Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • it kur. 648-649
  • Kulima

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kulima
  • Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Habari Zinazolingana
  • Je! Wewe Utajifunza Kutokana na Majira?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Maisha Katika Nyakati za Biblia—Mkulima
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • ‘Kaeni Katika Neno Langu’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Je! Mungu wa Upendo Angeweza Kutesa Nafsi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
Ufahamu wa Kina wa Maandiko
it kur. 648-649

KULIMA

Inawezekana kujua aina za plau walizotumia wakulima Wayahudi nyakati za Biblia kwa kutumia picha za zamani za plau zilizotumiwa katika nchi jirani na plau zilizotumiwa nyakati za karibuni na baadhi ya wakulima Waarabu. Baadhi ya plau zilitengenezwa kwa kipande cha mbao chenye ncha, labda ya chuma, kilichounganishwa na mpini na kuvutwa na mnyama mmoja au wanyama kadhaa. Huenda plau ya aina hiyo haingechimba ndani kabisa ardhini. Bila shaka, hakuna uthibitisho wa moja kwa moja unaopinga uwezekano wa kwamba plau za hali ya juu zaidi zilitumiwa katika Israeli.

Kwa kuwa jua kali la kiangazi lilifanya udongo uwe mgumu, kwa kawaida, kabla ya kuanza kulima, watu walisubiri mvua ya msimu wa kupukutika au wa baridi kali inyeshe ili kulainisha udongo. Kisha walilima na kupanda. Baridi, hali mbaya ya hewa, au mawingu meusi hayangemzuia mtu mwenye bidii kulima, lakini mkulima mvivu angetumia fursa hiyo kuepuka kufanya kazi. Jirani zake hawangemwonea huruma alipokosa mavuno kwa sababu ya uvivu wake wakati wa kulima. (Met 20:4; Mhu 11:4) Hata hivyo, hata wakati wa kulima, wakulima Waisraeli walipaswa kushika Sabato.​—Kut 34:21.

Ng’ombe dume na punda hawakupaswa kufungwa nira kwenye plau ileile, kwa sababu walitofautiana katika nguvu na kasi. (Kum 22:10) Kwa kawaida plau ilivutwa na jozi au ng’ombe wawili. (Lu 14:19; Ayu 1:14) Wanaume kadhaa, kila mmoja akiwa na jozi ya ng’ombe wangeweza kufanya kazi pamoja kwa kulima mistari sanjari, mmoja akiwa nyuma ya mwenzake. Katika kisa cha Elisha, kama inavyosimuliwa kwenye 1 Fa 19:19, alikuwa na plau ya 12, kwa hiyo angeweza kuacha kulima bila kuwavuruga wengine waliomfuata. Aliondoka shambani na kutumia plau yake ya mbao kama kuni ili kuwatoa ng’ombe dume hao kuwa dhabihu. (1Fa 9:21) Katika kitabu The Land and the Book (kilichosahihishwa na J. Grande, 1910, uku. 121), W. M. Thomson anasema kwamba mwanamume mmoja angeweza kupanda mbegu katika eneo ambalo lilihitaji kulimwa na wanaume kadhaa.

Matumizi Katika Mifano. Watu wengi walifahamu kazi ya kulima kwa hiyo ilitumiwa sana katika mifano. Wafilisti walipomshinikiza mke wa Samsoni amshawishi amtegulie kitendawili chake, Samsoni alisema kwamba walikuwa‘wamelima na ng’ombe wake mchanga,’ yaani, walitumia mtu ambaye alipaswa kuwa anamtumikia. (Amu 14:15-18) Mtu hawezi kulima kwenye mwamba, na kama Amosi anavyoonyesha, haikupatana na akili kwa viongozi wa Israeli kupotosha haki na kutenda ukosefu wa uadilifu na wakati uleule kutarajia mambo hayo yawanufaishe. (Amo 6:12, 13) Inaonekana Hosea 10:11 linatumia kulima (kazi iliyo ngumu zaidi kwa ndama-jike kuliko kupura) kuwakilisha kazi ngumu na ya utumwa ambayo watu wa Yuda walioasi wangelazimishwa kufanya na wanyanyasaji kutoka nchi za kigeni. Kulingana na Yeremia 4:3, 4 na Hosea 10:12, 13, Waisraeli walihitaji kubadili njia yao ya maisha, kutayarisha, kulainisha, na kusafisha mioyo yao (linganisha Lu 8:5-15) kana kwamba walikuwa wakilima na kuondoa miiba, ili wapate baraka kutoka kwa Mungu, badala ya kupoteza muda wao na nguvu zao wakifanya mambo mabaya ambayo yangewaletea mavuno mabaya.

Ufafanuzi wa utaratibu, kusudi, na busara anayotumia mkulima anapolima ili kusawazisha udongo, kupanda, na kupura, umetumiwa katika Isaya 28:23-29 kuelezea njia za Yehova ambaye “shauri lake linastaajabisha na ambaye ametimiza mambo makuu.” Kama vile kulima na kusawazisha udongo hufanywa kwa pindi fulani tu, yaani, udongo unapotayarishwa kwa ajili ya kupanda, Yehova hawatii nidhamu au kuwaadhibu watu wake milele, lakini kimsingi yeye huwatia nidhamu ili kuwalainisha na kuwafanya wawe wepesi wa kukubali ushauri na mwongozo wake ili wapate baraka. (Linganisha Ebr 12:4-11.) Ugumu wa udongo huamua utalimwa kwa nguvu kadiri gani, aina ya mbegu huamua uwezo na uzito wa vifaa vitakavyotumiwa kupura ili kuondoa makapi, na yote hayo yanaonyesha hekima ya Mungu kwa kuwasafisha watu wake na kuondoa chochote kisichopendeza akitumia njia tofauti-tofauti ikitegemea uhitaji na hali zilizopo.​—Linganisha Isa 21:10; 1:25.

Ikiwa jiji ‘lingelimwa kama shamba’ ilimaanisha kwamba jiji hilo lingeharibiwa kabisa na kubaki ukiwa. (Yer 26:18; Mik 3:12) Waisraeli wanaposema kwamba wale “wanaolima kwa jembe la plau wamelima mgongoni mwangu; wameirefusha mitaro yao,” inaelekea wanafafanua jinsi taifa hilo lilivyoteseka chini ya adui zake wengi wakatili na ambao waliendelea kulikandamiza bila huruma, huku taifa hilo likifanya mgongo wake uwe “kama ardhi . . . ya kutembea juu yake.” (Zb 129:1-3; Isa 51:23; linganisha Zb 66:12.) Katika unabii wa kurudishwa ulio katika Amosi 9:13-15, Yehova anaubariki udongo na unakuwa na rutuba hivi kwamba bado mavuno yanaendelea hata msimu wa kulima unapofika.​—Linganisha Law 26:5.

Yesu alisema kwamba wanafunzi wake wanapaswa kukubali chakula, vinywaji na makao yaliyoandaliwa na wale waliowatumikia, kwa sababu “mfanyakazi anastahili mshahara wake.” Kwa hiyo, mtume Paulo alionyesha kwamba wale wanaofanya kazi kwa bidii katika huduma ya Kikristo wana haki ya kupata msaada wa kimwili kutoka kwa wengine, kama vile mtu anayelima ana tumaini halali la kufurahia mavuno aliyoyafanyia kazi. Hata hivyo, Paulo aliamua kibinafsi na kwa hiari kufanya kazi ya kimwili ili aweze kutoa “habari njema bila gharama” kwa wale aliowahudumia.​—Lu 10:7; 1Ko 9:3-10, 15, 17, 18.

Yesu Kristo alitumia kazi ya kulima kukazia umuhimu wa kujitoa kwa moyo wote kuwa mwanafunzi. Mtu fulani aliposema kwamba angependa kuwa mwanafunzi lakini akaomba kwanza aruhusiwe kuwaaga watu wa nyumbani kwake, Yesu alimjibu hivi: “Yeyote anayeshika jembe la ng’ombe na kutazama vitu vilivyo nyuma hastahili Ufalme wa Mungu.” (Lu 9:61,  62) Ikiwa mkulima aliyetumia plau angejiruhusu kukengeuka anapolima, basi angetengeneza mitaro iliyo kombo. Vivyo hivyo, mtu anayealikwa awe mwanafunzi Mkristo lakini anakubali kukengeushwa asitimize majukumu yake akiwa mtumishi, hastahili Ufalme wa Mungu. Kama Mwana wa Mungu alivyoonyesha kutokana na mfano wake, kutimiza kwa uaminifu mapenzi ya Mungu ni muhimu kuliko uhusiano wa karibu katika familia.​—Mk 3:31-35; 10:29, 30.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki