Mashahidi Wenye Bidii wa Yehova Wasonga Mbele!
MASHAHIDI wa Yehova wa karne ya kwanza walikuwa watu wa kitendo cha ujasiri na bidii. Waliutekeleza utume wa Yesu kwa hamu nyingi: “Nendeni mkafanye wanafunzi kutoka kwa watu wa mataifa yote.”—Mathayo 28:19, 20, NW.
Lakini twajuaje kwamba wafuasi wa mapema wa Kristo walichukua utume huo kwa uzito? Kitabu cha Biblia cha Matendo huthibitisha kwamba walikuwa mashahidi wenye bidii wa Yehova, wenye kusonga mbele kweli kweli!
MANUFAA NA MAMBO MAKUU MENGINE
Ufanano katika namna ya usemi na mtindo kati ya Gospeli ya tatu na kitabu cha Matendo huonyesha mwandikaji alikuwa mmoja—Luka, “yule tabibu mpendwa.” (Wakolosai 4:14) Miongoni mwa mambo makuu ya kitabu hicho ni maongeo na sala zilizohifadhiwa katika Matendo. Karibu asilimia 20 ya kitabu hicho ni hotuba, kama zile zilizotolewa na Petro na Paulo katika kuunga mkono imani ya kweli.
Kitabu cha Matendo kiliandikwa katika Roma karibu 61 W.K. Yaonekana hiyo ndiyo sababu hakitaji kwenda kwa Paulo mbele ya Kaisari wala mnyanyaso ambao Nero alifanya dhidi ya Wakristo karibu 64 W.K.—2 Timotheo 4:11.
Kama Gospeli ya Luka, Matendo kilielekezwa kwa Theofilo. Kiliandikwa ili kuimarisha imani na kuripoti kuhusu mweneo wa Ukristo. (Luka 1:1-4; Matendo 1:1, 2) Kitabu hicho huthibitisha kwamba mkono wa Yehova ulikuwa pamoja na watumishi wake waaminifu-washikamanifu. Hutupa sisi habari juu ya nguvu ya roho yake na kuimarisha uhakika wetu katika unabii uliovuviwa kimungu. Pia Matendo hutusaidia tuvumilie mnyanyaso, hutusukuma tuwe Mashahidi wenye kujidhabihu wa Yehova, na hujenga imani yetu katika tumaini la Ufalme.
USAHIHI WA KIHISTORIA
Akiwa mshirika wa Paulo, Luka aliandika habari za safari zao. Pia alinena kwa mashahidi wenye kuona kwa macho yao wenyewe. Mambo haya na utafiti mwingi sana hufanya maandishi yake kuwa kazi ya ustadi mwingi kwa habari ya usahihi wa kihistoria.
Kwa hiyo mwanachuo William Ramsay angeweza kusema hivi: “Luka ni mwanahistoria wa daraja la kwanza: si kwamba tu taarifa zake za uthibitisho ni za kutumainika, bali pia yeye ni hodari katika kusimulia historia kikweli . . . Mtungaji huyu apaswa kuwekwa pamoja na wanahistoria walio mashuhuri kabisa.”
PETRO—SHAHIDI MWAMINIFU
Kazi ya kupewa na Mungu ya kujulisha rasmi habari njema yaweza kutekelezwa kwa nguvu ya roho takatifu ya Yehova tu. Hivyo, wafuasi wa Yesu wapokeapo roho takatifu, watakuwa mashahidi wake katika Yerusalemu, Yudea, na Samaria na “kwenye sehemu ya mbali zaidi ya dunia.” Kwenye Pentekoste 33 W.K., wao wajazwa roho takatifu. Kwa kuwa ni saa 3:00 tu asubuhi, hakika hawakulewa, kama vile watu fulani wafikirivyo. Petro atoa ushahidi wa kusisimua, na watu 3,000 wabatizwa. Wapinzani wa kidini wajaribu kunyamazisha wapiga mbiu ya Ufalme, lakini kwa kujibu sala, Mungu awezesha mashahidi wake kunena neno lake kwa ujasiri. Watishwapo tena, wao wajibu hivi: “Ni lazima sisi tutii Mungu kuwa mtawala kuliko wanadamu.” Kazi yafuliza mbele huku wao wakiendelea kuhubiri nyumba kwa nyumba.—1:1–5:42, NW.
Kutegemea roho ya Yehova kwawezesha mashahidi wake kuvumilia mnyanyaso. Kwa hiyo, baada ya Stefano shahidi mwaminifu kupigwa kwa mawe mpaka kufa, wafuasi wa Yesu watawanywa, lakini hiyo yaeneza tu lile neno. Filipo mweneza-evanjeli apainia (afungua kazi) katika Samaria. Kwa kushangaza, mnyanyasi mwenye jeuri Sauli wa Tarso aongolewa. Yeye akiwa mtume Paulo, ahisi joto la mnyanyaso katika Dameski lakini aponyoka mbinu za Wayahudi za kumwua. Kwa ufupi, Paulo ashirikiana na mitume katika Yerusalemu halafu asonga mbele katika huduma yake.—6:1–9:31.
Mkono wa Yehova upo pamoja na mashahidi wake, kama ambavyo Matendo chaendelea kuonyesha. Petro amwinua Dorkasi (Tabitha) kutoka kwa wafu. Akiitikia wito, katika Kaisaria ajulisha rasmi habari njema kwa Kornelio, watu wa nyumba yake, na marafiki. Wao wabatizwa wakiwa ndio wa kwanza kati ya Wasio Wayahudi kuwa wanafunzi wa Yesu. Hivyo “majuma sabini” yaisha, hiyo ikituleta kwenye 36 W.K. (Danieli 9:24) Muda mfupi baada ya hapo, Herode Agripa 1 aua mtume Yakobo na kuagiza Petro akamatwe. Lakini mtume apata ukombozi wa kimalaika kutoka gerezani, na ‘neno la Yehova laendelea kukua na kuenea.’—9:32–12:25, NW.
SAFARI TATU ZA PAULO ZA KIMISIONARI
Baraka zatiririkia wale ambao hujitumikisha sana katika utumishi wa Mungu, kama Paulo alivyofanya. Safari yake ya kwanza ya kimisionari yaanza Antiokia, Siria (Shamu). Katika kisiwa cha Saiprasi (Kipro), liwali Sergio Paulo na wengine wengi wawa waamini. Huko Perge katika Pamfilia, Yohana Marko aondoka kwenda Yerusalemu, lakini Paulo na Barnaba wasonga mbele kwenda Antiokia katika Pisidia. Katika Listra, Wayahudi wachochea mnyanyaso. Ingawa Paulo apigwa kwa mawe na kuachwa akidhaniwa ni mfu, apata nafuu na kuendelea mbele katika huduma. Mwishowe, yeye na Barnaba warudi Antiokia katika Siria, wakimaliza safari ya kwanza.—13:1–14:28.
Kama ilivyokuwa kwa kifano chalo cha karne ya kwanza, Baraza Linaloongoza la leo huamua masuala kwa mwongozo wa roho takatifu. Tohara haikuwa miongoni mwa ‘mambo ya lazima,’ ambayo ni kutia ndani “kushika mwiko wa vitu vinavyotolewa dhabihu kwa sanamu na wa damu na wa vitu vinavyonyongwa na wa uasherati.” (15:28, 29, NW) Paulo aanzapo safari ya pili ya kimisionari, Sila aandamana naye, na baadaye Timotheo ajiunga nao. Kitendo cha haraka chafanywa ili kuitikia wito wa kuvuka kuingia Makedonia. Huko Filipi, kutoa ushahidi kwatokeza fujo na kifungo gerezani. Lakini Paulo na Sila wafunguliwa na tetemeko la dunia nao wamhubiri mtunza-jela na watu wa nyumba yake, nao wawa waamini waliobatizwa.—15:1–16:40.
Watumishi wa Yehova wapaswa kuwa wanafunzi wa Neno lake wenye bidii ya uendelevu, kama Paulo na Waberoya wenye kuyachunguza Maandiko. Juu ya Areopago katika Athene, yeye atoa ushahidi juu ya uumba wa Yehova, na watu fulani wawa waamini. Upendezi mwingi sana wadhihirishwa katika Korintho hivi kwamba abaki katika jiji hilo kwa miezi 18. Akiwa huko, aandika Wathesalonike wa Kwanza na wa Pili. Wakati anapoagana na Sila na Timotheo, mtume aabiri kwenda Efeso, halafu apanda chombo kwenda Kaisaria, na kuendelea na safari hadi Yerusalemu. Arudipo Antiokia ya Siria, safari yake ya pili ya kimisionari imeisha.—17:1–18:22.
Kama vile Paulo alivyoonyesha, kutoa ushahidi nyumba kwa nyumba ni sehemu muhimu ya huduma ya Kikristo. Safari ya tatu ya mtume (52-56 W.K.) sana-sana ni ya kupitia njia ile aliyofuata katika safari yake ya pili. Huduma ya Paulo yachochea upinzani huko Efeso, ambako yeye aandika Wakorintho wa Kwanza. Aandika Wakorintho wa Pili akiwa katika Makedonia, na kuwaandikia Waroma akiwa katika Korintho. Huko Mileto, Paulo akutana na wazee wa Efeso na kunena juu ya jinsi alivyowafundisha peupe na nyumba kwa nyumba. Safari yake ya tatu yamalizika awasilipo Yerusalemu.—18:23–21:14.
MNYANYASO HAUNA MATOKEO
Mnyanyaso haushoni midomo ya mashahidi waaminifu wa Yehova. Kwa hiyo jeuri ya wanaghasia ifokapo dhidi ya Paulo kwenye hekalu katika Yerusalemu, kwa ujasiri yeye awatolea ushahidi wanaghasia hao wenye hamaki. Hila iliyopangwa ili kumwua yavurugwa wakati apelekwapo kwa Gavana Feliki kule Kaisaria akiwa na ulinzi wa kijeshi. Paulo atiwa minyororo kwa miaka miwili huku Feliki akingojea hongo lakini alipate wapi. Mwandamizi wake, Festo, asikia Paulo akiomba rufani kwa Kaisari. Hata hivyo, kabla ya kuelekea Roma, mtume atoa utetezi wa kusisimua mbele ya Mfalme Agripa.—21:15–26:32.
Bila kuogopeshwa na majaribu, watumishi wa Yehova waendelea kuhubiri. Hakika hiyo ilikuwa kweli kuhusu Paulo. Kwa sababu ya ombi lake la rufani kwa Kaisari, mtume afunga safari kwenda Roma akiwa na Luka karibu 58 W.K. Huko Mira katika Likia, wahamia meli nyingine. Ingawa wavunjikiwa meli na kufika mahali pakavu katika kisiwa cha Melita, baadaye chombo kingine chawapeleka Italia. Hata akiwa chini ya ulinzi wa kijeshi katika Roma, Paulo aita watu ndani na kujulisha rasmi habari njema kwao. Wakati wa kifungo hiki gerezani, aandikia Waefeso, Wafilipi, Wakolosai, Filemoni, na Waebrania.—27:1–28:31.
KUSONGA MBELE DAIMA
Kitabu cha Matendo chaonyesha kwamba kazi iliyoanzishwa na Mwana wa Mungu iliendeshwa kwa uaminifu na mashahidi wa Yehova wa karne ya kwanza. Ndiyo, chini ya nguvu ya roho takatifu ya Mungu, walitoa ushahidi kwa bidii.
Kwa sababu wafuasi wa mapema wa Yesu walitegemea Mungu kwa sala, mkono Wake ulikuwa pamoja nao. Hivyo maelfu wakawa waamini, na ‘habari njema zilihubiriwa katika uumbaji wote chini ya mbingu.’ (Wakolosai 1:23, NW) Kwa kweli, wakati huo na hata sasa, Wakristo wa kweli wamethibitika kuwa mashahidi wa Yehova walio na bidii huku wakisonga mbele!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
KORNELIO AMIRI-MIA: Kornelio alikuwa ofisa wa jeshi, au amiri-mia. (10:1, NW) Mshahara wa mwaka kwa amiri-mia ulikuwa karibu mara tano ule wa askari-miguu, au zapata dinari 1,200, lakini ungeweza kuwa zaidi sana ya hapo. Alipostaafu, alituzwa pesa au shamba. Mavao yake ya kijeshi yalikuwa ya kuvutia, kuanzia kofia ya fedha hadi vazi lililo kama rinda, joho la sufi safi, na kinga za miundi ya miguu zilizopambwa. Wenye kuandamana na amiri-mia walikuwa wanaume 100 kikanuni, lakini nyakati fulani walikuwa kama 80 tu. Yaonekana kwamba waajiriwa wapya kwenye “kikosi cha Italia” walitoka miongoni mwa raia Waroma na mahuru katika Italia.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
SALA KWENYE DARI YA NYUMBA:
Petro hakuwa akijionyesha aliposali akiwa peke yake juu ya dari. (10:9) Yaelekea kwamba ukingo wenye kuzungukia dari ile tambarare ulimficha asionwe. (Kumbukumbu 22:8) Pia paani palikuwa mahali pa kustarehe na kuepuka kelele za barabarani jioni.
[Sanduku katika ukurasa wa 25]
KUDHANIWA KUWA MIUNGU KATIKA UMBO LA KIBINADAMU: Kuponya kwa Paulo mtu mlemavu kulifanya wakaaji wa Listra wafikiri kwamba miungu ilikuwa imetokea ikiwa wanadamu. (14:8-18) Zeu, mungu mkuu wa Wagiriki, alikuwa na hekalu kwenye jiji hilo, na mwana wake Herme, mjumbe wa miungu, alijulikana kwa ufasaha wa kusema. Kwa kuwa watu walifikiri kwamba Paulo alikuwa Herme kwa sababu ndiye aliyeongoza katika kunena, walimwona Barnaba kuwa Zeu. Ilikuwa desturi kuvika sanamu zilizo miungu-bandia mashada ya maua au ya majani ya msaipresi au msunobari, lakini Paulo na Barnaba walikataa tendo hilo la ibada ya sanamu.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
MTUNZA-JELA AAMINI: Wakati tetemeko la dunia lilipofungua milango ya gereza na kulegeza minyororo ya wafungiwa ndani, mtunza-jela Mfilipi alitaka kujiangamiza. (16:25-27) Kwa nini? Kwa sababu sheria ya Kiroma iliamrisha kwamba mtunza-jela angepaswa kupewa adhabu ya mtu mwenye kutoroka. Yaonekana mtunza-jela alipendelea zaidi kifo cha kujiua kuliko kufa kwa kuteswa-teswa, ambacho labda kiliwangoja baadhi ya wafungwa. Hata hivyo, alizikubali habari njema, “kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo.”—16:28-34.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
OMBI LA RUFANI KWA KAISARI: Akiwa raia Mroma tangu kuzaliwa, Paulo alikuwa na haki ya kuomba rufani kwa Kaisari na kujaribiwa katika Roma. (25:10-12) Raia Mroma hakupasa kufungwa minyororo, kupigwa mijeledi, wala kuadhibiwa bila kujaribiwa.—16:35-40; 22:22-29; 26:32.
[Hisani]
Musei Capitolini, Roma
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
MTUNZA-HEKALU WA ARTEMI: Kwa kuudhiwa na kuhubiri kwa Paulo, Demetrio mfua-fedha alichochea ghasia. Lakini karani wa rekodi za jiji la Filipi akatawanya umati huo. (19:23-41) Wafua-fedha walifanyiza viabudiwa vya fedha vya sehemu iliyo takatifu zaidi ya hekalu mlimokuwamo sanamu ya Artemi mungu-mke wa nguvu za uzazi aliye na matiti mengi. Majiji yalishindana ili yapate heshima ya kuwa ne·o·koʹros au “mtunza hekalu” wake.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
MATATA BAHARINI: Meli yenye kubeba Paulo ilipotandikwa na upepo wenye dhoruba kali uitwao Euroakilo, ‘ilikuwa vigumu kwao kuweza kuiongoza mashua kwa usukani.’ (27:15, 16, NW) Hiyo ilikuwa mashua ndogo ambayo kwa kawaida ilivutwa na chombo. Meli ilibeba kebo ambazo zingeweza kupitishwa kwa kuzunguka fremu ya meli ili kuifunika chini na kuizuia isisuguliwe sana na mlingoti wakati wa dhoruba. (27:17) Mabaharia hawa walitupa nje nanga nne na wakalegeza mashikio ya makasia ya usukani, yaliyotumiwa kuongoza chombo. (27:29, 40) Meli ya Aleksandria yenye umbokichwa lililoandikwa “Wana wa Zeu”—Castor na Pollux, walioonwa kuwa walinzi wa mabaharia.—28:11.