Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w74 2/15 kur. 87-92
  • Je! Unautazamia Urithi kwa Bidii?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Unautazamia Urithi kwa Bidii?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • WALE WALIOTAZAMIA KARNE NYINGI MAPEMA
  • ULIZO LA SHUKRANI
  • UNAJISIKIAJE JUU YA URITHI?
  • Yakobo Alipewa Urithi
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Yakobo na Esau Wafanya Amani
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Linda Urithi Wako kwa Kufanya Maamuzi ya Hekima
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Mapacha Waliokuwa Tofauti
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
w74 2/15 kur. 87-92

Je! Unautazamia Urithi kwa Bidii?

Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.”​—Mt. 25:34.

1-3. (a) Kwa sababu gani urithi ambao tunayo nafasi ya kuutazamia ni wa maana zaidi kuliko fedha au mali? (b) Ni urithi gani mbalimbali ambao Biblia inaonyesha uko mbele kwa wale wanaomtumikia Mungu?

JE! Unajua kwamba waweza kuwa na urithi wa kutazamia? Siyo urithi wa fedha tu, inayoweza kuleta taabu. Siyo namna ya urithi inayowafanya watu wa udugu wawe maadui mara nyingi. Hapana, bali, urithi huu ni mmoja ambao warithi wote wenye kuutazamia wanajaribu kusaidiana waupate kabisa.

2 Mitume wake Yesu Kristo walizungumza mara nyingi juu ya urithi ulioko mbele kwa ndugu za kiroho za Mwana huyu wa Mungu​—urithi mbinguni pamoja na Kristo. Hawa watashiriki katika utawala wake wa ufalme. Wakiwa hivyo, urithi wao unatia ndani na zawadi za kutokuharibika na kutokufa.​—1 Kor. 6:9, 10; 15:50; Efe. 1:14; 1 Pet. 1:4.

3 Kisha huko mbele kuna urithi kwa wengine. Katika mmojawapo wa mifano yake Yesu alizungumza juu ya wale ambao wangewaonyesha ndugu zake za kiroho fadhili za upendo, warithi wa kimbinguni. Alisema kwa hawa watu wenye mioyo yenye fadhili: “Urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.” Alitaja kwamba hii ingemaanisha uzima wa milele kwao. Urithi huu usingekuwa kama ule wa warithi wa kimbinguni, bali kama ule wa wale watakaoshiriki katika makao ya kidunia watakaotawaliwa na ufalme wa Kristo mnamo utawala wake wa miaka 1,000.​—Mt. 25:34, 46; Ufu. 20:4, 6.

4, 5. Maana ya neno la Kigiriki lililotafsiriwa “-rithi” katika Biblia ni nini?

4 Neno la Kigiriki inalotumia Biblia kwa “-rithi” ni kle·ro·no·meʹo. Katika matumizi yaliyotajwa juu halimaanishi jambo fulani analolipata mtu kama haki kwa sababu tu ya ujamaa, kama vile mwana anayepokea urithi fulani kutoka kwa baba yake. Bali, linamaanisha kitu fulani kinachotolewa kama thawabu, zawadi inayotolewa kwa sababu ya mambo yaliyofanywa katika imani kwa mpango wa Yehova kupitia kwa Yesu Kristo.

5 Wote wale ambao wamemfikia Yehova Mungu juu ya msingi wa dhabihu ya Yesu Kristo na wanaoishi maisha yenye wakf wamo katika njia ya kuupata urithi huo. Lo! namna lilivyo zuri tumaini tunalolitazamia! Ni urithi usiolinganika na urithi wo wote wa kidunia kutoka kwa wazazi.

WALE WALIOTAZAMIA KARNE NYINGI MAPEMA

6-8. (a) Simulia namna wanaume waaminifu wa kale walivyouona urithi. (b) Ni mahali gani na wakati gani wanaume hawa walipotazamia kuupokea urithi?

6 Utapitia katika nini kusudi uupokee urithi, thawabu ya uzima wa milele? Mtume Paulo anasimulia namna wanaume wazee wa kale, karne nyingi mbali na urithi, walivyouona. Juu ya Ibrahimu, anaandika: “Kwa imani Ibrahimu . . . aliitika, atoke aende mahali . . . asijue aendako. . . . Maana alikuwa akiutazamia mji [Ufalme] wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.” “Kwa imani [yeye] . . . akamtoa Isaka awe dhabihu.”​—Ebr. 11:8-10, 17.

7 Juu ya mwanamume mwingine aliyeupendelea urithi wa kimungu kupita mambo mengine yote, Paulo anasema: “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; . . . kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo [kwa bidii].”​—Ebr. 11:23-26.

8 Wanaume hawa, na wengine wengi kama wao, walikuwa wenye bidii, si kwa ajili ya urithi wa kidunia katika hii taratibu ya mambo, bali kwa ajili ya urithi katika taratibu mpya ya Mungu. Paulo anasema: “Wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia . . . Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji [Ufalme].”​—Ebr. 11:13-16.

9. Ijapokuwa mashahidi wa Yehova wako karibu sana kuipata thawabu kuliko hao wanaume waaminifu walivyokuwa, je! wana uhakika zaidi wa kuipokea?

9 Wote wale walio mashahidi wa Yehova wanajua kwamba kunao urithi wa ajabu, thawabu, ulioko mbele, na wote wanatamani kuingia katika huo. Kwa kweli, si lazima tutazame mbali sana mbele yetu​—⁠ sasa tupo mlangoni. Lakini je! kuna hatari ya mtu kuudharau urithi, na kuupoteza? Ipo. Inahitaji fikira sikuzote kuuweka upendo wa urithi mahali pafaapo, kwa maana lazima uwemo si katika akili zetu tu lakini vile vile katika mioyo yetu. Kwamba kila mmoja wetu aweze kujichunguza mwenyewe, ingekuwa vizuri kujikumbusha habari ya Biblia inayoutilia mkazo umuhimu wa urithi. Ni kumbukumbu la ndugu-mapacha Yakobo na Esau.

10. Ni urithi gani wa maana sana aliokuwa nao Isaka?

10 Tunaingia katika habari ambapo vijana hawa wa kiume walikuwa wanakua. Wote wawili walikuzwa na baba yao Isaka na mama yao Rebeka waujue “uzao” ulioahidiwa ambao ungezibariki jamaa zote za dunia. (Mwa. 3:15) Wote wawili walijua kwamba babu yao Ibrahimu alikuwa amefundishwa kwamba “uzao” ungetokea katika ukoo wake, kupitia kwa Isaka, na kwamba baraka ya Mungu ilikuwa imekuwa juu ya baba yao Isaka. (Mwa. 21:12; 22:15-18; 25:11; 26:24) Huu ulikuwa urithi wenye maana kubwa sana. Vile vile Isaka alikuwa tajiri kwa kimwili. Vijana hao wangeurithi utajiri huu vile vile, mwana mzaliwa wa kwanza akipokea sehemu mbili. Lakini je! ni kijana gani ambaye angestahili kuupokea urithi, zaidi ahadi ya “uzao” kupitia kwa ukoo wa jamaa? Esau, mwana mzaliwa wa kwanza, alikuwamo katika cheo kilichopendelewa kwa kulingana na maoni ya kibinadamu.​—Mwa. 25:25, 26.

11, 12. Simulia nia za vijana wa kiume Yakobo na Esau walipozidi kukua.

11 Maandishi ya Biblia yanatuambia: “Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu [mnyofu], mwenye kukaa hemani.”​—Mwa. 25:27.

12 Maneno haya yanaonyeshaje ilivyokuwa nia ya vijana hawa? Yanafunua wazi yaliyokuwamo ndani ya moyo wa kila mmoja. Esau alikuwa mtu hodari wa kuwinda. Aliutumia wakati wake nje uwandani akijifunza ufundi wa mwindaji. Yakobo, kwa upande mwingine, alishughulikia nyumba ya jamaa. Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa “-nyofu” lamaanisha “-aminifu,” “-sio na hatia,” “kamili.” Yakobo, ingawa hakuonyesha nguvu yake au uwezo kama inavyoelekea kuwa Esau alifanya, hakuwa goigoi hata hivyo, kwa maana nyumaye Yehova alizungumza juu yake kama mwenye “nguvu nyingi.” (Hos. 12:3, NW) Ukweli ni kwamba Yakobo aliipendelea ahadi ya agano kwa Ibrahimu kupita kinginecho chote naye alivitoa vyote alivyokuwa navyo ajifunze juu ya ahadi kutoka kwa baba yake. Alijitoa mwenyewe ayaangalie mapendezi ya jamaa hii ambayo Mungu alikuwa ameitaja kama warithi. Alitaka kukaa karibu na wale ambao Mungu alikuwa anabariki, ijapokuwa alimtazama Esau kama aliyemtangulia, kwa maana Esau alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza.

13. Nyumaye, vijana hawa wa kiume walitoa ushuhuda wenye nguvu sana namna gani juu ya nia zao kwa urithi?

13 Nyumaye vijana hawa wawili wa kiume walitoa ushuhuda wenye nguvu zaidi wa nia zao. Twasoma:

“Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. . . . Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake.”​—Mwa. 25:29-34.

ULIZO LA SHUKRANI

14, 15. Je! Yakobo alikuwa akimtumia Esau kwa njia ya kichoyo kwa kuinunua haki ya uzazi, nayo maamuzi ya Yehova yalishuhudiwaje na tendo hilo?

14 Je! Yakobo alikuwa mchoyo, akimtumia Esau kwa njia mbaya? Huenda ielekee kuwa hivyo. Lakini angalia hili: Je! Kwa kweli Esau aliona ubora wa mambo ya ajabu yaliyosimamiwa na haki yake ya uzazi? Hakuwa kufani kweli, kama yeye alivyosema. Hii inaonyeshwa na kuondoka kwake nyuma ya kula na kwenda zake. Biblia yasema, “alikuwa amechoka sana.” Kwa sababu gani Esau alivutwa kufanya alichokifanya? Habari yatuambia: “Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.” Mtume Paulo aliyahakikisha maneno haya alipomwita Esau mtu “asiyethamini mambo matakatifu, . . . ambaye kwa kuzibadilisha na chakula kimoja alitoa haki zake kama mzaliwa wa kwanza.”​—Mwa. 25:34; Ebr. 12:16, NW.

15 Haya yote yalihakikisha maamuzi ya Mungu kuwa haki wakati, akitangulia kuziona tabia za vijana hawa, alikuwa amekwisha mwambia mama yao Rebeka mbele ya wao kuzaliwa: “Mkubwa atamtumikia mdogo.”​—Mwa. 25:23; Rum. 9:12.

16. Kwa sababu gani Yakobo alikuwa na haki ya kuipokea baraka ya mzaliwa wa kwanza kutoka kwa baba yake, lakini kwa sababu gani, kwa wazi, hakuchukua hatua ya kwanza kuiomba?

16 Yakobo sasa alikuwa ndiye mwenye haki ya mzaliwa wa kwanza kwa mambo mawili: kwa ahadi ya Mungu, na kwa haki ya ununuzi. Lakini yeye hakuwa na baraka ya Isaka bado juu ya mzaliwa wa kwanza. Hata hivyo kwa wazi Yakobo hakuwa akitenda kwa choyo, hakujaribu hata kidogo kumtangulia Esau katika hili. Bila shaka alikuwa akimngoja Yehova. Isaka sasa alikuwa kipofu, naye hakujua matukio yote yaliyokuwa yakitukia. Bila shaka akivutwa na Yehova kutenda, Rebeka, akiyakumbuka maneno ya Mungu kwake mbele ya kuzaliwa kwa vijana, alimwagiza Yakobo kusudi ampatie baraka.

17, 18. Onyesha kwamba Rebeka na Yakobo hawakuwa wadanganyifu, na kwamba mkono wa Yehova ulikuwamo katika shauri la Yakobo kuipata baraka.

17 Katika yaliyofuata, wasomaji wengine wa Biblia wanawashitakia Rebeka na Yakobo udanganyifu na werevu. Lakini je! ndivyo ilivyo? Kufikia hapo ni nani kweli aliyekuwa katika cheo cha mzaliwa wa kwanza kwa haki zote? Nani aliyeutunza urithi? Kwa sababu gani Esau alimficha Isaka asijue kwamba Yakobo alikuwa ameinunua haki ya uzazi, lakini mahali pake akajaribu kupata baraka iwe yake mwenyewe? Isaka, ni kweli, alimbariki Yakobo, kwa kosa akifikiri alikuwa akimbariki Esau. Lakini nyumaye aligundua kwamba tendo la Yakobo na Rebeka lilikuwa haki. Aliuona mkono wa Yehova katika shauri hilo, akimbariki Yakobo tena, wakati huu kwa makusudi, kwa unabii juu ya “uzao.” Kisha akampa Yakobo maagizo na kumtorosha akajipatie usalama kutoka kwa ndugu yake mwenye hasira Esau. Zaidi ya hayo, Mungu mwenyewe alimbariki Yakobo kwa ahadi kwamba “uzao” ungekuja kupitia kwa ukoo wake.​—Mwanzo sura ya 27; 28:1-4.

18 Uhakikisho zaidi kwamba tendo la Yakobo halikuwa kwa ajili ya faida ya kichoyo ni kwamba alihama nyumbani, bila ya kuchukua mali za nyumbani. Na hakuna ushuhuda kwamba alidai sehemu zake mbili wakati wo wote. Kilichokuwa bora zaidi kwake ni urithi utakaokuja. Yeye alitaka agano la Mungu likae na jamaa. Ufahamu wake wa Yehova na ahadi Yake ulirahisisha kufikiria kinginecho chote.

19. (a) Yakobo alionaje alipokaribia kukutana tena na Esau? (b) Ni hali gani isiyo ya kawaida kabisa iliyotukia mbele ya Yakobo na Esau kukutana?

19 Tofauti na kukosa shukrani alikokuwa ameonyesha Esau, heshima kubwa aliyokuwa nayo Yakobo kwa urithi wa Mungu ilishuhudiwa tena na jambo fulani lililotokea Yakobo aliporudia nyumbani miaka 20 nyumaye akamtembelee baba yake. Yakobo alikuwa na sababu ya kuamini kwamba Esau anaweza kumdhuru, na kwa sababu hii aliogopa kidogo na kuwa mwenye busara. Alimpelekea Esau zawadi iitangulie jamaa yake yenye kuhama. Kama Esau angeikubali, hii ingemaanisha kwamba kulikuwamo amani kati yao. Lakini mbele ya kukutana, hali fulani isiyo ya kawaida ilitukia. Biblia yatoa habari:

“[Yakobo] akaondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo. Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n’nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko. Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake.”​—Mwa. 32:22-31.

20. Kwa sababu gani Yakobo alipigana mweleka na malaika usiku kucha?

20 Hapa yafunuliwa tofauti iliyo kubwa kati ya nia za Yakobo na Esau kwa habari ya urithi. Ajapokuwa Esau hakutaka kuona njaa hata kidogo kwa ajili ya haki ya uzazi, Yakobo alipigana mweleka usiku kucha na malaika wa Mungu aliyekuwa amejivika mwili kama mwanadamu. Yakobo alifanya hivi ili apate habari za baraka kutoka kwa Yehova kupitia kwa malaika. Bila shaka Yakobo alijua kwamba malaika alitokea kwa kusudi fulani, naye alijua kwamba malaika walipotokea nyakati zilizopita walikuwa wameleta baraka au amri katika uhakikisho wa agano lililofanywa pamoja na Ibrahimu. (Mwa. 28:10-15; 31:11-13) Kwa hiyo alitamani sana kuendelea kwa Mungu kuwa naye, kama vile ambavyo Mungu alikuwa amekuwa na baba yake na babu, kwamba akajitoa mwenyewe katika kupigana mweleka wenye jitihada, wenye kuchosha na malaika, akimshikilia asimwache. Kwa hiyo Yakobo alionyesha tamaa yake kuu ya moyoni ya kibali cha Mungu.​—Linganisha Mwanzo 28:20-22.

21. Sababu ya malaika ya kutegua kifundo cha paja la Yakobo ilikuwa nini?

21 Bila shaka, kwa kweli Yakobo hakumshinda malaika wa Mungu nguvu. Kisa hiki kilitumikia kama jaribu la tamaa ya Yakobo kwa moyo wake wote apatikane mwenye kumpendeza Mungu. Kwa kweli, kwa mguso mmoja tu malaika, kwa uwezo upitao ule wa kibinadamu, alikitegua kifundo cha paja la Yakobo kwamba akachechemea nyuma ya hapo. Hili lilitumikia kama jambo la kunyenyekeza, ulinzi kwa Yakobo. Ulikuwa ukumbusho kumfundisha Yakobo kwamba ni kupitia kwa fadhili zake Mungu zisizostahili, na si kupitia kwa nguvu zo zote ama ustahili kwa upande wa Yakobo, kwamba Mungu alikuwa amembariki na kumtumia. Linganisha maono ya mtume Paulo, yaliyoandikwa katika 2 Wakorintho 12:6-10.

22. Ni baraka gani zilizofuata na zitakazomjia Yakobo kwa sababu ya heshima yake kubwa kwa urithi kutoka kwa Mungu?

22 Matokeo kwa Yakobo na Esau yanatupa kichocheo chenye nguvu sana kuwa waaminifu, kulishikilia tumaini la thawabu. Yakobo alibarikiwa kuwa mzazi wa taifa kubwa. Lakini la maana zaidi, lilikuwa taifa alilolitumia Yehova katika kutimiliza wokovu kwa taifa la kibinadamu. “Uzao,” Masihi, ulikuja kupitia kwa ukoo wa Yakobo. Kwa sababu ya imani yake yenye nguvu Yakobo ‘yu hai’ machoni pa Mungu, nao ufufuo wake kwenye urithi, kushiriki katika makao ya kidunia ya ufalme wa Mungu, ni hakika kwake. Yeye bila shaka atakuwa mmojawapo wa “wakuu” ambao Yesu Kristo ataweka kama mwangalizi na mchungaji wa watu wake.​—Luka 20:37, 38; Zab. 45:16.

UNAJISIKIAJE JUU YA URITHI?

23, 24. Ni maulizo gani tuwezayo kujiuliza wenyewe, na je! twaweza kujihakikishia urithi?

23 Tunapoyatazama maisha ya Yakobo na Esau, kila mmoja wetu aweza kuuliza, ‘Je! mimi nayatumiaje maisha yangu? Je! ni kwa kadiri gani ninavyoona ubora wa urithi ulioahidiwa wa uzima katika taratibu mpya ya Mungu? Je! mimi nina nia ya kujitia katika taabu kwa ajili ya urithi? Je! nataka kuushikilia nisiuache kwa nguvu zangu zote?’

24 Sawa na alivyofanya Yakobo, twaweza kuuhakikisha urithi. Akili yake na moyo vilikuwa juu ya ahadi tangu ujana wake. Kwa wazi aliutumia wakati wake akijifunza yote aliyoweza juu ya matendo ya Mungu kwa baba yake Isaka na babu yake Ibrahimu. Alikuwa mwanamume aliyesali kwa Mungu. Alijitahidi naye akavumilia majaribu mengi lakini, mpaka mwisho, akashika upole wa roho na imani yenye nguvu.

25. Ni maulizo gani tuwezayo kuuliza kufahamu kama tunaona ubora wa haja yetu ya kiroho?

25 Yehova amekuwa mwenye fadhili sana katika kuitoa haja yetu ya kiroho. Je! wewe u kama Yakobo katika kuona ubora wake? Je! unaisoma Biblia yenyewe kwa kawaida? Je! unasoma Mnara wa Mlinzi, siyo makala za mafunzo tu lakini vile vile na makala nyingine humo? Humo mna habari nyingine nzuri ambazo usingezipata kwa njia nyingine yo yote.

26, 27. Yakobo alikuwa mfano wa subira namna gani katika kumngoja Yehova kwa urithi?

26 Je! wewe u mwenye subira na asiye mchoyo, kama alivyokuwa Yakobo? Je! una nia ya kutumikia kwa moyo wote, ukimngoja Yehova akubariki? Yakobo hakuona uchungu kwa sababu, katika umri wa miaka 77, alishauriwa na baba yake aondoke nyumbani, bila ya kuchukua cho chote cha urithi. Katika nia alikuwa tofauti kabisa na mwana mpotevu wa mfano wa Yesu, aliyetaka kuondoka nyumbani na vile vile akataka urithi wake, akautumie kwa tamaa zake mwenyewe. Yakobo alikuwa mwenye umri wa miaka 97 alipoanza safari ya kurudia nyumbani, siyo kwa sababu ya tamaa ya kudai urithi wa kidunia, bali kwa amri ya Mungu.​—Mwa. 31:3.

27 Yesu Kristo alisema: “Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.” (Marko 10:29, 30) Yakobo alijisikia hivi.

28, 29. Mfano wa Yakobo unaonyeshaje jitihada ambayo kwa hiyo yatupasa kuutazamia urithi kwa bidii?

28 Kwa hiyo ni shauri, siyo la kutumikia tukiwa na kusudi la kukoma wakati fulani, wala la kutafuta starehe za kimwili na raha kwa ajili yetu wenyewe wala kuvumilia chini ya majaribu machache tu. Ni shauri la wakati wa maisha yote, kuweka urithi mbele ya macho yetu sikuzote.

29 Ni shauri la kuushikilia urithi tusiuache, kwa jitihada na kutaabika tukifanya mambo ambayo mikono yetu yayapata kufanya, kama vile Yakobo alivyopigana mweleka usiku kucha na malaika. (Mhu. 9:10) Na kila kitu alichokifanya Yakobo alikifanya vyema, kwa nguvu zake zote. Vile vile, aliyaweka mapendezi ya mwenzake mbele ya yake mwenyewe. Tazama namna Yakobo alivyojibidiisha kwa ajili ya mapendezi ya Labani mtu wa udugu na tajiri wake. Yeye alisema:

“Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba, wala waume katika wanyama wako sikuwala. Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku. Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu.”​—Mwa. 31:38-40.

30. Kwa sababu gani Yakobo alijitahidi sana kwa ajili ya Labani kwa miaka 20?

30 Sasa Yakobo hakuwa akifanya kazi ya kimwili amsaidie Labani tu, wala akusanye utajiri wa kimwili. Yakobo alikuwa akikusanya kundi lake la wanyama akikusudia kurudia nyumbani nyumaye akiwa na jamaa yake mwenyewe. Kwa sababu gani? Kwa sababu alijua kwamba Ibrahimu na Isaka vile vile walikuwa wageni nchini na kwamba mwishowe Mungu angeitoa awape wazao wa Ibrahimu. Yakobo aliiamini ahadi hii. Nafsi yake yote ilifungamana na hili. Alitaka awe na nyumba iliyo huru, moja ambayo ingeweza kumtumikia Mungu kabisa. Naye Mungu alimbariki kwamba jamaa yake, wana wake kumi na wawili, wakawa msingi kweli wa taifa kuu la Israeli.

31. Wakristo wana kazi gani leo inayofanana na ya Yakobo?

31 Wakristo leo wanayo kazi ya kufanya inayohitaji uangalifu wa moyo wote. Kazi hiyo inatia ndani kuzitunza faida za Ufalme. Lazima habari njema zitangazwe. Uaminifu unahitajiwa. Kazi ya uchungaji yapaswa ifanywe kwa bidii ile ile na jitihada ambavyo Yakobo alivitumia akiwa na makundi yake ya wanyama na ya Labani. Sawa na kwa Yakobo, urithi ulioko mbele wastahili kutazamiwa kwa bidii. Neno la Kigiriki lililotafsiriwa “alitazamia kwa bidii,” katika Waebrania 11:26, NW, linamaanisha kuondosha macho katika mambo mengine yo yote na kutazama kitu kimoja.

32. Maana yake nini kweli kuutazamia urithi au thawabu kwa bidii?

32 Tukiwa na bidii hiyo juu ya urithi hakuna kitakachotukwaza. Hakuna kitakachotuondoshea kando. Tutahakikishiwa urithi wa ajabu, kama huo utakuwa katika mbingu, kama vile kwa habari ya ndugu za Yesu Kristo waliozaliwa kwa roho, au katika makao ya kidunia ya Ufalme. Tumaini hili la pili linakubaliwa na walio wengi wa mashahidi wa Yehova duniani leo. Vikundi vyote viwili vinayo nia ya mtume Paulo, aliyekuwa na tumaini la mwito “wa juu” (NW, wa kimbinguni). Yeye aliandika: “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” Watu wote wa Mungu na waishike bidii hiyo.​—⁠Flp. 3:13, 14.​—

Kutoka The Watchtower, Aug. 15, 1973.

[Picha katika ukurasa wa 89]

Yakobo aliipendelea ahadi ya agano kwa Ibrahimu, lakini Esau aliuuza urithi wake kwa chakula kimoja. Je! wewe unaona ubora wa mambo matakatifu, kama alivyofanya Yakobo? Je! unautazamia urithi wa uzima kwa bidii katika taratibu mpya ya Mungu na kuonyesha hivyo kwa njia unavyoyatumia maisha yako?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki