Thamani ya Nasaba ya Biblia
Hivyo Israeli wote walihesabiwa kwa nasaba; na tazama, hizo zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli; na Yuda wakachukuliwa mateka mpaka Babeli, kwa sababu ya makosa yao.
2 Basi wenyeji wa kwanza waliokaa katika hozi zao katika miji yao walikuwa Israeli, na makuhani, na Walawi, na Wanethini.
3 Na huko Yerusalemu walikuwa wakikaa baadhi ya wana wa Yuda, na wana wa Benjamini na wana wa Efraimu na Manase;
4 Uthai, mwana wa Amihudi, mwana wa Omri, mwana wa Imri, mwana wa Bani, wa wana wa Peresi, mwana wa Yuda.
5 Na wana wa Washiloni; Asaya, mzaliwa wa kwanza, na wanawe.
LABDA umeanza kusoma Biblia yote kutoka Mwanzo mpaka Ufunuo ukaona kusoma kukiwa kwenye kuvutia sana. Walakini ulipofikia vitabu vya Mambo ya Nyakati na kuona mstari kwa mstari na sura kwa sura zikitoa orodha ya majina ya nasaba ambayo hukuweza kuyatamka ambayo hayakuwa na maana yo yote kwako, labda ulisema, ‘Sababu gani hii iko hapa? Sababu gani kuwe na mambo haya yote yenye kuchosha?’
Ni kweli kwamba, orodha kama hiyo inaweza kuchosha, ikiwa imewekwa kwa ajili ya kusomwa tu. Hata hivyo, orodha hizi za nasaba ni zenye faida kubwa sana. Sababu gani? Sababu moja ni kwamba zinategemeza ukweli wa Biblia. Zinatoa ushuhuda wa kwamba Mungu anataka wale wanaomwabudu wamwabudu katika roho na KWELI, si kama kwamba alikuwa mungu wa kuwaziwa tu. (Yohana 4:23, 24) Je! si kweli kwamba unaposikia au kusoma habari ya tukio fulani, unataka kujua majina na mahali? Mara hiyo unauliza, Nani? Wapi? Unapojua mambo hayo, habari inayosemwa au kuandikwa inaelekea kuwa ya kweli, na yenye uhakika zaidi. Vilevile, ukiwa na habari hizi unaweza kufanya uchunguzi zaidi upate mambo mengi zaidi kuhakikisha yale yaliyosemwa kwa kuangalia sehemu nyingine za Biblia au vitabu vya historia vya kilimwengu. Kama Biblia ilikuwa hadithi tu, au kama iliandikwa na watu wa kujisingizia tu bila shaka ingeepuka kutoa habari kama hizo. Lakini habari hizi zilizo katika Biblia zinapatana na habari nyingine nazo husaidia kuifanya Biblia kiwe kitabu kimoja chenye upatano. Kinatoa mambo yaliyo ya hakika ya historia kwa unyofu.
Zaidi ya hayo, lazima tukumbuke kwamba Maandiko ya Kiebrania ndiyo yaliyokuwa katiba, sheria na kitabu cha kumbukumbu cha Waebrania. Yalikuwa ndiyo maandishi makuu ya taifa ya kuandikwa tarehe na hati. Orodha nyingi za nasaba ziliandikwa kutokana na maandishi mengine halali, kwa kuwa miji ilikuwa ikiandika majina ya wale waliokuwa wakizaliwa mahali pao. Yalikuwa sehemu ya historia ya kweli.—Luka 2:1-5.
INASAIDIA KUMJUA MASIHI
Nasaba ni zenye thamani katika njia nyingine yenye maana sana. Yaani, hutusaidia kumjua Masihi. Yesu Kristo alipotokea, yeye hakutangaza ‘Mimi ndiye Masihi (au, Kristo).’ (Yohana 5:31-37) Watu wengine wengi wamefanya hivyo katika nyakati zilizopita, walakini hawakuwa na vitambulisho. Madai tu ya mtu hayatoshi kuwafanya wengine wamwamini. Kati ya ushuhuda mwingi wa kuonyesha kwamba Yesu ndiye Masihi, habari za nasaba za Wayahudi, zilizowekwa katika vitabu vyao vya orodha katika miji yao, zilishuhudia kwamba yeye alikuwa wa ukoo halali—ule wa Mfalme Daudi wa kabila la Yuda. (Luka 2:1-6) Yesu alisema kwamba yeye ndiye KWELI, akitimiza mambo yote yaliyompasa yaliyosemwa na Maandiko ya Kiebrania, kutia na nasaba yake.—Yohana 14:6.
Uhitaji wa kuweka maandishi ya nasaba ulionekana katika unabii wa kwanza, ambao katika huo Mungu aliahidi “uzao,” ambao ungekomboa wanadamu. (Mwa. 3:15) Kama miaka 2,000 baadaye, Mungu alimpendelea Ibrahimu kwa sababu ya imani yake kubwa, akamwahidi kwamba uzao huo ungekuja kupitia katika ukoo wake. (Mwa. 22:17, 18) Baada ya muda kupita, nasaba hiyo ya ahadi ilipunguzwa ikaachiwa Yuda, mmoja wa wale wana 12 wa Yakobo, kilembwe wa Ibrahimu, kisha, ikapunguzwa tena, ikaachiwa ukoo wa Mfalme Daudi. (Mwa. 49:10; 2 Sam. 7:8, 12-16) Kuzaliwa kwa Yesu katika mwili wa kibinadamu kulitimiza mambo hayo yote, kwa kuwa alikubaliwa kuwa wa kabila la Yuda na mwana wa Daudi.—Mt. 9:27; 2 Tim. 2:8; Ebr. 7:14.
MAANDISHI YA UKOO WA KIKUHANI NI YA MAANA
Licha ya kuweka maandishi ya ukoo wa kifalme kupitia kwa Daudi, Wayahudi walipaswa kuweka maandishi ya ukoo wa Haruni, wa kabila la Lawi. Hii ilikuwa hivyo kwa sababu ukuhani wao wote ulipaswa kuwa wa kabila hilo. (Kut. 28:1-3; Hes. 3:5-10) Sehemu kubwa ya maandishi ya nasaba katika Mambo ya Nyakati yanatimiza kusudi hilo. Kabla Daudi hajakufa alifanya mipango kwa utumishi wa hekalu, akawagawia Walawi utumishi mbali-mbali wa pekee. (1 Nya. sura 24-27) Baada ya Israeli kurudi kutoka uhamishoni katika Babeli, maandishi hayo yalikuwa ya maana sana kwa sababu ukuhani pamoja na utumishi wa hekalu ulipaswa kurudishwa. Vitabu vya Mambo ya Nyakati hutoa mambo makuu ya mipango hii iliyofanywa na Daudi, navyo pamoja na vitabu vya Ezra na Nehemia, huonyesha namna ibada ilivyoanzishwa tena kufuata mfano ule ule baada ya kurudishwa. Ukoo ulifuatwa sana. Hiyo inaonyeshwa na uhakika wa kwamba wanaume wengine waliokuwa wakifikiri kwamba walikuwa wa jamaa ya kikuhani lakini wakashindwa kuthibitisha nasaba yao hawakuruhusiwa kutumikia mpaka wathibitishe nasaba yao kwanza.—Neh. 7:64, 65.
Kwa hiyo, ukweli wa Biblia unategemezwa na, nasaba hizi. Ezra, mwandikaji wa ‘Mambo ya Nyakati, anataja vyanzo 20 mbalimbali vya kiserikali alivyotumia kupata habari alizoandika. Haya yalikuwa maandishi ya kiserikali, wala hayakuwa mawazo tu ya waandikaji waliokuwa na makusudi ya kutukuza taifa au ya kichoyo. Lakini nasaba hizi zaweza kutufaidije leo?
INAONYESHA NAMNA MATAIFA YOTE YALIVYOTOKA KATIKA MTU MMOJA
Nasaba ya Biblia inatusaidia katika njia nyingine. Inategemeza maneno ya mtume Paulo kwamba “[Mungu] alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika [mtu] mmoja, wakae katika uso wa nchi yote.” (Matendo 17:26) Maandishi hayo yanaonyesha wazi kwamba Adamu na Hawa ndio waliokuwa wazazi wa jamii nzima ya kibinadamu. (Mwa. 1:28; 3:20) Orodha ya wazao wao kupitia kwa mwana wao Sethi imeandikwa kufikia wakati wa Gharika. (Mwa. sura 5, 7) Halafu jamaa ya Nuhu (jumla ya wafu wanane) iliokoka, ikaongezeka kufikia jamaa 70, ambazo kutoka hizo dunia yote ilienezwa wafu.—-Mwa. sura ya 10.
UKOMBOZI KWA MTU MMOJA
Tena, habari hii inafunua namna ilivyowezekana kwamba, kwa kuwa mtu mmoja ndiye aliyekuwa baba ya jamaa nzima ya kibinadamu, mtu mmoja angeweza kutoa uhai wake uwe bei ya ukombozi kwa ajili ya wokovu wa wanadamu. (Mt. 20:28; Yohana 11:49-52) Kwa kuwa, akiwa “Adamu wa mwisho,” Yesu anaweza kununua jamaa ya kibinadamu, atumie thamani ya dhabihu yake, katika njia hiyo awe “Baba wa milele” kwa wale wote wanaoushika ukombozi. Kama kungalikuwa na mababa wengi wa jamaa ya kibinadamu haingewezekana mtu mmoja atumiwe kama ukombozi.—1 Kor. 15:45; Isa. 9:6; 53:10.
UTARATIBU WA VIPINDI VYA NYAKATI
Huenda faida nyingine za maandishi ya nasaba ya Biblia ziwe na maana ndogo, hata hivyo ni zenye faida. Katika sehemu nyingine za Biblia, zinasaidia kujua urefu wa utaratibu wa vipindi vya nyakati. Kwa mfano, katika Mwanzo sura ya 5 na 7:6, 11, wakati wa kuanzia na kuumbwa kwa Adamu mpaka Gharika unaonyeshwa kuwa miaka 1656. Halafu, katika sura ya 11 tunaonyeshwa kipindi cha wakati cha miaka 427 kuanzia na Gharika mpaka kufanywa kwa agano na ibrahimu.—Mwa. 12:4.
Pasipo maandishi haya haingewezekana kujua wanadamu wamekuwa hapa duniani kwa muda gani. Urefu wa vipindi vya uumbaji wa wanyama haukufunuliwa, au katika vipindi vya uumbaji vilivyotangulia. Ijapokuwa wanafunzi wa Biblia hawawezi kujua barabara muda uliopita kabla mwanadamu hajaumbwa, wanajua barabara kwamba muda ambao Mungu amekuwa akishughulika na wanadamu mpaka sasa ni miaka kama 6,000.a
KUNAKOELEKEA KUWA KUTOPATANA
Kuongezea hayo, orodha ya nasaba inatusaidia kufahamu mambo ambayo pengine hayangefahamika. Kwa mfano, Samweli anaonekana kuwa Mwefraimi katika 1 Samweli 1:1, ampapo baba ya Samweli, Elkana, anaitwa Mwefraimi. Kama ndivyo, kunaonekana kukiwa na kasoro fulani, kwa kuwa Samweli alitumikia hemani, akimsaidia Eli kuhani mkuu, vilevile alivaa naivera ya kitani, vazi lililoonyesha kazi yake kuwa alitumikia mahali hapo.—1 Sam. 2:11, 18.
Orodha ya nasaba katika 1 Mambo ya Nyakati 6:19-28 inatusaidia katika tatizo (gumu) hili. Hapa orodha ya wana wa Levi imeandikwa, kama mstari wa 19 unavyoonyesha. Katika mstari wa 27 na 28, Elkana na Samweli wanatajwa. Kwa hiyo, kwa kweli Samweli alikuwa Mlawi, aliyestahili kutumikia hemani. Babaye aliitwa Mwefraimi kwa sababu aliishi Ramathaimu-sofimu, au Rama, katika nchi ya kabila la Efraimu. Hii inalingana na desturi yetu leo ya kuita mtu mtu wa pwani kwa sababu ameishi huko kwa muda fulani, hali huenda akawa alizaliwa bara.
UTUMIZO WA UNABII
Kwa habari ya kuonyesha utimizo wa unabii, mfano mmoja unaonekana katika agano la kinabii ambalo Yehova alifanya na Finehasi, mwana wa Eleazari Kuhani Mkuu, la “ukuhani wa milele kwake yeye na kizazi chake baada yake.” (Hes. 25:13, NW) Ahadi hii ilitimizwaje?
Kwa wazi ukuhani mkuu uliendelea katika ukoo wa Finehasi mpaka wakati wa Kuhani Mkuu Eli, wa ukoo wa Ithamari mjomba wa Finehasi. Labda badiliko hili lilisababishwa na kutokustahili fulani kulikotokea kwa kitambo katika ukoo wa Finehasi. Walakini, Mfalme Sulemani alimwondoa Abiathari, wa ukoo wa Ithamari, kwa sababu alikuwa amejiunga na Adonija mwana’ wa Mfalme Daudi katika jaribio la kunyakua kiti cha enzi cha Yuda wakati Mfalme Daudi alipokuwa mgonjwa. (1 Fal. 1:1-14; 2:26,27) Alimweka Sadoki, wa ukoo wa Finehasi, awe kuhani mkuu mahali pake. (1 Fal. 2:35) Kama yanavyoonyesha maandishi ya historia, ukuhani mkuu uliendelea katika ukoo huu kwa muda wa miaka mingi baada ya hapo.
HUFANYA WATU WAJULIKANE
Maandishi ya nasaba mara nyingi yanatusaidia kujua uhusiano kati ya watu fulani wanaotajwa. (Mwa. 35:21-26) Tunaposhindwa kujua mtu tunayesoma habari zake, tunafurahi kuona kwamba tunaweza kutofautisha kati ya watu wenye jina lile lile moja kwa sababu mara nyingi nasaba inamtaja baba, mama, ndugu, au mwana, au inaonyesha mji au sehemu alikotoka mtu huyo.—Luka 6:14; Matendo 12:12; Mt. 10:2-4; Marko 15:43; Matendo 5:37; 1 Sam. 17:4, 58; Mwa 11:29; 28:9.
ILIHITAJIWA NA WAYAHUDI KWA MAMBO YA KISHERIA
Mambo mengine yenye maana katika orodha ya nasaba yalikuwa haya: Wayahudi waliihitaji ili kuthibitisha uhusiano wa kikabila katika kugawa Nchi ya Ahadi na katika kuthibitisha uhusiano wa jamaa kwa ajili ya urithi wa mashamba wa watu mmoja mmoja. Nasaba ilionyesha kwamba mtu wa jamaa aliye karibu ndiye aliyekuwa na daraka kulingana na sheria la kumwoa mke mjane wa nduguye ili aendeleze jina la ndugu yake. Mtu huyu wa jamaa ya karibu ndiye vilevile aliyetenda kama mkombozi wa kukomboa mtu wa jamaa yake kutokana na utumwa, na kuwa mlipiza kisasi cha damu juu ya mwuaji.—Kum. 25:5, 6; Law. 25:47-49; Hes. 35:19.
Kwa hiyo, ijapokuwa orodha ya nasaba huenda ikaonekana kuwa yenye kutatiza, tunaweza kushukuru kwa kuwa ilihifadhiwa kwa kusudi, kwa ajili ya wale walioishi katika nyakati zilizopita na kwa ajili ya wale wanaotaka kupata ufahamu wa Neno la Mungu leo.
[Maelezo ya Chini]
a Kuanzia na wakati wa agano la Ibrahimu (kama miaka 2,083 hivi tangu Adamu aumbwe), maneno katika Kutoka 12:40, 41; 1 Falme 6:1, na maandishi ya wafalme wa Yuda na Israeli pamoja na uhamisho katika, Babeli, tunaingizwa katika wakati wa orodha ya tarehe za kilimwengu yenye kuaminika.