.
“Alimpatia anwani yake. . . . Akampatia kibeti hicho, kikiwa salama, kutia ndani zile dola 260.
“Alikuwa amemwona mwizi akichomoa kibeti chake na kupiga mayowe. Huyo mwizi aliangusha hicho kibeti na kukimbia. Kufikia wakati huo mwanangu alikuwa ametoweka machoni pake, hivyo alikipeleka kibeti nyumbani na kupiga simu.
“Yeye na familia yake ni Mashahidi wa Yehova. Wao kwa wazi huzingatia mazoezi yao ya kidini.”
Mashahidi wa Yehova hawaonyeshi ufuatiaji haki ili wapokee sifa kutoka kwa wanadamu. (Waefeso 6:7) Badala ya hivyo, wao hutamani kwa bidii kumletea sifa Baba yao wa kimbingu, Yehova. (1 Wakorintho 10:31) Upendo wao kwa Mungu na kwa jirani huwasukuma kupiga-mbiu juu ya “habari njema” ya Ufalme wa Mungu. (Mathayo 24:14) Kupitia Ufalme, Mungu aahidi kuigeuza umbo dunia kuwa paradiso nzuri. Kisha dunia itakuwa si mahali penye uzuri wa kimaumbile tu bali pia penye ubora wa kiadili ambapo ufuatiaji haki utaenea milele.—Waebrania 13:18; 2 Petro 3:13.