Wewe ‘Umeacha Kuweka Hazina Duniani’?
“Acheni kujiwekea hazina duniani ambapo nondo na kutu zinakula, na ambapo wevi wanavunja na kuiba.”—Mt. 6:19, NW.
1. (a) Kusudi la wafanya biashara leo ni nini? (b) Kwa sababu gani hakuna uradhi unaotokana na kutosheleza tamaa zilizotiwa ndani ya mtu na wengine?
ULIMWENGU katika nyakati za kisasa umejawa na bidhaa na mali za kimwili. Hakuna kikomo cha namna mbalimbali za vitu vya kimwili ambavyo pesa zinaweza kununua. Wakijua hivyo, wafanya biashara leo wanakusudia kujipatia faida kubwa badala ya kutosheleza mahitaji yaliyo makubwa ya watu. Kwa hiyo, wafanya biashara wanatumia pesa nyingi sana wakitangaza vitu vyao, na kuvitangaza na kuvitangaza. Wana kusudi gani? Kusudi lao ni kukutamanisha wewe vitu vyao, ili waweze kukutumia kwa faida yao wenyewe. Ukiisha anza kutosheleza mahitaji yako ya kweli na kujaribu kutosheleza pia tamaa hizo walizotia ndani yako, unajikuta katika mwendo usio na kikomo utakaokumalizia sehemu kubwa ya wakati wako, nguvu zako na fikira zako bila kukupa uradhi unaotaka mwishowe. Maneno ya Sulemani mwenye hekima ni ya kweli sana: “Mpenda fedha tu hatatosheka na fedha, wala mpenda utajiri ye yote hatatosheka na [faida za] mapato. Huu pia ni ubatili”!—Mhu. 5:10, NW.
2, 3. (a) Yesu alitoa shauri gani bora juu ya hazina ya kidunia? (b) “Mabaki” na “kondoo wengine” pia wanawezaje kufaidika kutokana na shauri hilo?
2 Katika Mahubiri yake juu ya Mlima Sulemani Mkuu Zaidi, Yesu Kristo, alionyesha kwamba wenye kutafuta baraka za ufalme wa Mungu wa Kimasihi wangejishughulisha na hazina iliyo ya maana zaidi. Kwa hiyo, shauri lake kwa wanafunzi wake linafaa sana leo: “Acheni kujiwekea hazina duniani, ambapo nondo na kutu zinakula, na ambapo wevi wanavunja na kuiba. Bali, jiwekeeni hazina mbinguni, ambako wala nondo wala kutu hazili, na ambako wevi hawavunji wala kuiba”!—Mt. 6:19, 20, NW.
3 Hilo ni shauri zuri sana kwa mabaki ya wanafunzi watiwa mafuta wa Bwana Yesu Kristo walio na tumaini la “urithi usioharibika” katika mbingu za kiroho! (1 Pet. 1:4; Efe. 1:18) Kwa sababu mwishoni mwa mwendo wao wa kidunia, wanalazimika kuacha mali zao ZOTE za kimwili nyuma yao. Hawawezi kwenda nazo mbinguni. Ndivyo ilivyo pia kwa “mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine” walio na tumaini la kuokoka “dhiki kubwa” iliyoko karibu hapo mbele, watakaoishi milele katika dunia ya paradiso. (Ufu. 7:9-14; Mt. 24:21, 22; Zab. 37:29) Yehova Mungu hakuahidi “kondoo wengine” hawa kwamba atahifadhi mali zao zote za kimwili hapa duniani zipite “dhiki kubwa” hiyo wakazitumie baadaye.
MIFANO YA KIHISTORIA
4. Petro anaonyeshaje uwezo wa Yehova wa kukomboa, nasi tunajifunza nini kutokana na mfano wa Nuhu?
4 Kwa hakika, hatuna sababu ya kutia mashaka juu ya uwezo wa Yehova wa kuhifadhi na kukomboa. Uwezo huo umeonyeshwa mara nyingi na kwa njia nyingi katika nyakati zilizopita. Mtume Petro anatukumbusha juu ya hilo na kutuhakikishia kwamba Yehova “ajua kuwaokoa watauwa na majaribu.” (2 Pet. 2:9) Katika habari hii anatupa mifano yenye kutazamisha, kama vile Yehova “hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu.” (2 Pet. 2:5) Kwa uwazi na usahihi Neno la Mungu linatuhifadhia masimulizi hayo, likirudi nyuma zaidi ya miaka elfu nne kufikia wakati ambao Yehova alimkomboa mzee huyo wa ukoo aliyekuwa mwaminifu, Nuhu, na jamaa yake kupita gharika ya dunia wakiwa katika safina ambayo yeye alipewa pendeleo la kuijenga kulingana na maagizo aliyopewa na Mungu. (Mwa. 6:14-16) Walakini, lazima tuangalie kwamba haitajwi kwamba Mungu alihifadhi makao, au nyumba halisi ya Nuhu na jamaa yake iliyojengwa duniani. Bila shaka, mali hizo za kidunia, za kimwili zilifagiliwa mbali wakati “chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku.”—Mwa. 7:11, 12.
5. Kukombolewa kwa Lutu kunaendeleaje kukazia jambo hilo?
5 Kisha Petro anataja wakati wa mpwa wa Ibrahimu Lutu. Wakati Mungu alipoikomesha kwa moto miji yenye ufisadi ya Sodoma na Gomora, “akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa [nafsi] yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria.” (2 Pet. 2:7, 8) Hapa pia, tunaona kwamba, wakati Lutu alipokimbia pamoja na mkewe na binti zake wawili, maandishi hayasemi walikwenda na mali zao za kimwili. Wasingeweza kufanya hivyo. Agizo walilopewa na malaika lilisema: “Kimbia ukaiponye nafsi yako!” Lakini bila shaka mke wa Lutu alikuwa bado na “tamaa” ya mali za kimwili zilizoachwa nyuma. Alikosa kutii maagizo yaliyotolewa na malaika kwa kutazama nyuma, akawa nguzo ya chumvi.—Mwa. 19:17, 23-26, NW.
6. Wayahudi waliofanywa kuwa Wakristo walipewa maagizo gani juu ya Yerusalemu?
6 Vivyo hivyo, katika karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida, baada ya Mji Mtakatifu wa Yerusalemu kuzingirwa kwa muda na majeshi ya Kirumi yakiongozwa na jemadari wa Kirumi Sesho Galo, Wayahudi waliofanywa’ kuwa Wakristo walipaswa kutii shauri la Bwana Yesu Kristo. Iliwapasa kuacha mali zao katika Yerusalemu na Uyahudi na ‘kukimbia’ milimani nje ya jimbo la Uyahudi, wakiacha nyuma yao karibu kila kitu. Waliokuwa nje ya wilaya hiyo wakati huo hawakupaswa kuingia na kudai kitu cho chote cha kimwili ambacho pengine walikuwa wamekuwa nacho.—Luka 21:20-24.
7, 8. Katika mwaka wa 607 K.W.K., ni wanaume gani wawili waliopokea baraka ya pekee ya Yehova, na kwa njia gani?
7 Tukirudi nyuma katika historia, tunaona hali inayofanana na hiyo. Neno la Mungu linaonyesha kwamba mwaka wa 607 K.W.K. walikuwako wanaume wawili waliotajwa waziwazi na Yehova Mungu ambao wangepokea baraka zake za pekee wakati Mji Mtakatifu wa Yerusalemu ungeharibiwa na majeshi ya Kibabeli. Mmoja wa wanaume hao alikuwa Mwethiopia aliyeitwa Ebedmeleki. Yeye ndiye aliyemsihi Mfalme Sedekia wa Yerusalemu kwa ajili ya nabii Yeremia, ili mfalme amwokoe Yeremia, ambaye alikuwa katika hatari ya kufia shimoni. (Yer. 38:6-13) Akizungumza juu ya thawabu ya huruma ya Ebedmeleki kwa mtumishi wa Yehova, Yehova alimwambia hivi: “Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema [Yehova].”—Yer. 39:18.
8 Mwanamume yule mwingine aliyetajwa na Yehova alikuwa Baruku, katibu (mwandishi) mwaminifu wa nabii Yeremia. Alikuwa na pendeleo la ajabu la kuandika vitabu viwili vya kukunja, akielezwa mambo ya kuandika na Yeremia, akitangaza ujumbe wa unabii wa maangamizi ya Yerusalemu. Alipokuwa akiandika kitabu cha kwanza cha kukunja, ambacho baadaye kilichomwa kipande kwa kipande na Yehoyakimu, Baruku alilalamika juu ya uchovu. Yehova akamwonya: “Je! unajitafutia mambo makuu? usiyatafute.” Walakini, kwa sababu ya uaminifu wake aliahidiwa kuhifadhiwa na kusalimishwa, si wakati wa mazingiwa hayo ya kuogofya ya Yerusalemu tu bali baadaye pia wakati watoro waasi walipomshurutisha yeye na Yeremia washuke hata Misri pamoja nao. (Yer. 36:4-32; 43:4-7) Lakini angalia kile ambacho kingehifadhiwa: “Kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema [Yehova]; lakini [nafsi] yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.” (Yer. 45:1-5) Kwa hiyo Baruku na Ebedmeleki pia hawakuahidiwa kingine ila “nafsi” zao, maisha zao tu, wakati wa mazingiwa na uharibifu wa mji wa Yerusalemu.
MAULIZO YA KUJIULIZA WENYEWE
9. Kwa sababu ya wakati tunamoishi, imetupasa tufikirie maulizo gani kwa uzito?
9 Tunapofikiria mifano myema hiyo na kufahamu leo kwamba “mwisho wa mambo yote umekaribia” (1 Pet. 4:7), kwamba tunaishi katika kipindi cha wakati kilicho kibaya zaidi na chenye kukaribiwa na uharibifu mkubwa zaidi, inatufanya tujiulize wenyewe kwa uzito hivi: Je! ni jambo la akili kwetu kutumia wakati mwingi na jitihada juu ya mazoezi ya pekee ya kupata kazi ya kitaalamu katika taratibu hii ya kilimwengu ya mambo, ili tuweze kuongeza mapato yetu? Je! ni jambo la busara kwetu kutaka kuongeza mali zetu za kidunia zizidi kiasi tunachohitaji ili tuwe na maisha yenye starehe na anasa zaidi hapa duniani katika wakati mfupi unaobaki kabla ya “dhiki kubwa”? Je! tunakosa kuona kwamba kuna jambo la maana zaidi na la kuthaminika zaidi tunalopaswa kuhangaikia sasa? Je! tunakosa imani kwamba, Mhifadhi wetu Mkuu atatuangalia siku za usoni tukimweka Yeye kwanza katika maisha zetu? Haya ni maulizo ambayo kila mmoja wetu lazima afikirie peke yake. Maisha zetu zinategemea kuyafikiria!
10. Kwa sababu gani imetupasa tufikirie maneno ya Yesu katika Luka 17:26-30?
10 Tukiwa tunaishi katika kizazi ambamo mna mambo mengi sana yanayoweza kumaliza wakati wetu na fikira zetu, imetupasa tukumbuke sana maneno ya unabii wa Yesu. Yeye alisema: “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.” (Luka 17:26-30) Ukiwa umejua hivyo mapema, wewe wajiona wapi? Je! unashughulika sana na mambo ya maisha ya kila siku? Je! hapo ndipo hazina yako ilipo, ndipo moyo wako ulipo? (2 Pet. 3:17; Mt. 6:21) Kwa hiyo, ni jambo linalofaa kama nini kwamba Yesu Kristo ameshauri wanafunzi wake wote, kutia na sisi leo tunaoishi katika mwisho wa taratibu hii ya mambo, wajiwekee hazina mbinguni! Itakuwa baraka iliyoje kwetu tukifanya hivyo!
11, 12. (a) Maana yake nini ‘kuweka hazina mblnguni’? (b) Inawezekanaje?
11 Lakini huenda ukauliza, Maana yake nini kuweka hazina mbinguni? Ni vipi hasa jambo hilo linavyoweza kufanywa? Hii ndiyo maana: Kwamba tujaribu kupata na kuendeleza uhusiano mwema na Muumba wetu, Yehova Mungu. Maana yake ni kufuatia mwendo katika maisha wa kuwa ‘matajiri kwa Mungu.’ (Luka 12:21) Kumbukumbu la mtu la “kazi nzuri” ni kama utajiri uliowekwa kwa Muumba mbinguni, likimhakikishia kupata faida za milele ambazo hata mauti yenyewe haiwezi kuziondoa. (Ebr. 10:24; Yak. 3:13; Yohana 11:25) Uhusiano huo unaendelezwa tunapoendelea kuwa thabiti katika imani na ushikamano wetu kwa Mungu, Yehova, na kwa kufanya mapenzi ya kimungu.—Rum. 11:20; 2 Kor. 1:24.
12 Yesu aliendelea kukazia hazina hizo za kimbinguni akatuwekea kielelezo. (1 Pet. 2:21; Ebr. 10:5-10) Baada ya kuwashauri wanafunzi wake habari za hazina za kidunia, aliwasihi hivi: “[Endeleeni kutafuta] kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” (Mt. 6:33) Kwa hiyo ili tuweke hazina hizo za kimbinguni, ni jambo la maana sana sana tuishi na kutenda sasa kwa kutumainia kupata kumbukumbu la kukubaliwa na Baba yetu wa mbinguni, Yehova Mungu.—Zab. 5:12; Mit. 12:2; Yohana 6:27.
13, 14. Zakayo alikuwa nani, na ni badiliko gani la kutazamisha lililotokea katika maisha yake?
13 Katika karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida tunao mfano wa mtu aliyefanya hivyo, aliyeacha hazina zake hapa duniani ili apate kujitoa kwa faida za ufalme wa Kimasihi. Ni nani huyo? Ni mtu aliyekuwa tajiri sana aliyeitwa Zakayo, mkuu wa watoza kodi aliyeishi katika mji wa Yeriko. Mpaka leo hii wilaya iliyo karibu ya Yeriko, ambayo iko magharibi ya Mto Yordani, ni yenye rutuba nyingi nayo inazaa sana. Bila shaka, nyakati za kale ilizaa mazao mengi yenye kustahili kutozewa kodi. Kama watoza kodi wengi wa siku zake Zakayo alikuwa na mazoea mabaya ya kutumia cheo chake ajipatie sehemu ya utajiri wake uliojulikana sana.—Luka 19:2, 8.
14 Yesu alikuja Yeriko katika masika ya 33 W.K. kabla hajakwenda Yerusalemu akafe. Zakayo alipiga mbio atangulie mbele akapanda mti kwa kutaka kumwona Yesu, kwa sababu ya kuwa mfupi wa kimo asiweze kumwona akiwa kati ya kundi la watu. Kwa wazi hii ilivuta fikira za Yesu akamwita ashuke na kumwambia kwamba angekaa nyumbani kwake wakati yuko Yeriko. Jambo hilo liliudhi watu wa mji huo, wakalalamika wakisema: “Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” (Luka 19:3-7) Lakini, ushirika wa Yesu ulikuwa na matokeo ya ajabu juu ya Zakayo. Kwa kumsikiliza Yesu, kwa wazi alipata kuthamini hazina halisi, kwa maana alipaza sauti akisema: “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.” Naam, alionyesha tamaa yake ya kukaa bila utajiri wake na kuwa mfuasi mwaminifu wa Bwana Yesu Kristo. Lo! Zakayo alifurahije Yesu alipomwambia hivi: “Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu”!—Luka 19:8, 9.
MIFANO YA KISASA
15. Ni mfano gani wa kisasa tulio nao wa kutanguliza kwa mtu hazina za kimbinguni katika maisha yake?
15 Kwa hiyo leo, tunafurahi kuona mifano ya kiasi ya watu ambao wameona inafaa kukaza fikira zao juu ya mambo ya Ufalme na kuupa kisogo ukusanyaji zaidi wa utajiri hapa duniani. Mfano mmoja ni ule wa ndugu ambaye habari zake za kweli zilielezwa katika The Watchtower la Mei 15, 1968, naye alikuwa mfanya biashara mwenye kufanikiwa sana. Majaliwa yake yalimwezesha kufanikiwa sana katika ununuzi, uuzaji na usimamizi wa mashamba makubwa kweli kweli. Wakati mmoja wafanya biashara wenzake waliomfahamu kuwa stadi wa biashara walimfikia na toleo lenye kutamanisha bure la kibiashara. Hilo lilikuwa toleo gani? Lilikuwa shauri ambalo kwalo angeweza kujipatia dola milioni moja (shilingi 8,000,000 au 500,000Z) kwa mwaka mmoja tu! Yeye alifanya nini? Alilikataa toleo hilo! Kwa sababu gani? Kwa sababu ingemlazimu kutumia wakati wake wote kipindi hicho akijishughulisha na mambo mengi sana ya kibiashara. Kama alivyosema: “Siwezi kuacha mapendeleo yangu mazuri ajabu ya kumtumika Yehova hapa hata kwa mwaka mmoja tu, hasha, hata nipewe pesa ZOTE ulimwenguni. Kutumikia ndugu zangu hapa Washington, D.C., ni kwa thamani nyingi zaidi kwangu, kwa maana hapa najua nina baraka ya Yehova. Bila shaka ningejipatia dola milioni moja (shilingi 8,000,000 au 500,000Z) lakini mwishoni mwa mwaka wa namna hiyo ya maisha nitakuwaje kiroho au hata kimwili?” Je! wewe ungefanya uamuzi kama huo ukiwekewa toleo hilo kwa njia yenye kushawishi?
16. Ni mfano gani mwingine tunaoweza kuthamini leo? Kwa sababu gani?
16 Fikiria pia mfano mwingine wa mapema zaidi, ule wa mwanamume aliyekuwa akianza umri wake wa miaka ishirini miaka ya 1870, katika Allegheny County, Pennsylvania. Alikuwa akifanya biashara na baba yake, wakiendesha maduka mengi yenye vifaa vya wanaume naye alikuwa akielekea kuwa milionea. Hiyo ilikuwa kabla John D. Rockefeller hajaanza biashara ya mafuta akawe milionea wa kupindukia. Lakini kijana huyo wa Allegheny alifanya nini? Aliuona ubora mkubwa zaidi wa kujifunza Biblia, wa kutafuta mafundisho yake na ujumbe wake kwa leo. Mwaka wa 1879 aliona uhitaji wa kuchapa gazeti jipya la kidini, Zion’s Watch Tower and Herald of Christ’s Presence (ambalo sasa ni Mnara wa Mlinzi). Baadaye akawa msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Bible and Tract Society. Jina lake alikuwa Charles T. Russell, naye alitoa mali zake zote ziwe za kuhubiri habari njema za Ufalme. Lo! ni mifano bora namna gani tuliyo nayo, ya zamani na ya sasa, ya watu wenye kutanguliza faida za Ufalme katika maisha zao! Je! wewe unafanya maamuzi hayo mema kujiwekea hazina mbinguni?
17, 18. (a) Inawezekanaje tukapata hasara ya kiroho bila kujua? (b) Ni mwendo gani wa Yesu unaotusaidia kufahamu ubora wa kweli wa utajiri wa ulimwengu huu?
17 Namna gani kama mtu angekutolea dola 10,000 (shillingi 80,000 au 5,000Z) uache kumwamini Yehova na uache pendeleo lako la kumtumikia? Je! ungekubali? Namna gani dola 100,000 au 1,000,000 (shilingi 800,000 au 8,000,000)? “Aaah, hilo haliwaziki,” huenda ukasema hivyo. “Hakuna kiasi cha pesa ulimwenguni ambacho kingenifanyiza hilo!” Huo tu ndio uamuzi unaofaa kufanywa, sivyo? Lakini, ni wangapi wamechukua madaraka makubwa zaidi, pengine kazi ya ziada au kufanya kazi jioni “chache” kwa juma au mwishoni mwa juma ndio wapate “kitu kidogo zaidi” au kitu wanachotamani sana! Bila shaka, hiyo inawazuia kuhudhuria mikutano ya kundi inayopangwa kwa kawaida na kuwazuia wasifaidike kutokana na ushirika mwema unaokuwako. Inazuia pia utendaji wao wa kuhubiri na inaharibu maongozi ya roho ya Mungu katika maisha zao. Bila ya wao kujua wanapata hasara ya kiroho, wakiacha kumpenda na kumthamini Yehova na tengenezo lake. Naam, wao ni matajiri zaidi kimwili, lakini maskini zaidi kiroho. Lo! hiyo ni gharama iliyoje inayosababishwa na kutafuta “kitu kidogo zaidi” au mali ya ziada, licha ya kujitahidi sana waipate!
18 Wakati Ibilisi alipompeleka Yesu juu ya mlima mrefu akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari yazo na kumwambia zote zingekuwa zake “ukianguka kunisujudia” tu, Yesu alisema: “Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” (Mt. 4:8-10) Sisi pia na tuthamini ubora wa hazina ya kimbinguni, tukifanya maamuzi yanayotuletea sifa kwa Mungu na kupata kibali yake.
UBORA WA HAZINA YA KIMBINGUNI
19. Ni kwa njia gani ni hekima kutii shauri la Yesu juu ya mali za kimwili?
19 Acheni sikuzote tuthamini hekima ya maneno ya Yesu kwa habari ya mali za kimwili. Alisema zinaharibika, sikuzote zinakuwa katika hatari ya kupotea, kuibwa au kuharibiwa. Kadiri mtu alivyo na zaidi, ndivyo anavyokuwa na wasiwasi zaidi juu yazo. Mara nyingi huo ni mzigo usio wa lazima. Mtu akifikiria mali hizo za kimwili kupita kiasi zinaweza kumfanya yeye pia apoteze “uzima ulio kweli kweli.” (1 Tim. 6:19) Tunao mfano wa karne ya kwanza juu ya jambo hili.
20-22. (a) Yesu alimpa mtawala kijana tajiri shauri gani, naye kijana huyo alionyesha ni kitu gani kilichokuwa cha kwanza katika maisha yake? (b) Ikiwa aliishi mpaka mwaka wa 70 W.K., pengine mtawala kijana huyo alipatwa na nini?
20 Karibu na mwaka wa 33 W.K. Yesu alikuwa anapita katika Jimbo la Peraea, upande wa mashariki wa Mto Yordani. Mtu mmoja, mtawala kijana tajiri, alikuja akipiga mbio kumwelekea Yesu akamwuliza: “Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?” (Mt. 19:16) Yesu akamwambia la kufanya akamshauri asiache mali zake za kimwili zilizo duniani zimzuie asiipate hazina ya milele mbinguni. Yesu alisema hivi: “Enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” (Mt. 19:21) Kwa kuwa alikuwa chini ya Torati alikuwa na wajibu wa kusaidia Waisraeli wenye shida. (Law. 25:35; Kum. 15:7-11; Isa. 58:6, 7; Eze. 18:5, 7-9) Lakini yeye alilithamini shauri hilo la Yesu? Hata! (Mt. 19:22) Ni jambo gani lililompata kijana huyo? Je! aliendelea kufanikiwa akawa na utajiri zaidi? Ikiwa aliishi miaka 37 zaidi mpaka 70 W.K., yalimpata mabadiliko makubwa sana.
21 Kama ilivyotajwa, alikuwa akiishi katika jimbo ambako wengi wa Wayahudi waliofanywa kuwa Wakristo walikimbilia mwaka wa 66 W.K., ili kujiokolea maisha zao na uharibifu wa Yerusalemu, ambao ulikuwa ukikaribia sana. Askari wa Kirumi hawakujiona wenye wajibu wa kushambulia Jimbo la Peraea wakomeshe uasi wa Wayahudi huko. Lakini namna gani juu ya mtawala kijana tajiri huyu aliyekuwa akiishi katika jimbo hilo akiwa na mali zake zote za kidunia? Yeye alikuwa mshika torati ya Musa aliye mwaminifu sana. (Mt. 19:20) Ikiwa aliendelea kuwa hai mpaka mwaka wa 70 W.K. pengine mshika Torati huyo mwaminifu alivuka Mto Yordani akawa upande wa magharibi, akaingia katika Jimbo la Uyahudi na kupanda kwenye mji wa Yerusalemu akaadhimishe kwa Mungu siku kuu ya Kupitwa (Passover) ya kila mwaka.—Kum. 16:1, 2.
22 Akiwamo mjini wakati huo, angenaswa na majeshi ya Kirumi yaliyopazingira Mahali Patakatifu. Kwa hiyo ama angetoweka katika uharibifu wa Yerusalemu au angeokoka achukuliwe mateka na askari wa Kirumi na kupelekwa utumwani mahali fulani katika Milki ya Kirumi. Kwa vyo vyote, ingemlazimu kuacha nyuma kila kitu kilichokuwa juu ya dunia hii, lakini si kwa ajili ya Yesu Kristo, wala akiwa mmoja wa wafuasi wake. Ni upumbavu ulioje kwa upande wa kijana huyo! Lo! ni namna gani kila mmoja wetu anavyohitaji kuwa na sifa nzuri, uhusiano mwema na Mungu huko juu katika mbingu! Nayo sifa nzuri au uhusiano pamoja naye ni jambo lenye kuthaminika zaidi litakalokuwako milele.
23. Hekima ya Mithali 23:4, 5 yawezaje kuonekana?
23 Serikali za dunia hii haziwezi kuhakikisha kabisa kwamba mali zetu za kimwili hazitapoteza thamani baada ya muda fulani, ama kwa kushuka kwa bei za vitu, kupanda kwa bei za vitu, kubadilika kwa thamani ya pesa au kwa kupungukiwa sana na vifaa vya kuuza. Neno la Mungu linatuhakikishia, katika Mithali 23:4, 5: “Usijitaabishe ili kupata utajiri; acha kuzitegemea akili zako mwenyewe. Je! utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, kama tai arukaye mbinguni.”
24. Ni nini kinachoonyesha upumbavu wa kutumainia hazina za kidunia?
24 Hiyo ni kweli namna gani tunapofikiria hali za kiuchumi zilizomo katika kizazi kiki hiki! “Katika Ujeremani mwishoni mwa mwaka 1923 mark za karatasi (pesa za Kijeremani) 1,200,400,000,000 ndizo zilizonunua kitu kilichonunuliwa kwa mark 35 tu miaka miwili tu kabla ya hapo, na katika Hungary mwaka wa 1946 pengo (pesa za Hungary) nonilioni 1.4 ndizo zilizonunua kitu ambacho pengo moja tu ingeweza kununua mwaka wa 1938. (Nonilioni moja ni 1,000,000,000,000,000,000,000,000,000,000.)” (Tazama Money and Economic Activity kilichoandikwa na Houghton Mifflin.) Katika Uruguay, Amerika ya Kusini, gharama za maisha zilipanda kwa karibu persenti 500 mwaka mmoja wa majuzi. Katika nchi ya jirani ya Chile zilipanda kwa persenti 375. Bila shaka tukiweka hazina mbinguni, hazitapungukiwa thamani hivyo na mwishowe ziwe za bure.—Luka 12:33.
25, 26. (a) Kwa sababu ya wakati, imetupasa tuwe tukifuatia mwendo gani? (b) Wakati ujao ukoje kwa wale wanaoweka “hazina mbinguni”?
25 Kwa hiyo, basi, imetupasa leo tufuate shauri la Bwana Yesu Kristo na, badala ya kujishughulisha sana na utafutaji wa utajiri zaidi, tujishughulishe na kazi iliyo ya maana zaidi kupita nyingine za nyakati zote: kuzihubiri habari njema za ufalme na kufanya watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi. (Mt. 28:19, 20; Matendo 1:8) Na tukumbuke kwamba hakuna kiasi cho chote cha utajiri wa kimwili kitakachotupitisha “dhiki kubwa” inayokuja. Ni kama ilivyoandikwa katika Mithali 11:4: “Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; bali haki huokoa na mauti.”
26 Na tuamue kutazama mbinguni na kuutanguliza ufalme wa Mungu na kuuhangaikia kwanza katika maisha zetu. Tukifanya hivyo, tunajihakikishia kupata baraka zisizohesabika, baraka zisizoelezeka, za kimwili na kiroho pia sasa, na pia baada ya Har–Magedoni tupate uzima wa milele katika taratibu mpya ya mambo ya Mungu. Hilo ni jambo lisiloweza kununuliwa na pesa zote ulimwenguni. Je! ndilo jambo unalotamani? Basi ujue kwamba uzima wa milele, amani na furaha katika taratibu mpya yenye haki ya Mungu ikiwa chini ya ufalme wa Kristo ndiyo thawabu ya wote wale wanaoacha leo kujiwekea hazina duniani.—Isa. 9:7; 1 Tim. 6:17-19.