Kukimbia kwa Wakristo Kwenda Pela
KATIKA mwaka 33 W.K., Yesu Kristo alionya wafuasi wake waanze “kukimbilia milimani” wakati wangeona “Yerusalemu umezungukwa na majeshi” yaliyopiga kambi. (Luka 21:20-24) Lakini wao walikimbilia wapi hasa? Mchunguzi Mfaransa wa mambo ya nchi za mashariki mwanahistoria, Joseph Ernest Renan, anajibu: “Mahali palipochaguliwa na vichwa vya jamii [ya Kikristo] pawe mahali pakuu pa kukimbilia Kanisa lenye kukimbia palikuwa Pela, mmoja wa miji ya Dekapoli, uliokuwa karibu na ukingo wa kushoto wa Mto Yordani katika mahali penye kusifika, penye kukabiliana upande mmoja na uwanda wote wa Ghori, na upande ule ukiwa na miamba-miamba yenye kutelemka sana, chini yayo kukiwa na bubujiko la maji. Mahali hapo palichaguliwa kwa hekima na ndipo palipofaa zaidi ya penginepo pote. Yudea, Idumea, Perea, na Galilaya zilikuwa na fitina juu ya serikali; Samaria na eneo la pwani palikuwa na msukosuko mwingi . . . Hivyo Skaithopoli na Pela ndiyo miji ya karibu zaidi na Yerusalemu isiyokuwa na fujo. Kwa sababu Pela ulikuwa ng’ambo ya Yordani, bila shaka ulikuwa na utulivu mwingi kuliko Skaithopoli ambao ulikuwa umekuwa mmoja wa ngome za Kiroma. Pela ulikuwa mji huru kama miji ile mingine ya Dekapoli . . . Kukimbilia huko kulikuwa kutangaza waziwazi kwamba uasi wa [Kiyahudi] ulikuwa wa kuogopesha sana . . . Ni katika mji huo wenye kupinga Wayahudi ndimo Kanisa la Yerusalemu lilikimbilia wakati wa hofu kuu za mazingiwa.”