“Mwe na Chumvi Ndani Yenu”
1. “Maneno” yetu yanapaswa yakolezwe kitu gani, na kwa sababu gani?
CHUMVI ya vitu vilivyo hai kama mboga ni ya maana sana kwa afya ya miili yetu. Kuna chumvi fulani iliyo ya maana sana kwa afya ya tengenezo la waabudu wa Mungu. Jambo hilo linapatana na shauri lililotolewa na mmoja wa walinzi wakubwa sana wa afya ya kiroho ya kundi la Kikristo la karne ya kwanza, yaani, mtume Paulo. Alipokuwa akiandikia kundi ambalo hakuwa amefahamiana nalo, alisema hivi: “Maneno yenu yawe na neema sikuzote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.”—Kol. 4:6.
2. Kwa hiyo ni ulizo gani linalotokea juu ya mitume waliojaribu kuzuia mtu fulani asifukuze mashetani kwa kutumia jina la Yesu?
2 Hiyo inatufanya tushangae ni kwa kadiri gani “munyu” huo ulikolea maneno ya watu wakati wa kisa ambacho mtume Yohana alimtajia Mwalimu wake, Yesu Kristo. Juu ya wakati huo tunasoma hivi: “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.”—Marko 9:38.
3, 4. Labda Yohana alikuwa akitazamia nini, na kwa sababu gani? (b) Yohana alionyesha choyo gani katika maelezo yake, na maelezo hayo yanaonyesha alikuwa na maoni gani?
3 Inasikika kama kwamba Yohana alikuwa akitazamia asifiwe, apigwe-pigwe mgongoni akisifiwa na Mwalimu aliyekuwa akiwafundisha njia ya Kikristo. Labda Yohana alifikiria jinsi Yesu alivyomponya yule kivulana aliyekuwa na shetani mwenye kichwa kigumu sana, huko kaskazini karibu na Kaisaria Filipi. Labda alidhani alikuwa akilinda haki ya Yesu isitumiwe na watu wengine kufukuza roho wachafu au mashetani katika watu walio hoi. Kwa maoni ya Yohana, mtu asiyepewa ruhusa na Yesu hakuwa na haki ya kutumia jina lake kuu kufukuza mashetani waovu. Lakini sababu ambayo Yohana alitoa ya kujaribu kumzuia mtu huyo asiyetajwa jina asifukuze mashetani inaonyesha alikuwa na choyo. Yohana alisema kwamba walimzuia mtu huyo “kwa sababu hafuatani nasi.”
4 Yohana alipotaja neno “nasi” alionyesha kwamba hakuwa akimfikiria Yesu tu, bali aliwafikiria pia mitume wote kumi na wawili. Wakati fulani uliotangulia Yesu alikuwa amewatuma mitume hao kumi na wawili wakazihubiri habari njema za Ufalme na kuponya watu, hata kuwakomboa na mashetani waliokuwa ndani yao. (Mt. 10:1-8; Marko 6:7-13) Kwa hiyo Yohana aliwaona mitume kama kikundi cha pekee chenye haki ya kuponya watu.
5. Ili kuwapa uongozi mitume wake wenye hasira na juhudi, Yesu alisema nini juu ya mtu huyo?
5 Basi, kama Yohana na mitume wenzake walivyowaza, mtu huyo alikuwa na haki gani ya kutumia jina la Mwalimu wao ili kufukuza mashetani? Walidhani kwamba kwa kufanya hivyo alikuwa akiingilia haki za Yesu na mitume wake. Lakini, je! ndivyo Yesu alivyoliona jambo hilo? Maandishi ya Biblia yanaonyesha kwamba hakukubaliana na mitume wake wenye hasira na juhudi. Marko 9:39-41 inaendelea kunena kwamba, Yesu alisema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake.”
6. Kwa kutumia jina la Yesu kufukuza mashetani, mtu huyo alikuwa akilifanyia nini jina hilo?
6 Kwa sababu gani mtu huyo azuiwe kuendesha kazi yake ya kufukuza mashetani kwa jina la Yesu? Je! alikuwa amekuwa akijaribu kutukana jina la Yesu kwa kufanya hivyo? Je! alikuwa amekuwa akichafua jina la Masihi, kuliletea sifa mbaya? Yeye hakuwa akilitumia jina la Yesu kama walivyofanya baadaye wale wana saba wa Skewa kuhani mkuu Myahudi, wakilitumia kama jina la kufanyia miujiza ya kiuchawi. (Matendo 19:13-16) Shetani huyo hakumwambia mtu huyo hivi: ‘Yesu namjua, lakini wewe ni nani?’ kisha akakataa kumtoka mtu aliyemwingia. Mtu huyo alikuwa na imani kabisa katika jina la Yesu, basi alifaulu kufukuza mashetani. Kwa kufanya hivyo alikuwa akitukuza jina la Yesu, kuonyesha wazi uwezo wa jina hilo.
7. Ingawa mtu huyo hakuwa akifuatana na Yesu na mitume wake, kwa sababu gani alikuwa akiwaunga mkono?
7 Kwa hiyo, mtu huyo asiyekuwa akifuatana na Yesu na mitume wake hakuwa akiwapinga wala hakuwa akizuia watu wasiifikirie kazi yao ya kutoa ushuhuda. Basi, ikiwa hakuwa akiwapinga, ni wazi kwamba alikuwa akiwaunga mkono, ingawa hakuwa akifuatana nao. Ingaliweza kuwa vigumu kutazamia kwamba safari hii alikuwa akifanya miujiza ya kutukuza jina la Yesu na kulisifu, halafu safari ile nyingine akawa akimnenea Yesu mabaya. Tungekuwa tukijipinga, tena tungekuwa hatuna kiasi tukitazamia kwamba mtu huyo alikuwa akifanya mwujiza mkubwa ili kuletea jina hilo heshima, halafu baadaye akiwa peke yake akawa akilinenea jina hilo mabaya na kufanya mambo ya kumpinga mwenye jina hilo pamoja na mitume wake. Kwa hiyo mitume hawakupaswa kuendelea kumzuia.
8. Bila shaka mtu huyo angepewa thawabu kulingana na kanuni gani?
8 Mtu huyo asiyetajwa jina asingekosa kupewa thawabu ya kazi aliyokuwa akifanya. Ni wazi kwamba alikuwa akielekea kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo. Alikuwa akifanya jambo zuri kama lile ambalo Yesu alisema lilistahili thawabu, yaani, kumpa mtu mwenye kiu kikombe cha maji kwa sababu ni mwanafunzi wa Kristo. Huenda hicho kikaonekana kuwa kitendo kidogo sana cha kusaidia mtu, lakini kingeonyesha mtu amemtendea Yesu Kristo jambo kubwa sana. Kingeonyesha kwamba mwenye kutoa maji alimpendelea Yesu kama Masihi na kutumia nguvu zake zote aunge mkono kazi ya Kristo. Kanuni iliyotolewa baadaye na Yesu inatumika hapa: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” (Mt. 25:40) Bila shaka Mfalme Yesu Kristo angewapa thawabu watu wa namna hiyo.
KUKWAZA WENGINE MAKUSUDI NA KUWAANGUSHA VIBAYA
9. Tunataka kujua nini juu ya lililompata mtu ambaye kazi yake ilikatizwa na mitume wa Yesu? Kwa sababu gani tunataka kujua?
9 Wakati mitume walipojaribu kumzuia mtu huyo asiendelee kufukuza mashetani kwa jina la Yesu, je! maneno waliyomwambia yalikuwa na neema, yakiwa yamekolea chumvi, au yakiwa yenye ladha nzuri? Tuna mashaka. Jambo tunalotaka kujua ni kwamba, Mtu huyo alikwazwa na maneno na matendo ya mitume alipokuwa akifanya kazi njema isiyokataliwa na Mwalimu wao? Hilo si jambo la mchezo, kwa maana Yesu aliendelea kusema: “Ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini.”—Marko 9:42.
10. Kukwaza makusudi mmojawapo wa “wadogo” wa namna hiyo kungekuwa sawa na kufanya nini, na kwa sababu gani?
10 Huenda mtu anayekwazwa na kuangushwa akawa ni ‘mdogo,’ lakini hiyo haionyeshi mwenye kumkwaza hakufanya jambo kubwa. Kwa sababu gani? Kwa sababu amekwaza “mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio.” Maana yake ni kwamba mtu huyo anaamini Yesu ndiye Mwana wa Mungu aliye Masihi. Imani ya watu “wadogo” namna hiyo inawaweka katika njia ya uzima wa milele. Kwa hiyo, mtu ye yote akiudhi sana mtu ‘mdogo’ namna hiyo na kumwondoa katika njia ya uzima wa milele, huo ungekuwa sawa na uuaji. Angeonyesha hampendi mtu aliyekwaza.
11. Kukwaza mtu bila kujua kunatofautianaje na kumkwaza makusudi?
11 Katika 1 Yohana 3:15 imeandikwa hivi: “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.” Huenda tukaudhi watu bila kujua—na hilo si jambo dogo—nasi tunatumaini kwamba hawataanguka waiache kabisa imani ya Kikristo. Tukijua kwamba tumewaudhi, tutachukua hatua za kumaliza jambo hilo. Lakini ikiwa mtu hajali hali ya kiroho ya mwamini mwenzake, huku akitoa ubishi na kusema kwamba kila mtu ana uhuru wa kutumia dhamiri yake na haki zake zote, anaonyesha kwamba hajali hata mtu huyo akipoteza uzima wa milele au uhusiano wake na Mungu. Anashusha ubora wa mwamini huyo aliyefiwa na Kristo.—Rum. 14:15.
12. Yesu alionyeshaje kwamba anachukizwa na mtu anayekwaza mwenzake makusudi na kumwangusha?
12 Itakuwaje mtu anayejiita Mkristo asipojali kukwaza “mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio” na kuonyesha kwa njia hiyo kwamba hajali hata mtu huyo akikosa uzima wa milele? Ikiwa yeye hajali, naye Yesu Kristo hajali uzima wake. Yesu alionyesha kwamba anaudhiwa na mtu mwenye kukwaza mwenzake kwa makusudi. Jinsi gani? Alisema kwamba ingekuwa vizuri zaidi na salama zaidi kwa wengine mtu huyo asiyejali akizamishwa katikati ya bahari, na kuzuiwa na jiwe kubwa la kusagia asije akaelea.
13. Hasa inatupasa tuangalie tusikwaze nani?
13 Kwa hiyo tunapata faida tusipokwaza wengine na kuwaangusha, hata mtu aliye mdogo sana. Wala haifai tujiache tukwazwe na watu ambao hatukutazamia kwamba wanaweza kutuudhi kwa sababu ni Wakristo. Lakini je! tunathamini sana matumaini yetu ya kupata uzima wa milele kiasi cha kujiangalia tusijikwaze wenyewe? Ala—tujikwaze wenyewe? Naam, ndivyo. Jinsi gani?
14. Kulingana na maonyo ya Yesu, tunaweza kujikwazaje wenyewe na kuanguka?
14 Baada ya kusema habari za kukwaza mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio,” Yesu aliongeza onyo hili: “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto.”—Marko 9:43, 45, 47-49.
15. Jehanum aliyotaja Yesu ni nini, naye aliitumia kama mfano wa nini?
15 Katika mifano hiyo, Yesu anataja uharibifu wa moto. Siku za Yesu, Jehanum au Bonde la Hinomu alilotaja lilikuwa kusini na magharibi ya kusini ya Yerusalemu. Maneno yake yanahakikisha kwamba Jehanum hiyo ilitumiwa kama tanuru ya kuchomea takataka za mji, na kwamba mizoga ya wavunja sheria walioonekana hawastahili kuzikwa kwa heshima wakiwa na tumaini la ufufuo ilitupwa humo. Ikiwa mzoga ulikosa kuanguka motoni, ukakwama katika mtelemko au ukingo wenye joto la moto wa Jehanum, ulioza na kuliwa na funza wenye kuzaana. Moto huo ulitiwa vitu vya kuufanya uwake nyakati zote, mchana na usiku, ili kuteketeza kabisa vitu vilivyotupwa katika bonde hilo la takataka za mji. Kwa hiyo Jehanum ikawa mfano wa uharibifu wa milele, kama wakati Yesu alipowauliza waandishi na Mafarisayo Wayahudi hivi: “Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?”—Mt. 23:33.
16. Ni kwa njia gani wanaotupwa katika Jehanum hawaingii uzimani wala katika ufalme wa Mungu?
16 Wanaohukumiwa kwenda Jehanum hawaingii katika ufalme wa Mungu kutawala mbinguni pamoja na Kristo wala kukaa duniani wakati wa utawala wake wa mileani moja. Wale wanaohukumiwa na Mungu kuingia Jehanum hawapati uzima hata kidogo, ingawa wanakuwa na viungo vyote vya miili yao. Kwa hiyo, Jehanum inafananisha hali ya kutokuwako, kuangamia, kuharibiwa na hukumu kali ya Mungu. Kama vile waandishi na Mafarisayo wanafiki wa siku za Yesu walivyojikwaza wakaingia Jehanum, Mkristo aliye wakf na aliyebatizwa anaweza leo kujikwaza mwenyewe ahukumiwe na Mungu kuingia Jehanum, yaani, kupata uharibifu wa milele. Na tumkumbuke Yuda Iskariote.
17. Yuda Iskariote alijikwazaje mwenyewe akaanza wivi?
17 Yuda huyo wa Keriothi alipata kuwa mweka-hazina wa Yesu na mitume wake kumi na wawili. Baada ya muda fulani alianza kutamani kilichowekwa katika sanduku la pesa. Basi alinyosha mkono akajitwalia kadiri alivyotaka, akazitia mfukoni. Aliacha jicho na mkono wake umkwaze aibe, hata akamnyang’anya Masihi wa Yehova. Siku tano kabla ya Yesu kufa, Yuda alisema maneno ya unafiki kujifanya anapenda kusaidia wenye shida, walipokuwa kwenye karamu ya kumheshimu Yesu katika Bethania (karibu na Yerusalemu). Tunasoma hivi: “Aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo.”—Yohana 12:6.
18. Mwishowe, Yuda aliacha viungo vya mwili vimkwaze na kumwingiza katika jambo gani, na kwa njia gani?
18 Mwishowe, akitafuta pesa zaidi, Yuda aliuacha mguu wake umpeleke akakutane na wakuu wa makuhani na wa hekalu, kisha akapiga nao bei ya kumsaliti Yesu Bwana wake kwa vipande 30 vya fedha. (Luka 22:1-6) Ndipo miguu ya Yuda ilipoongoza kikosi cha watu wenye silaha wakamkamate Yesu katika Bustani ya Gethsemane usiku wa Kupitwa, akiwa na kusudi la kupewa malipo ya usaliti katika mikono yake yenye kunyakua vitu. (Luka 22:47, 48; Marko 14:10, 11, 43-46; Mt. 26:14-16, 47-50; 27:3-5) Baada ya usaliti wake, Yuda alifurahi kwa muda kuvitazama vipande hivyo 30 vya fedha alivyokuwa ameshika kwa mikono yake mwenyewe. Sasa hakuwa na njia ya kubadili mambo ambayo jicho lake liliyafanya kwa kushirikiana na mkono wake na mguu wake. Alikuwa ameviacha viungo hivyo vya mwili vimkwaze na kumwingiza katika dhambi asiyoweza kusamehewa mtu. (Mt. 27:4) Hakuwa na tumaini, basi akajiua. Hata ikiwa mwili wake uliotokwa na matumbo haukutupwa katika Jehanum halisi ya Yerusalemu, “nafsi” yake iliharibiwa katika kilichofananishwa na Jehanum. (Matendo 1:16-19; Mt. 10:28, NW) Kweli Yesu alikuwa na haki ya kumwita “mwana wa upotevu.”—Yohana 17:12.
19. Yesu alikuwa na maana gani aliposema kwamba “lazima kila mtu atiwe chumvi kwa moto”?
19 Yesu alimaliza mazungumzo yake juu ya vile mwanafunzi anavyoweza kuacha mkono, mguu na jicho lake limkwaze na kumwingiza Jehanum kwa kusema hivi: “Kwa maana lazima kila mtu atiwe chumvi kwa moto.” (Marko 9:49, NW) Ndiyo kusema, kila mtu mwenye hatia ya kuacha viungo vya mwili vimkwaze hata asiweze kusimama alipaswa ‘kutiwa chumvi kwa moto.’ Moto ambao lazima atiwe chumvi kwao ni “moto” wa Jehanum ambao Yesu alikuwa ametaja muda mfupi tu kabla ya hapo. Mtu mwenye kutiwa chumvi kwa moto angepatwa na jambo gani? Asingekuwa sawa na yule mwenye kutiwa chumvi kwa chumvi. Huyu angeharibiwa. Wakati miji ya kale ya Sodoma na Gomora iliponyunyiziwa moto au ‘ikatiwa chumvi’ kwa moto kutoka mbinguni katika ujirani wa Bahari ya Chumvi, iliharibiwa. (Luka 17:28, 29) Kama vile Yehova anavyodumisha milele “agano la chumvi” lisilovunjika, ndivyo anavyoshikamana na kanuni hiyo ya kuharibu milele watu wanaojikwaza wenyewe.—Law. 2:13; Hes. 18:19; 2 Nya. 13:5.
20. Ili kujilinda tusije ‘tukatiwa chumvi kwa moto,’ tunawezaje kuuondoa mkono, mguu na jicho lenye kutukosesha?
20 Ili kujilinda tusije ‘tukatiwa chumvi kwa moto,’ tutaukataje mkono au mguu wetu wenye kutukosesha, au tutalitupaje jicho letu lenye kutukosesha? Hatuwezi kuondoa mawazo mabaya yanayoonyeshwa kupitia kwa mkono, mguu na jicho halisi kwa kuvikata vitu hivyo. Lazima tuviondoe kwa njia ya mfano. Mtume Paulo alituonyesha jinsi ya kufuata shauri la Yesu, akisema: “Basi, vifisheni [vitu gani?] viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu: kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.”—Kol. 3:5, 6.
21. Tunaifanyaje kazi hii ya ‘kufisha’ (kuua)?
21 Ili ‘kuvifisha’ viungo vyetu halisi vya mwili vilivyo duniani, inatupasa tuviweze sana vitu hivyo. Kwa mfano, lazima tuzuie macho yetu yasisome vitabu vyenye mambo ya uasherati wala yasitazame sinema chafu au maonyesho machafu ya televisheni, wala tusitumie mikono yetu katika wivi au ufisadi, wala tusifurahishe miguu yetu kwa kucheza dansi zenye kuamsha nyege wala tusiende na ‘rafiki wa ulimwengu huu’ katika maeneo ambako tunaweza kushawishwa. Lazima tuuue kiroho upendo wetu wa “vitu vilivyomo katika ulimwengu,” yaani, “tamaa ya mwili na tamaa ya macho na kujionyesha kwa mtu mali yake.”—1 Yohana 2:15-17, NW; Mit. 6:16-19.
“CHUMVI” INAYOPASWA KUWA NDANI YETU
22, 23. (a) Mwishowe, Yesu alitaja kutiwa chumvi kwa njia gani? (b) Ni chumvi ya namna gani ambayo Yesu aliambia mitume wake wawe nayo, na kwa sababu gani akawaambia wao?
22 Yesu hakumaliza mazungumzo yake kwa kutaja chumvi kwa njia mbaya. (Marko 9:33-49) Aliendelea kusema hivi: “Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena [au, ikiacha kuwa na uchumvi wake], mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.”—Marko 9:50, na maelezo ya pembeni katika tafsiri ya New World.
23 Chumvi halisi ni kikolezo kizuri kwa kawaida. “Je! kitu kisicho na ladha humkini kulika pasipo chumvi,” auliza Ayubu (6:6), “au je, uto wa yai una tamu iwayo yote?” Hakika chumvi inaweza kuongeza ladha ya vyakula. Lakini kama chumvi iliyotumiwa sana siku za Yesu ilimalizika nguvu, isingeweza kusafishwa iondolewe vitu vilivyochanganyika nayo, kwa hiyo haikufaa tena kutumiwa katika upishi wala ulaji. Chumvi yenyewe isingeweza kukolezwa tena iliwe na wanadamu. Basi ilifaa Yesu akatumia chumvi kama mfano. Aliwaambia mitume wake kumi na wawili hivi: “Mwe na chumvi ndani yenu.” Lakini kwa sababu gani Yesu aliwaambia wao hivyo? Ni kwa sababu walionyesha kwamba chumvi hiyo haikuwa ndani yao walipobishana wakati wa kurudi Kapernaumu.
24. “Chumvi” hiyo ya mfano ni nini?
24 Chumvi ya namna hiyo ilifananisha sifa ya utu wa mtu inayomfanya atendee watu mambo yenye kuwapendeza. Inafanya mambo anayosema yawe na ladha nzuri zaidi kwao na kumezeka kwa wepesi zaidi, kutumiwa kwa wepesi zaidi na akili zao. Basi sifa hiyo inawafanya wamfurahie, naam, watamani kuwa karibu naye.—Mit. 16:21, 23.
25. Kula pamoja hata chumvi halisi kulileta faida namna gani?
25 Kula chumvi pamoja, kama vile mkaribishaji na mgeni wake, kunaleta hali ya kufurahiana na uhusiano mzuri kati ya wenye kuila. Chumvi hata ilitumiwa wakati wa kulipa mfanya kazi mshahara wake. (Ezra 4:14) Mtume Paulo alitia mkazo kuonyesha kwamba ni jambo la maana sana tuwe na chumvi hiyo ya mfano katika utu wetu, alipoandika hivi: “Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema sikuzote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” (Kol. 4:5, 6) Angalia Mithali 15:1 pia.
26. Tukiwa na “chumvi” ya mfano ndani yetu, tunasaidika tufuate onyo gani la mwisho ambalo Yesu aliwapa mitume wake kwa upole, na kwa kufanya hivyo sisi wanafunzi wake tutakuwa na hali gani?
26 Tukiwa na “chumvi” ndani yetu na kuitumia kukoleza maneno yetu, tutasaidika tufanye alivyosema Yesu alipokuwa akimaliza kuongea na mitume wake kumi wawili: “Mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.” (Marko 9:50) Sisi wanafunzi wa Kristo tutaendelea kuwa na uhusiano wenye amani tukiwa wenye busara, tukifikiria wenzetu, tukisema na kuenenda kwa njia inayofaa na yenye kuleta amani. Kufanya hivyo kutaonyesha kwamba roho ya Mungu imo ndani yetu, kwa maana “matunda ya roho ni upendo, furaha, amani.” (Gal. 5:22, NW) Vilevile, “hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani.” (Yak. 3:17) Kwa hiyo tunaonyesha kwamba tuna hekima nyingi tunapotii onyo la upole la Yesu la kuwa na amani. Hiyo ni alama ya uanafunzi wa kweli wa Kikristo katikati ya ulimwengu wenye mashindano, mafarakano, na wenye kugawanyika sana. Inatuunganisha na kutufanya watu wa Mungu waliopangwa vizuri chini ya Kristo. —Kutoka The Watchtower, Aug. 15, 1977.
[Picha katika ukurasa wa 18]
‘Kuwa na chumvi ndani yako’ ni kuwa na sifa inayokufanya utendee watu mambo yenye kuwapendeza