Wachungaji wa Uongo Waondolewa Katika Utumishi wa Mungu
Makala hii ni ya kutumia kwa mafunzo ya kitabu ya kundi
1. Imewapasa wachungaji katika kundi la Kikristo watendeje?
WAKATI Mungu alipoanzisha kundi la Kikristo, alipanga kupitia kwa Kristo kuwe na wachungaji na waalimu. (Efe. 4:11) Mtume Petro ambaye mwenyewe alikuwa mchungaji wa Kikristo alionya hivi kwa ukali: “Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”—1 Pet. 5:2, 3.
2. (a) Biblia inazungumza juu ya “wachungaji” wengine mbali na wale waliomo katika kundi la Kikristo? (b) Je! wana wajibu kwa Mungu kwa namna wanavyofanya uchungaji wao?
2 Wachungaji katika kundi la Kikristo si watawala. Walakini, katika mataifa yanayojidai kuwa ya Kikristo, wako watawala wa kidini na wa kiserikali pia wanaojidai wanaangalia watu kama wachungaji. Nao wanazungumzwa kuwa wachungaji katika Maandiko. Mungu awaona wale wanaojionyesha kuwa wachungaji wawe waliwekwa na Mungu katika vyeo hivyo au sivyo, kama wenye wajibu mkubwa kwake kwa sababu maisha na hali njema ya watu inahusika. Wo wote wa wanaume hao wenye madaraka wakiwa wa uongo, watapata hukumu nzito. (Yak. 3:1) Ili kutufariji na kuonya wale waliomo katika vyeo hivyo, Mungu alimtumia nabii Zekaria kama mfano wa unabii wa mambo yatakayokuja.
MFANO WA UNABII
3, 4. (a) Hali ya Waisraeli ilikuwa nini Mungu alipomweka Zakaria kama mchungaji? (b) Baada ya kuwekwa, Zekaria alichukua hatua gani?
3 Wakati huo Yehova Mungu alikuwa na “kundi,” yaani, watu wake wa agano Israeli. Yeye mwenyewe ndiye aliyemweka Zekaria kama mchungaji, akisema hivi: “Lilishe kundi la machinjo, ambalo wenye kundi hilo huwachinja, kisha hujiona kuwa hawana hatia; na hao wawauzao husema, Na ahimidiwe [Yehova], kwa maana mimi ni tajiri; na wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.”—Zek. 11:4, 5.
4 Kundi la Mungu lilikuwa limeingizwa katika hali mbaya sana na wachungaji wao wasiopendezwa kundi likiwa na hali njema na wasioona huruma juu ya hali yao ya kuonewa. Wakati Zekaria alipowekwa alikaza fikira zake kwa wengine wa wachungaji hao. Atuambia hivi: “Nami nikawakatilia mbali wachungaji watatu katika mwezi mmoja; maana nafsi yangu ilikuwa imechoka kwa ajili yao, na nafsi zao pia walinichukia.” (Zek. 11:8) Hatuambiwi wachungaji hao watatu walikuwa akina nani. Lakini kwa kuwa Zekaria alikuwa amewekwa na Mungu Aliye Juu Zaidi, alikuwa na mamlaka kati yao, hata angeweza kuwaondoa wanaume hao watatu.
5. Zekaria ‘alichoka’ kwa ajili ya nani, nao wachungaji watatu hao waasi walionaje juu ya Zekaria?
5 Kama alivyosema, Zekaria alikuwa akitimiza kazi yake “kwa ajili yenu, Enyi mliotaabishwa wa kundi.” (Zek. 11:7, NW) Yeye alipenda kundi la Mungu. Kwa hiyo aliochoka kwa ajili yao hawakuwa kondoo waliotaabishwa, bali ni wale wachungaji watatu waasi. Kwa upande wao, ‘walimchukia’ Zekaria kwa sababu alikuwa mwaminifu na mwenye huruma katika kuchunga kundi. Yeye alizikataa njia zao na hila zao.
6. Zekaria alimfananisha nani, nayo hali ya Waisraeli ilikuwa nini wakati huyu alipotokea?
6 Kwa kuwekwa kuwa mchungaji, Zekaria alimfananisha “mchungaji mwema,” Bwana Yesu Kristo. Yesu alipotumwa na Baba yake akawe mchungaji wa kundi la Mungu la Israeli, watawala wao, hasa viongozi wa kidini, walikuwa wamekuwa wakiwatendea watu kwa njia ya kuhuzunisha. Yesu alikuta hali gani? Twasoma hivi: “Alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.”—Mt. 9:36.
7. Kwa wazi, “wachungaji watatu” ambao Yesu alikutana nao walikuwa akina nani?
7 Ni akina nani wakati huo waliokuwa “wachungaji watatu” ambao alikatilia mbali, akawaondoa katika vyeo vyao vya kusingizia? Maandishi ya maisha ya Yesu hayaonyeshi kama wanaume watatu walitimiza mfano huo wa unabii wakiwa mmoja mmoja. Kwa wazi wachungaji watatu ambao nabii Zekaria aliondoa katika kazi zao wanafananisha jamii tatu za watu wa nyakati za Yesu. Jamii tatu ambazo zilikuwa na uwezo wa kiserikali na wa kidini pia katika Israeli zimeandikwa katika maandishi. Hao walikuwa (1) Mafarisayo na (2) Masadukayo, nazo jamii zote hizi mbili ziliwakilishwa katika Sanhedrin (Baraza Kuu) katika Yerusalemu. Baraza ya hukumu ilikuwa na kazi fulani za kiserikali na za kidini pia, ikisimamiwa na gavana wa Kirumi. Hivyo mtu fulani aliyeitwa Nikodemo, mshiriki Farisayo wa Sanhedrin, alikuwa “mkuu wa Wayahudi.” (Yohana 3:1, 2; 7:50-52) Sanhedrin iligawanywa sana kati ya Mafarisayo na Masadukayo. (Matendo 23:1-9) Zaidi ya wafuasi hao wa madhehebu za Kiyahudi, walikuwako pia (3) Maherodi, “wafuasi wa chama cha Herode.”—Marko 12:13, NW.
YESU KRISTO AONDOA “WACHUNGAJI WATATU” KATIKA UTUMISHI
8. “Wachungaji watatu” wa mfano ‘walimchukiaje’ Yesu, nayo nafsi ya Yesu ‘ilichokaje’ kwa ajili yao?
8 Kama vile wale “wachungaji watatu” ‘walivyomchukia’ Zekaria kama mchungaji, vikundi hivyo vitatu upesi ‘vilimchukia’ Yesu Kristo kama mchungaji wa Kimasihi. Walifanya hila au wakashirikiana pamoja wamwaibishe Yesu machoni pa kundi la Israeli. (Mt. 22:15, 16, 23; Marko 3:6) Tangu pale pale mwanzoni mwa huduma yake ya kidunia Yesu alikataa kuwa na uhusiano wo wote na watu hao wa vikundi vyenye kutawala vikijitafutia faida zao wenyewe, yaani, alikataa kujiunga navyo. Mwishowe, kuelekea mwishoni mwa huduma yake, nafsi yake ‘ilichoka’ kwa ajili yao. Alinyamazisha vikundi vyote vitatu hadharani kwa habari iliyohusu serikali na mafundisho. “Mwezi mmoja” wa mfano ambao katika huo Yesu aliviondoa vikundi hivyo katika utumishi unafananisha kipindi kifupi mwishoni mwa huduma yake.
9. Ni wakati gani Yesu alipofikia upeo wa kuchukua hatua kuondoa “wachungaji watatu” hao katika utumishi, nasi twapata maandishi ya jambo hilo wapi?
9 ‘Kukatiliwa mbali’ kwao kulifikia upeo Nisani 11, 33 C.E., siku chache tu kabla hawajamfisha Yesu mikononi mwa Warumi. Mtume Mathayo (22:15-46) atoa habari za vile Yesu alivyopinga kabisa, akafunua ubaya wa kila moja ya jamii hizi tatu na kuzinyamazisha kwa zamu, kama zisizostahili kuchunga kundi. Mathayo aandika hivi juu ya Mafarisayo na Maherodi:
10. Eleza vile alivyoaibisha Mafarisayo na Maherodi.
10 “Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.”
11-13. Yesu alipingaje fundisho la uongo la Masadukayo?
11 Baadaye Masadukayo wakaja, nao waondolewe katika utumishi:
12 “Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama [“ufufuo,” NW], wakamwendea, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye.
13 Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kwa habari ya kiyama ya wafu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake.”
14, 15. Eleza vile Yesu alivyonyamazisha Mafarisayo mwishowe.
14 Mwishowe, Yesu alimaliza kuondoa wale “wachungaji watatu” katika utumishi kwa kuonyesha Mafarisayo kosa lao la kukana kwamba yeye hakuwa Mwana wa Mungu:
15 “Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika [roho] kumwita Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu; Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwawekapo adui zako kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.”
16. Baada ya kufunua wazi kwamba “wachungaji watatu” hao walikuwa hawafai kitu, Yesu aliwachukulia hatua gani zaidi?
16 Hapo wakili wa Mungu mwenyewe, Mchungaji Mwema wake, Yesu Kristo, alionyesha hadharani kwamba jamii hizo zilikuwa wachungaji wasiofaa kitu, kwamba zilikataliwa na Yehova Mungu. Muda mfupi baada ya hapo aliwatolea hasira kali.—Mt. sura ya 23.
KARIBUNI WACHUNGAJI WOTE WA UONGO WATATOWEKA
17. Zekaria alitoa unabii gani juu ya “mchungaji asiyefaa” kitu?
17 Kwa kuwa Yehova aliwachukulia hatua wachungaji wa uongo siku za Zekaria na wakati Kristo alipokuwa duniani, tunaweza kuwa na hakika kwamba atachukua hatua juu ya wachungaji wa uongo wa kisasa. Zekaria aliongozwa na Mungu kutoa unabii juu ya hukumu inayostahiliwa itakayokuja juu ya “mchungaji asiyefaa” kitu: “Hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao. Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kuume; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kuume litakuwa limepofuka.”—Zek. 11:15-17.
18. (a) “Mchungaji asiyefaa” kitu wa leo amelitendeaje kundi? (b) Ni hukumu gani ambayo Mungu atailetea jamii hii?
18 Hali iliyo kati ya watu leo ni nini? Je! wao si kama kondoo ‘waliokatiliwa mbali’ au waliosahauliwa kabisa, waliovunjika na wasioponywa, wakilishwa na wachungaji wapotovu wenye kujifaidi wenyewe kwa kuwatumia, wanaowala hata “kwato” zao? Yehova asema kwamba, kwa sababu hawamwakilishi kweli na hawana baraka yake, “mkono” wao wa mamlaka na uwezo utakauka kabisa nalo ‘jicho lao la kuume,’ jicho lao bora la kuonea dawa na la uangalizi wa kiserikali, litapofuka zaidi na zaidi. Tunaweza kuona hata sasa watu walio katika vyeo vya ‘uchungaji’ wamevurugika akili sana nao wana wasiwasi mwingi. Katika ‘dhiki kubwa’ inayokuja juu ya ulimwengu huu Yehova ataiharibu kabisa jamii hiyo ya “mchungaji asiyefaa” kitu.
19. Uharibifu wa wachungaji wa uongo utafanyia nini wale wanaomtegemea “mchungaji mwema”?
19 Uharibifu wa wachungaji wa uongo utakomboa wanaomtegemea Yesu Kristo kama “mchungaji mwema” katika uonezi. (Yohana 10:11) Kupitia kwa nabii wake Isaya, Mungu asema hivi: “Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.” (Isa. 49:9, 10; linganisha Ufunuo 7:9-17.) Acheni wote wanaotaka kuishi kwa amani na furaha waichunguze Biblia, wauone uongozi wa “mchungaji mwema” wa Mungu na kufuata njia ya uzima kama aamuruvyo.
—Kutoka Kitabu Paradise Restored to Mankind—by Theocracy!