Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 5/1 kur. 195-198
  • Sababu Mungu Mwenye Upendo Hukaripia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sababu Mungu Mwenye Upendo Hukaripia
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ‘KAMA VILE BABA AKARIPIAVYO MWANAWE’
  • WACHUNGAJI WA KUBURUDISHA NA KULINDA KUNDI
  • Waonaje Adabu?
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
  • Nidhamu Inazaa Tunda Lenye Kuamanika
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • ‘Makaripio Ndiyo Njia ya Uzima’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Wenye Furaha ni Wale Ambao Mungu huwatia adabu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 5/1 kur. 195-198

Sababu Mungu Mwenye Upendo Hukaripia

“Ee [Yehova], heri mtu yule umwadibuye, na kumfundisha sheria yako.”​—Zab. 94:12.

YEHOVA MUNGU ataka watu waishi, naam, wafurahie maisha. Yeye hafurahii hata kifo cha waovu, bali “aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi.”​—Eze. 33:11.

Kwa sababu ya kuhangaikia wanadamu hivyo, Mungu alitoa ukombozi kwa kumtumia Mwanawe mpendwa atoe uhai wake mwenyewe mkamilifu kama dhabihu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu [yaani wanadamu], hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”​—Yohana 3:16.

Kupendezwa na wanadamu hivyo ndiko humfanya Mungu awakaripie na kuwatia adabu. Ni wazi kabisa kwamba hakuna ye yote kati yetu aliye mkamilifu. Mara nyingi sisi hupungukiwa, tunashindwa kufanya mambo jinsi tunavyojitahidi tuyafanye, na hiyo ndiyo maana halisi ya maneno ya Kiebrania na Kigiriki ya “dhambi,” yaani, “kukosa shabaha.” Kwa hiyo, sote twahitaji kusahihishwa na kutiwa adabu. Yatupasa tushukuru kwa jambo hilo kwa maana laonyesha Mungu anatupenda, nalo kusudi lake si kutuadhibu tu, bali kutuzoeza katika haki kama baba azoezavyo wanawe.​—Ebr. 12:5-11.

Kwa mfano, fikiria mtu akiwa mashuani, akiwa peke yake baharini na kupungukiwa na chakula na maji. Akipotea njia ashindwe kurudia nchi kavu, atakufa. Bila shaka yampasa ashukuru mtu fulani akimtolea ishara ya kufuata njia inayofaa, na kuokoa maisha yake. Angekuwa mpumbavu kuchukia au kukataa sahihisho hilo lenye kumfaa.

Vivyo hivyo, kwa kuwa sote tulirithi dhambi tunahitaji kusahihishwa kwa kawaida ili tuingie katika njia nyembamba iongozayo uzimani, au tudumu ndani yake. Tusiposahihishwa bila shaka tutaingia katika njia iongozayo uharibifuni.​—Mt. 7:13, 14.

Tangu utoto na kuendelea inaonekana wazi wanadamu hawakukamilika na wanahitaji kusahihishwa. Ndiyo sababu, kama mzazi ye yote awezavyo kuthibitisha, upendo mwingi sana unatakiwa ili kumlea mtoto ifaavyo, kukaza thamani ya kanuni za haki katika akili na moyo wake. Mithali 22:15 inasema kweli itajapo kwamba “ujinga umefungwa ndani ya moyo” wa mtoto, naye mtoto ataweza kuongozwa na matukio halisi ya maisha akitiwa adabu, badala ya kuongozwa na mawazo ya kipumbavu na ya kitoto.

Hayo yote yanajaribu saburi na nia ya mzazi ya kuwa mstahimilivu anapofundisha na kuelimisha mtoto afuate njia ya maisha itakayomletea furaha wakati ujao. Mtoto akiitikia polepole, asiposikiliza na kukataa kutii, huenda mzazi akajisikia anataka kuacha kumsaidia; huenda akaelekea kudhani ni kazi bure. Huenda akaudhika au akakasirika kwa urahisi. Lakini upendo haufanyi mtu akate tamaa kwa sababu hali inachukiza tu. Mzazi akikosa kumpa mtoto mafundisho anayoyahitaji na adhabu aliyofikiria vizuri kwa saburi, angeonyesha hampendi mtoto wake, kwa sababu upendo huendelea kutafuta faida bora za sasa na za wakati ujao, za mwenye kupendwa. (Tazama Mithali 13:24.) Tena, upendo “hauoni uchungu; hauhesabu mabaya.” “Hutumaini yote.”​—1 Kor. 13:5, 7.

Kwa hiyo mzazi mwenye upendo huendelea kuwa na tumaini kwamba mtoto wake atakuwa mwema maadamu kuna msingi wa kuwa na tumaini hilo. Akina baba na mama wanaojali kweli kweli hawachoshwi na mtoto wao ye yote; hawaepuki kumpa uongozi na sahihisho analohitaji kwa akili na upendo. Wanaonyesha sifa ya ustahimilivu.

‘KAMA VILE BABA AKARIPIAVYO MWANAWE’

Lo! inaburudishaje kusimama na kufikiria kwamba wakati wazazi wanaposaidia mtoto hivyo, wanafuata mfano bora wa Mungu mwenyewe! Kwa sababu yeye hachoshwi na watumishi wake kwa urahisi; bali, yeye huwaonyesha ustahimilivu mwingi ajabu. Hivyo, siku za Nehemia, wakati Walawi walipokuwa wakisali kwa Mungu, walitaja mambo yaliyowapata Waisraeli katika jangwa la Sinai wakasema:

“Wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu . . . wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.”​—Neh. 9:16, 17.

Zaidi ya Mungu kuwa mwenye saburi, twaweza kuona kwamba, ingawa adhabu na sahihisho analotoa kama baba laweza kumletea maumivu mwenye kusahihishwa, sikuzote linakuwa na kusudi jema. Yeye anaadhibu na kusahihisha watu ili kuwafaidi. Ndiyo sababu Mithali 3:11, 12 inasihi hivi: “Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na [Yehova], wala usione ni taabu kurudiwa naye. Kwa kuwa [Yehova] ampendaye humrudi, kama vile baba mwanawe ampendezaye.”​—Linganisha Waebrania 12:5-11.

Kwa hiyo Mungu si mtawala mwenye kukasirika sana akitaka kujilipiza kwa sababu mtu fulani amekosa kuheshimu sheria zake. Ni kweli kwamba Mungu hukasirishwa na dhambi kubwa, tena ana haki ya kukasirishwa nayo. (Hes. 25:1-3) Lakini hakasiriki kwa sababu ya choyo wala kwa sababu ya kiburi. Yeye ajua kuliko mtu mwingine ye yote matokeo mabaya sana yanayoweza kuletwa na dhambi, anajua jinsi maongozi ya dhambi yanavyoweza kuleta msiba mkubwa, jinsi yanavyoharibu furaha ya wanadamu. Kudharau enzi kuu yake hakuwezi kufaidi mtu, kwaweza kumdhuru tu. Kunamdhuru mwenye kuzoea dhambi na wengine pia. Kwa hiyo Mungu mwenye upendo lazima achukie dhambi, naye hawezi kuiachilia hivyo tu. Ingawa Mungu “si mwepesi wa hasira,” wakati anapochukulia mtu hatua kwa sababu ya dhambi anafanya hivyo azuie madhara zaidi yasitokee.​—Kut. 34:6; linganisha Zaburi 106:36-40.

Si hilo tu bali Yehova hupima pia ukali (au upole) wa karipio lake, si kulingana na utaratibu usioweza kubadilika, bali kulingana na uhitaji uliopo. Akitumia mfano wa mkulima, Yehova asema katika Isaya 28:23-29 hivi:

“Tegeni masikio, sikieni sauti yangu, sikilizeni mkasikie neno langu. Je! mwenye kulima alima daima, ili apande? afunua daima madongoa ya nchi yake, na kuyavunja? Akiisha kuulainisha uso wa nchi yake, je! hamwagi huko na huko kunde, na kutupa-tupa jira na kuitia ngano safu safu, na shayiri mahali pake palipochaguliwa na kusemethi karibu na mipaka yake? Kwa maana Mungu wake anamwagiza vizuri na kumfundisha. Kwa maana kunde zile hazipurwi kwa chombo kikali, wala gurudumu la gari halipitishwi huko na huko juu ya jira ile, bali kunde zile hupurwa kwa fimbo, na jira ile kwa ufito [kifikichio, NW]. Ngano ya mkate husagwa; kwa maana haipuri sikuzote bila kukoma; na ingawa gurudumu la gari lake na farasi wake huitawanya ngano ile, haisagi. Hayo nayo yatoka kwa [Yehova] wa majeshi, mwenye shauri la ajabu, apitaye wote.”

Mkulima haendelei kulima udongo bila kuacha, bali huulima kadiri kulivyo na uhitaji. Mkulima Mwisraeli alitawanya au akatupa mbegu ndogo zaidi katika eneo kubwa, lakini mbegu nyingine zenye kuthaminiwa zaidi zilipangwa safu safu. Na wakati wa kutwanga, mbegu zile ndogo au nyororo zaidi hazikutwangwa kwa chombo kizito ambacho kingezisaga, bali hutumia fimbo au kijiti cha kufikichia. Hata mbegu kubwa na ngumu zaidi zilizotwangwa kwa vyombo vizito, kama ubao wa kutelezea au gurudumu la gari, hazikutwangwa hata zikasagika kabisa. Kwa hiyo, Yehova pia hupima karipio, adhabu na sahihisho kwa hekima, haki na upendo​—kuona kama litakuwa jepesi, la kiasi, zito au hata kali​—kulingana na uhitaji wa kila hali moja moja. Wale wanaopinga kwa makusudi jitihada yake yenye saburi ya kuwasaidia ndio peke yao watakaoharibiwa naye.

WACHUNGAJI WA KUBURUDISHA NA KULINDA KUNDI

Ni vizuri sana pia kuangalia mfano wa Mwana wa Mungu, “Mchungaji mwema” wa kondoo za Mungu! (Yohana 10:11) Alipokuwa duniani alionyesha sifa za Mungu akawekea mfano wote wale ambao wangekuwa wachungaji katika kundi la Kikristo. Yeye alishughulikaje na hata sasa anashughulikaje na wanaokuwa wanafunzi wake? Yeye mwenyewe alitoa ukaribishaji mchangamfu huu:

“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”​—Mt. 11:28-30.

Nia yake yenye kuburudisha watenda dhambi wenye kutubu yaonyeshwa katika mfano wa mtu apotezaye kondoo mmoja kati ya mia na kuacha wale 99 akamtafute aliyepotea. Akiisha kumpata kondoo aliyepotea mtu huyo hampigii makelele wala hampigi mateke kwa sababu alipotea, bali, kama Yesu alivyosema, “humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.” Yesu aliendelea kusema kwamba “vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.”​—Luka 15:1-7.

Mtume Paulo alisema kila mzee Mkristo atakiwa ‘kulishika sana lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na [kuwakaripia, NW] wenye kupinga.’ (Tito 1:9) Naam, nyakati nyingine huenda ikawa lazima wazee wakaripie watu fulani katika kundi wanalotumikia. Wao hawafurahishwi na kukaripia watu, wala hilo si jambo jepesi. Lakini wanajua kwamba “makaripio ya kutia adabu ndiyo njia ya uzima,” na kwamba ‘wote wapendwao na Yehova hukaripiwa naye,’ kutia na wazee wenyewe. (Mit. 6:23; 3:11, 12, NW; Ebr. 12:6) Wanauona ukweli wa kwamba “yeye anayekaripia mtu atapata baadaye upendeleo zaidi kuliko yule anayejipendekeza kwa ulimi wake.” (Mit. 28:23, NW) Kwa hiyo wazee hawaachi kuwaonyesha waziwazi wenye kufanya makosa jinsi wanavyoweza na wanavyopaswa kusahihisha mwendo wao, hali zinapofanya iwe lazima kuwaonyesha. (Mit. 27:5) Wao wanakuwa na mradi mwema wa kufanya hivyo, kama Mungu.

Mzee apaswa kufikiaje mtu ambaye amefuata mwendo mbaya? Mzee akiwa na nia ya kujiona mkubwa zaidi, kama polisi anayeshughulika na mhalifu au wakili mwenye kushtaki mtu anayedhaniwa kuwa mkosaji, matokeo hayatakuwa yenye faida. (1 Pet. 5:2, 3, 5) Lakini mzee akionyesha huruma, akijua kwamba yeye mwenyewe hajakamilika, kwamba aweza kufanya kosa, ataonyesha roho ya kidugu. (Gal. 6:1) Yeye yupo pale kusaidia, si kulaumu, naye mkosaji ataelekea zaidi kuitikia njia hiyo. (1 Pet. 3:8) Kila hali iko tofauti naye mtu mwenye hekima atatafuta kupata maarifa na ufahamu juu ya hali zinazohusika, si kufanya haraka haraka ya kuamua hivi au vile.​—Mit. 18:15; 21:11.

Ingawa huenda mwenye kukosa akawa hataki kuongea au hata akawa akiepa kidogo, saburi na fadhili zinaweza kusaidia sana kumaliza tatizo hilo. (Mt. 25:15; 2 Tim. 2:24-26) Apaswa kusadikishwa kwamba wazee wanataka afaidike kweli kweli; wao ni ndugu zake. Hata ikiwa hali zahitaji apewe mashauri makali, akaripiwe vikali, ni jambo la maana mzee akumbuke sikuzote kosa ndilo linalochukiwa na kulaumiwa, si mtu mwenyewe. (Yuda 23) Bila shaka, wale wanaokataa jitihada zote za kuwasaidia, wanaokuwa wakaidi wasitubie kosa zito, wanajionyesha kuwa hatari kundini na kuonekana wataharibu faida zake, hivyo wanahitaji kutengwa na ushirika. Hata inapokuwa hivyo mashauri ya Maandiko yanaweza kutolewa na yapaswa yatolewe kuwafahamisha kwamba wakitubu kwa unyofu wanaweza baadaye kurudishwa kundini.

Lakini ni nini maana ya ‘kukaripia’ mtu hasa? Katika kundi la Kikristo, je! kusudi la karipio ni kuaibisha hasa au kukemea mtu? Je! kutoa “karipio” kungekuwa kutangaza tu kwamba mtu fulani ameingia katika mwenendo mbaya na kuonyesha mwenendo huo unakataliwa? Tutaona sasa yanayoonyeshwa na Biblia.

[Picha katika ukurasa wa 196]

“Kwa kuwa [Yehova] ampendaye humrudi, kama vile baba mwanawe ampendezaye.”​—Mit. 3:12.

[Picha katika ukurasa wa 197]

KITELEZEO

KIFIKICHO

FIMBO

GURUDUMU

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki