“Jifungeni Unyenyekevu”
“Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”—1 Pet. 5:5.
1. Ni sifa gani ambazo Wakristo wanatiwa moyo wazisitawishe? Kwa sababu gani?
JE! WEWE unawajua watu wenye majivuno, wenye kiburi, wenye kujiona, wenye majisifu, wenye vichwa vikubwa? Wengi wetu wanawajua. Lakini lo! namna tunavyopendelea zaidi kushirikiana na watu wasiotaka makuu, wanyenyekevu wa akili, wasiojitanguliza, wapole, wasiojivuna! Kwa kweli, sifa za kutotaka makuu na unyenyekevu wa akili ni sifa ambazo Wakristo wote wanatiwa moyo wazisitawishe. Wakati mmoja Yesu alijua kwamba wanafunzi wake walikuwa wamekuwa wakibishana kati yao wenyewe juu ya aliyekuwa mkubwa zaidi, naye akawaambia hivi: “Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.” Kisha aliendelea kuonyesha kwamba mtu hakuruhusiwa awe mwenye kujikuza, akionyesha kwamba kama wangewakubali watu waliokuwa kama watoto wadogo kwa sababu ya jina lake ingekuwa sawa na kumkubali yeye na Baba yake Yehova pia. Kwa hiyo bila shaka aliwatia moyo wanafunzi wake wawe wanyenyekevu wa akili. (Marko 9:33-37) Miaka mingi baadaye Petro aliandika hivi: “Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu,” naye akaendelea kueleza sababu gani, akisema, “kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.” (1 Pet. 5:5) Basi, si sisi tu tunaoona unyenyekevu wa akili kuwa sifa ya kutamanika, bali Mungu pia anauona hivyo, naye authawabisha kwa neema.
2. Kwa sababu gani imetupasa tufikirie Wafalme wa Pili, sura ya tano?
2 Twataka tupate kibali ya Mungu, kwa hiyo yafaa tulifikirie kwa uzito shauri hili la unyenyekevu. Kwa kuwa Biblia yasema kwamba yaliyoandikwa humo “yaliandikwa ili kutufundisha sisi,” je! twaweza kupata habari fulani katika Maandiko zitakazotufundisha kuwa wanyenyekevu? (Rum. 15:4) Habari za namna hii zinazostahili kufikiriwa zapatikana katika Wafalme wa Pili, sura ya tano. Hapo twajifunza juu ya mtu mmoja nyakati za kale aliyesitawisha unyenyekevu, na kwa kuzisoma habari na kuzichanganua twaweza kufaidika wenyewe huku kila mmoja wetu akijaribu kujifunga unyenyekevu wa akili.
NAAMANI AJIFUNZA UNYENYEKEVU
3. Twajifunza nini juu ya mwanamume Naamani?
3 Katika karne ya kumi B.C.E., Shamu, iliyokuwa kaskazini ya Israeli, ilikuwa na jemadari wa jeshi aliyeitwa Naamani, aliyeongoza Washamu kwenye ushindi. Bila ya Naamani kujua wakati huo, Yehova ndiye aliyekuwa amemtumia kuipa Shamu wokovu. Naamani “alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, . . . tena alikuwa mtu hodari wa vita.” (2 Fal. 5:1) Bila shaka kwa sababu ya cheo chake na matendo yake hodari ya kijeshi, Naamani alikuwa mwenye majivuno, lakini alikuwa amepatwa na ukoma. Ugonjwa huu wa kuchukiza sana haukumzuia asiwe na cheo cha jemadari wa jeshi katika Shamu kama ambavyo ingalikuwa katika Israeli, bali, baadaye, ulimsaidia ajinyenyekeze na kumfaidi kwa njia ya ajabu sana.—Law. 13:46.
4. Mfalme wa Shamu alipataje kujifunza juu ya Elisha?
4 Vikundi vya wanyang’anyi vya Washamu vilikuwa vimemteka msichana mdogo Mwisraeli katika nchi ya Israeli, naye msichana huyu akawa kijakazi wa mke wa Naamani. Msichana huyu (asiyepewa jina katika Biblia) alikuwa na habari za nabii wa Yehova aliyeitwa Elisha na miujiza aliyokuwa ameifanya. Alimwamini Mungu wa Elisha, Yehova, na kuishuhudia imani yake. Wakati mmoja alipokuwa akisema na mke wa Naamani, bibiye, msichana huyu alisema hivi: “Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! maana angemponya ukoma wake.” Ushuhuda wa msichana huyu Mwisraeli halafu ukamfikia mfalme wa Shamu.—2 Fal. 5:2-4.
5. Naamani alionanaje na Elisha?
5 Mfalme wa Shamu, yaelekea Ben-hadadi wa Pili, akamwandikia Yehoramu mfalme wa Israeli barua, akamtuma jemadari wake wa jeshi Naamani aipeleke karibu maili mia moja. Akapeleka zawadi za thamani zifuatane na Naamani. Yehoramu aliipokea barua na kusoma hivi: “Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.” Yehoramu alifadhaishwa na barua hiyo akahofu kwamba mfalme wa Shamu alikuwa “anataka kugombana” naye. Elisha, nabii wa Mungu wa kweli, akazipata habari hizi na kupeleka ujumbe kwa Mfalme Yehoramu, akisema: “[Naamani] na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.” Kumbe! mwishowe Naamani angeangaliwa na mtu ambaye yule msichana mdogo Mwisraeli alisema angeweza kumponya!—2 Fal. 5:5-8.
6. (a) Ni nini lililotukia Naamani alipofika nyumbani kwa Elisha? (b) Elisha hakuwa akijaribu kufanya nini, naye alipendezwa na nini?
6 “Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha.” Elisha angetendaje mkuu huyo akiwapo? Je! angehangaika sana kwa sababu ya jemadari huyu wa jeshi mwenye sifa? Habari zinaendelea kusema hivi: “Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi.” Sivyo, Elisha hakuwa akijaribu kujipendekeza apate kibali ya watu wenye vyeo vikubwa. Alipendezwa na kupata kibali ya sikuzote ya Yehova na kuhakikisha kwamba mapenzi Yake yametimia.—2 Fal. 5:9, 10.
7. Naamani aliyaitikiaje maagizo ya Elisha?
7 Je! Naamani alipendezwa kujua namna ilivyokuwa vyepesi kwake kuponywa na hali yake ya ukoma? Sivyo; bali, habari zinaendelea kusema hivi: “Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la [Yehova], Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.”—2 Fal. 5:11, 12.
8. Majivuno ya Naamani yalikuwa yakimfanya akose kuona nini ambalo watumishi wake walimsaidia alione?
8 Ilionekana kana kwamba majivuno ya Naamani yangemzuia asiponywe. Yeye hakupendezwa na namna alivyopokewa bila sherehe na kwa dawa hiyo ya vivi hivi tu. Ilionekana kana kwamba yeye alipendezwa zaidi na sherehe na heshima iliyohusianishwa na kuponywa kuliko kupendezwa na kuponywa kwenyewe. Majivuno yalikuwa karibu kukatiza utiifu kwa maagizo ya unabii wa Mungu. Lakini watumishi wa Naamani walimsaidia kuyaona mambo ifaavyo. Walisema hivi: “Kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? je! si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?” (2 Fal. 5:13) Wao walikuwa na maoni yaliyofaa. Walifahamu kwamba jambo kubwa lilikuwa Naamani aponywe ugonjwa ule, nayo mazungumzo yao na bwana wao yalipata matokeo.
9. Ni nini lililotukia Naamani alipoyatii maagizo ya Elisha?
9 “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu.” Ndiyo, alianza kuonyesha unyenyekevu wa akili; alijifunga unyenyekevu akaufuata utaratibu uliopendekezwa. Alikwenda Yordani akajichovya majini, mara moja, ya pili, na kuendelea hivyo mpaka mara sita, lakini asiponywe. Ndipo alipojichovya mara ya saba, na matokeo? “Nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.” Lo! aliponywa!—2 Fal. 5:14.
10. (a) Naamani alitendaje alipoponywa? (b) Kwa sababu gani Elisha alilikataa toleo la Naamani la zawadi?
10 Lakini hii ilimnyenyekeza Naamani kwa kadiri gani? Je! sasa angerudi nyumbani, akijivunia hali yake ya kuponywa lakini asishukuru kwa lililokuwa limetendwa? Habari zinaendelea kuonyesha kwamba alimrudia mtu wa Mungu wa kweli, umbali wa karibu maili 25 au zaidi, pamoja na farasi wake na magari ya vita. Wakati huu Elisha alitokea mbele yake, naye Naamani akasema: “Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli.” Lo! ungamo la imani namna gani! Kwa shukrani alimtolea Elisha zawadi ya baraka. Lakini, Elisha hakupendezwa na kujifaidi kutokana na kumtumikia Yehova, na kwa hiyo akasema: “[Yehova] aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu.” Ijapokuwa Naamani aliendelea kusihi, Elisha ‘alikataa’ asipate zawadi yo yote, kwa maana alijua kwamba Yehova ndiye aliyekuwa Mponyaji naye hakutaka ajipatie faida kutokana na cheo ambacho Yehova alikuwa amempa.—2 Fal. 5:15, 16.
11, 12. Sasa Naamani alionyesha kupendezwa na nini? Kwa njia gani?
11 Mwishowe Naamani akasema: “Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa [Yehova].” Kwa unyenyekevu Naamani aliionyesha tamaa yake ya kumwabudu Mungu wa Elisha, lakini alitaka afanye hivyo akiwa katika nchi ya Israeli ijapokuwa ilikuwa lazima arudi akamtumikie mfalme wa Shamu.—2 Fal. 5:17.
12 Naamani sasa alikuwa amekuwa mnyenyekevu wa akili namna gani, asipendezwe na kujionyesha au kutukuzwa mwenyewe, bali akipendezwa na kumfurahisha Yehova, yeye ambaye sasa alimtambua kama Mungu wa kweli! Aliendelea kusema hivi kwa Elisha: “Jambo hili [Yehova] amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni [mungu wa uongo ambaye mfalme wa Shamu aliabudu] ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, [Yehova] amwachilie mtumwa wako jambo hili.” Naamani asingekuwa akimwabudu tena Rimoni huyu wa sanamu, lakini kuinama kwake kungekuwa kwa kumrahisishia mfalme kuinama tu. Elisha aliamini kwamba Naamani alikuwa mnyofu, na kwa hiyo akamwambia, “Enenda kwa amani.”—2 Fal. 5:18, 19.
13. ‘Kujifunga unyenyekevu’ kwa Naamani kulimletea matokeo gani?
13 Je! haipendezi kuona namna ambavyo Naamani alijifunza kwa muda mfupi ‘kujifunga unyenyekevu’ na kwa sababu hiyo akawa mwabudu wa Yehova na kupata kibali Yake na baraka? Lakini wakati uu huu, mtu mwingine alikuwa anajifikiria mwenyewe, anajikuza. Alikuwa nani huyu?
GEHAZI AVUTWA NA PUPA
14, 15. Gehazi alionyeshaje kilichompendeza kweli?
14 Elisha alikuwa na mtumishi aliyeitwa Gehazi ambaye yaelekea alikuwapo wakati Naamani alipokuwa akizungumza na Elisha. Gehazi aliyaona mambo tofauti na alivyoyaona Elisha. Anasemekana alisema hivi, yaelekea akijiambia mwenyewe: “Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama [Yehova] aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake.” Gehazi alipendezwa na faida ya kitu cha kimwili, kujipatia faida kutokana na kazi ya roho ya Yehova; kwa hiyo mambo ya kiroho siyo aliyoyafikiria.—2 Fal. 5:20.
15 Naamani alishuka garini mwake amlaki Gehazi naye akauliza, “Je! ni amani?” Gehazi akajibu, “Amani,” kisha akaendelea na kusema uongo apate alichotaka. “Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana wa manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili.” Kwa kusema uongo Gehazi alimtia bwana wake Elisha na wana wa manabii katika hila yake.—2 Fal. 5:21, 22.
16. Kulitukia nini Gehazi alipomrudia Elisha?
16 Naamani bado aliionyesha roho ile ile ya ukarimu aliyokuwa amemwonyesha Elisha mapema na kusema, “Uwe radhi, ukatwae talanta mbili.” Kisha Naamani ‘akazidi kumsihi’ (NW) Gehazi, na kwa hiyo mtu huyu mwenye pupa akazichukua zile talanta mbili za fedha na yale mavazi mawili akayaweka nyumbani mwake. Halafu, Gehazi akamrudia Elisha mikono mitupu. “Watoka wapi, Gehazi?” akauliza Elisha. Akiongezea uongo mwingine aufiche ule mwingine aliomwambia Naamani, na kuuficha ukweli, Gehazi alijibu, “Mtumwa wako hakuenda mahali.” Lakini, bila shaka, Yehova alijua Gehazi alivyokuwa amefanya naye akamfunulia Elisha jambo hili. Na kwa hiyo Elisha akamwambia Gehazi hivi: “Je! moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng’ombe, na watumwa, na wajakazi?”—2 Fal. 5:23-26.
17. (a) Kwa sababu gani Elisha aliudhika kwa kufaa? (b) Kilichompata Gehazi kwa sababu ya pupa yake ni nini?
17 Je! Waweza kuwazia namna ambavyo Gehazi aligutuka? Kumbe! bwana wake alijua jambo lenyewe alilokuwa amelifanya! Wazia pia ghadhabu yenye haki aliyopatwa nayo Elisha. Yeye alikuwa ametumikia faida za Yehova kwa kuponya ukoma wa Naamani naye alikuwa amekataa kuthawabishwa kwa fedha katika mwujiza huu. Hali sasa mtumishi wake, asiyehusika moja kwa moja, alikuwa ameondoka na kuchukua kitu kwa pupa akijisingizia. Elisha, aliendelea kumwambia Gehazi hivi, kwa wazi Yehova akimwunga mkono: “Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele.” Nazo habari zamalizika kwa kusema hivi: “Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.”—2 Fal. 5:27.
SIFA ZA KUIGWA AU KUEPUKWA
18. Twaweza kurudia kufikiria nini katika Wafalme wa pili, sura ya tano?
18 Fikiria tena habari zilizomo katika Wafalme wa Pili sura ya tano tulizoziangalia sasa hivi. Bila shaka twaona sifa fulani na nia za ajabu za watu mbalimbali. Itafaa sana turudie kuyafikiria mambo haya mbalimbali.
19. (a) Ni sifa gani za kupendeza alizokuwa nazo yule msichana mdogo Mwisraeli? (b) Twawezaje kudhihirisha sifa hizo?
19 Ebu mfikirie yule msichana mdogo Mwisraeli. Alitekwa kutoka Israeli, lakini hii haikuidhoofisha imani yake katika Yehova wala katika uwezo wake wa kutumia mmoja wa watumishi wake waaminifu kufanya miujiza. Elisha hakuwa ameponya wenye ukoma wo wote Israeli, kama vile Yesu alivyoonyesha baadaye. (Luka 4:27) Lakipi huyu msichana mdogo alikuwa na imani kweli kweli. Yeye hakuwa na shaka lo lote akilini mwake; aliamini kabisa kwamba kama Naamani angekwenda na kuuliza, Yehova angejibu. Ijapokuwa alikuwa kijakazi tu, yeye alikuwa na ushujaa wa kuishuhudia imani yake katika Yehova. Bila shaka alifanya hivyo kwa shauku na kwa kusadikisha kuweza kuupitisha ujumbe wake hata ukafuatwa, na kutoonwa kama upuzi wa kitoto tu. Imetupasa tuseme kweli kwa ushujaa kama mtumishi huyu mnyenyekevu wa Mungu asiyetajwa jina aliyeweka mfano mzuri ajabu wa imani, kusudi wote walio na mioyo minyofu wafaidike. Tusisite kamwe kueleza habari zake Yehova na makusudi yake, tukiogopa kwamba hatustahili kusema na mtu mwenye cheo kikubwa zaidi maishani kuliko sisi. Imetupasa tuwe na matumaini kabisa katika Yehova na uwezo wake wa kutuongoza.—Zab. 56:11.
20. Twawezaje kumwiga Elisha?
20 Halafu yuko Elisha. Biblia inatuambia mengi sana juu ya huyu mtumishi wa Yehova mwenye kufanya miujiza. Alitumiwa na Mungu hata kumfufua mtu kwa wafu. (2 Fal. 4:32-37) Lakini tamaa yake haikuwa kuwa tajiri, bali, kusaidia watu waongeze ufahamu wa Yehova na makusudi yake. Mapendezi yake bila shaka hayakuwa kujifanyia jina bali kulitukuza jina la Mungu wake, Yehova. Imetupasa tumwige Elisha katika kumshughulikia Yehova hasa, kuuweka upendo wetu kwake kwanza na kusaidia wengine wamwitie yeye wapate wokovu.—Mt. 22:37, 38; Rum. 10:13.
21, 22. Ni mambo gani mengine yaliyompasa Naamani ayafanye ili kujinyenyekeza?
21 Ingawa Naamani alikuwa “mtu hodari” kabla hajakutana na Elisha, alijifunza kujifunga unyenyekevu wa akili. Alipata kufahamu kwamba alikuwa mtu tu machoni pa Yehova, wala si mtu aliyestahili heshima ya pekee au kufikiriwa kwa njia ya pekee na watumishi Wake. Ni furaha namna gani aliyoiona alipotoka katika Mto wa Yordani mara ya saba na kuiona ngozi yake imesafishwa kabisa! Alikuwa mwenye furaha namna gani kwamba alijinyenyekeza na kulifuata pendekezo la Elisha lililopewa kupitia kwa mjumbe!
22 Fikiria pia ilihitaji imani kama nini kwa mtu wa cheo chake kufanya alivyofanya. Si kwamba tu alitii neno la msichana mdogo aliye mtumwa wa taifa la adui; bali ilimpasa aiache miungu yake mwenyewe nyuma, pengine akidhani angeikasirisha, na kwenda nchi iliyo adui na yake na kumwomba nabii wa Mungu mgeni amfanyie jambo. Kuwa mnyenyekevu kwa Naamani kulimaanisha jambo lenye thamani kubwa zaidi kuliko kusafishwa na ukoma. Hilo lilikuwa nini? Kulimwongoza akawe mwabudu wa Yehova, mtu mwenye kutaka kuwa na kibali ya Mungu mmoja aliye wa kweli. Ilikuwa thawabu nzuri kwa kujivika kwake unyenyekevu. Kama vile kwa habari ya Naamani, sisi pia twaweza kufaidika sana kwa kiroho ‘tukijifunga vazi la unyenyekevu’ na kujua kwamba Mungu anawapendelea wanyenyekevu.—1 Pet. 5:5, New English Bible.
23. Twawezaje kufaidika kwa kurudia kuufikiria mwendo wa Gehazi?
23 Yule mtu mwingine ambaye matendo yake yanakaziwa fikira zetu katika sura hii ya Biblia ni mtu ambaye yafaa tusiuige mfano wake. Gehazi alikuwa amekuwa akitumikia pamoja na Elisha kwa muda fulani naye alikuwa na nafasi za kutosha kuona namna Yehova alivyokuwa akimtumia Elisha na lo! ni pendeleo namna gani alilokuwa nalo kuwa pamoja na Elisha. Lakini alikuja kutamani utajiri wa vitu vya kimwili. Pupa yake ilimkaza sana alipomwona bwana wake akiikataa fedha yote na mavazi yaliyotolewa na Naamani. Tamaa yake ilichukua mimba ikamwongoza kwenye dhambi. (Yak. 1:14, 15) Alifanya hila akajitungia hadithi apate sehemu ya vitu hivyo vya kimwili ambavyo Naamani alikuwa akirudi navyo nyumbani. Hata alifikia hatua ya kusema uongo kwa bwana wake, kwa sababu hiyo akisema uongo kwa Yehova, aliyekuwa amemweka Elisha. Na lo! ni matokeo gani yenye msiba yaliyompata, kwa maana alipigwa kwa ukoma! Pupa yake ilimpotezea afya yake na pendeleo alilokuwa nalo la kutumikia pamoja na Elisha. Twaweza kufaidika kutokana na mfano huu wa mwendo wenye msiba wa kuwa wenye pupa, wenye kujipenda mno. Twajifunza kwamba kujaribu kujipatia faida kutokana na utumishi wa Yehova ni jambo la hatari sana lipasalo tuliepuke.—Linganisha Yohana 12:4-6.
ULINGANIFU WA KINABII KWA LEO
24. Elisha na Naamani wanaweza kuonwa kama wakifananisha nani?
24 Elisha alikuwa mtumishi aliyetiwa mafuta wa Mungu. Yaani, aliwekwa kwa njia ya pekee na Yehova afanye kazi fulani. Kwa hiyo aweza kutumiwa kama mfano wa unabii wa mabaki ya bibi-arusi wa Kristo walioko duniani bado, mabaki ya 144,000 watakaoungana na Kristo mbinguni. (Ufu. 14:1-3) Wanadamu kwa ujumla wako katika hali aliyokuwa nayo Naamani. Badala ya kupatwa na ukoma, wao wanataabishwa na pigo lenye kufisha la dhambi, nao wakiwa katika hali hiyo, wengi wao wanapigana na washiriki waliobaki wa bibi-arusi wa Kristo ambao wangali duniani na wale wanaoshirikiana nao.—Rum. 5:12; Mt. 24:9.
25. “Mkutano mkubwa” wenye mfano wa Naamani wamesaidiwaje?
25 Walakini, kwa kutolewa kwa ushuhuda wa Ufalme, kama ule wa kijakazi mdogo Mwisraeli wa mke wa Naamani, wengi wa hawa wameelekezwa katika njia ifaayo wakaponywe na hali yao ya ugonjwa, tukisema kwa njia ya kiroho. Wameonana na jamii iliyotiwa mafuta ya Elisha wakaelezwa anayoyahitaji Yehova kwao wapate kuponywa kwa kiroho na kuwa na dhamiri njema kumwelekea yeye. Kama vile imani na kujinyenyekeza kulivyohitajiwa kwa habari ya Naamani, ndivyo kunavyohitajiwa pia kwa habari ya watu hawa. Wametiwa moyo wakatii nao wana furaha ya kusafishwa kuwa katika hali yenye kukubalika machoni pa Mungu. Sasa wanakuwa sehemu ya “mkutano mkubwa” ambao tumaini lao ni kuishi milele katika taratibu mpya yenye haki milele katika dunia iliyosafishwa. (Ufu. 7:9) Wale wa huu “mkutano mkubwa” wamepata kujua kwamba hakuna Mungu ko kote isipokuwa kati ya mashahidi wa Mungu wa kweli, Yehova. Wanafahamu kwamba kuponywa kwa kiroho kunatolewa bure, kupatana na maagizo ya Yesu.—Mt. 10:1, 8.
26. Wale ambao kwa kujisingizia wanamtumikia Mungu huku wakitumia wengine kwa faida yao wenyewe wanaonwaje?
26 Jamii ya Elisha haitaki kuutumia “mkutano mkubwa” kwa faida yake yenyewe inapowasaidia wapone kwa kiroho na pigo la dhambi. Wanakataa wasilipwe cho chote kwa kusaidia watu mmoja mmoja wapone kwa kiroho, kama vile Elisha alivyokataa zawadi yo yote kutoka kwa Naamani, ya fedha au mavazi. Wanatumia wakati wao kwa hiari wasaidie wengine wanaotaka kujifunza Neno la Mungu. Na ikiwa wo wote wanaoshirikiana na kundi la watu wa Mungu duniani wanajaribu kujipatia faida ya vitu vya kimwili kwa hasara ya “mkutano mkubwa,” hao wanaadhibiwa kama wenye pupa, wenye hatia ya kujipenda mno. Hao wanaondolewa katika tengenezo, ikipatana na Gehazi alivyotendwa na Elisha kwa sababu ya tamaa yake ya vitu visivyo vyake na pupa. Hii inapatana na kanuni hii: “Waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, . . . wala [wenye pupa], . . . wala wanyang’anyi.”—1 Kor. 6:9, 10.
27, 28. Watu leo wanaweza kufanya nini wajitambulishe kama sehemu ya “mkutano mkubwa”?
27 Hawa wanaoufanyiza “mkutano mkubwa” wanaoshirikiana na watumishi wa Mungu waliotiwa mafuta lazima pia wajifunge unyenyekevu wa akili. Katika 1 Petro 5:5, Today’s English Version of the Bible inasema hivi: “Nanyi nyote lazima mjivike kitambaa cha unyenyekevu cha kujizuia na uchafu, mkatumikiane; kwa maana andiko lasema, ‘Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa neema wanyenyekevu.’” Kitambaa cha kujizuia na uchafu kinatufanya tumfikirie mtu anayetumikia, akiangalia mapendezi ya wengine, akitayarishia wengine chakula. Kwa hiyo kuvaa “kitambaa cha unyenyekevu cha kujizuia na uchafu” kungetia ndani kuwa asiyetaka makuu, mnyenyekevu wa akili, mwenye kupendezwa na kuwatumikia wengine.
28 Je! una nia ya ‘kujifunga unyenyekevu wa akili,’ ‘kujivika kitambaa cha unyenyekevu cha kujizuia na uchafu’? Je! una nia ya kuikubali njia ya Yehova ya wokovu? Katika hii karne ya ishirini tunao mfano wa kutotaka makuu, unyenyekevu wa akili, unaoonekana ulimwenguni pote. Umo katika tengenezo la mashahidi wa Yehova. Kwa sababu gani usiendelee kusoma uone namna ambavyo wamejipatanisha na njia ya Yehova ya wokovu kwa unyenyekevu?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Kwa kuonyesha unyenyekevu wa akili jemadari wa jeshi la Shamu aliponywa ukoma kwa mwujiza
[Picha katika ukurasa wa 6]
Pupa ya Gehazi ilimwongoza ajipatie faida kutokana na kazi ya roho ya Yehova na ukarimu wa Naamani. Ilimfanya Gehazi apoteze afya yake na pendeleo la kutumikia pamoja na Elisha