Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w76 10/1 kur. 444-450
  • Ubora Uliojaribiwa wa Imani Yetu Waleta Sifa na Heshima

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ubora Uliojaribiwa wa Imani Yetu Waleta Sifa na Heshima
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • CHUKI KWA MASHAHIDI WAKRISTO
  • SAULI AWA MWANAFUNZI
  • MFANO WA IMANI
  • WAAMINI WENZAO WALETA MABISHANO
  • PAULO HAVUNJWI MOYO NA UPINZANI
  • Fanya Maendeleo ya Kiroho kwa Kufuata Mfano wa Paulo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • “Kujawa na Shangwe na Roho Takatifu”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Watu wa Yehova Waimarishwa Katika Imani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Kitabu Cha Biblia 44—Matendo
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
w76 10/1 kur. 444-450

Ubora Uliojaribiwa wa Imani Yetu Waleta Sifa na Heshima

“Kwa sababu hii mnafurahi sana, ingawa sasa kwa muda mfupi, ikiwa lazima, mmehuzunishwa na majaribu mbalimbali, ili kwamba ubora uliojaribiwa wa imani yenu . . . upate kuonekana waleta sifa na utukufu na heshima katika ufunuo wa Yesu Kristo.”​—1 Pet. 1:6, 7, NW.

1. Toa mifano ya kweli ya mateso yaliyopata waabudu wa Yehova.

KATIKA historia nzima ya wanadamu watu wenye imani wamejaribiwa, wakasumbuliwa na kuteswa na wenye kuwapinga. Ndivyo Habili alivyofanyiwa, aliyeuawa na ndugu yake mwenyewe kwa sababu dhabihu aliyomtolea Mungu ilipendelewa hali ya Kaini haikupendelewa. Ndivyo alivyofanyiwa nabii Myahudi Yeremia, aliyetupwa katika tangi lenye matope kwa sababu ya kulitangaza neno la Mungu wake kwa uaminifu. Ndivyo alivyofanyiwa mwanzishi wa Ukristo, Yesu, kwa sababu alifunua unafiki wa kidini na kwa sababu alikuwa na nia ya kutimiza mapenzi ya Baba yake.

2. Kitabu cha Waebrania kinasimuliaje majaribu ya waaminifu?

2 Majaribu na imani ya wateswa wengi wa namna hiyo, wanaume na wanawake wa zamani zilizopita, yameandikwa kwa ajili yetu katika sura ya kumi na moja ya Waebrania. Watumishi wa Mungu hawa walipaswa kuwa na ushujaa mwingi sana kuweza kuendeleza imani yao walipoteswa kikatili, walipofanyiwa mzaha, wakapigwa mijeledi, wakafungwa pingu na kufungwa gerezani, hata kupigwa kwa mawe au kuuawa kwa upanga! Ni kama vile Paulo, mwanafunzi wa Yesu, alivyoeleza: “Ulimwengu haukustahili kuwa nao.” Hata hivyo wote walikuwa na imani imara, “hakika ya mambo yatarajiwayo,” na vilevile matumaini ya kwamba ‘Mungu alitangulia kuwawekea kitu kilicho bora.’ (Ebr. 11:1, 2, 38, 40) Walitazamia nini kwa hakika hivyo hata wakawa na nia ya kuvumilia jaribu la namna yo yote?

3. Walitazamia nini kwa hakika?

3 Wanaume na wanawake hao waaminifu walikuwa na hakika juu ya ufalme wa kimbinguni, “ufalme usioweza kutetemeshwa,” ufalme wa Mungu wenye haki. Paulo aliwakumbusha Waebrania waamini wa siku zake juu ya wonyesho wa kuogofya wa fahari ya Yehova Mungu katika Mlima Sinai wakati agano la Torati lilipotolewa. Lakini alieleza kwamba kitu chenye fahari zaidi kingekuja, kusimamishwa kwa ufalme wa kimbinguni ambao ungetawala dunia nzima, si Israeli peke yake. “Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na tuwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho.”​—Ebr. 12:18-28.

CHUKI KWA MASHAHIDI WAKRISTO

4. Wakristo wa kwanza walitendewaje?

4 Neno martyr (mfia imani), ambalo asili yake ni Kigiriki, lamaanisha kwa halisi “shahidi,” kwa maana ni mashahidi wengi wa kwanza Wakristo waliovumilia mateso hata wakafia imani, wasiiache. Paulo mwenyewe alihusika katika mambo hayo, kwa maana baadaye ashuhudia hivi: “Mimi nami nalikuwa nikiwafunga gerezani wale [wenye kumwamini Bwana Yesu] na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali na kuzitunza nguo zao waliomwua.”​—Matendo 22:19, 20.

5. Mingine ya mifano mmoja mmoja ya uaminifu ni nini?

5 Mkristo mwingine wa kwanza aliyefia imani alikuwa Yakobo ndugu yake Yohana, ambaye ndiye wa kwanza wa mitume kumi na wawili kufia imani, kwa kuuawa na Herode Agripa I kwa upanga. (Matendo 12:1, 2) Na kama Petro pia asingalilindwa na Yehova, angaliuawa na Herode. (Matendo 12:11) Jitihada zilifanywa pia mara nyingi kumwua mtume Paulo. (Matendo 22:22) Kuelekea mwisho wa karne ya kwanza mtume Yohana mzee aliandika habari za Mkristo mwingine aliyekufa kwa uaminifu: “Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu.”​—Ufu. 2:13.

6. (a) Yesu alisema nini juu ya wapinzani wake? (b) Kwa sababu gani hawakuwa na udhuru wa upinzani wao?

6 Kwa sababu gani wanafunzi wa kwanza wa Yesu walipingwa sana? Kwa sababu gani viongozi wa watu walifikia hatua za kushawishi watu watoe ushuhuda wa uongo hata Stefano akauawa? Yesu alikuwa amekwisha ambia wengine wa wapinzani wa kidini bila kuwaficha hivi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli.” (Yohana 8:44) Kwa hiyo sababu haikuwa kwamba hawakujua ukweli juu ya mafundisho ya Yesu au usahihi wa ushuhuda wa Stefano. Hakika walijua ushuhuda wa Petro juu ya kumiminwa kwa roho ya Mungu wakati wa Pentekoste tena walikuwa wameona au walikuwa wamepata habari za zawadi ya kusema kwa lugha nyingi iliyoonyesha Wakristo hao walikuwa watu wa Mungu. “Watu wapata elfu tatu” walibatizwa wakati huo, na baadaye hata “jamii kubwa ya makuhani” iliukubali ujumbe. Lakini chuki ya kidini juu ya wale waliofuata “Njia hii” iliwaka kama moto. (Matendo 2:41; 6:7; 9:2) Bila shaka wakuu wa makuhani waliyakumbuka sana maneno ya Yesu ya kuwalaani. (Mathayo sura ya 23) Kwa hiyo upinzani wao juu ya Wakristo hawa wa kwanza uliwaonyesha kuwa waliupinga utendaji wa roho ya Mungu.

SAULI AWA MWANAFUNZI

7. Maisha ya kwanza ya Paulo yalikuwaje kabla hajawa Mkristo?

7 Lakini si wote waliotenda hivyo. Sauli (aliyepata kujulikana kwa jina lake la Kirumi Paulo) alikuwa mmoja wa waliofanya mabadiliko makubwa maishani mwao. (Matendo 13:9) Ingawa alilelewa chini ya agano la Torati akiwa na maoni ya Mafarisayo, aliacha cheo chake cha heshima katika imani ya Kiyahudi akashiriki kutesa vikali Wakristo wa kwanza. (Flp. 3:5, 6) Alijua sana matokeo ya badiliko hilo, lakini hakusita-sita aliposadikishwa yaliyofaa. Huo ulikuwa wakati wa mateso makali juu ya kundi la Kikristo. Sauli mwenyewe alikuwa amekuwa akitenda kwa hasira kuu juu ya Wakristo wa kwanza, akiingilia nyumba baada ya nyumba, na kuburuta wanaume na wanawake wakatiwe gerezani. (Matendo 8:1-3) Alipokuwa akielekea Dameski na barua za kuhani mkuu zenye kumruhusu aende akalete Yerusalemu wakiwa wafungwa wo wote waliopatikana wakidai kuwa Wakristo, wanaume au wanawake, ndipo tukio lilipotukia likabadili sana maisha yake.​—Matendo 9:1, 2.

8. Paulo (au Sauli) alipatwa na nini ndiyo akajifunza kweli, naye aliitikiaje?

8 Kwa ghafula aliduwazwa na nuru ya kimbinguni. “Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.” Akiwa amepofushwa bado na nuru ile, Sauli aliongozwa mpaka Dameski. Baada ya siku tatu mwanafunzi jina lake Anania aliagizwa aende akamsaidie. Baada ya kuhakikishiwa kwamba yalikuwa mapenzi ya Bwana akamsaidie, Anania alimwambia: “Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe [roho takatifu].” Wewe ungaliitikiaje? Ungaliona ni vigumu kubadilika, ukijua kwamba pengine ungeteswa na kupatwa na magumu mwenyewe? Sauli hakutia mashaka akilini, kwa maana twasoma: “Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.”​—Matendo 9:3-5, 17, 20.

MFANO WA IMANI

9. (a) Ni kwa njia gani mambo yaliyompata Sauli yanatia moyo Wakristo wa kisasa? (b) Ni kwa njia gani alikuwa karibu kuuawa Dameski alipoanza kumhubiri Kristo?

9 Tunapofikiria mfano wa Sauli wa imani, uvumilivu wake chini ya majaribu, na uongozi na ulinzi ambao Yehova alimpa, twatiwa moyo tushinde majaribu yanayopata Wakristo wa kweli katika kizazi hiki. Hata alipojua angepingwa kama Wakristo wengine wa siku hizo, Sauli hakurudi nyuma ijapokuwa Bwana alikuwa amemwambia Anania hivi: “Nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.” Baada ya kukaa siku chache akiwa na wanafunzi Dameski, Sauli alianza kuhubiri kwa juhudi. Muda si muda Wayahudi walipanga wamwue wakaanza kumnyemelea penye malango ya mji mchana na usiku. Lakini Yehova asingekubali “chombo kiteule” chake kisukumiwe kando kwa vyepesi hivyo. (Matendo 9:15, 16) Sauli alijulishwa mpango huo, wanafunzi wake wakamsaidia aukimbie mtego huo, wakamshusha kapuni katika nafasi iliyokuwa ukutani. Huo ulikuwa mwanzo tu wa maisha yenye wasiwasi katika kazi ya kuhubiri ya huyu aliyekuwa mtesi wa Wakristo hapo kwanza.

10. Yaliyotukia kati ya Sauli na Elima yaonyeshaje mashetani walileta upinzani?

10 Sauli na Barnaba walichaguliwa kwa njia ya pekee na roho takatifu watimize kazi ya kulitangaza neno la Mungu kwa Wayahudi na vilevile kwa wasiokuwa Wayahudi. Katika safari yao ya kwanza ya umisionari walikuta mtu aliyesimuliwa kuwa nabii wa uongo na mlozi aliyekuwa na gavana Sergio Paulo. Wakati Elima mlozi alipoanza kuwapinga Sauli na Barnaba, akijaribu kumfanya gavana asiusikilize ujumbe wao, Sauli (ambaye wakati huo alikuwa Paulo) akiwa amejawa na roho takatifu, alimwuliza: “Huachi kuzipotoa njia za [Yehova] zilizonyoka?” Mara hiyo mlozi huyo akapofuka kwa muda. Kwa sababu hiyo, gavana mwenye kushangaa sana aliamini mambo aliyoona na kusikia.​—Matendo 13:6-12.

11. (a) Ni kwa sababu gani na kwa msingi gani wa Maandiko Paulo na Barnaba waliwahubiri Mataifa Antiokia na Ikonio? (b) Walifanya nini baada ya kufukuzwa katika miji hiyo?

11 Paulo na Barnaba walisonga mbele wakafika Antiokia ya Pisidia, ambako walitolea watu wa mji ushuhuda wa ujasiri. Wayahudi walipokasirikia sana kuhubiri kwao kuhusu ufufuo, watu hao wawili walielekea watu wa mataifa, wakitaja maneno ya unabii wa Isaya: “Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.” (Matendo 13:47) Na wakati Mataifa waliokuwa na nia ya haki walipoanza kufurahia hilo, Wayahudi walifukuza Paulo na Barnaba mjini. Hata hivyo waliendelea kusonga mbele wamejawa na furaha na roho takatifu. Katika kituo chao kilichofuata, katika Ikonio, walipatwa na ayo hayo. Kwa sababu ya kuhubiri kwao, umati mkubwa wa Wayahudi na Wagiriki wakawa waamini, lakini wasioukubali ujumbe walichochea watu, hata Wayahudi na Mataifa pia wakakaza nia wawatende jeuri, hata wakalazimika kukimbilia kwingine wakaendelee kuzihubiri habari njema.

12, 13. (a) Paulo alipatwa na nini Listra? (b) Paulo alionyeshaje alimtumaini Yehova?

12 Katika Listra, watu walidhani hao wawili walikuwa miungu, baada ya Paulo kuponya mtu aliyekuwa kilema tangu kuzaliwa. Wakamwita Barnaba Zeu, na Paulo wakamwita Herme, kwa maana ndiye aliyekuwa akiongoza katika kunena. Walakini, Paulo na Barnaba waliwazuia, wakasema: “Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema.” (Matendo 14:15) Karibu na wakati huo Wayahudi wa Antiokia na Ikonio waliokuwa bado wakimfuatia Paulo walifika, nao walipomwona, walimpiga kwa mawe wakamburuta nje ya mji, wakidhani amekufa. Lakini kwa fadhili zisizostahilika za Yehova Paulo aliokoka, kesho yake akaondoka na Barnaba waelekee Derbe, ambako aliendelea kuhubiri akafanya wanafunzi kadha.

13 Pengine unawaza, ‘Baada ya kutendwa hayo yote mimi ningaliacha nisiuawe.’ Lakini Paulo hakuwaza hivyo. Kwa kweli, masimulizi katika Matendo 14:21 yasema Paulo na Barnaba walirudi Listra na Ikonio na Antiokia, ambako walikuwa wamepingwa sana, kwa maana walitaka kuwatia wanafunzi nguvu na moyo. Waliwakumbusha, “Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.” Kwa hiyo waliendelea na kazi yao ya kujenga makundi na kutia nguvu wale waliomwamini Yehova.​—Matendo 14:22.

WAAMINI WENZAO WALETA MABISHANO

14. Wengine walitokeza ubishi gani, nao ulimalizwaje?

14 Linalosikitisha ni kwamba, si wapinzani waliowatatiza peke yao, bali hata waamini wenzao walileta mabishano, kwa mfano wakidai kwamba Mataifa wasingeweza kuokolewa wasipotahiriwa kulingana na desturi ya Musa. (Matendo 15:1, 2) Baada ya mabishano mengi juu ya jambo hilo, iliamuliwa Paulo na Barnaba na wengine wapelekee mitume na wanaume wazee wa kundi kuu la Yerusalemu shauri hilo. Waliposikia ushuhuda wao na wa Petro na wengine, waliamuaje? Ili wasitatize watu wa mataifa waliokuwa wakimgeukia Mungu isipokuwa kwa mambo ya lazima, waliamua wajiepushe na vitu vilivyotiwa unajisi na sanamu na uasherati na damu.​—Matendo 15:12-20.

15. Paulo alimsahihisha Petro kwa sababu ya hali gani?

15 Paulo alisimamia kweli kwa imara. Anapoeleza habari za ziara yake Yerusalemu, asema kwamba ‘ndugu za uongo walipoingia kwa siri,’ “hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi.” Katika Antiokia, wakati hata Petro alipojisingizia kwa kukataa kula au kushirikiana na ndugu zake wa Mataifa ili asiudhi Wakristo fulani Wayahudi waliomtembelea, Paulo alishindana “naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu.” Aliwaeleza Wagalatia hivi: “Siibatili neema ya Mungu; maana, ikiwa haki hupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure.” (Gal. 2:4, 5, 11, 21) Hiyo iliwasaidia Wagalatia wafahamu kwamba Wakristo wanatangazwa haki kwa imani katika Kristo, si kwa kujipatanisha na matendo ya sheria ya Musa. Agano la Torati lilikuwa limeondolewa, na sasa agano jipya lilikuwa likifanya kazi. Ingawa wengine walikuwa wakawivu wa kufahamu hilo, Paulo hakuvunjika moyo kwa sababu walionyesha mawazo ya kibinadamu.

PAULO HAVUNJWI MOYO NA UPINZANI

16. Majaribu ya Paulo na Sila katika Filipi yalipataje kuwa baraka?

16 Katika Filipi, alipokuwa katika safari yake ya pili ya umisionari, Paulo alifurahia kuletea mwanamke mfanya biashara jina lake Lidia kweli, ambaye alifungua wazi moyo wake asikie mambo yaliyonenwa na Paulo na kuonyesha ukaribishaji mwingi kwa ndugu hawa. Hapa Filipi pia, Paulo alipatwa na magumu, wakati huu kutoka kwa wenyeji wa kijakazi mmoja aliyekuwa na uwezo wa kuagua. Kila siku alikuwa akipaza sauti kusema, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.” (Matendo 16:17) Mwishowe Paulo alichoshwa na jambo hilo akaliagiza shetani hilo limwache msichana kwa jina la Yesu. Wenyeji wake waliokuwa wamefaidiwa na matabiri yake walipoona amepoteza uwezo huo usio wa kibinadamu, walipeleka Paulo na Sila kwa mahakimu wakapigwa na kutiwa gerezani. Tena hayo yalitosha kuvunja wengi moyo, kwanza kupigwa kisha kutupwa jelani, lakini Paulo na Sila hawakuvunjika moyo. Masimulizi yatueleza kwamba usiku wa manane, walipokuwa wakisali na kumsifu Mungu kwa wimbo, tetemeko la nchi lilitukia kwa ghafula, likafungua wazi milango ya jela na kuwafungua wafungwa. Badala ya kujaribu kukimbia, Paulo alibaki amwondolee mtunza gereza mashaka, ambaye alikaribia kujiua, akapata nafasi ya kumweleza neno la Yehova pamoja na jamaa yake. Kwa hiyo, walibatizwa usiku uo huo.

17. Paulo aliyaonaje majaribu yake, na aliendelea kuwa na nia gani?

17 Ijapokuwa mambo yalitokea ya namna zote, Paulo hakuvunjika moyo. Aliendelea kuwa na nia inayofaa. Ni kama vile alivyowaandikia ndugu zake Wakorintho: “Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi.” (1 Kor. 4:12, 13) Angeweza kuona ukweli wa maneno ya Yesu: “Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi.” (Yohana 15:20) Paulo aliliona kuwa pendeleo kupatwa na majaribu kwa ajili ya habari njema.​—Flp. 1:27-30.

18. Mfua fedha alipingaje mahubiri ya Paulo, lakini mwishowe kulitokea nini?

18 Katika safari yake ya tatu ya umisionari, Paulo alipingwa tena, wakati huu kutokana na mafundi wa vihekalu. Demetrio, mfua fedha aliyefaidika kwa kufanya vihekalu vya mungu-mke Artemi, alionya watu kwamba Paulo alikuwa akifundisha kwamba miungu iliyofanywa kwa mikono si miungu na kwamba karibuni kazi ya wafanya vihekalu ingekuwa na sifa mbaya. Mji ulijaa ghasia kwa sababu hiyo, naye karani wa mji aliwatuliza watu kwa shida nyingi akawatawanya. (Matendo 19:23-41) Naam, maisha ya Paulo yalitishwa imani yake ikajaribiwa mara kwa mara.​—2 Kor. 4:7-12; 6:3-10; 11:23-27.

19. Paulo alipewa onyo gani, lakini sababu gani hakulegezwa na tumaini la kufa?

19 Mwishowe, Paulo alipokuwa Kaisaria, nabii Agabo alimwonya kwamba angefungwa Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa watu wa mataifa. Paulo angefanyaje? Je! angekimbilia kwingine? Sivyo, kwa maana alisema: “Licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.” (Matendo 21:10-13) Aliona kwamba, hata apatwe na jambo gani, alikuwa amekuwa mwaminifu katika mgawo wake wa utumishi na kwamba hakuwa na “hatia kwa damu ya mtu awaye yote.”​—Matendo 20:26.

20. Paulo alipata pendeleo la kumtolea nani ushuhuda, naye aliutumiaje wakati wa kifungo chake?

20 Kama ilivyotabiriwa, Paulo alishtakiwa kwa uongo Yerusalemu hekaluni akaburutwa nje. Aliokolewa asife na amiri-jeshi Mrumi aliyejiingiza upesi katika mambo hayo. Baada ya hapo Paulo alipata pendeleo la kujitetea mbele ya mahakma kuu zaidi ya Kiyahudi iliyoitwa Sanhedrin. Lakini hapa, pia, fitina ilitokea juu ya ujumbe aliounena. Usiku huo malaika alisimama kando yake akamwambia awe na ushujaa mwingi. Angetoa ushuhuda kamili Rumi kama vile alivyokuwa ameutoa Yerusalemu. (Matendo 23:11) Baada ya hapo kesi ya Paulo ilisikiwa na Gavana Feliki, kisha na mrithi wake, Porkio Festo, na mwishowe na Mfalme Agripa II, kabla hajapelekwa Rumi. Alikaa kifungoni miaka miwili akingojea kesi, akihubiri wote waliokuja kumtembelea. Yaelekea alitangazwa hana hatia akafunguliwa na Kaisari Nero.​—2 Tim. 4:16, 17.

21, 22. (a) Tuna ushuhuda gani kwamba Paulo alitazamia kufa baada ya kifungo chake cha pili? (b) Kwa sababu gani Paulo alikuwa na imani yenye nguvu hivyo?

21 Walakini, Paulo alifungwa tena Rumi karibu na mwaka wa 65 W.K. Wakati wa kifungo hiki ndipo alipoandika barua yake ya pili kwa Timotheo akaonyesha kwamba kifo chake kilikaribia. (2 Tim. 4:6-8) Yaelekea aliuawa kwa sababu ya imani na Nero mwaka wa 66 W.K.

22 Hakukuwa na shaka kwamba ubora wa imani ya Paulo ulijaribiwa. Alikuwa na sababu nzuri ya kuwa na imani. Si kwamba alikuwa ameitwa kwa mwujiza tu, bali pia alikuwa ameona mara nyingi utendaji wa roho ya Mungu katika mambo aliyopendelewa kufanya na pia malaika walipokuja kumsaidia. Ijapokuwa alichukiwa sana na mashetani na wanadamu pia, hakuacha imani yake itikisike wala hakuondoshwa katika kazi aliyokuwa ameitiwa. Alimtumaini Bwana na ufufuo.​—1 Kor. 15:14, 21, 22.

23. Twajuaje kwamba Paulo hakuona haya juu ya mwendo wake wa maisha?

23 Paulo hakuona haya juu ya mwendo wake wa maisha. Kama alivyomwambia Mfalme Agripa: “Namwomba Mungu kwamba . . . si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.” (Matendo 26:28, 29; Rum. 1:16) Ijapokuwa alipatwa na majaribu, alitia wengine moyo wafuate mwendo ule ule. Aliandikia ndugu wa Korintho akawaambia: “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.” (1 Kor. 11:1) Yeye hakuwa mtu wa kwenda kutafuta-tafuta ugomvi wala wa kupendezwa na magumu au kufia imani ajipatie utukufu. Hata hivyo alisimamia kweli kwa imara. Alipowaandikia Wathesalonike, alifurahi kwamba habari njema hazikuwafikia katika maneno tu, “bali na katika nguvu, na katika [roho takatifu], na uthibitifu mwingi . . . nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya [roho takatifu].”​—1 The. 1:5, 6.

24. Twapata baraka gani kwa kuonyesha imani kama ya Paulo?

24 Ni wachache kati yetu watakaopatwa na majaribu yote yaliyompata Paulo. Hata hivyo tunaweza sote kuonyesha imani kama yake. Tunaweza kuyakumbuka maneno yake kwa Waebrania yenye kutia moyo: “Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa [nafsi] zetu.” (Ebr. 10:38, 39) Tukijua kwamba ubora uliojaribiwa wa imani yetu waleta uvumilivu, yatupasa tumwige Paulo kama alivyomwiga Kristo Yesu. Tukivumilia kwa uaminifu hata tunapopatwa na majaribu, twajua kwamba ubora uliojaribiwa na wenye kudumu wa imani yetu pia ‘utaleta sifa na utukufu na heshima katika ufunuo wa Yesu Kristo.’​—1 Pet. 1:5-7, 9; Yak. 1:2, 3.

[Picha katika ukurasa wa 446]

Sauli wa Tarso ‘hakuyaasi yale maono ya mbinguni,’ bali akawa mwanafunzi wa Yesu na mfano wa imani na uvumilivu.​—Matendo 26:19.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki