Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w77 12/1 kur. 547-549
  • Usimdharau Maskini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Usimdharau Maskini
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KUHESABU UBORA WA MTU
  • MUNGU ANA MAON! GANI?
  • KUHESHIMIANA
  • Baraka ya Yehova Inatajirisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Je, Ni Lazima Wakristo Wawe Maskini?
    Amkeni!—2003
  • Je, Wewe Ni “Tajiri Kwa Mungu”?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
  • Usiache Utajiri Wala Umaskini Uwe Uangamivu Wako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
w77 12/1 kur. 547-549

Usimdharau Maskini

WEWE ungeonaje rafiki yako, mfanya kazi asiye na mshahara mkubwa akirudi kutoka likizoni akiendesha motokaa ya anasa, ya shilingi 160,000 (17,-000Z)? Klabu ya motokaa ya Ujeremani ya Magharibi ilitaka kujua jinsi watu wangeona mtu maskini akiendesha motokaa ya bei kubwa sana. Basi, muda wa juma tatu ilitayarisha motokaa ya namna hiyo itumiwe na mtayarishaji wa habari za kompiuta asiyepata mshahara mkubwa, aliyekuwa akiendesha motokaa ndogo. Alikuwa akiishi katika ujirani wa Munich usio wa matajiri, naye hakupasha jirani, watu wa ukoo na wafanya kazi wenzake kwamba angetayarishiwa motokaa ya namna hiyo.

Watu fulani waliomfahamu walichukia kumwona akiwa katika gari hilo la bei. Wengine waliona mashaka juu ya jinsi alivyolipata. Lakini mambo mengine yalitokea pia. Kwa mfano, hoteli moja ilikuwa imepigiwa simu kuulizwa kama ina nafasi ya mahali pa kulala ikasema nafasi imekwisha, lakini watu waliokuwa wakiendesha gari hilo la bei walipokuja walitafutiwa chumba. Vilevile, mlinzi mmoja ambaye hapo kwanza alikuwa amewaambia waondoe kigari chao katika maegesho ya magari nje ya hoteli hiyo hakusema lo lote walipoegesha gari lao la bei.

Naam, watu walitenda mambo tofauti wakati wa jaribio hilo. Hakika wengine wao walibadili maoni yao kwa sababu sasa watu hao walikuwa matajiri. Walikuwa na nia ya kuwaheshimu sana kwa sababu ya utajiri.

KUHESABU UBORA WA MTU

Lakini, tafadhali fikiria maoni yako mwenyewe. Wewe unahesabu ubora wa mtu namna gani? Je! unadhani unaweza kujua ubora wa mtu kwa sababu ya mali zake? Kabla hujajibu, jiweke katika hali hii: Tuseme wewe ulikuwa katika kizazi chenye pendeleo la kuishi katika jimbo la Kirumi la Uyahudi wakati wa karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida. Walikuwa na nafasi ya kumtambua Masihi aliyetumwa na Yehova Mungu akakomboe wanadamu. (Yohana 3:16) Masihi alikuwa katikati ya Wayahudi hao, nalo tumaini lao la kupata uzima wa milele lilitegemea kuweza kufahamu sifa bora zilizomtofautisha sana na wanadamu wengine wote.

Inaonekana kwamba Wayahudi wengi walidhani Masihi angeweza kuwa mtu tajiri tu, mwenye mamlaka. Walimdharau Yesu, wakamwona kama “ka-mtu” tu ka Nazareti! Wao walimwona kuwa mwana wa seremala maskini, Yusufu, aliyelazimika kufanya kazi nyingi ili kupatia jamaa yake riziki. (Mt. 13:55) Lakini Yesu alitiwa mafuta na roho takatifu ya Mungu alipobatizwa akiwa na umri wa miaka 30. (Mt. 3:13-17) Nao waliomkubali Yesu kuwa Masihi, mtiwa mafuta wa Mungu, walilazimika kumtumaini mtu maskini. Badala ya kuwa na mali, mashamba na nyumba, yeye ‘hakuwa na pa kujilaza kichwa chake.’​—Luka 9:58.

Ijapokuwa kulikuwa na ushuhuda mwingi sana, hata miujiza, yenye kuhakikisha kwamba Yesu alikuwa ndiye Masihi, watu wa siku zake waliona hakufaa kitu, wakamtoa auawe kifo cha aibu pamoja na wavunjaji sheria wa kawaida. (Yohana 12:37) Huo ndio uliokuwa mwisho wa dharau kwa mtu waliyedhani hakuwa na kitu bora cha kufaidi wenzake. Kama wewe ungalikuwako, ungalimdhihaki Yesu, kama watu wengi walivyofanya? Au, ungalifahamu ubora wake na kuwa mmoja wa wanafunzi wake?

Ni wazi kwamba si hekima kuhesabu ubora wa mtu kwa kutegemea mali alizo nazo. Kupata utajiri hakuonyeshi mtu amepata ujuzi, uamuzi mzuri au uwezo wa kuongoza watu. Matajiri wengi walirithi tu utajiri wao. Kwa hiyo, utajiri wao hauonyeshi kwamba wana ujuzi. Tena ni mara ngapi tunaposikia habari za biashara za udanganyifu zinazofanywa na matajiri fulani ili kujiongezea utajiri? Mara nyingi sana matajiri hawaadhibiwi wanapovunja sheria, kwa sababu wanahonga wanaopaswa kufikiliza hukumu! Kwa hiyo mtu anapodhani kwamba tajiri anapaswa kuheshimiwa kwa sababu ya utajiri wake, anakuwa na maoni mabaya juu ya wengine.

Ndivyo ulivyo upande ule mwingine. Kuwa maskini hakuonyeshi kwamba mtu ameshindwa kupata mali. Huenda akawa ameamua kuishi maisha ya kiasi. Huenda yeye mwenyewe akawa ameamua kuepuka masumbufu na migogoro inayotokana na kutafuta mali yake. Au, huenda akawa na afya mbaya, asitake kutumia nguvu nyingi akitafuta mali. Labda anabaguliwa vibaya kwa sababu ya kabila au taifa. Huenda mapato yake ya kiasi yakaonyesha kwamba yeye hataki kutumia ujanja ili kuwa na mali nyingi kuliko watu wengine. Huenda akaona ni afadhali kutumia wakati mwingi akiwa pamoja na jamaa yake badala ya kutafuta pesa nyingi zaidi za kuwapelekea. Kwa hiyo, mtu akikosa utajiri hiyo haina maana ya kwamba ameshindwa kuupata.

Basi, kwa sababu gani watu wengi wana maelekeo ya kuheshimu zaidi matajiri, kama wengine walivyofanya wakati wa jaribio la motokaa lililotajwa? Wanadamu wana maelekeo ya kuwa wachoyo kwa sababu ni watenda dhambi. Mithali moja ya Biblia inasema hivi: “Maskini huchukiwa hata na jirani yake; bali tajiri ana rafiki wengi.” (Mit. 14:20) Tajiri anaweza kuwapa watu zawadi. Kwa hiyo nyakati zote anapata watu wa kuwa pamoja naye, watu wa kumsifu-sifu kwa kutumia ulimi mwororo. Lakini inakuwaje utajiri wake umalizikapo kwa ghafula? Wengi wa wanaoitwa “rafiki” zake wanamalizika pia. Pesa zake zinapokwisha, hakuna anayetaka kuwa rafiki yake. Kwa hiyo, ikiwa sisi tuna maelekeo ya kufurahisha matajiri, na tukumbuke kwamba watu wamekuwa na maelekeo ya kusifusifu matajiri muda mrefu ili kujifaidi wenyewe. Kutumia “maneno ya kujipendekeza” au “maneno ya juujuu ya kuficha choyo” hakupatani na uungu.​—1 The. 2:5.

MUNGU ANA MAON! GANI?

Je! utajiri unatofautisha watu machoni pa Yehova Mungu? Je! tunaweza kumpa mali yo yote asiyokuwa nayo? Wapi! Kwa kuwa ‘yeye ndiye aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo,’ ana haki ya kudai utajiri wote uliomo. (Zab. 50:7-12, tafsiri ya New World; Matendo 17:24) Kujaribu kununua upendeleo wa Mungu bila unyofu wa moyo na matendo ya kimungu ni sawa na kumhonga. Lakini “kwa [Yehova], Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.” (2 Nya. 19:7) Utajiri haufanyi mtu apate hukumu nzuri zaidi kutoka kwa Mungu.

Vilevile, umaskini hauzuii mtu asihukumiwe vizuri. Maskini hawana haja ya kuogopa kwamba cheo chao cha chini kinawazuia wasistahili kupata kibali ya Mungu. Zaburi 69:33 inatuhakikishia kwamba ‘Yehova huwasikia wahitaji.’ Mungu hapendelei matajiri kuliko maskini. “Tajiri na maskini hukutana pamoja; [Yehova] ndiye aliyewaumba wote wawili.” (Mit. 22:2) Wakati Yehova anapotoa hukumu, yeye hatazami jinsi mfuko wa mtu umetoboka au jinsi wa mwingine umejaa pesa. ‘Anauchunguza moyo, kumpa kila mtu kiasi cha njia zake.’​—Yer. 17:10.

Yesu Kristo ana maoni yaliyo sawa na ya Baba yake. Kristo alikaribisha watu wote wamjie wapate burudisho la kiroho, matajiri kwa maskini, vijana kwa wazee, wafungwa kwa mahuru. (Mt. 11:28) Matajiri na maskini, walifaidika kutokana na mafundisho na miujiza yake. Waliokuwa matajiri zaidi hawakupendelewa zaidi ya maskini wala maskini hawakupendelewa zaidi ya matajiri. Wote walipewa nafasi ya kuzisikia habari njema na kuzikubali, naye Yesu aliwafundisha kupenda jirani zao kama nafsi zao wenyewe.​—Mt. 22:39.

Kwa kuwa matajiri wengi walimpuza Yesu, watu maskini wenye hali za chini ndio waliofaidika zaidi kutokana na uangalizi wake. Aliwalaumu waandishi na Mafarisayo wanafiki kwa sababu walikuwa na pupa ya kujidaia vilivyo bora. (Mt. 23:2-7) Vilevile, yeye hakuwaachilia wanafunzi wake wakati walipotaka kuwa wakubwa kuliko wenzao.

KUHESHIMIANA

Ili tuhukumiwe vizuri na Yehova Mungu, lazima tutendee watu haki, bila upendeleo. “Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake,” lakini “yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.” (Mit. 17:5; 14:31) Yehova anawapa thawabu wale wanaohurumia wenye shida, tena “mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu.” (Mit. 28:27) Ibada yetu inaweza kuwa ya bure tu tukifanya “ubaguzi” unaoshushia wengine heshima.​—Yak. 3:17, tafsiri ya New World.

Kwa hiyo, Wakristo wanafurahi kueleza watu wote habari njema za ufalme wa Mungu, ikiwa wanataka kusikiliza. Wao wana nia ya kutembelea watu katika makao ya maskini, vilevile makao ya wenye mali. Wanamwona kila mtu kama mmoja wa wale waliofiwa na Yesu. (Mt. 20:28) Watu wo wote wanaoonyesha sifa kama za kondoo wanastahili kupewa misaada yote ya kiroho inayotolewa na kundi la Kikristo.

Kundi halina nafasi ya kutenda matendo ya upendeleo. Katika karne ya kwanza W.K., wenye kupendelea matajiri waliambiwa waziwazi kwamba walikuwa wakitenda dhambi. (Yak. 2:1-9) Maskini na matajiri pia wanapaswa kupokea uangalizi wa kiroho bila upendeleo.​—Law. 19:15.

Maskini wanahitajiwa katika kundi. Kwa hiyo, wasitengwe kando peke yao ili matajiri washirikiane na matajiri wenzao tu. “Maskini” walikuwa kati ya watu ambao Yesu alipendekeza wakaribishwe karamuni, ili kuonyesha ukaribishaji wa kweli. (Luka 14:12-14) Tena, ikiwa Wakristo fulani wamepata mali ambazo waamini wenzao hawawezi kuzipata, ‘hawatajionyesha mali zao.’​—1 Yohana 2:16, tafsiri ya New World.

Basi, wewe unaheshabu ubora wa mtu namna gani? Mtazame sana alivyo, wala usitazame vitu alivyo navyo. Amua ubora wake kwa jinsi ameweza kusitawisha sifa za Kikristo. Je! anamwogopa Yehova? (Zab. 111:10) Je! ana imani yenye nguvu? (Ebr. 10:38, 39) Je! ni mkaribishaji? (Rum. 12:13) Je! anaonyesha watu fadhili, na je! ana nia ya kuwasamehe? (Efe. 4:32) Je! yeye ana sifa ya kusema kweli, kusema mambo yanayofaa? (Efe. 4:29; Tito 2:6-8) Je! mtu huyo anaonyesha upendo ambao unapasa utambulishe wanafunzi wa Kristo? (Yohana 13:35) Hakika huyo ndiye mtu unayepaswa kutaka awe rafiki yako!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki