Watawala kwa Ajili ya Faida za Watu
Makala hii ni ya kutumia kwa mafunzo ya kitabu ya kundi
1-3. (a) Historia imeonyesha nini juu ya watawala na uangalizi wao wa faida za watu? (b) Twaweza kutazama wapi tupate jibu la ugumu huu?
JE! WEWE waona kwamba watawala wa dunia wameziangalia faida za watu wanaowatumikia? Bila shaka, wengine wamejaribu kufanya hivyo. Lakini wale wanaojaribu kwa kawaida wanaona kwamba upotovu katika serikali yao wenyewe unabatilisha jitihada zao, hata faida za watu zinatupiliwa mbali. Ndivyo ambavyo imekuwa tangu siku za Nimrodi, karibu miaka elfu nne iliyopita.
2 Je! maendeleo yaweza kufanywa? Je! wanaweza kupatikana watawala wanaoweza kutumikia faida za raia zao wote na watakaofanya hivyo hasa? Wewe ungetazama wapi?
3 Kuna mahali pamoja penye mamlaka pa kutazama. Hapo ndipo Biblia. Je! wewe unayaamini yale ambayo inayasema? Je! wamwamini Mungu? Je! waiamini ahadi yake ya kuleta serikali itakayotawala kwa ajili ya faida ya watu, na je! waamini kwamba yeye aweza kuchagua watawala watakaotumikia hasa faida za watu?
KUMJUA MTAWALA MKUU
4. Ikiwa twaamini Biblia inavyosema, tunavutwa kwenye mkataa gani usiopingika juu ya Mtawala Mkuu wa Ufalme wa Mungu?
4 Ikiwa umekwisha soma Biblia, unajua kwamba Mungu atatoa Mtawala mwenye haki, Masihi au Mfalme aliyetiwa mafuta, kama Mtawala Mkuu, pamoja na watawala washirika. Ikiwa wewe waamini hivi, basi, bila ya kujali u Myahudi au Mtaifa, huwezi ukauepuka mkataa wa kwamba Mtawala Mkuu amekwisha tokezwa naye aweza kujulikana waziwazi kama Yesu Kristo. Namna gani hivyo? Kwa maana haiwezekani kwa mtu mwingine ye yote kuyatimiza matakwa. Jambo hili lawezaje kusemwa kwa uhakika huo?
5. N’nini lililokuwa mojawapo la matakwa imara yaliyoandikwa katika Maandiko ya Kiebrania kwa Mfalme wa Mungu aliyetiwa mafuta wa dunia yote?
5 Basi, yaangalie mambo ya hakika. Katika Maandiko ya Kiebrania, Biblia iliweka sifa fulani zilizo imara kwake yeye ambaye angekuwa Masihi, Mfalme aliyetiwa mafuta ambaye angetawala dunia kwa haki kwa miaka elfu. Kati ya matakwa haya, alipaswa aketi juu ya “kiti cha enzi cha Daudi.” (Isa. 9:6, 7; Yer. 33:20, 21; Matendo 2:29, 30) Alipaswa kuwa mrithi wa asili wa Mfalme Daudi wa kabila la Yuda. Na alipaswa kuwa wa ukoo wa kifalme, akiirithi haki ya kifalme, iliyokuwa mikononi mwa wazao wa Daudi kupitia kwa mwanawe na mrithi Mfalme Sulemani.
6. Twawezaje kuhakikisha kwamba Yesu Kristo ndiye anayestahili peke yake?
6 Je! Yesu Kristo anayo hakika ya hili kutokana na maandishi ya ukoo? Ndiyo, anayo. Yeye alikuwa wa kabila la Yuda na ukoo wa Daudi kwa uzaliwa wa asili kupitia kwa mamaye, aliyezaliwa kupitia kwa mwana wa Daudi Nathani. (Luka 3:23-38) Naye alikuwa na haki ya kisheria aliyopokezwa kupitia kwa baba yake mlezi Yusufu, ambaye alitoka kwa Daudi kupitia kwa Mfalme Sulemani. (Mt. 1:1-17) Habari zote juu ya ukoo huu zilizoandikwa katika Biblia zinajulikana na watu wote. Ni maandishi ya Biblia peke yake ya ukoo huu yaliyobakia. Hakuna maandishi mengine yo yote yaliyobakia ya wazao wa Daudi, kwa maana yaliharibiwa wakati jeshi la Kirumi lilipouharibu Yerusalemu na kuliteketeza hekalu lake katika mwaka wa 70 C.E. Maandishi yote yaliyoandikwa yasomwe na watu wote, sehemu zote za kuwekea hati na tarehe, zilifutiliwa mbali. Hakuna awezaye kufuatisha ukoo wake nyuma mpaka kwa Daudi tangu wakati huo. Kwa kuwa kusudi la Mungu haliwezi likashindwa, hii maana yake ni kwamba Yesu Kristo ndiye Masihi pasipo shaka, Mfalme aliyechaguliwa na Mungu.
7. Toa ushuhuda wa kwamba ukoo wa Yesu kama ulivyoonyeshwa katika Biblia ni wa kweli.
7 Twajuaje kwamba maandishi ya ukoo wa Yesu ni ya kweli? Kwa maana maandishi hayo yanayoonekana katika Mathayo 1:1-17 na Luka 3:23-38 yalilingana na orodha rasmi za siku hizo zilizoandikwa zisomwe na watu wote (na yaelekea maandishi haya yalitolewa katika orodha hizo), zilizokuwa wazi kwa wote ili wazichunguze. Hii yaeleza sababu gani Wayahudi wenye elimu nyingi, waandishi na Mafarisayo na Masadukayo, waliompinga Yesu vikali, hawakusema hata neno moja la kuupinga ukoo huu. Vile vile inapendeza kwamba hakuna adui wa Ukristo wa Mataifa yasiyo ya Kiyahudi, ambao kati yao walikuwako watu werevu, aliyetoa lawama yo yote juu ya ukoo wa Yesu mpaka mwaka wa 70 C.E. ulipokwisha kupita. Bila shaka, wangeweza kufanya madai ya uongo wakati huo kwa maana hakuna mtu ambaye angeweza kujikagulia orodha za watu wote ayagundue madai yao ya uongo.
WATAWALA WASHIRIKA
8. Twaweza kuwa na uhakika wa nini kwa habari ya Kristo kama mtawala, lakini ni ulizo gani linalotokea juu ya serikali yake?
8 Kwa hiyo hakuna sababu ya kutia shaka kwamba Yesu Kristo siye Yeye aliyekusudiwa na Mungu aitawale dunia hii kama Mfalme kwa miaka elfu. Lazima tukubali hili iwapo twajidai kuiamini Biblia. Nao mwendo wake wa maisha wahakikisha yeye atakuwa Mtawala, si mwenye kutafuta faida zake mwenyewe, bali mwenye kuziangalia faida za watu kupatana na mapenzi ya Mungu. Lakini namna gani watawala wake washirika, tengenezo zima la kiserikali? Kwa maana Biblia inazungumza juu ya washirika wa kifalme wa Kristo ‘walionunuliwa katika wanadamu.’ Inaonyesha hesabu yao kuwa 144,000, ambao “watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.”—Ufu. 14:1, 4; 20:6.
9. Kwa sababu gani hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya utawala wa washirika wa Kristo 144,000?
9 Wafalme hawa hawatakuwa warithi wa Yesu Kristo, ama katika ukuhani ama katika ufalme. Yeye ndiye Mfalme. 144,000 ni wafalme washirika wakiwa chini ya uongozi wake. Kristo hawezi kufa; yeye anaishi milele. (1 Tim. 6:16; Ebr. 7:24) Bila shaka hakuna cha kuogopa kutokana na utawala wa Yesu Kristo, ambaye aliutoa uhai wake kwa ajili ya wanadamu. Na vivyo hivyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya utawala wa 144,000 ambao wakati fulani walikuwa wanaume wa kawaida na wanawake. Mungu mwenyewe alipanga zamani sana serikali hii iwepo kwa sababu ya upendo wake mwenyewe kwa wanadamu. Twajuaje?
10. Mtume Paulo aliandika nini kwa warithi wenzake wa Ufalme juu ya matendo ya Mungu pamoja nao kama wanaotazamia kuwa watawala?
10 Basi, mtume Paulo aliwaandikia warithi wenzake wa Ufalme hivi: “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale [aliowatambua kwanza], aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki.”—Rum. 8:28-30.
11. Ni kwa njia gani ambavyo Mungu ‘aliitambua kwanza’ jamii hii ya kiserikali ya taratibu mpya ya mambo juu ya wanadamu?
11 Wakati mwanadamu alipomwasi Mungu katika Bustani ya Edeni, Mungu alifikiria serikali ya taratibu mpya ya mambo juu ya wanadamu. Kwa hiyo yeye ‘aliitambua kwanza’ jamii hii ya kiserikali naye akaonyesha hivyo wakati alipotangaza hukumu juu ya “nyoka wa zamani,” Shetani Ibilisi, akisema hivi: “Nami nitaweka uadui katika yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”—Mwa. 3:15; Ufu. 12:9.
12. N’nani hasa aliye “uzao wa mwanamke,” lakini ni akina nani wanaotiwa ndani?
12 Yesu Kristo ndiye hasa anayetajwa katika unabii huu, lakini washirika wake 144,000 wanashirikishwa naye vile vile katika kukiponda kichwa cha Nyoka, kama vile mtume Paulo alivyoonyesha alipowaandikia Wakristo wenzake: “Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi.”—Rum. 16:20.
JE! WATAWALA WASHIRIKA NI WENYE KUTUMAINIKA?
13. Ni maneno gani yenye kufariji sana kwa wakaaji wa dunia tunayoyapata katika Warumi 8:28-30?
13 Kwa habari ya kuweza kuwatumaini watawala washirika wa Kristo, yaangalie maneno haya yenye kufariji: “Wale ambao aliwatambua kwanza vile vile alitangulia kuwaamuru wafuatishwe na mfano wa Mwanawe.” (Rum. 8:29, NW) Hii yahakikisha kwamba watakuwa wenye haki, watawala wenye kutumainika, hata kama vile Mwana alivyo. Wanapokuwa duniani wanageuza utu wao kwa msaada wa roho takatifu ya Mungu. (Efe. 4:22-24) Kama ndugu za Kristo, hawana migawanyiko kati yao wenyewe wanapokuwa duniani, na atakapowafufua waende mbinguni Yehova atawafanya wenye haki kama watu wakamilifu wa kiroho kupatana na utu wao wenye haki.—1 Kor. 1:10.
14. Kanuni yenye kutenda inayotajwa na Mfalme yaonyeshaje nia ambayo wafalme wote wa dunia wa wakati ujao watakuwa nayo?
14 Yesu aliifunua kanuni ambayo kwayo watawala wake washirika watatenda wakati aliposahihisha roho mbaya katika mitume wake, akisema hivi: “Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.”—Luka 22:24-27.
15, 16. Yesu alitumikiaje alipokuwa duniani, nayo hii ina maana gani kwa ndugu zake washirika wa kiroho?
15 Wanapokuwa duniani, washirika hawa wanakuwa wamepokea mazoezi yao ya utawala kwa kutumikia kama mabalozi wa ufalme wa Mungu kwa ajili ya watu. Wao wanamfuata Kiongozi wao, Kristo, aliyetumikia watu kama Balozi wa kutoka kwa Mungu moja kwa moja. Yeye alikuja duniani, siyo akiwa na utume wa kisiasa, bali afanye kile ambacho hakuna mtawala wa kisiasa anaweza kufanya au alichoweza kufanya, yaani, apatanishe watu wa mataifa yote na Mungu, awarudishe katika ukamatano wa amani na wa kirafiki na Mpaji wa Uzima aliye mkuu, Yehova.—Rum. 5:8-11.
16 Kwa kuwa wanafanya kazi kama ile aliyoifanya Kristo, watawala hawa washirika wanaweza kusema hivi: “Kwa hiyo sisi tu mabalozi badala ya Kristo, kana kwamba Mungu alikuwa akisihi kupitia kwa sisi. Kama badala ya Kristo tunaomba: ‘Mpatanishwe na Mungu.’”—2 Kor. 5:20, NW.
KAZI ISIYO YA KISIASA LEO
17. Nia na kazi ya ndugu za Kristo waliotiwa mafuta ni nini wanapokuwa duniani?
17 Kama mabalozi wa namna hiyo wao hawayaendei mataifa ya kisiasa, wakijaribu kuleta mapatano ya taifa zima mara hiyo, wala wao hawajiingizi katika mambo ya kisiasa. Bali, wanawaendea watu moja kwa moja—watu mmoja mmoja. Lakini hawajaribu kupinganisha watu na mtawala ye yote wa kidunia, au kujaribu kuwavuta kwenye maoni yo yote ya kisiasa. Wao wanakiri: “Wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo.” (Flp. 3:20) Wanawaomba watu wautazamie ufalme wa Mungu kwa faraja. Kwa hiyo, kama wakijitia katika mambo ya ulimwengu huu, wakishiriki katika matendo ya kisiasa, wakishika vyeo au kufanya uchaguzi, watapoteza cheo chao kama mabalozi na ndugu za Kristo, nao hawatapata kamwe utawala wa kimbinguni pamoja naye.
18, 19. Mabalozi wa Ufalme wanasimama wapi kwa habari ya serikali za ulimwengu huu, na kwa sababu gani?
18 Leo twaona utukuzo wa taifa ukiongezeka katika nchi zote. Mkazo zaidi na zaidi unawekwa juu ya watu wamtolee “mnyama” ibada, tengenezo la kisiasa la kibinadamu la ulimwengu huu likiongozwa na Shetani Ibilisi. (Ufu. 13:1, 2, 11, 12) Lakini mabalozi wa Ufalme na wanaotazamia kuwa watawala na Kristo hawamwabudu “mnyama,” wakijua kwamba karibuni ataharibiwa, atatupiliwa mbali, ili kwamba Ufalme uweze kuwa na enzi kamili juu ya dunia kwa miaka elfu. (Ufu. 19:19-21; Dan. 2:44) Hata hivyo, wao wanaziheshimu serikali za dunia maadamu Mungu anaziruhusu serikali hizi ziendelee kuwapo. Hii ni kwa sababu wanaviheshimu vyeo vyenye madaraka ambavyo watawala wanashika na uwezo na nafasi waliyo nayo ya kutendea raia zao mema.
19 Kwa hiyo “mabalozi” hawa wanaifuata amri ya Mungu katika Warumi 13:1-7 ‘kuitii mamlaka iliyo kuu’ ya ulimwengu huu, wakilipa kodi zao na kuzitii sheria za mataifa. Wakati tu watawala wanapofikia hatua ya kutunga au kufikiliza sheria zinazopingana na sheria na kanuni za Mungu Aliye Juu Zaidi ndipo Wakristo hawa wanapokataa kutii. Wanafanya hivi kwa kufuata kanuni na mfano uliowekwa na mitume wa Bwana Yesu Kristo walipokuwa mbele ya Baraza Kuu Yerusalemu. Walipoagizwa waache kuzihubiri habari njema za Ufalme, kwa njia hiyo wakiuacha ubalozi wao waliopewa na Mungu, walijibu hivi: “Inatupasa kumtii Mungu kama mtawala kuliko wanadamu.”—Matendo 5:29, NW.
20. Twajuaje kwamba wale 144,000 hawatapeleka uchafu wo wote wa kisiasa wa ulimwengu huu katika Ufalme wa kimbinguni?
20 Kwa hiyo wale 144,000 walio waaminifu hawatapeleka uchafu wo wote wa kisiasa wa ulimwengu huu wenye kiburi katika ufalme wa kimbinguni wa Kristo. Wao wamepitia katika majaribu makali duniani na kusimama imara kwa ajili ya enzi yote ya Mungu na kwa ajili ya ufalme wake, wakizihubiri baraka zake zijazo kwa watu. Juu yao, yasemekana hivi: “Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira.” (Ufu. 14:4) Ndiyo, ni waaminifu kwa Kristo, siyo wazinzi, kama vile wengine walivyoonywa na mwanafunzi Yakobo: “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”—Yak. 4:4.
21. Maneno yaliyomo katika Ufunuo 14:5 yanawatofautishaje mabalozi wa Ufalme na wanasiasa?
21 Vile vile juu ya watawala hawa washirika, inasemwa hivi: “Katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.” (Ufu. 14:5) Leo uongo unaonwa kama njia ya kushughulika ya watawala wa kisiasa. Hii imetokeza upotovu mwingi na kuharibu sifa yao kati ya watu. Lakini watawala washirika wa Kristo hawawezi kufuata mfano huu wakakubaliwa na Kristo. Wanahakikishwa kuwa wasema kweli. Maneno haya yote juu yao, yaliyoongozwa na roho ya Mungu mwenyewe, yanahakikisha kabisa wao hawapendezwi na utukuzo wao wenyewe (kwa kweli, kama watawala wa kimbinguni wasingeweza kutamani kitu cho chote cha kimwili kutoka kwa raia zao), bali wanapendezwa na faida za watu na hali njema ya milele.
22. Je! inawapasa wale wanaowasikia mabalozi wa Ufalme waitikie ujumbe akilini mwao tu, au namna gani?
22 Watu mmoja mmoja wanaotaka uzima kama raia za ufalme huo wenye haki, wasikiapo yale yanayosemwa na “mabalozi” hawa wa Mungu, lazima wafanye mengi zaidi kuliko kuitikia akilini mwao tu, wakingoja tu Ufalme uiponde-ponde hii taratibu ya mambo ya ulimwengu. Tendo linalovutwa na moyo lahitajiwa. Wote wanaoamini kwamba Mungu atawapa wanadamu watawala kwa ajili ya faida za watu lazima waiunge mkono kazi ya “mabalozi” hawa kwa kushiriki na wengine habari njema za Ufalme. Ni utendaji wa kuokoa uhai usioweza kuepukwa na mtu ye yote anayemwamini Mungu kwa unyofu wa moyo.
—Kutoka Kitabu God’s Kingdom of a Thousand Years Has Approached.
[Picha katika ukurasa wa 381]
SERIKALI YA KIMBINGUNI
YESU KRISTO Mfalme juu ya dunia yote kwa miaka elfu. Aliuhakikisha upendo wake kwa wanadamu kwa kutoa uhai wake kwa ajili yao.
WATAWALA WASHIRIKA 144,000 Ukamilifu wao kwa Mungu unajaribiwa kabisa duniani. Mungu anawafuatisha na mfano wa Mwana wake mwenyewe mbinguni.
RAIA ZA KIDUNIA