Kitabu Cha Biblia 44—Matendo
Mwandikaji: Luka
Mahali Kilipoandikiwa: Rumi
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 61 W.K.
Wakati Uliohusishwa: 33–c. (karibu) 61 W.K.
1, 2. (a) Ni matukio na utendaji gani mbalimbali wa kihistoria unaosimuliwa katika Matendo? (b) Kitabu hiki chahusu kipindi gani cha wakati?
KATIKA kitabu cha 42 cha Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu, Luka atoa simulizi linalohusu maisha, utendaji, na huduma ya Yesu na wafuasi wake mpaka wakati wa kupaa kwa Yesu. Maandishi ya kihistoria ya kitabu cha 44 cha Maandiko, Matendo ya Mitume, yaendeleza historia ya Ukristo wa mapema kwa kueleza kuanzishwa kwa kundi likiwa ni tokeo la utendaji wa roho takatifu. Pia yaeleza upanuzi wa ushahidi, kwanza miongoni mwa Wayahudi na kisha kwa watu wa mataifa yote. Sehemu kubwa zaidi ya habari katika sura 12 za kwanza yahusu utendaji mbalimbali wa Petro, na zile sura 16 zinazosalia, utendaji mbalimbali wa Paulo. Luka alikuwa na ushirika wa kindani pamoja na Paulo, akiambatana naye katika nyingi za safari zake.
2 Kitabu hicho kimeelekezwa kwa Theofilo. Kwa kuwa arejezewa kuwa “mtukufu,” yawezekana kwamba yeye alikuwa na cheo fulani rasmi, au yaweza kuwa ni uneni tu wa staha kubwa. (Luka 1:3) Simulizi hilo latoa maandishi sahihi ya kihistoria ya kusimamishwa na ukuzi wa kundi la Kikristo. Yaanza kwa mionekano ya Yesu kwa wanafunzi wake kufuatia ufufuo wake na kisha yaandika matukio ya maana ya kipindi cha kutoka 33 mpaka karibu 61 W.K., yakihusisha miaka kama 28 kwa ujumla.
3. Ni nani aliyeandika kitabu cha Matendo, na uandikaji ulikamilishwa lini?
3 Tangu nyakati za kale mwandikaji wa Gospeli ya Luka amehesabiwa uandikaji wa Matendo. Vitabu vyote viwili vyaelekezewa Theofilo. Kwa kurudia matukio ya kumalizia ya Gospeli yake katika mistari ya ufunguzi ya Matendo, Luka aunganisha masimulizi hayo mawili kuwa kazi ya mtungaji yule yule. Yaonekana kwamba Luka alikamilisha Matendo karibu 61 W.K., yawezekana kuelekea umalizio wa ukaaji wa miaka miwili katika Rumi alipokuwa pamoja na mtume Paulo. Kwa kuwa chaandika matukio mpaka mwaka huo, haiwezekani kikawa kilikamilika mapema zaidi, na kuwacha kwacho rufani ya Paulo kwa Kaisari ikiwa yangojewa kwaonyesha kwamba kilikamilika mwaka huo.
4. Ni nini kinachothibitisha kwamba Matendo ni chenye kukubalika na ni asilia?
4 Tangu nyakati za kale zaidi, Matendo kimeonwa na wanachuo wa Biblia kuwa chenye kukubalika. Sehemu za kitabu hicho zapatikana miongoni mwa hati-mkono za kale zaidi za mafunjo ya Maandiko ya Kigiriki zilizopo leo, hasa Michigan No. 1571 (P38) ya karne ya tatu au nne W.K. na Chester Beatty No. 1 (P45) ya karne ya tatu. Zote mbili zadokeza kwamba Matendo kilikuwa chazunguka pamoja na vile vitabu vingine vya Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu na kwa hiyo kilikuwa sehemu ya orodha katika tarehe ya mapema. Uandikaji wa Luka katika kitabu cha Matendo waonyesha usahihi ule ule wa kutokeza kama ambavyo tumekwisha kuona watia alama Gospeli yake. Sir William M. Ramsay akadiria mwandikaji wa Matendo kuwa “miongoni mwa wanahistoria wa daraja la kwanza,” naye aeleza maana ya hilo kwa kusema: “Sifa ya kwanza na ya muhimu ya mwanahistoria mkubwa huyo ni ukweli. Yale anayosema hakuna shaka ni yenye kutegemeka.”a
5. Toa kielezi cha kuripoti kwa usahihi kwa Luka.
5 Katika kutoa kielezi cha kuripoti kwa usahihi ambako kwatambulisha maandishi ya Luka, twanukuu Edwin Smith, kamanda wa kikosi cha merikebu za vita za Uingereza katika Mediterranea wakati wa Vita ya Ulimwengu 1, akiandika katika jarida The Rudder, Machi 1947: “Vyombo vya kale havikuendeshwa kama vile vya nyakati za kisasa kwa usukani mmoja ulioangikwa kwenye mlingoti wa shetri, bali kwa makafi au makasia mawili makubwa, moja kila upande wa omo; ndiyo sababu Mt. Luka ataja mengi. [Mdo. 27:40] . . . Tumeona katika uchunguzi wetu kwamba kila taarifa juu ya miendo ya merikebu hii, tangu wakati ilipotoka Bandari Nzuri mpaka ilipotia nanga kule Melita, kama ilivyoandikwa na Mt. Luka imehakikishwa na uthibitisho wa nje na ulio tofauti ulio kamili kabisa na wenye kuridhisha; na kwamba taarifa zake juu ya wakati ambao merikebu ilibaki baharini zakubaliana na umbali ulioendwa; na hatimaye maelezo yake juu ya mahali palipowasiliwa yapatana na mahali hapo kama palipo. Yote hayo yaonyesha kwamba Luka alifunga safari hiyo kihalisi kama inavyoelezwa, na zaidi amejionyesha kuwa mtu ambaye maono na taarifa zake zaweza kuonwa kuwa za kutegemeka na kutumainika kwa kiwango cha juu zaidi.”b
6. Ni vielelezo gani vinavyoonyesha jinsi magunduzi ya kiakiolojia yanavyothibitisha usahihi wa Matendo?
6 Magunduzi ya kiakiolojia pia yathibitisha usahihi wa simulizi la Luka. Kwa kielelezi, machimbuzi kule Efeso yamefukua hekalu la Artemi na pia uwanja wa maonyesho wa kale ambako Waefeso walimfanyia mtume Paulo ghasia. (Mdo. 19:27-41) Nakshi zimegunduliwa zinazothibitisha usahihi wa matumizi ya Luka ya taji “wakubwa wa mji” kuhusu maofisa wa Thesalonika. (17:6, 8) Nakshi mbili za Kimelita zaonyesha kwamba Luka alikuwa sahihi pia katika kurejezea Publio kuwa “mkuu,” NW, wa Melita.—28:7.c
7. Uneni ulioandikwa waonyeshaje kumbukumbu ya Matendo kuwa ya hakika?
7 Zaidi ya hayo, hotuba mbalimbali zilizotolewa na Petro, Stefano, Kornelio, Tertulo, Paulo na wengine, kama zilivyoandikwa na Luka, zote ni tofauti katika mtindo na mtungo. Hata hotuba za Paulo, zilizotolewa mbele ya wasikilizaji tofauti-tofauti, zilibadilika katika mtindo ili kufaana na pindi hiyo. Hilo laonyesha kwamba Luka aliandika yale ambayo tu alisikia au yale ambayo mashahidi wengine waliojionea waliripoti kwake. Luka hakuwa mwandikaji wa kubuni hadithi.
8. Maandiko yatuambia nini juu ya Luka na ushirika wake na Paulo?
8 Ni machache sana yanayojulikana juu ya uhai wa kibinafsi wa Luka. Luka mwenyewe hakuwa mtume bali alishirikiana na wale waliokuwa. (Luka 1:1-4) Pindi tatu mtume Paulo amtaja Luka kwa jina. (Kol. 4:10, 14; 2 Tim. 4:11; Flm. 24) Kwa miaka kadhaa alikuwa mwandamani mwaminifu wa Paulo, ambaye akamwita “tabibu mpendwa.” Kuna badiliko-badiliko katika simulizi hilo kati ya “waka-” na “tuka-,” kuonyesha kwamba Luka alikuwa na Paulo kule Troa wakati wa safari ya pili ya umisionari ya Paulo, kwamba yaweza kuwa alibaki kule Filipi mpaka Paulo aliporejea miaka kadhaa baadaye, na kwamba kisha alijiunga tena na Paulo na kuandamana naye kwenye safari yake ya kwenda Rumi kwa ajili ya kujaribiwa mahakamani.—Mdo. 16:8, 10; 17:1; 20:4-6; 28:16.
YALIYOMO KATIKA MATENDO
9. Wanafunzi waambiwa mambo gani wakati wa kupaa kwa Yesu?
9 Matukio mpaka Pentekoste (1:1-26). Luka afunguapo simulizi lake la pili, Yesu aliyefufuliwa aeleza wanafunzi wake wenye hamu kwamba watabatizwa katika roho takatifu. Je! Ufalme wa Mungu utarudishwa wakati huu? La. Lakini wao watapokea nguvu na kuwa mashahidi “hata mwisho wa nchi [dunia, NW].” Yesu anapoinuliwa juu na waachapo kumwona, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wawaambia hivi: “Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo.”—1:8, 11.
10. (a) Ni mambo gani ya kukumbukwa yanayotukia siku ya Pentekoste? (b) Petro atoa maelezo gani, na matokeo yalo ni nini?
10 Siku ya kukumbukwa ya Pentekoste (2:1-42). Wanafunzi wote wamekusanyika katika Yerusalemu. Ghafula kelele kama ya upepo unaopita haraka yajaza nyumba hiyo. Ndimi kama kwamba za moto zakalia wale waliopo. Wajazwa kwa roho takatifu na kuanza kunena katika lugha tofauti-tofauti juu ya “matendo makuu ya Mungu.” (2:11) Watazamaji wababaika. Sasa Petro asimama na kunena. Aeleza kwamba umwagaji huu wa roho takatifu ni kwa utimizo wa unabii wa Yoeli (2:28-32) na kwamba Yesu Kristo, aliyekwisha fufuliwa na kutukuzwa kwenye mkono wa kulia wa Mungu, ‘amekimwaga kitu hiki wanachokiona na kukisikia.’ Kwa kuchomwa moyoni, karibu 3,000 walikubali neno na kubatizwa.—2:33.
11. Yehova afanikishaje kazi ya kuhubiri?
11 Ushahidi wapanuka (2:43–5:42). Kila siku, Yehova aendelea kuwaunganisha na wale wanaookolewa. Nje ya hekalu Petro na Yohana wamkuta mtu aliyepooza ambaye hajapata kamwe kutembea maishani mwake. “Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende” aamuru Petro. Mara moja mtu huyo aanza ‘kuenda, akirukaruka, na kumsifu Mungu.’ Kisha Petro awasihi watu watubu na kugeuka, “zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana [Yehova, NW].’ Kwa kuudhiwa kwamba Petro na Yohana wanafundisha ufufuo wa Yesu, viongozi wa kidini wawakamata, lakini hesabu za waamini zaongezeka mno kufikia karibu wanaume 5,000.—3:6, 8, 19.
12. (a) Wanafunzi watoa jibu gani wanapoamriwa waache kuhubiri? (b) Anania na Safira waadhibiwa kwa ajili ya nini?
12 Siku inayofuata, Petro na Yohana wapelekwa mbele ya watawala wa Kiyahudi wakaulizwe maswali. Petro ashuhudia kwa kusema wazi kwamba wokovu ni kupitia tu kwa Yesu Kristo, na wanapoamriwa waache kazi ya kuhubiri, Petro na Yohana wajibu: “Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” (4:19, 20) Wao waachiliwa, na wanafunzi wote waendelea kunena neno la Mungu kwa ujasiri. Kwa sababu ya hali, wakusanya mali zao za kimwili pamoja na kufanya ugawanyaji kwa kulingana na uhitaji. Hata hivyo, Anania fulani na mke wake, Safira, wauza sehemu fulani ya mali yao na kisiri-siri waweka sehemu ya bei huku wakitoa wazo la kupeana hesabu yote. Petro awafichua, nao waanguka na kufa kwa sababu wamefanya ubandia kwa Mungu na roho takatifu.
13. Mitume washtakiwa nini, na wajibuje, nao waendelea kufanya nini?
13 Kwa mara nyingine viongozi wa kidini waliofoka kwa hasira wawatupa mitume ndani ya gereza, lakini safari hii malaika wa Yehova awafungua. Siku ifuatayo kwa mara nyingine waletwa mbele ya Sanhedrini na kushtakiwa kwa ‘kujaza Yerusalemu mafundisho yao.’ Wao wajibu: “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Wajapopigwa mijeledi na kutishwa, bado wakataa kuacha, na ‘kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao [nyumba kwa nyumba, NW], hawaachi kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo.’—5:28, 29, 42.
14. Stefano afikiaje kufia imani?
14 Kufia imani kwa Stefano (6:1–8:1a). Stefano ni mmoja wa wale saba wanaowekwa na roho takatifu wagawanye chakula mezani. Pia yeye atolea kweli ushahidi wenye nguvu, naye ategemeza imani kwa bidii sana hivi kwamba wapinzani wake wenye ghadhabu wamleta mbele ya Sanhedrini juu ya shtaka la kufuru. Katika kujitetea, Stefano aeleza kwanza juu ya ustahimilivu wa Yehova kuelekea Israeli. Kisha, kwa ufasaha usio na hofu, ataja hivi: ‘Enyi wenye shingo ngumu, sikuzote mnapinga roho takatifu, ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.’ (7:51-53) Kwao maneno hayo yamepita cheo. Wamrukia, wamtupa nje ya jiji, na kumpiga kwa mawe hata akafa. Saulo atazama kwa kukubali.
15. Ni nini matokeo ya mnyanyaso, na Filipo ajionea nini katika kuhubiri?
15 Minyanyaso, kuongoka kwa Paulo (8:1b–9:30). Mnyanyaso unaoanza siku hiyo juu ya kundi katika Yerusalemu watawanya wote katika bara isipokuwa mitume. Filipo aenda Samaria, ambako wengi wakubali neno la Mungu. Petro na Yohana wapelekwa huko kutoka Yerusalemu ili waamini hawa wapokee roho takatifu “kwa kuwekewa mikono ya mitume.” (8:18) Kisha malaika aelekeza Filipo kusini kwenye barabara ya Yerusalemu-Gaza, ambako akuta towashi wa baraza la kifalme la Ethiopia (Kushi) akiwa amepanda kigari-farasi chake na akisoma kitabu cha Isaya. Filipo amwelimisha juu ya maana ya unabii huo na kumbatiza.
16. Kuongolewa kwa Sauli kwatukiaje?
16 Wakati ule ule, Sauli, “akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana,” aondoka akakamate wale walio wa “Njia hii” katika Dameski. Ghafula nuru kutoka mbinguni yamulika kumzunguka, naye aanguka kwenye ardhi amepofuka. Sauti kutoka mbinguni yamwambia: “Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.” Baada ya siku tatu katika Dameski, mwanafunzi mmoja jina lake Anania amhudumia. Sauli apata kuona tena, abatizwa, na kujazwa roho takatifu, hivi kwamba awa mhubiri mwenye bidii na mwenye uweza wa habari njema. (9:1, 2, 5) Katika badiliko hilo la matukio lenye kustaajabisha, mnyanyasaji awa mnyanyaswa na alazimika kukimbiza uhai wake, kwanza kutoka Dameski na kisha kutoka Yerusalemu.
17. Habari njema zawaendeaje watu wasiotahiriwa ambao si Wayahudi?
17 Habari njema zaenda kwa wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa (9:31–12:25). Sasa kundi ‘lapata raha, likijengwa; likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Yehova na faraja ya roho takatifu.’ (9:31) Kule Yafa, Petro ainua Tabitha (Dorkasi) mpendwa kutoka kwa wafu, na akiwa hapa ndipo apokea wito wa kwenda Kaisaria, ambako ofisa mmoja wa jeshi jina lake Kornelio amngojea. Yeye ahubiri kwa Kornelio na nyumba yake nao waamini, na roho takatifu yamwagwa juu yao. Akiisha fahamu “kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Petro awabatiza—waongofu wa kwanza wasiotahiriwa ambao si Wayahudi. Baadaye Petro aeleza tukio jipya hilo kwa ndugu katika Yerusalemu, nao kisha wamtukuza Mungu.—10:34, 35.
18. (a) Kisha ni nini kinachotukia Antiokia? (b) Ni mnyanyaso gani unaotokea, lakini je! huo watimiza lengo lao?
18 Habari njema zinapoendelea kuenea kwa haraka, Barnaba na Sauli wafundisha umati mkubwa katika Antiokia, ‘na ni kwanza katika Antiokia kwamba wanafunzi waitwa Wakristo kwa uongozi wa kimungu.’ (11:26, NW) Kwa mara nyingine mnyanyaso waanza. Herode Agripa 1 afanya Yakobo ndugu ya Yohana auawe kwa upanga. Pia atupa Petro katika gereza, lakini kwa mara nyingine malaika wa Yehova aweka Petro huru. Ni vibaya kama nini kwa Herode mwovu! Kwa sababu ashindwa kumpa Mungu utukufu, aliwa na funza na kufa. Kwa upande mwingine, ‘neno la Yehova lazidi na kuenea.’—12:24.
19. Safari ya umisionari ya kwanza ya Paulo ni ya kadiri gani, na nini yanayotimizwa?
19 Safari ya umisionari ya kwanza ya Paulo, pamoja na Barnaba (13:1–14:28).d Barnaba na “Sauli, ambaye ndiye Paulo,” watengwa na kutumwa kutoka Antiokia na roho takatifu. (13:9) Kwenye kisiwa cha Kipro (Saiprasi), wengi wawa waamini, kutia ndani liwali Sergio Paulo. Kwenye bara la Asia Ndogo, wafanya mzunguko wa majiji sita au zaidi, na kila mahali hadithi ni ile ile: Mgawanyo ulio wazi watokea kati ya wale wanaokubali kwa furaha habari njema na wapinzani wenye shingo ngumu wanaochochea wafanya ghasia wenye kutupia mawe wajumbe wa Yehova. Baada ya kuweka wanaume wazee katika makundi yaliyotoka kuundwa karibuni, Paulo na Barnaba warejea Antiokia ya Shamu (Siria).
20. Suala la kutahiriwa latatuliwa kwa uamuzi gani?
20 Kutatua suala la kutahiriwa (15:1-35). Kwa sababu ya mmiminiko mkubwa wa wasio Wayahudi, swali latokea juu kama wao wapaswa kutahiriwa. Paulo na Barnaba wapeleka suala hilo kwa mitume na wanaume wazee katika Yerusalemu, ambako mwanafunzi Yakobo asimamia nao wapanga kutuma uamuzi wa kauli moja kwa barua rasmi: “Roho takatifu na sisi wenyewe tumependelea tusiongeze mzigo zaidi kwenu nyinyi, isipokuwa mambo haya ya lazima, kuendelea kushika mwiko wa vitu vinavyotolewa dhabihu kwa sanamu na wa damu na wa vitu vinavyonyongwa na wa uasherati.” (15:28, 29, NW) Kitia-moyo cha barua hii chasababisha ndugu katika Antiokia washangilie.
21. (a) Ni nani wanaoshirikiana na Paulo kwenye safari yake ya umisionari ya pili? (b) Ni matukio gani yanayotia alama ziara yake ya Makedonia?
21 Huduma yapanuka kwa safari ya pili ya Paulo (15:36–18:22).e “Baada ya siku kadha” Barnaba na Marko waabiri (wasafiri) kwenda Kipro, ambapo Paulo na Sila waondoka kupitia Shamu na Asia Ndogo. (15:36) Yule mwanamume kijana Timotheo ajiunga na Paulo kule Listra, nao waendelea na safari yao mpaka Troa kwenye pwani ya Aegea. Hapa katika njozi Paulo aona mwanamume mmoja akimsihi hivi: “Vuka, uje Makedonia utusaidie.” (16:9) Luka ajiunga na Paulo, nao watwaa merikebu mpaka Filipi, jiji kuu la Makedonia, ambako Paulo na Sila watupwa gerezani. Tokeo la hilo lawa ni kuwa mwamini na kubatizwa kwa mtunza gereza. Baada ya kufunguliwa kwao, wasonga mbele mpaka Thesalonika, na huko Wayahudi wenye wivu wachochea wafanya ghasia juu yao. Kwa hiyo wakati wa usiku akina ndugu watuma Paulo na Sila waende Beroya. Hapa Wayahudi waonyesha uelekevu kwa kupokea neno “kwa uelekevu wa moyo, wak[i]yachunguza maandiko kila siku” katika kutafuta uthibitisho wa mambo waliyojifunza. (17:11) Akiacha Sila na Timotheo pamoja na kundi jipya hilo, kama alivyokuwa ameacha Luka katika Filipi, Paulo asonga mbele kusini mpaka Athene.
22. Ni nini matokeo ya uneni wa ustadi wa Paulo katika Areopago?
22 Katika jiji hili la sanamu, wanafalsafa Waepikureo na Wastoiko wenye kujitakia makuu wamdhihaki Paulo kuwa “mpuzi” na “mtangaza habari za miungu migeni,” nao wampeleka mpaka Areopago, au Kilima Marsi. Kwa ustadi wa kusema Paulo atoa hoja (sababu) za kutetea utafutaji wa Mungu wa kweli, “Bwana wa mbingu na nchi,” ambaye hutoa uhakikisho wa hukumu ya uadilifu kupitia yule ambaye Yeye amefufua kutoka kwa wafu. Mtajo wa ufufuo wagawanya wasikilizaji wake, lakini baadhi yao wawa waamini.—17:18, 24.
23. Ni nini yanayotimizwa katika Korintho?
23 Kisha, katika Korintho, Paulo akaa na Akila na Prisila, akijiunga nao katika biashara yao ya kutengeneza hema. Upinzani juu ya kuhubiri kwake wamlazimisha ahame sinagogi na kufanya mikutano yake katika chumba cha kando, katika makao ya Tito Yusto. Krispo, ofisa msimamizi wa sinagogi, awa mwamini. Baada ya kukaa miezi 18 katika Korintho, Paulo aondoka pamoja na Akila na Prisila kwenda Efeso, ambako awaacha na kuendelea mbele mpaka Antiokia katika Shamu, hivyo kukamilisha safari yake ya pili ya umisionari.
24, 25. (a) Wakati wa Paulo kuanza safari yake ya tatu, ni nini kinachotukia katika Efeso? (b) Ni fujo gani inayotia alama umalizio wa ukaaji wa miaka mitatu wa Paulo?
24 Paulo atembelea makundi tena, safari ya tatu (18:23–21:26).f Myahudi mmoja aitwaye Apolo aja Efeso kutoka Aleksandria (Iskanderia), Misri, akinena kwa ujasiri katika sinagogi juu ya Yesu, lakini Akila na Prisila waona lazima ya kusahihisha fundisho lake kabla hajaenda Korintho. Sasa Paulo aendelea na safari yake ya tatu na baadaye aja Efeso. Ajuapo kwamba waamini hapa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana, Paulo aeleza ubatizo katika jina la Yesu. Kisha awabatiza wanaume wanaokaribia 12; na awekapo mikono yake juu yao, wapokea roho takatifu.
25 Wakati wa ukaaji wa miaka mitatu wa Paulo katika Efeso, ‘neno la Bwana [Yehova, NW] lazidi kukua na kushinda kwa nguvu,’ na wengi waacha ibada yao ya miungu-mke mlinda jiji, Artemi. (19:20) Wakiwa na kasirani kwa sababu ya kutarajia hasara ya biashara, watengeneza vinyago (sanamu) vya fedha wavuruga jiji sana hata yachukua saa nyingi kutawanya wafanya ghasia. Upesi baada ya hapo Paulo aondoka kwenda Makedonia na Ugiriki, akizuru waamini njiani.
26. (a) Paulo afanya miujiza gani katika Troa? (b) Ni ushauri gani anaotoa kwa waangalizi kutoka Efeso?
26 Paulo akaa miezi mitatu katika Ugiriki kabla ya kurudi kwa kupitia Makedonia, ambako Luka ajiunga naye tena. Wavuka mpaka Troa, na hapa, Paulo akiwa anatoa hotuba mpaka usiku, mwanamume kijana alala usingizi na kuporomoka chini kutoka dirisha ya orofa ya tatu. Anyanyuliwa ali amekufa, lakini Paulo amfufua. Siku inayofuata Paulo na kikundi chake waondoka kwenda Mileto, ambako Paulo asimama akiwa safarini kwenda Yerusalemu, ili akutane na wanaume wazee kutoka Efeso. Awajulisha hawataona uso wake tena. Basi, jinsi lilivyo jambo lenye uharaka kwao kuchukua uongozi na kuchunga kundi la Mungu, ‘ambalo miongoni mwalo roho takatifu imewaweka kuwa waangalizi’! Akumbusha juu ya kielelezo ambacho ameweka miongoni mwao, naye awaonya kwa upole waendelee kuwa macho, wasijihurumie katika utoaji kwa ajili ya ndugu. (20:28, NW) Ajapoonywa asikanyage Yerusalemu, Paulo harudi nyuma. Waandamani wake wakubali, wakisema: “Mapenzi ya Bwana [Yehova, NW] na yatendeke.” (21:14) Kuna shangwe kubwa wakati Paulo aripotipo kwa Yakobo na wanaume wazee kuhusu baraka ya Mungu juu ya huduma yake miongoni mwa mataifa.
27. Ni karibisho gani analopokea Paulo kwenye hekalu?
27 Paulo akamatwa na kujaribiwa mahakamani (21:27–26:32). Paulo anapojitokeza hekaluni Yerusalemu, apokewa kwa uaudi mkali. Wayahudi kutoka Asia wakoroga jiji lote liinuke juu yake, na askari Warumi wamponyoa chupuchupu.
28. (a) Ni swali gani analotokeza Paulo mbele ya Sanhedrini, na tokeo lawa nini? (b) Kisha yeye apelekwa wapi?
28 Vurugu yote hii ni ya nini? Paulo huyu ni nani? Uhalifu (kosa) wake ni nini? Kamanda wa jeshi mwenye mshangao ataka kujua majibu. Kwa sababu ya uraia wake wa Kirumi, Paulo aponyoka mjeledi wenye meno na aletwa mbele ya Sanhedrini. Lo! mahakama iliyogawanyika ya Mafarisayo na Masadukayo! Kwa hiyo Paulo atokeza swali la ufufuo, na hivyo kuwapiganisha. Farakano hiyo inapokuwa yenye jeuri, askari Warumi walazimika kumnyakua Paulo kutoka miongoni mwa Sanhedrini kabla hajararuliwa vipande-vipande. Apelekwa kisiri wakati wa usiku kwa Liwali Feliki katika Kaisaria chini ya ulinzi mkali wa askari.
29. Akiwa ameshtakiwa uhaini, Paulo awa na mfululizo gani wa majaribio au masikizo ya kesi, naye akata rufani gani?
29 Akiwa ameshtakiwa uhaini na washtaki wake, Paulo ajitetea mwenyewe kwa ustadi mbele ya Feliki. Lakini Feliki aahirisha akitumaini kupokea hongo ili Paulo aachiliwe. Miaka miwili yapita. Porkio Festo afuatia Feliki kuwa liwali, na jaribio jipya laagizwa. Kwa mara nyingine, mashtaka mazito yafanywa, na kwa mara nyingine Paulo ajulisha rasmi kutokuwa kwake na hatia. Lakini Festo, ili apate kibali cha Wayahudi, adokeza kuwe jaribio zaidi mbele yake katika Yerusalemu. Kwa hiyo Paulo ajulisha rasmi hivi: “Nataka rufani kwa Kaisari!” (25:11) Muda zaidi wapita. Mwishowe, Mfalme Herode Agripa 2 atembelea Festo kirafiki, na Paulo kwa mara nyingine aletwa kwenye jumba la hukumu. Ushuhuda wake ni wenye mkazo mwingi na wenye kusadikisha hivi kwamba Agripa asukumwa amwambie hivi: “Kwa muda mfupi wewe ungenishawishi mimi niwe Mkristo.” (26:28, NW) Vivyo hivyo Agripa atambua kutokuwa na hatia kwa Paulo na kwamba angaliachiliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari.
30. Ni mambo gani yanayofuatana na safari ya Paulo kufikia Melita?
30 Paulo aenda Rumi (27:1–28:31).g Mfungwa Paulo na wengine wapelekwa kwa mashua kwa ajili ya hatua ya kwanza ya safari ya kwenda Rumi. Pepo zikiwa za mbisho (kimbele), mwendo ni wa pole. Kwenye bandari ya Mira, wabadili merikebu. Wanapofika Bandari Nzuri, katika Krete, Paulo apendekeza wakae hapo wakati huo wa kipupwe, lakini walio wengi washauri kung’oa nanga. Wakiwa hawajaenda sana baharini wakamatwa na tufani inayowasukuma bila huruma. Baada ya majuma mawili chombo chao hatimaye chavunjwa-vunjwa vipande kwenye miamba kando ya pwani ya Melita. Kulingana na uhakikisho aliotangulia kutoa Paulo, hakuna hata mmoja wa wale abiria (wasafiri) 276 anayepoteza uhai wake! Wakaaji wa Melita waonyesha fadhili za kibinadamu zisizo za kawaida, na wakati wa kipupwe hicho Paulo aponya wengi wao kwa uwezo wa kimwujiza wa roho ya Mungu.
31. Paulo alakiwaje awasilipo Rumi, naye ajishughulisha na nini huko?
31 Masika yanayofuata Paulo afika Rumi, na akina ndugu waja barabarani kumlaki. Awaonapo Paulo ‘ashukuru Mungu na kuchangamka.’ Ingawa yungali mfungwa, Paulo aruhusiwa akae katika nyumba yake mwenyewe aliyokodi akiwa na ulinzi wa askari. Luka amalizia simulizi lake, akieleza juu ya Paulo akipokea kwa fadhili wale wote waliomjia na ‘kuwahubiria habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.’—28:15, 31.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
32. Kabla na wakati wa Pentekoste, Petro alishuhudiaje uasilia wa Maandiko ya Kiebrania?
32 Kitabu cha Matendo chaongezea ushuhuda wa yale masimulizi ya Gospeli katika kuthibitisha uasilia na kupuliziwa na Mungu kwa Maandiko ya Kiebrania. Pentekoste ilipokuwa ikikaribia, Petro alitaja utimizo wa unabii mara mbili ‘ulionenwa na roho takatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda.’ (Mdo. 1:16, 20; Zab. 69:25; 109:8) Petro pia aliuambia umati wa Pentekoste uliostaajabu kwamba kwa kweli wao walikuwa mashahidi wa utimizo wa unabii: “Jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli.”—Mdo. 2:16-21; Yoe. 2:28-32; linganisha pia Matendo 2:25-28, 34, 35 na Zaburi 16:8-11 na 110:1.
33. Petro, Filipo, Yakobo, na Paulo walionyeshaje Maandiko ya Kiebrania yamepuliziwa na Mungu?
33 Ili kusadikisha umati mwingine nje ya hekalu, Petro kwa mara nyingine alielekeza kwa Maandiko ya Kiebrania, kwanza akinukuu Musa na kisha akasema: “Na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi.” Baadaye, mbele ya Sanhedrini, Petro alinukuu Zaburi 118:22 katika kuonyesha kwamba Kristo, jiwe ambalo walikataa, alikuwa amekuwa “jiwe kuu la pembeni.” (Mdo. 3:22-24; 4:11) Filipo alieleza towashi Mwethiopia jinsi unabii wa Isaya 53:7, 8 ulikuwa umetimizwa, na alipoelimishwa, kwa unyenyekevu yeye aliomba ubatizo. (Mdo. 8:28-35) Vivyo hivyo, akinena na Kornelio juu ya Yesu, Petro alitoa ushuhuda huu: “Huyo manabii wote humshuhudia.” (10:43) Wakati habari ya kutahiriwa ilipokuwa ikijadiliwa, Yakobo alitegemeza uamuzi wake kwa kusema: “Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa.” (15:15-18) Mtume Paulo alitegemea mamlaka izo hizo. (26:22; 28:23, 25-27) Ukubali wa mara moja ulio wazi wa wanafunzi na wasikiaji wao wa Maandiko ya Kiebrania kuwa sehemu ya Neno la Mungu watia muhuri wa kibali kilichopuliziwa na Mungu juu ya maandishi hayo.
34. Matendo chafunua nini kuhusu kundi la Kikristo, na je! hilo ni tofauti leo?
34 Matendo ni chenye mafaa sana katika kuonyesha jinsi kundi la Kikristo lilivyoundwa na jinsi lilivyokua chini ya uwezo wa roho takatifu. Katika simulizi lake lote lenye matukio ya kusisimua, twaona baraka za Mungu za mpanuko, ujasiri na shangwe ya Wakristo wa mapema, msimamo wao wa kutoachilia masharti yao usoni pa mnyanyaso, na nia yao ya kutumikia, kama ilivyotolewa kielezi na kujibu kwa Paulo miito ya kuingia utumishi wa kigeni na kwenda Makedonia. (4:13, 31; 15:3; 5:28, 29; 8:4; 13:2-4; 16:9, 10) Kundi la Kikristo leo haliko tofauti, kwa maana limefungamanishwa pamoja katika upendo, umoja, na masilahi (faida) yale yale linaponena “matendo makuu ya Mungu” chini ya uongozi wa roho takatifu.—2:11, 17, 45; 4:34, 35; 11:27-30; 12:25.
35. Matendo chaonyeshaje jinsi ushahidi ulivyopasa kutolewa, na ni sifa gani inayokaziwa katika huduma?
35 Kitabu cha Matendo chaonyesha jinsi utendaji wa Kikristo wa kutangaza Ufalme wa Mungu wapasa kutimizwa. Paulo mwenyewe alikuwa kielelezo, akisema hivi: “Sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa, bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba.” Kisha aendelea kusema: “Mimi nilitoa ushahidi kikamili.” (NW) Habari kuu ya ‘kutoa ushahidi kamili’ yavuta uangalifu wetu katika kitabu hiki chote, na yajitokeza sana katika mafungu ya kumalizia, ambapo ujitoaji wa moyo wote wa Paulo kwa kuhubiri na kufundisha kwake, hata chini ya vifungo vya gereza, washuhudiwa kwa maneno haya: “Akawaeleza kwa taratibu na kuushuhudia [akitoa ushahidi kamili, NW] ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni.” Daima sisi na tuwe wenye moyo mmoja katika utendaji wetu wa Ufalme!—20:20, 21; 28:23; 2:40; 5:42; 26:22.
36. Ni shauri gani lenye kutumika analotumia Paulo kwa njia yenye mkazo kwa waangalizi leo?
36 Hotuba ya Paulo kwa waangalizi kutoka Efeso ina shauri jingi lenye kutumika kwa ajili ya waangalizi leo. Kwa kuwa hawa wamewekwa na roho takatifu, ni jambo la maana kwamba ‘wajiangalie wenyewe na kundi lote,’ (NW), wakiwachunga kwa wororo na kuwalinda na mbwa-mwitu waonevu wanaotafuta kuwaangamiza. Hilo si daraka jepesi! Waangalizi wahitaji kuwa macho na kujijenga wenyewe juu ya neno la fadhili zisizostahiliwa za Mungu. Wanapotaabika kuwasaidia wale walio dhaifu, ni lazima “kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”—20:17-35.
37. Ni kwa hoja gani yenye busara Paulo alielewesha wazo lake juu ya Areopago?
37 Zile hotuba nyingine za Paulo pia zameta kwa maelezo yaliyo wazi ya kanuni za Biblia. Kwa kielelezo, kuna hoja nzuri ya hotuba yake kwa Wastoiko na Waepikureo katika Areopago. Kwanza anukuu maandishi haya ya madhabahu, “KWA MUNGU ASIYEJULIKANA,” na aitumia kuwa sababu ya kueleza kwamba yule Mungu mmoja wa kweli, Bwana wa mbingu na dunia, aliyefanya kwa mtu mmoja kila taifa la watu, “hawi mbali na kila mmoja wetu.” Kisha anukuu maneno ya washairi wao, “Kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu,” katika kuonyesha jinsi ulivyo ujinga kudhani kwamba walitokana na sanamu zisizo na uhai za dhahabu, fedha, au jiwe. Kwa hiyo Paulo athibitisha kwa busara enzi kuu ya Mungu aliye hai. Ni katika maneno ya kumalizia tu kwamba atokeza suala la ufufuo, na hata hapo hataji Kristo kwa jina. Alielewesha wazo lake la enzi kuu iliyo juu zaidi yake yule Mungu mmoja wa kweli, na baadhi wakawa waamini kama tokeo.—17:22-34.
38. Ni baraka gani zitakazotokana na aina ya funzo linalotiwa moyo katika Matendo?
38 Kitabu cha Matendo chatia moyo funzo lenye kuendelea, la bidii la “kila andiko.” Kwa kuwa Wayahudi wa Beroya “walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo” wakati Paulo alipohubiri mara ya kwanza huko, walipongezwa kuwa “waungwana.” (17:11) Leo, kama ilivyokuwa wakati huo, utafutaji huo wenye hamu wa Maandiko kwa kushirikiana na kundi la Yehova lililojazwa roho utatokeza baraka za usadikisho na imani yenye nguvu. Ni kupitia funzo hilo kwamba mtu aweza kuja kwenye uthamini ulio wazi wa kanuni za kimungu. Taarifa njema ya baadhi ya kanuni hizo imeandikwa katika Matendo 15:29. Hapa baraza linaloongoza la mitume na ndugu wazee katika Yerusalemu lilijulisha kwamba ingawa kutahiriwa hakukuwa takwa kwa Israeli wa kiroho, kulikuwako vizuizi vya waziwazi juu ya ibada ya sanamu, damu, na uasherati.
39. (a) Wanafunzi walitiwaje nguvu wakabiliane na minyanyaso? (b) Walitoa ushuhuda gani wa ujasiri? Je! ulikuwa na matokeo?
39 Wanafunzi hao wa mapema walijifunza Maandiko yaliyopuliziwa na Mungu na wangeweza kunukuu na kuyatumia kulingana na uhitaji. Wao walitiwa nguvu kupitia maarifa sahihi na kwa roho ya Mungu wakabili minyanyaso mikali. Petro na Yohana waliweka kigezo kwa Wakristo wote waaminifu walipowaambia kwa ujasiri hivi watawala wenye kupinga: “Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Na walipoletwa tena mbele ya Sanhedrini, iliyokuwa ‘imewaamuru kwa nguvu’ wasiendelee kufundisha kwa msingi wa jina la Yesu, bila kusita walisema: “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Ushuhuda huo usio na hofu ulitokeza ushahidi mwema kwa watawala, na uliongoza yule mwalimu maarufu wa Sheria, Gamalieli atoe taarifa yake inayojulikana sana ya kupendelea uhuru wa ibada, ambayo iliongoza kwenye kuachiliwa kwa mitume.—4:19, 20; 5:28, 29, 34, 35, 38, 39.
40. Matendo chatoa kichocheo gani kwetu ili tutoe ushahidi kamili kwa Ufalme?
40 Kusudi tukufu la Yehova kuhusu Ufalme wake, ambalo lanyooka kama uzi wa dhahabu katika Biblia yote, lajitokeza wazi sana katika kitabu cha Matendo. Pale mwanzoni Yesu aonyeshwa wakati wa zile siku 40 kabla ya kupaa kwake ‘akinena mambo yaliyohusu ufalme wa Mungu.’ Ilikuwa katika kujibu swali la wanafunzi juu ya kurudishwa kwa Ufalme kwamba Yesu aliwaambia ni lazima kwanza wawe mashahidi wake mpaka sehemu ya mbali zaidi ya dunia. (1:3, 6, 8) Kuanzia Yerusalemu, wanafunzi walihubiri Ufalme kwa ujasiri usiosita. Minyanyaso ilitokeza kupigwa mawe kwa Stefano na kutawanya kwa wengi wa wanafunzi katika maeneo mapya. (7:59, 60) Imeandikwa kwamba Filipo alijulisha rasmi “habari njema za ufalme wa Mungu” kwa kufanikiwa sana katika Samaria na kwamba Paulo na washiriki wake walitangaza “ufalme” katika Asia, Korintho, Efeso, na Rumi. Wakristo hao wote wa mapema waliweka vielelezo vizuri sana vya utegemeo usioyumba-yumba kwa Yehova na roho yake yenye kuegemeza. (8:5, 12; 14:5-7, 21, 22; 18:1, 4; 19:1, 8; 20:25; 28:30, 31) Kwa kuona bidii na moyo mkuu wao usioshindwa na kwa kuona jinsi Yehova alivyobariki sana jitihada zao, sisi pia tuna kichocheo bora sana cha kuwa waaminifu katika ‘kutoa ushahidi kamili kuhusu ufalme wa Mungu.’—28:23, NW.
[Maelezo ya Chini]
a St. Paul the Traveller, 1895, ukurasa 4.
b Yamenukuliwa katika Amkeni! (Kiingereza) ya Julai 22, 1947, kurasa 22-3; ona pia Amkeni! (Kiingereza) ya Aprili 8, 1971, kurasa 27-8.
c Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 153-4, 734-5; Buku 2, ukurasa 748.
d Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 747.
e Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 747.
f Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 747.
g Insight on the Scriptures, Buku 2, ukurasa 750.