Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w74 9/1 kur. 403-406
  • Je! Tunahitaji Ukuhani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Tunahitaji Ukuhani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UKUHANI WA ISRAELI
  • UKUHANI ULIO BORA
  • “KWA MFANO WA MELKIZEDEKI”
  • UKUHANI WA KRISTO UNAVYOMAANISHA KWETU
  • Kuhani Mkuu
    Ufahamu wa Kina wa Maandiko
  • Makuhani Wawezao Kutusaidia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Ukuhani wa Kifalme Utawanufaisha Wanadamu Wote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Je! kwa Kweli Twahitaji Makuhani?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
w74 9/1 kur. 403-406

Je! Tunahitaji Ukuhani?

Makala hii ni ya kutumia kwa mafunzo ya kitabu ya kundi

1-3. (a) Je! watu wanahitaji msaada leo? (b) Je! mapadre wa dini za ulimwengu wametoa msaada unaohitajiwa?

PASIPO shaka watu wanahitaji msaada. Ugonjwa unaua wengi. Uvunjaji wa sheria unaleta hatari inayoongezeka wakati wote. Ufisadi unaleta magonjwa ya kuchukiza sana na vile vile namna zote za msiba na jeuri. Watu wengi wamekata tamaa, hawana tumaini, hawajui la kufanya.​—Luka 21:25, 26.

2 Yako maelfu ya mapadre leo, wanaowakilisha matengenezo mbalimbali ya kidini. Wako mapadre wa matawi mbalimbali ya Kanisa la Katoliki, mapadre wenye kuamriwa na Maaskofu, Mabanyani pia, Washinto na mapadre wengine wasio wa Kikristo. Je! wameipunguza taabu na wakakomesha kuongezeka kwa uvunjaji wa sheria, ufisadi, ugonjwa na kifo?

3 Wengi wa mapadre hawa, hasa kati ya dini za Kristendomu, wanasema Hapana, nao wanauacha upadre wafuate jambo wanalodhani lina matokeo zaidi na ni lenye kuridhisha zaidi. Kila mmoja wetu aweza kuiangalia hali ya ulimwengu mwenyewe na kujiamulia juu ya kama mapadre wa ulimwengu wamewafaidi watu kweli.

4. Padre aweza kuwafanyia nini watu anaowatumikia?

4 Imempasa padre afanye nini? Je! aweza kutazamiwa aziondoshe hizi hali zote mbaya kati ya wanadamu? Hakuna padre wa kidunia anayeweza kufanya hivyo, lakini anaweza kusaidia watu anaowatumikia wakae katika msimamo mzuri na Mungu, iwapo yeye ni namna inayofaa ya padre. Anaweza kuwasaidia wabadili maisha zao na utu wawe wenye amani, wenye kuheshimika, wawe watu wenye kuishi maisha mema. Anaweza kuwasaidia waondoshe sababu za taabu ambazo wanadamu kwa ujumla wanazipata katika maisha zao. Anaweza kuwapa tumaini na kuwaelekeza kwenye njia ya maisha yenye kusudi.

5. Twaweza kupata wapi mfano wa vile ambavyo ukuhani waweza kufanyia taifa?

5 Kwa kweli hatuwezi tukaona namna ambavyo imempasa kuhani wa Mungu awe kwa kuwatazama mapadre wa dini za ulimwengu. Lakini tukiutazama ukuhani ambao Mungu mwenyewe aliweka kwa ajili ya Israeli nyakati za kale, twaona kwamba makuhani waliwafaidi watu sana. Walinenea watu mbele za Mungu. Waliwafundisha watu njia njema ya kuishilia. Waliilinda afya ya watu sana. Walifanya hivi kwa kuhakikisha watu ni wenye adili na safi kwa kimwili pia.​—Law. sura za 11-15.

6, 7. Kwa sababu gani mambo yaliyozungumzwa sasa hivi siyo kazi ya serikali kwa ujumla, na kwa hiyo kwa sababu gani ukuhani wahitajiwa?

6 Huenda mtu akasema, ‘Lakini hii si kazi ya serikali?’ Kwa upande mmoja ndiyo, lakini yako mambo ambayo serikali haiwezi ikayafanya peke yake. Hiyo ni sababu moja kwa nini namna ya serikali isiyomcha Mungu ya Kikomunisti haiwezi ikaleta amani na furaha kwa raia zake wakati wo wote. Israeli wa kale walikuwa na serikali nzuri, serikali iliyosimamishwa na Mungu, nazo sheria za Mungu zilifikilizwa wakati wafalme wema walipotawala. Hata hivyo, Mungu aliwawekea ukuhani pia. Kwa sababu gani?

7 Kama kusingetendwa dhambi juu ya Mungu aliye hai, kusingekuwa na haja ya kuhani. Mwanadamu mkamilifu Adamu hakuhitaji kuhani katika Edeni, kwa maana yeye aliumbwa pasipo dhambi na Yehova Mungu. (Mwa. 2:7, 8; Mhu. 7:29) Lakini sote leo tumerithi hali ya dhambi kwa sababu Adamu alitenda dhambi kwa makusudi, nasi tu wazao wake. ‘Tumepungukiwa na utukufu wa Mungu,’ ambao imewapasa wanadamu wauonyeshe. (Rum. 3:23) Dhambi ni kuasi sheria ya Mungu pia. (1 Yohana 3:4) Kwa hiyo kuhani anahitajiwa, kusudi kwamba aweze kutoa dhabihu itakayolipia au itakayoifunika dhambi hiyo na kumsaidia mwenye kosa pia arudishwe kwenye mwendo ufaao, na kwenye kibali na Mungu.​—Ebr. 5:1.

UKUHANI WA ISRAELI

8. Nyingine za kazi alizozifanya kuhani mkuu wa Israeli zilikuwa nini?

8 Katika Israeli kuhani mkuu ndiye hasa aliyeongoza ukuhani. Yeye ndiye aliyefanya upatanisho kwa ajili ya taifa zima kila mwaka, katika siku ya upatanisho. (Law. sura ya 16) Yeye ndiye aliyemwomba Mungu kwa ajili ya taifa, na maulizo yaliyolipasa taifa aliulizwa Mungu na kuhani mkuu. Jibu lilitolewa na Mungu kwa kura takatifu, Urimu na Thumimu (maana yake “mianga” na “makamilifu”). Pia yeye alikuwa ndiye mwalimu mkuu wa sheria ya Mungu.​—Kut. 28:30; Hes. 27:21; Neh. 7:65.

9. Twaonaje kwamba hata kuhani mkuu wa Israeli alihitaji msaada mwenyewe?

9 Ijapokuwa kuhani mkuu wa Israeli wa kale aliwasaidia watu sana, yeye mwenyewe hakuwa mkamilifu au asiyetenda dhambi. Juu yake, Biblia katika Waebrania 5:1-3 inasema hivi: “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi.”

UKUHANI ULIO BORA

10. Ni ukuhani gani ulio bora ambao Mungu amepanga uwepo?

10 Kwa hiyo, makuhani wakuu waliotumikia Israeli miaka yote hiyo walihitaji msaada wenyewe. Lakini Mungu amepanga kuwepo ukuhani utakaofanya mambo kwa njia ya kiroho na ya kimwili pia ambayo ukuhani wo wote haujapata kuyafanya. Biblia inasema kwamba makuhani hawa watakuwa na kipindi kisichokatizwa cha miaka elfu moja wawarudishe wanadamu kwenye ukamilifu. Twasoma hivi juu ya kundi hili la kikuhani: “Watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.” (Ufu. 20:6) Mungu atalitoa kundi hili la kikuhani kutoka kwa akina nani, nao ukuhani huo utaleta faida gani?

11, 12. Ni nani Kuhani Mkuu wa Mungu, naye ni mkuu zaidi kwa njia gani?

11 Kama ilivyokuwa katika Israeli wa kale, yeye tunayetaka kujua juu yake hasa ndiye Kuhani Mkuu, ambaye wengine wanatumikia pamoja naye kama makuhani wadogo, wakitimiza amri zake na kuzisimamia faida bora za dhabihu yake. Je! yeye alichaguliwaje, naye alipaswa kutimiza sifa gani ili aweze kukistahili cheo hiki kikubwa, na kujihakikisha kuwa mwenye kutumainika na wanadamu?

12 Huyu Kuhani Mkuu si mwingine ila Yesu Kristo. Yeye anaitwa “Adamu wa mwisho” kwa maana anaweza akatokeza “watoto” kutoka kwa taifa la kibinadamu lenye dhambi kwa kuwasafisha na kuwazaa mara ya pili, akiwapa uzima kwa sababu ya dhabihu yake. Yeye alizaliwa katika taifa la watenda dhambi, lakini yeye mwenyewe hakuwa na dhambi naye hakuhitaji kuhani ye yote wa kumsaidia, tofauti na makuhani wengine. Hii ni kwa sababu alizaliwa kwa njia safi kabisa na Mariamu nao uhai wake ulitoka kwa Mungu moja kwa moja. Aliendelea kuwa asiye na dhambi mpaka wakati wa kifo chake cha dhabihu.​—1 Kor. 15:45-47; Ebr. 7:26; 1 Pet. 2:21-24.

13. Mwana mzaliwa wa pekee wa Mungu alipewaje dhabihu iliyofaa?

13 Yesu Kristo alikuwa kama Mwana mzaliwa wa pekee wa Yehova kabla hajawa mwanadamu, kwa kuwa yeye alikuwa ameshiriki katika kuumbwa kwa vitu vingine vyote. (Yohana 1:3; Kol. 1:15, 16) Baba yake Yehova Mungu alihamisha uhai wake na kuuweka katika tumbo la uzazi la Mariamu, na kwa njia hiyo akafanya azaliwe kama mwanadamu. Hivyo Mungu ‘alimwekea mwili tayari.’ Hii ilimpa kitu cha kutoa dhabihu​—uhai mkamilifu wa kibinadamu, kama ule ule ambao Adamu alikuwa nao, lakini alioupoteza kwa kutenda dhambi. (Ebr. 10:5; 8:3) Kwa hiyo, kitu hiki chenye thamani kingeweza kuwanunua wazao wa Adamu wakati alipoutoa uhai wake kama dhabihu. Wakati yeye alipotoa dhabihu ya dhambi kama Kuhani Mkuu, dhabihu yenyewe haikuwa mnyama, bali ilikuwa uhai wake mwenyewe wa kibinadamu. Ndiyo sababu toleo lake lilipaswa litolewe mara moja tu.​—Ebr. 7:26, 27.

“KWA MFANO WA MELKIZEDEKI”

14. Yesu aliupokeaje ukuhani wake?

14 Lakini Yesu hakuwa wa kabila la Lawi, kabila la kikuhani, wala hakuwa wa jamaa ya Haruni, ambaye kupitia kwa ukoo wake ukuhani ulitenda kazi. Basi, angewezaje kuwa kuhani? Je! alijiweka mwenyewe? Sivyo, asingeweza kufanya hivyo. Hii yaelezwa katika Waebrania 5:4-6: “Hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni. Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa. Kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.”

15. Yesu akawaje “kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki”?

15 Kwa kumfufua Yesu Kristo kwa wafu, Mungu Mwenye Nguvu Zote aliyatimiza maneno hayo yaliyotajwa kutoka Zaburi 2:7 kama yalivyoandikwa na Daudi. Hivyo Mungu akawa Baba wa milele kwa Yesu Kristo aliyefufuliwa naye akawa Mwana wa milele wa Mpaji wake wa Uzima, Yehova Mungu kwa kufufuliwa kama asiyeweza kuharibika. Akiwa Mwana asiyeweza kuharibika sasa, angeweza kufanywa “kuhani milele” asihitaji mrithi, na hivyo angeweza kuwa kuhani “kwa mfano wa Melkizedeki!”​—Matendo 13:33-37; Zab. 110:4.

16. Mbali na kutoa dhabihu kamilifu, Yesu angeweza kufanya nini kingine ambacho kuhani mwingine ye yote hakupata kukifanya?

16 Kwa kuwa alikuwa amefufuliwa na akathawabishwa na uhai usioharibika mbinguni, sasa Kristo angeweza kufanya kitu ambacho kuhani mwingine ye yote hakupata kukifanya, yaani, kuonekana mbele za Mungu hasa. Ilimpasa kufanya hivi ili amlipe Mungu bei ya ununuzi wa taifa la kibinadamu​—yaani, ubora wa uhai wake wa kibinadamu, aliokuwa ameutoa kwa nia ukiwa mkamilifu.​—Ebr. 9:24; 4:14; 1Kor. 7:23.

17, 18. Melkizedeki aliishi wakati gani, nazo habari za Biblia zinasema nini juu yake?

17 Habari zilizomo katika Biblia juu ya Melkizedeki ni fupi tu. Yeye hakuwa Mwebrania, Mwisraeli wala Mlawi. Mtumishi wa Mungu, “Abramu Mwebrania,” alikutana naye alipokuwa akitoka vitani ambamo Abramu alikuwa amemwokoa mpwa wake Lutu kutoka kwa watekaji. Tukio hili lilitukia kati ya miaka ya 1943 na 1933 B.C.E., muda mwingi kabla taifa la Israeli pamoja na ukuhani wake halijafanyiswa. Habari zinasema hivi:

18 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.”​—Mwa. 14:17-20.

19. Kwa sababu gani Biblia haitaji ukoo na kifo cha Melkizedeki?

19 Biblia haionyeshi ukoo wa Melkizedeki wala kifo chake. Bila shaka kusudi lake lilikuwa ni kutangulia kuonyesha kwamba Yesu Kristo, Mfalme mkuu wa Mungu na Kuhani Mkuu, alipokea ukuhani wake, si kama walivyopokea makuhani wa Kiharuni kupitia kwa ukoa wa kimwili, bali kwa kuwekwa moja kwa moja na Yehova. Zaidi ya hayo, Kristo anaishi milele naye hana warithi. Kwa hiyo, Kristo ni Kuhani Mkuu, siyo kwa urithi kutoka kwa Melkizedeki, bali ukuhani wake ni wa “mfano” tu kama ule wa huyo kuhani-mfalme wa Salemu.​—Ebr. 7:1-3, 15-17.

UKUHANI WA KRISTO UNAVYOMAANISHA KWETU

20. Katika Waebrania 7:11-14, Biblia yaonyeshaje kwamba twahitaji kuhani mkuu kama Yesu Kristo?

20 Kwa hiyo, Kuhani Mkuu wetu Yesu Kristo ni mkamilifu. Sote twahitaji Kuhani Mkuu mkamilifu kwa kuwa sote tu wanadamu wasiokamilika na wenye dhambi. Hili ndilo linaloelezwa katika Waebrania 7:11-14: “Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine ainuke, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni? Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hiyo aliyeihudumia madhabahu. Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda.”

21. Kwa hiyo, Yesu aweza kuwafanyia nini makuhani wake wadogo?

21 Huyu Kuhani Mkuu mkamilifu anaweza akawakamilisha makuhani wake wadogo. Mwandikaji wa kitabu cha Waebrania anaendelea kusema hivi: “Kwa maana ile sheria haikukamilisha neno; na pamoja na hayo kuliingizwa matumaini yaliyo mazuri zaidi, ambayo kwa hayo twamkaribia Mungu.” Kisha Yesu anatajwa kama akiwa “mdhamini wa agano lililo bora zaidi.” Hili ndilo agano jipya, ambalo kwalo kundi la makuhani laweza kupata ukamilifu kwa kuwa pamoja naye.​—Ebr. 7:19-22.

22, 23. Hii ina maana gani kwa watu walio hai sasa, na akina nani walioishi duniani wakati uliopita?

22 Hii maana yake nini kwa umati mkubwa wa watu walioko duniani, na kwa wale waliokufa? Ina maana ya nafasi ya kupata ukamilifu wa kibinadamu. Yesu anauhesabu kila uhai kama wenye thamani nyingi kwa maana taifa la kibinadamu ni lake na hata aliutoa uhai wake wa kibinadamu alinunue. Kwa hiyo, yeye atashughulika na uhai huu kwa upendo na kwa uangalifu, akiharibu watu mmoja mmoja wanaokataa kuukubali utumishi wake wa kikuhani na kuzitii kanuni za Mungu kwa kumpenda Mungu na wanadamu wenzao, na kupenda yaliyo haki. Hatuna haja ya kuhofu kwamba yeye hataweza kuhakikisha tumekamilika mnamo utawala wake wa miaka elfu, kwa maana “aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.”​—Ebr. 7:25.

23 Je! wewe watamani uzima katika dunia ukitazamia afya kamili na uzima wa milele? Basi imekupasa ujifunze mengi zaidi juu ya ukuhani huu na namna ambavyo twaweza tukamkaribia Mungu kupitia kwa Kuhani Mkuu wake. Hili litazungumzwa katika matoleo yafuatayo ya Mnara wa Mlinzi.

​—Kutoka Kitabu God’s Kingdom of a Thousand Years Has Approached.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki