Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w74 3/1 kur. 103-109
  • Lugha ya Watu Wote

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Lugha ya Watu Wote
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UWEZO WENYE KUUNGANISHA WA KWELI
  • UPINZANI KWA LUGHA ILIYO SAFI
  • Je, Unazungumza Ile “Lugha Safi” kwa Ufasaha?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Unganishweni Na Lugha Iliyo Safi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Namna Lugha Moja Itakavyoleta Umoja kwa Wanadamu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Lugha Safi Kwa Ajili Ya Mataifa Yote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
w74 3/1 kur. 103-109

Lugha ya Watu Wote

“Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la [Yehova], wamtumikie kwa nia moja.”​—Sef. 3:9.

1. Ni maulizo gani yanayotokea juu ya lugha?

JE! KWA kweli lugha ilikuwa na vyanzo vyake wakati mwingi uliopita watu walipokuwa wakijifunza kupashana habari kwa kuiga kuguna, kuzoma na mbweko wa wanyama? Ikiwa lugha ya kwanza ilikuwa ya kishenzi namna hii, yawezekanaje kwamba lugha zijulikanazo kuwa za kale zaidi zilikuwa na sarufi ngumu kufahamika? Hata hivyo lugha zote zilitoka wapi? Lugha nyingi namna hiyo zilisitawi namna gani kwamba leo zipo lugha 2,796 au zaidi zinazozungumzwa, hata kabila lisilostaarabika zaidi la mwituni likisema lugha fulani? Je! yawezekana kwamba ulimwengu wa wanadamu utaunganishwa wakati wo wote kwa lugha moja, lugha ya watu wote, kuliko kuwa ulimwengu uliopambanuliwa na kugawanywa na vizuizi vya lugha?

2. Lugha ilianzaje, na je! matumizi yake ni ya duniani tu?

2 Maandiko Matakatifu, sehemu yake ya zamani sana kama inavyoonekana leo ikiwa ni ya tangu mwaka wa 1513 B.C.E., yanafahamisha sana juu ya ukuzi na kuenea kwa lugha. Yanafunua wazi kwamba lugha ilianzishwa na Mungu. Hata mbele ya mwanadamu kuumbwa, lugha ilikuwako. Yehova Mungu anasemekana katika habari ya kuumba kama akizungumza na Mwana wake mzaliwa wa kwanza katika makao ya kimbinguni na kusema, “Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” Kwa kufaa, Mwana huyu wa Mungu alikuja kuitwa “Neno” naye alitumikia kama mnenaji wa Baba yake, katika kupashana habari si na kuumba kwingineko kwa kiroho kwa kimbinguni tu lakini vile vile na mwanadamu.​—Mwa. 1:26; Yohana 1:1-3.

3. Ni nyakati gani malaika walipopashana habari na wanadamu?

3 Karne nyingi nyuma ya hapo mtume Paulo aliufahamu uwezo wa wale waliomo katika makao ya kiroho wa kupashana habari, kama inavyoonyeshwa na mtajo wake wa “lugha za wanadamu na za malaika.” (1 Kor. 13:1; linganisha Ayubu 1:7-12; 2:2-6.) Maandiko yanashuhudia uhakika wa kwamba malaika walipashana habari na wanadamu nyakati mbalimbali. Malaika ndiye aliyempasha Ibrahimu maneno ya Yehova ya baraka na ahadi kwamba kupitia kwa uzao wake jamaa zote za dunia zingebarikiwa, hali wakati mwingine malaika wa Yehova aliwatangazia wachungaji karibu na Bethlehemu habari njema za kuzaliwa kwa Yesu.​—Mwa. 22:15-18; Luka 2:8-11.

4. Ni uwezo gani aliopewa Adamu, na twajuaje hili?

4 Kama vile Yehova alivyowapa wana wake wa kiroho zawadi hii ya usemi, ndivyo alivyomfanyia na mwana wake wa kibinadamu Adamu. Yehova alimpa uwezo, siyo wa kusema na kufahamu usemi tu, lakini vile vile na wa kubuni maneno mapya, kwa njia hiyo akiiongezea lugha, kama alivyofanya katika kuwapa wanyama majina. (Mwa. 2:19) Uhakika ule ule wa kwamba Yehova alimwagiza Adamu katika kazi aliyopaswa kufanya katika kuijaza dunia, kuilima na kuwatawala wanyama, na vile vile akimwonya juu ya kuiasi sheria yake Yeye, ulionyesha kwamba Mungu alikuwa amempa Adamu maneno yaliyohitajiwa na ujuzi wa lugha kumruhusu ayafahamu maagizo haya.

5. Kwa sababu gani ujuzi wa lugha ni wa maana sana kwetu?

5 Lakini, zawadi hii ya lugha haikushirikiwa na wanyama. Wangawa huenda wakaweza kuonyesha maoni ya woga, hasira, tamaa na uradhi kwa milio, hata hivyo kama alivyoandika mbuni kamusi Koehler: “Wanakosa wazo na fikira, nguvu iliyo ya muhimu ya lugha ya kibinadamu.” Kwa hiyo lugha ya kuzungumza ni zawadi anayoishiriki mwanadamu pamoja na malaika, lakini si na namna za chini za kuumba. Lugha ni ufunguo wa ujuzi kweli kweli na ushirikiano wa kibinadamu, nayo inafanyiza msingi wa wingi mkubwa wa namna zote za kupashana habari. Kama vile kilivyosema kitabu kimoja cha maarifa yote: “Kufikiri na maneno vinakwenda pamoja.” Bila ya maneno mtu angekuwa mwenye mafundisho machache na mawazo ambayo angeweza kushiriki na mtu mwingine, kama msafiri ye yote katika nchi ya ugenini alivyoona. Bila ya maneno, yaelekea, hata uwezo wetu wa kufikiri ungekuwa haba.

6. Ni kwa njia gani na kwa sababu gani lugha nyingi mbalimbali zikapata kutokea?

6 Kwa zaidi ya karne kumi na nane nyuma ya kuumbwa kwa mwanadamu wa kwanza Adamu, wanadamu wote walizungumza lugha aliyokuwa amepewa mwanzoni na Mungu. (Mwa. 11:1) Hali sasa twaona karibu lugha 3,000 zikizungumzwa ulimwenguni mwote, bila ya kutia ndani matamko mengi sana ya mahali. Hii ilitukiaje? Maandiko yanasema kwamba ilikuwa katika uwanda katika Shinari, nyuma ya Gharika, kwamba wanadamu wakaamua kujifanyia jina kwa kujenga mji wenye mnara ukielekea kwenye mbingu. Kwa wazi pangekuwa mahali pa kati pa ibada ya uongo, kwa maana jitihada zao zilikuwa tofauti na maagizo yaliyotangulia ya Yehova kwa Nuhu na wana wake watatu waliooa ya kutawanyika na kuijaza dunia. Kama matokeo, Yehova alisema: “Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, . . . na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo [Yehova] alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko [Yehova] akawatawanya waende usoni pa nchi yote.”​—Mwa. 11:6, 7, 9.

7. (a) Nini maana ya “namna za lugha”? (b) Ni vikundi vingapi vya kitaifa na kilugha vilivyogawanyikana kutoka Babeli?

7 Mungu alichafuaje ufahamu wao wa Kiebrania cha kwanza, akiwafanya wanadamu wagawanyikane katika vikundi mbalimbali vya lugha? Kwa wazi ilikuwa ni kwa kulifuta kumbukumbu lao la iliyokuwa lugha yao na kuweka mahali pake maneno mapya na sarufi. Kama wajuavyo wanafunzi wa lugha, kuna namna mbalimbali za lugha. Hakuna ushuhuda wa kwamba zote zinarudia nyuma kwenye lugha ya kwanza ya Adamu ama kwamba zote zimegeuka kutoka Kiebrania, bali, zinatokana na namna nyingi za lugha zilizoanza wakati wa Babeli. Kwa mfano, kila moja ina maneno yake yenyewe na njia ya kufanyiza mawazo, hivi kwamba watu zaidi wanafikiri katika namna tofauti za lugha, ikitegemea sarufi na miisho ya maneno. Hivyo Mwanzo sura ya kumi unazungumza juu ya vikundi vya kitaifa 70 vilivyotoka kwa Nuhu na lugha ambazo Mungu alitoa katika Babeli, ukisema: “Kwa hao nchi za pwani za mataifa ziligawanyikana kuwa nchi zao, kila moja kwa lugha yake, kwa jamaa zao, kufuata mataifa yao.”​—Mwa. 10:5, 20, 31.

8. Wanafunzi wamejifunza kitu gani juu ya lugha?

8 Wakati ulivyozidi kupita, matamko, hata lugha mpya zilizokamatana na lugha hizi za kwanza, yalianza kusitawi kwa sababu ya mambo mbalimbali, kama vile vizuizi vya mambo ya asili ya dunia, umbali, ushirika na makundi mengine ya watu na mateka. Lakini, mbali na Kiebrania, vikundi hivi vyote au namna za lugha zaweza kufuatishwa nyuma kwenye mwanzo wa lugha mpya za ulimwengu katika nyanda za Shinari. Hivyo mwanafunzi wa lugha Sir Henry Rawlinson alisema: “Kama tungeongozwa na kukingamana tu kwa njia za lugha, na bila ya kutegemea habari zo zote katika kumbukumbu la Maandiko, bado tungeongozwa kukazia fikira zetu kwenye nyanda za Shinari, kama mahali penyewe ambapo mistari mbalimbali ilikuwa imetoka.” Jambo jingine la kupendeza juu ya lugha hizi zilizotolewa kwa njia ya kimungu ni kwamba, kuliko kuwa za vivi hivi, Science News Letter kinasema, zilikuwa ngumu zaidi kufahamika kuliko lugha za kisasa za Ulaya. Hii ingewezekanaje ikiwa lugha zilitokea katika hali ya kuguna na kuzoma?

9. Maandiko yanaonyesha nini juu ya uwezo wa mwanadamu kwa habari ya lugha?

9 Matamko na tofauti katika namna za lugha tulizo nazo leo vyaweza kuuhesabia sifa uwezo ambao Yehova alimpa mwanadamu kwa habari ya lugha. Kama vile Adamu alivyokuwa na uwezo wa kuongezea maneno yake, ndivyo na mwanadamu alivyoweza kuongezea maneno yake na hata kujifunza lugha mpya. Kwa mfano, Ibrahimu kwa wazi hakuwa na shida ya kuzungumza na watu wa ukoo wa Hamu wa Kanaani, wala uhitaji wa wakalimani hautajwi. (Mwa. 23:7-15) Yawezekana alijua Kiakadia, kilichotumiwa sana katika eneo alilohamia. Nyumaye, habari ya Biblia yaonyesha, Yusufu alijifunza Kimisri alipokuwa Misri, yaelekea sana alipokuwa mtumwa wa Potifa, na kwa hiyo angeweza kuzungumza bila shida na Farao. Lakini ili kuepuka kujijulisha wazi mapema isivyofaa kwa ndugu zake za Kiebrania alipokuwa akizungumza nao kwanza alitumia mkalimani.​—Mwa. 42:23.

10. Ni kwa njia gani na kwa sababu gani Yehova aliuonyesha uwezo wake kwa habari ya lugha katika Pentekoste?

10 Ni katika Pentekoste ya mwaka wa 33 C.E. Yehova alipouonyesha uwezo wake tena wa kuogofisha kwa habari ya lugha kwa maana Wakristo wa kwanza katika Yerusalemu kwa ghafula walipewa zawadi ya roho takatifu pamoja na uwezo wa kusema katika lugha nyingi wasizozijua hapo kwanza. Lakini wakati huu Yehova aliuzidisha ujuzi wa lugha ambao wanafunzi hawa wa Yesu walikuwa nao tayari, kuliko kufuta katika kumbukumbu lugha ya kwao, kama alivyokuwa amefanya katika Babeli. Kusudi la zawadi hii ya lugha zaidi vile vile lilikuwa tofauti​—siyo kuwaondosha watu kwenye kusudi baya, lakini kuendeleza maenezi ya ibada ya kweli na ujuzi wa Muumba kati ya watu wa lugha nyingi. (Matendo 2:1-11) Nyuma ya wakati wa Pentekoste, wajapokuwa wale walioifuata ibada safi hawakusema lugha moja, waliunganishwa na kifungo cha kawaida cha ujuzi wao wa makusudi ya Mungu.

UWEZO WENYE KUUNGANISHA WA KWELI

11. Ni katika njia gani mbili roho ya Mungu ilitenda juu ya wanafunzi katika Pentekoste?

11 Yesu alikuwa amekwisha kuwaambia mitume wake mapema kwamba “msaidizi, roho takatifu, ambayo Baba atapeleka katika jina langu, huyo atawafundisheni mambo yote na kuwakumbusheni mambo yote niliyowaambieni.” (Yohana 14:26, NW) Ni chini ya uongozi wa roho hii kwamba Petro akatoa ushuhuda wenye nguvu kwa makusudi ya Yehova alioutoa katika Pentekoste, matokeo yake yakiwa ni ubatizo wa karibu wafuasi wapya 3,000 kwenye imani ya Kikristo. Wayahudi wanyenyekevu kutoka katika nchi mbalimbali zisizopungua kumi na tano waliokuwa wamekusanyikia Yerusalemu walistaajabu kuwasikia wanafunzi 120 wakizungumza katika lugha nyingi za nchi zao. Kama vile walivyosema: “Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? . . . tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”​—Matendo 2:7, 8, 11, 41.

12. Petro alitoa ushuhuda wa kitu gani, na kwa matokeo gani?

12 Petro aliendelea kueleza katika Kiebrania tukio hili lenye kustaajabisha kwa kuutaja unabii wa Yoeli juu ya kumiminwa kwa roho ya Mungu. Alikazia kwamba Yehova ndiye aliyekuwa akitoa njia ya wokovu, alipoukazia mtajo wa nabii wa “siku za mwisho,” wakati ambapo “kila atakayeliitia jina la [Yehova] ataokolewa.” Alipokuwa akikazia fikira kwenye kazi zenye nguvu alizokuwa amefanya Yesu zikielekeza kwenye kifo chake na ufufuo wa mwujiza, Petro alikikazia cheo chenye fahari cha Yehova kama Mwenye Enzi Yote Aliye Mkuu Zaidi Sana. Aliyatumia maneno ya Daudi kwa Yesu, “Nalimwona [Yehova] mbele yangu sikuzote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.” Ujumbe huu wenye nguvu uliwavuta maelfu kulikubali kwa moyo tumaini la Maandiko lililotolewa kwao na watoto wao, ijapokuwa nyuma ya hapo lilileta upinzani na mateso juu yao.​—Matendo 2:17, 21, 25; Yoeli 2:32.

13. Ukristo ulionyeshwa kuwa nguvu yenye kuunganisha namna gani?

13 Matokeo yenye kuunganisha ya ujumbe uliotangazwa huko yalikuwa ya ajabu. Watu wa nchi nyingi waliletwa pamoja kama mmoja katika imani. Kama vile Paulo alivyoeleza nyumaye: “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Hapana Myahudi wala Myunani. . . . Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.” (Gal. 3:26, 28) Wajapokuwa walizungumza lugha nyingi, ujumbe wao ulikuwa ule ule. Kama vile Paulo alivyokazia kwa ndugu za Kigiriki katika Korintho, wote wamepaswa ‘wanene mamoja’ na kuwa ‘waliohitimu katika nia moja na shauri moja.’​—1 Kor. 1:10.

14. Ni kwa njia gani imepaswa zawadi yetu ya usemi itumiwe, kwa kulingana na Daudi na Paulo?

14 Jambo la muhimu katika akili za Yesu na wanafunzi wake wa kwanza lilikuwa ni kuutumia ulimi wao kumsifu Muumba wao. Walijisikia kama Daudi alivyokuwa amejisikia aliposali, “Ee [Yehova], uifumbue midomo yangu, na kinywa changu kitazinena sifa zako.” (Zab. 51:15) Wajapokuwa waliambiwa na watawala waikomeshe huduma yao, wao walitangaza: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” (Matendo 4:20) Lakini, hawakuonyesha tamaa yao ya usemi ufaao kwa kuzungumza tu juu ya mambo ya makusudi ya Mungu, lakini vile vile kwa njia yao ya usemi katika kila kitu. Kama vile Paulo alivyolishauri kundi la Efeso: “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.”​—Efe. 4:9.

15. Ni ahadi gani inayotolewa katika Sefania 3:9, na kwa sababu gani ni ya maana kwetu?

15 Je! twaweza kuitumia zawadi ya lugha kutoka kwa Yehova katika njia ile ile leo? Bila shaka twaweza, nao unabii wa Sefania ulitangulia kuonyesha kwamba hili lingefanyika. Maneno yanayozunguka yanaonyesha kwamba Yehova amekusudia kuyakusanya mataifa ayamiminie hasira yake yenye kuwaka, inayotokezwa na uamuzi wake wa hukumu juu yao. Je! wengine watauokoka uamuzi huu wa hukumu na hasira ya Yehova? Kwamba twaweza kufurahia kibali chake yaonekana katika uhakikisho wake wa unabii: “Maana hapo [au wakati wa “siku za mwisho”] ndipo [mimi Yehova] nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la [Yehova], wamtumikie kwa nia moja.” Kweli, kama isingalikuwa ni kwa sababu ya kuisema lugha iliyo safi na kuliitia jina la Yehova, kama alivyokuwa ameeleza Petro, kusingekuwako njia ya kuokokea kisasi cha Yehova juu ya mataifa. Hali Yoeli anatuhakikishia: “Watakuwako watu watakaookoka, kama [Yehova] alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao [Yehova].”​—Sef. 3:8, 9; Yoeli 2:32.

16. (a) Twawezaje kujifunza “lugha iliyo safi”? (b) Nini kinachoonyesha kwamba Kristendomu hakuijua sana?

16 Je! wewe umekuwa ukijifunza “lugha iliyo safi” iliyo ya lazima kwa wokovu? Kama vile kila lugha ilivyo na namna yake tofauti ya maneno na sarufi, ndivyo na kweli, kama inavyokuja katika neno la Mungu Biblia na kama alivyotufunulia ufahamu wake katika hizi “siku za mwisho,” ilivyo na namna yake tuwezayo kuja kujifunza, umoja wa ndani. Msingi wake ni habari ya ufalme wa Mungu wa haki. Mara mtu ajifunzapo hiki “kielelezo cha maneno yenye uzima,” kama Paulo alivyokisimulia, kwa kuja kwenye ujuzi wa kweli wa Maandiko, ndipo anapoweza kuwaeleza wengine juu yake bila ya kusita-sita, bila ya kukifanyia mageuzi yasiyofaa ya mafundisho. (2 Tim. 1:13; 2 Pet. 3:16) Kwamba Kristendomu hakuijua hii “lugha iliyo safi” ni wazi kutokana na mchanganyiko wenye kutatanisha wa “matamko” ya Maandiko na ya kifilosofia anayoyazungumza. Na kuliko kuliitia ‘jina la Yehova,’ wanadini wa kiorthodokis wa Kristendomu wanapendelea kulikataa jina hilo na kulikubali neno lisilofahamika sawasawa “Bwana.”​—2 Pet. 2:1; Mt. 7:15-23.

17. Ni kwa njia gani lugha hii ni “safi,” na inasemwa kwa kadiri gani?

17 Twaweza kuwa na furaha kama nini kujua kwamba Yehova anao mashahidi waaminifu duniani mwote waliojifunza hii “lugha iliyo safi”​—zaidi ya milioni moja na elfu sita katika zaidi ya nchi 200​—ambao wanapendezwa kuliitia jina lake na kumtumikia “kwa nia moja,” wajapokuwa wanatoka katika vikundi vingi mbalimbali vya kitaifa, kikabila na kilugha. Wana umoja kama walivyokuwa Wakristo wa kwanza katika ibada safi kwa sifa ya Yehova. Bila ya kujali matumizi yao ya tafsiri yo yote kati ya zilizo mbalimbali za Biblia katika lugha 1,500 ambazo katika hizo imetafsiriwa, hata ikiwa ni sehemu yake, wangali wanasema kwa mapatano juu ya mafundisho yake ya msingi. Kwa njia hiyo lugha yao ni “safi,” siyo kwa kuwa yenye kukubalika kwa watu wamchao Mungu tu, lakini vile vile kwa kuwa isiyoharibiwa ama kupotoshwa katika utoaji wake wa makusudi ya Yehova.​—Yohana 8:42-47; Yak. 3:10, 11.

18. Zekaria alitabirije nyongeza kwa kazi inayotajwa katika Matendo 15:14 kwa siku zetu?

18 Matokeo ya kuwaeleza wengine kweli kwa hiari yalisemwa mapema katika maneno ya Zekaria: “Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo yake yeye aliye Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.” (Zek. 8:23) Je! wewe vile vile umejiunga na wale ambao Yehova amekuwa akikusanya kutoka mataifa yote kama watu wa jina lake? Ni jambo la haraka kufanya hivyo sasa.​—Matendo 15:14.

19. Ni kwa njia gani tunavyofahamishwa “lugha iliyo safi”?

19 Kusema lugha yo yote, pamoja na “lugha iliyo safi” ya kweli, hakutokei bila ya jitihada. Mbele ya kuweza kuyasema yanayompendeza Muumba wetu lazima tujifunze hayo ni nini. Kama vile katika kujifunza lugha mpya, twayaona maneno yaliyokuwa mageni kwanza katika “lugha iliyo safi.” Twajifunza namna ufalme wa Mungu ulivyo kweli, juu ya “mkutano mkubwa” wanaomtumikia Yehova katika “siku za mwisho,” juu ya uharibifu unaokaribia wa “Babeli Mkuu” mbele tu ya sehemu nyingine yote ya hii “taratibu ya mambo” ya kilimwengu kutoweka penye “Har–​Magedoni.” Vile vile, twaonywa mapema juu ya shambulio linalokuja la “Gogu wa Magogu.” Hatuna haja ya kuvunjika moyo ikiwa kwanza inakuwa vigumu kujifunza kweli fulani za kiroho zilizo ngumu kufahamika. Ni kwa sababu ya kumiminwa tu kwa roho ya Yehova kwamba ufahamu ulio wazi wa kusudi la Yehova ulipata kuonyeshwa wazi kwa wafuasi wa kwanza wa Yesu katika Pentekoste, na leo ni kwa sababu ya roho ya Yehova juu ya jamii ya “mtumwa mwaminifu mwenye akili” kwamba tunao ufahamu wa makusudi ya Yehova, tuwezao kuushiriki na wengine.​—Mt. 24:45-47.

20. Ni mambo gani yanayotiwa ndani katika kuizungumza “lugha iliyo safi”?

20 Ufahamu huu ulioongezeka wa Neno la Yehova na ujamaa wetu kwake unatuvuta ‘tukimbilie kwenye jina la Yehova.’ Unatokeza mageuzi katika tumaini letu la wakati ujao, hivi kwamba tunaweka tumaini letu sasa katika ufalme wa Yehova wa haki kuliko kuliweka katika mambo ya ulimwengu huu. Unatuvuta kulishiriki tumaini hili la ajabu na wengine. Twajifunza kwamba wale wazungumzao “lugha iliyo safi” vile vile lazima waishi kulingana nayo. Wao “hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao.” (Sef. 3:12, 13) Lo! ni furaha ya namna gani kuweza kushiriki na watu zaidi ya milioni moja na mia sita elfu ambao tayari wamejifunza hii “lugha iliyo safi” katika kuwafundisha wengine hiyo! Ni ujuzi huu wa kweli tu kama unavyofunuliwa na Yehova kupitia kwa tengenezo lake leo unaoweza kuunganisha watu wa mataifa yote na lugha wafanye kazi bega kwa bega ‘kwa ajili ya imani ya Injili.’​—Flp. 1:27, 28.

UPINZANI KWA LUGHA ILIYO SAFI

21. Wanafunzi wa Yesu walitendaje juu ya jitihada za kuikomesha huduma yao?

21 Kwa kuwa Yesu alikutana na upinzani kutoka kwa wapinzani wa kweli, lile lile laweza kutazamiwa na wale wanaoufuata mwendo wake sasa. (Yohana 15:20) Tutatendaje hili likitukia? Kumbuka kwamba wajapokuwa Petro na Yohana walitiwa gerezani kwa ajili ya kuzitangaza habari njema za kuja kwa “nyakati za kuburudishwa” zinazokuja kutoka kwa Yehova, hawakuogofishwa hata kuacha, bali waliendelea siku ile ile iliyofuata kutoa ushuhuda wenye uhodari kwa watawala wa kidini wa watu. Hata nyuma ya kukatazwa kabisa wasiseme jambo lo lote zaidi, wao walitangaza: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Kwa kweli, waliomba kwamba Yehova awape nguvu za ‘kunena neno lake kwa ujasiri wote.’​—Matendo 3:11,19; 4:20, 29.

22, 23. Jitihada za kukomesha kuhubiriwa kwa habari njema zimeshindwaje katika Gabon na Cameroon?

22 Jitihada zimefanywa katika nyakati za kisasa vile vile kukomesha kuhubiriwa kwa habari njema. Habari kutoka Gabon katika Afrika ya Magharibi zasema: “Ingawa hali zingali zenye magumu mengi, akina ndugu hawakuvunjika moyo. Wao wanajifunza tu kuzizoea hali hizi mpya. Mwangalizi mmoja aeleza: ‘Uwezo wa Yehova waonekana wazi naye anatutia nguvu wakati wa mateso yetu. Woga tuliokuwa nao mwanzoni mwa marufuku umegeuka kuwa uhodari, nako kujihatirisha bure kuwa busara. Tumeacha hali ya udhaifu tukawa wenye nguvu nayo hali yetu isiyo na mazao imegeuka ikawa yenye matunda. Tumekwisha ona ongezeko la wahubiri kumi wapya katika miezi sita katika kundi letu, na kwa muda unaopungua mwaka mmoja tumebatiza watu kumi na wanne. Utiifu kwa Yehova umeileta baraka yake.’”

23 Katika Cameroon iliyo jirani, ndugu kumi na mmoja walizungukwa wakiwa nyumbani mwao na polisi nao wakapelekwa jela. Wakati walipokamatwa hata hawakuwa wakifanya mkutano wala kutoa ushuhuda kwa wengine! Kwa majuma matatu walifungiwa katika kijumba cha jela ambamo joto lilielekea kutovumilika. Lakini wao walijua hili lilikuwa shamba lisiloguswa la kuhubiri. Kwa hiyo mchana kutwa wakatoa ushuhuda; wafungwa walipoondoka na wengine wakaja mahali pao, wao walizidi tu kuwahubiri watu mbalimbali, sawa kabisa na walivyokuwa wakifanya walipokuwa huru kwenda nyumba kwa nyumba. Habari za mwisho zilisema kwamba ndugu mmoja alikuwa angali hajafunguliwa ati kwa sababu vitabu vya Biblia vilikuwa vimepatikana nyumbani mwake. Lakini wale kumi waliofunguliwa walitoka gerezani wakilifurahia pendeleo la kuweza kukabidhiwa habari njema juu ya ufalme wa Mungu na kwamba walikuwa wamekuwa na nafasi ya kuwaeleza wengine juu yake.​—1 The. 2:1-4.

24. “Lugha iliyo safi” imekuwa na matokeo gani juu ya watu wa Yehova, nao wanatazamia kitu gani?

24 Kama tu chini ya upinzani au sivyo, jambo lililo la maana kwa kila mmoja wetu ni kuitumia zawadi ya lugha kumpendeza Muumba wetu. Tukiwa tumejifunza makusudi ya Yehova ya ajabu, tunalo pendeleo la kuwaletea wengine ujumbe huu wa tumaini na uzima. Kama tuna elimu nyingi au sivyo, Yehova aweza kututia nguvu tuyashiriki makusudi yake na wale wanaoyapenda yaliyo haki. Zijapokuwa lugha zilizo nyingi zinazozungumzwa na watumishi wa Yehova duniani mwote, wote hata hivyo wanaunganishwa na “lugha iliyo safi” ya kweli ya Maandiko. Ikiwa tu wenye shukrani kweli kweli kwa ajili ya zawadi hii ya lugha, basi tutataka kuitumia kwa sifa ya Yehova. Tukifanya hivi sasa, ndipo twaweza kutazamia kuuona wakati ambapo ‘kila ulimi utakiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba’ mnamo utawala wa Ufalme wa Kristo. (Flp. 2:11) Yaelekea kuwa busara kumalizia kwamba wakati huo wanadamu wote waaminifu wataunganishwa siyo na vifungo vya ibada safi tu lakini vile vile na baraka zaidi ya lugha moja ya watu wote, yenye kufahamiwa na wote, na iliyowezeshwa na utawala wa kimbinguni wa Ufalme wa Muumba mkuu wa lugha, Yehova.

[Ramani katika ukurasa wa 104]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Bustani ya Edeni​—LUGHA YA KWANZA ILIKUWA KIEBRANIA

Mto Hidekeli

Mto Frati

Babeli​—LUGHA NYINGINE ZOTE ZILIANZIA BABELI

Nyanda za Shinari

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki