DEKAPOLI
(Dekapoli) [Eneo lenye Majiji Kumi].
Umoja au Muungano wa majiji kumi (kutokana na neno la Kigiriki deʹka, linalomaanisha “kumi,” na poʹlis, “jiji”). Jina hilo lilitumiwa pia kurejelea eneo ambalo mengi kati ya majiji hayo yalikuwa.—Mt 4:25.
Baada ya ushindi wa Aleksanda Mkuu mwaka wa 332 K.W.K. hivi, makoloni ya Ugiriki yalianzishwa katika maeneo ya Siria na Palestina, na inaonekana kwamba wanajeshi wa Aleksanda waliostaafu na baadaye wahamiaji waliozungumza Kigiriki waliishi katika majiji hayo. Katika visa vingi, makoloni hayo yalijengwa katika maeneo yaliyokuwa na miji ya Wayahudi, na mengine yalijengwa katika maeneo mapya, hasa Mashariki mwa Mto Yordani. Yalikuwa na utajiri mwingi wakati wa utawala wa Waseleuko wa Siria na Tolemi wa Misri, lakini kuanzishwa kwa miji yenye Wamakabayo na Wayahudi (kuanzia mnamo 168 K.W.K.) kulihatarisha uhuru wao kwa kiasi fulani. Ijapokuwa idadi kubwa ya watu katika majiji hayo ilitia ndani Wayahudi wengi, bado majiji hayo yalikuwa vituo vya utamaduni na ustaarabu wa Kigiriki na tofauti kabisa na mipango ya Wamakabayo. Pompey aliposhinda na kupanga upya Palestina mwaka wa 63 K.W.K., majiji haya ya Wagiriki yalikuja kuwa chini ya usimamizi na uhusiano mzuri na Waroma. Waliruhusiwa kutengeneza sarafu zao wenyewe, na kwa kiwango fulani kuwa na serikali yao wenyewe ingawa bado walipaswa kutii Roma na serikali katika jimbo la Siria na walipaswa kulipa kodi na kutoa wanaume wao kwa ajili ya utumishi wa jeshi.
Kufanyizwa kwa Ushirika. Huenda muda fulani kati ya ushindi wa Pompey na kifo cha Herode Mkuu (mnamo 1 K.W.K.) majiji kumi kati ya hayo ya Wagiriki yalianzisha shirika lililoitwa Dekapoli. Inaonekana kwamba lengo la kuwa na shirika hilo lilikuwa kuboresha mahusiano ya kibiashara na pia kujilinda dhidi ya waliochukia Wagiriki ndani ya Palestina au makabila ya wahamaji wenye jeuri katika maeneo ya jangwani huko Mashariki. Neno “Dekapoli” linapatikana kwa mara ya kwanza katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo na maandishi ya Yosefo na Plini Mkubwa (wote waliishi katika karne ya kwanza W.K.). Plini, alionyesha kwamba tayari kulikuwa na maoni yaliyotofautiana, aliorodhesha majiji yafuatayo kati ya yale kumi ya kwanza: Damasko, Filadelfia, Rafana, Skithopoli, Gadara, Hipo (Hiposi), Dioni, Pela, Galasa (Gerasa), na Kanatha. (Natural History, V, XVI, 74) Kati ya majiji hayo, jiji la Skithopoli ndilo tu lililokuwa Magharibi mwa Yordani; na kwa sababu lilikuwa katika eneo zuri kwenye Bonde la Esdraeloni, lilikuwa sehemu muhimu iliyounganisha Pwani ya Mediterania na bandari nyinginezo. Jiji la Damasko, lililokuwa mbali huko Kaskazini mwa Siria, lilitiwa ndani kwa sababu ya umuhimu wake wa kibiashara. Jiji la Filadelfia (zamani liliitwa Raba, sasa ni ʽAmman) lilikuwa kusini zaidi kati ya majiji hayo kumi, kilomita 40 hivi upande wa Kaskazini Mashariki wa ncha ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi. Yale majiji mengine yalikuwa katika eneo lenye rutuba la Gileadi au eneo jirani la Bashani. Inaaminiwa kwamba mengi kati ya majiji hayo yalikuwa kando au karibu na barabara kuu za eneo hilo. Inawezekana kwamba jiji la Kanatha ni jiji la Kenathi linalotajwa kwenye Hesabu 32:42.
Katika karne ya pili W.K., Ptolemy aliyaita majiji 18 yaani “Dekapoli,”jambo linalodokeza kwamba jina hilo lilitumika kwa njia ya kawaida na idadi ya majiji hayo haikuwa hususa. Baadhi ya wasomi wanataja jiji la Abila, lililoorodheshwa na Ptolemy, badala ya Rafana kuwa kati ya yale majiji kumi ya mwanzoni. Inaonekana kwamba eneo la Dekapoli halikuwa na mipaka hususa na kwamba eneo la Dekapoli halikuwa na utawala mmoja bali kila jiji lilikuwa chini ya mamlaka ya wilaya yake.
Eneo la Dekapoli Wakati wa Huduma ya Yesu. Ingawa watu kutoka Dekapoli walikuwa kati ya umati uliokuja kusikiliza mafundisho ya Yesu huko Galilaya (Mt 4:25), Maandiko hayataji kihususa kwamba Yesu alihubiri katika majiji hayo ya Kigiriki. Yesu aliingia katika eneo la Dekapoli wakati wa huduma yake huko Galilaya alipovuka Bahari ya Galilaya na kuingia katika nchi ya Wagerasene (au Wagadarene kulingana na Mt 8:28). (Mr 5:1) Akiwa huko, aliwafukuza roho waovu na kuwaruhusu waingie katika kundi la nguruwe, na wote wakafa, kisha watu wa majiji yaliyokuwa karibu na maeneo ya mashambani wakamwambia Yesu ‘aondoke katika eneo lao.’ Yesu aliondoka lakini mtu ambaye hapo awali alikuwa na roho waovu alitii agizo la Yesu la kwenda kuwahubiria watu wake wa ukoo, na kutangaza kazi za Yesu za kuponya huko Dekapoli. (Mr 5:2-20) Baadhi ya wasomi wanaamini kwamba lile kundi la nguruwe linathibitisha zaidi kwamba watu katika eneo hilo hawakufuata utamaduni wa Wayahudi.
Baada ya Pasaka ya mwaka wa 32 W.K., aliporudi kutoka safari yake katika maeneo ya Tiro na Sidoni huko Foinike, Yesu alipitia “Dekapoli, na kufika kwenye Bahari ya Galilaya.” (Mr 7:31) Akiwa katika eneo hilo alimponya kiziwi aliyekuwa na tatizo la kuzungumza na baadaye alilisha kimuujiza umati wa watu 4,000.—Mr 7:32–8:9.
Historia ya Baadaye. Kulingana na mwanahistoria Eusebio, kabla ya kuharibiwa kwa Yerusalemu mwaka wa 70 W.K., Wakristo huko Yudea walikimbilia jiji la Pela huko Dekapoli kwenye eneo lenye milima la Gileadi, na hivyo kutii onyo ambalo Yesu alikuwa ametoa.—Lu 21:20, 21; The Ecclesiastical History, III, V, 3.
By no means alone among the cities of Palestine in their Hellenistic leanings, majiji ya Dekapoli yalikuwa uthibitisho wenye nguvu wa utawala Ugiriki. Inaaminiwa kwamba majiji hayo yalifikia kilele katika karne ya pili W.K., na katika karne iliyofuata muungano huo ukaanza kuvunjika. Uthibitisho wa uvutano mkubwa wa Ugiriki, na pia utajiri wa majiji ya Dekapoli, unaonekana kupitia majumba ya maonyesho, viwanja vya michezo, mahekalu, mabafu, mifereji, na majengo mengine huko Gerasa (sasa ni Jarash) na katika majiji mengine.
[Ramani kwenyue ukurasa wa 602]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
DECAPOLI—Barabara
Bahari Kuu
Damasko
Rafana (?)
Hiposi
Bahari ya Galilaya
Dioni
Kanatha
Abila (?)
Gadara
Skithopoli (Beth-sheani)
Pela
Gerasa
Filadelfia (Raba)
Bahari ya Chumvi