Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w76 11/1 kur. 502-504
  • Ukuu Ni Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ukuu Ni Nini?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Habari Zinazolingana
  • Kusitawisha Maoni ya Kristo Kuhusu Umashuhuri
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Ukuu wa Yehova Hauchunguziki
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Kutumikia kwa Umoja Kama Ushirika wa Ndugu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Iweni Wanafunzi wa Kweli wa Kristo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
w76 11/1 kur. 502-504

Ukuu Ni Nini?

NI NINI hufanya mtu awe mkuu? Wengi hudhani ni umashuhuri, kuweza kuambia wengine jambo la kufanya na kutumikiwa nao. Lakini kuwa na mamlaka nyingi sana ndiko hufanya mtu awe mkuu kwa kweli?

Maoni ya Mungu ya ukuu ni tofauti sana na ya watu wengi. Yesu Kristo, aliyeonyesha kwa ukamilifu nia ya Baba yake juu ya mambo, alieleza hilo waziwazi. Akiwaambia wanafunzi wake, alisema: “Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi vyenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu.” (Mt. 20:25-27) Yesu Kristo aliunga mkono maneno hayo kwa kuweka mfano wa kutumikia. Aliendelea kusema hivi. “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika.” Naam, Yesu hakuja akitafuta kutumikiwa, bali yeye mwenyewe ndiye aliyetumikia, hata akatoa “nafsi yake iwe fidia ya wengi.”​—⁠Mt. 20:28.

Mwana wa Mungu alikuwa wa ajabu kwa kutofikiria sana kuwa na cheo. Kabla hajawa mwanadamu alikuwa na cheo kikubwa zaidi kati ya mamilioni ya wana wa kiroho wa Mungu. Lakini aliacha cheo hicho kwa nia akatumikie wanadamu wenye dhambi. Akikaza fikira juu ya hili, mtume Paulo alitia moyo waamini wenzake hivi: “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.”​—⁠Flp. 2:5-7.

Alipokuwa mwanadamu, Yesu alikuwa “mdogo punde kuliko malaika” na hata hakuwa na ukubwa wa pekee kati ya wananchi wenzake. (Ebr. 2:7) Ingawa walizaliwa katika ukoo wa kifalme wa Daudi, baba yake mlezi wala mama yake Mariamu hawakuwa na mali wala hawakuwa mashuhuri. Alipokuwa akitoa toleo la kutakaswa kwake, Mariamu hakuweza kupata kondoo wa kutolewa dhabihu na kwa hiyo alifuata sheria iliyoruhusu kutoa badala yake “hua wawili au makinda ya njiwa wawili.” (Luka 2:24; Law. 12:8) Yesu alisema hivi wakati mmoja juu ya hali zake mwenyewe: “Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.”​—⁠Mt. 8:20.:

Katika mbingu, Mwana wa Mungu hakuwa amekosa kitu cho chote. Ndiyo sababu mtume Paulo angeweza kuandika kwamba “ingawa alikuwa tajiri akawa maskini.” (2 Kor. 8:9, NW) Yesu alitumikia wengine kwa unyenyekevu, akiwa maskini duniani kwa kulinganishwa na wengine. Aliponya wengi kiroho na kimwili, akafungua macho ya vipofu, akazibua masikio ya viziwi na kuponya waliolemaa. Yesu alifanya kila jambo kwa kuongozwa na upendo.

Biblia yasema kwamba alipokuwa peke yake bila kutaka mtu mwingine karibu, mkutano mkubwa wa watu ukaja, “akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji.” (Marko 6:32-34) Alionyesha wazi nia ile ile ya kujitoa alipokuwa akiponya watu. Alitaka sana kuwafariji wenye kutaabika. Wakati mmoja mtu mwenye ukoma alimwomba sana akisema: “Ukitaka, waweza kunitakasa.” Naye Yesu “akamhurumia, akanyosha mkono wake,” akamwambia, “Nataka, takasika.” (Marko 1:40, 41) Mapozo hayo yalichukua nguvu za Yesu. Maandiko yatuambia kwamba, wakati fulani alipoponya kwa mwujiza, Yesu ‘aliona ya kuwa nguvu zimemtoka.’ (Luka 8:46) Hata hivyo, alikuwa na nia na moyo wa kutumikia wanadamu wenye dhambi kwa njia hiyo.

Mfano wa Yesu Kristo wa kutumikia kwa unyenyekevu ulitia mkazo kwa mafundisho yake juu ya maana ya “ukuu.” Alipokuwa akionyesha wanafunzi wake kwamba hawapaswi kujiongoza kama wafalme wa kilimwengu na wengine wenye kuitwa “Wenye fadhili,” Yesu alielekeza fikira kwenye mfano wake mwenyewe: “Maana aliye mkubwa ni yupi? yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye. Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.”​—⁠Luka 22:25-27.

Ule uitwao “ukuu” wa wenye kutumia mamlaka nyingi sana na kutumikiwa na wengine mara nyingi huongoza kwenye matatizo makubwa. Mtu mwenye cheo cha umashuhuri hujitahidi kuendeleza mamlaka yake kwa kuzuia wengine wasifike aliko. Nao wadogo wake huenda wakaanza kumchukia. Kati ya wenye kujitakia cheo kama hicho cha “ukuu” mnatokea roho ya mashindano kwa kawaida. Hiyo huleta mabishano makali, kijicho na fadhaa. Kwa upande mwingine, mtu anayejitoa bila kufikiria faida zake tu hufanya wengine wampende naye huwa na furaha nyingi.

Naam, ukuu wa kweli hutokana na utumishi wa unyenyekevu, ukiongozwa na kumpenda Mungu na wanadamu wenzetu. Je! hiyo ndiyo namna ya ukuu unayotafuta kwa bidii? Je! umeacha maoni ya ulimwengu ya ukuu, maoni yanayotegemea kuweza kuamuru wengine badala ya kuwa na nia ya kumtumikia Mungu na wanadamu wenzako? Ukuu unaotokana na kutumikia ndio unaofaidi zaidi. Ukuu huo huleta furaha nyingi kwake alio nao na kutia wengine moyo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki