Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w78 11/15 kur. 7-9
  • Mwanamume Aliyepinga Mapenzi ya Mungu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwanamume Aliyepinga Mapenzi ya Mungu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • WAJUMBE WA KWANZA
  • WAJUMBE WENYE HESHIMA ZAIDI WATUMWA
  • BALAAMU ANATAKA ZAWADI
  • BALAAMU ASHINDWA KULAANI ISRAELI
  • BALAAMU APINGA MAPENZI YA MUNGU MPAKA MWISHO
  • Punda wa Balaamu Anazungumza
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Punda Anasema
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Yehova Anawabariki Walio Waaminifu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Hesabu—Yaliyomo
    Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
w78 11/15 kur. 7-9

Mwanamume Aliyepinga Mapenzi ya Mungu

BALAAMU alikuwa mwaguzi aliyejulikana sana kwa uwezo wake wa kunena laana na baraka zilizokuwa na matokeo. Sifa yake ilienea hata kupita mipaka ya nchi yake. Mji wake ulikuwa Pethori, uliokuwa katika sehemu ya juu ya bonde la Frati karibu na Mto Sajur. Karibu na hapo ulikuwako Harani, walimoishi wanaume wenye kumwogopa Mungu kama Ibrahimu, Lutu na Yakobo. Uhakika huu unaweza kuwa sababu ya mwaguzi huyu Balaamu kujua habari za Mungu wa kweli, hata akimtaja kuwa “[Yehova], Mungu wangu”​—Hes. 22:18.

Lakini Balaamu alikujaje kuwa mpingaji wa mapenzi ya Mungu? Waisraeli walipokaribia kuingia katika Nchi ya Ahadi, Mfalme Balaki Mmoabi na watu wake waliogopa sana kwa kuona mkutano mkubwa, labda ukiwa na hesabu ya watu 3,000,000. Mawakili wa taifa la Moabu walishauriana na wazee wa Midiani wakaamua kwamba Israeli alikuwa tisho kwa hali yao njema. (Hes. 22:1-4) Walijua kabisa yale Yehova alikuwa amewafanyia Israeli kwa kuwakomboa kutoka Misri na vilevile kuwapa ushindi juu ya falme zenye nguvu za Waamori upande wa mashariki wa Mto Yordani. Kwa hiyo, hawakuwa na tumaini lo lote la kushinda Israeli katika vita. Lakini waliwaza hivi: ‘Namna gani kama Waisraeli wangelaaniwa? Je! hilo halingewadhoofisha, tuweze kuwafukuzia mbali?’ Kwa hiyo, Mfalme Balaki, akitaka kushinda Israeli, alilazimika auombe utumishi wa Balaamu.

WAJUMBE WA KWANZA

Upesi ujumbe wa wazee au wakuu Wamoabi na Wamidiani ulielekea Pethori. Ujumbe uliopelekewa Balaamu ulikuwa: “Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. Basi, njoo wewe, nakusihi, unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”​—Hes. 22:5-7.

Balaamu aliwaambia wajumbe hao wakae usiku huo akaahidi kuwaeleza neno la Yehova siku iliyofuata. Ufunuo wa kimungu kwa Balaamu ulikuwa nini? “Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.” (Hes. 22:8, 12) Kwa sababu hiyo, Balaamu aliwaambia watu hao: “Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana [Yehova] amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi.” (Hes. 22:13) Kutokana na maneno hayo, wajumbe hao wangeweza kufahamu kwamba kwa kweli Balaamu alitaka kwenda walakini hakukubaliwa kufanya hivyo. Walipokuwa wakiripoti yaliyotukia, walimwambia Balaki hivi: “Balaamu anakataa kuja pamoja nasi.”​—Hes. 22:14.

WAJUMBE WENYE HESHIMA ZAIDI WATUMWA

Kwa hiyo, inaelekea Balaki aliamua kwamba Balaamu hakuvutiwa sana na toleo alilotolewa pamoja na wajumbe aliotumiwa. Mfalme huyo Mmoabi aliwaza kwamba Balaamu alikuwa akitaka kiasi fulani, naye alikuwa ameazimia kumleta mwaguzi huyo ili laana yenye matokeo zaidi iweze kutolewa. Kwa hiyo, mfalme huyo alituma wajumbe wengi na wenye kuheshimiwa zaidi, na kumhakikishia Balaamu kwamba angetukuzwa sana kwa kulaani Israeli.​—Hes. 22:15-17.

BALAAMU ANATAKA ZAWADI

Sasa Balaamu atafanya nini? “Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu,” akasema, “siwezi kupita mpaka wa neno la [Yehova] Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.” (Hes. 22:18) Balaamu alifahamu vizuri sana kwamba jaribio lo lote la kulaani Israeli lingekuwa kinyume cha mapenzi ya Yehova. Hata hivyo, yeye hakuwaacha watu hao waende zao lakini aliwaza kwamba huenda Yehova akamruhusu aende pamoja na wajumbe hao. Kwa hiyo aliwaambia hivi: “Nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua [Yehova] atakaloniambia zaidi.” (Hes. 22:19) Hata ingawa alisema kwamba hakuna kiasi ambacho kingemfanya alaani Israeli, Balaamu kwa kweli alitaka zawadi hiyo. Bila shaka alikuwa akiwaza hivi: ‘Laiti ningekuwa na ruhusu ya Mungu, singalisita kwenda Moabu mara moja.’

Matukio yaliyofuata yanafunua kwamba haya ndiyo yaliyokuwa mawazo ya Balaamu. Usiku uo huo alipata kile akichokuwa akitafuta​—ruhusa ya Mungu aende pamoja na wajumbe hao. Walakini, hii ilitia ndani onyo hili la Mungu: “Lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalotenda, basi.” (Hes. 22:20) Balaamu hakukawia. Asubuhi aliondoka, akatandika punda wake akaelekea Moabu pamoja na wakuu waliokuwa wametumwa na Balaki. Kwa kuwa sasa alikuwa na ruhusa ya kwenda, Balaamu aliazimia kulaani Israeli ili apate zawadi aliyoahidiwa. Hakukuwa na jambo lingalimzuia. Au, je! lilikuwako?

Yehova Mungu hakufurahi Balaamu alipokwenda na watu hao, akiazimia kulaani Israeli ijapokuwa alikuwa ameagizwa asifanye hivyo. Balaamu alishtushwa sana. Punda wake alianza kufanya mambo yasiyo ya kawaida. Kwa sababu gani? Malaika wa Yehova alikuwa amesimama njiani. Balaamu alionyeshwa kwa nguvu sana kwamba kupinga mapenzi ya Mungu kungemletea kifo. Alikumbushwa tena kwamba jambo aliloruhusiwa kufanya ni kunena yale atakayotakiwa na Yehova kunena.​—Hes. 22:22-35.

Je! Balaamu alibadili yale aliyotaka kufanya baada ya hayo? Huenda ikaonekana hivyo kutokana na yale aliyomwambia Mfalme Balaki: “Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema.” (Hes. 22:38) Walakini, kwa kweli, bado Balaamu alitaka ile zawadi naye alikuwa na nia ya kufanya lo lote awezalo ili aipate.

Huenda hii ikatokeza maulizo haya: Kwa sababu gani Mungu wa kweli akachagua kusema kupitia kwa mwaguzi? Kwa sababu gani hakumwachilia tu alaani Israeli, laana ambayo baada ya kupita muda ingeonekana kwamba haikufaulu? Juu ya jambo hili, lazima tukumbuke kwamba Wamoabi na Wamidiani walifahamu kwamba uwezo wa kijeshi peke yake haungeshinda Israeli. Kulingana na maoni yao, walikuwa na silaha yenye nguvu zaidi ya kupigana na Israeli katika Balaamu, yaani, njia ya kulaani Israeli kwa matokeo. Zaidi ya hayo, Balaamu alitaka kushirikiana nao ili apate zawadi yenye mali nyingi za kimwili aliyotolewa. Lakini namna gani ikiwa mwaguzi huyu mwenye sifa, angelazimishwa awabariki Waisraeli kabisa, mahali pa kuwalaani kinyume cha alivyotaka? Je! hilo halingalionyesha kwamba hakuna silaha itakayofaulu juu ya watu wa Mungu? Kwa hiyo, bila shaka ilitimiza kusudi la Yehova akatumia Balaamu abariki Israeli, kwa mshangao wa Mfalme Balaki Mmoabi.

Lazima mfalme Mmoabi awe alifurahi sana, Balaamu alipofika. Balaki alitoa sadaka, bila shaka kwa kuithamini miungu ya Moabu iliyomwezesha afaulu kumleta mwaguzi huyo. Toleo hilo la sadaka lilitoa nafasi ya kujifurahisha karamu ya sadaka ambayo Balaamu na wale wakuu walishiriki kwa kupelekewa sehemu yake.​—Hes. 22:40.

BALAAMU ASHINDWA KULAANI ISRAELI

Baadaye, Balaki alimpeleka Balaamu katika sehemu iliyoinuka, ambapo kutoka huko angeweza kuwaona vizuri zaidi Waisraeli waliokuwa wamepiga kambi. Bila kukawia Balaamu alianza kufanya jambo lile alilokuwa ameitwa afanye. Alimwuliza Balaki amjengee madhabahu saba na kutoa juu yake ng’ombe waume saba na kondoo waume saba. Kisha, Balaamu akaenda peke yake juu ya kilima, bila shaka akafanye huko kawaida za uaguzi kwa kusudi la ‘kupata ishara ya bahati.’ Lakini hapo Yehova alimlazimisha Balaamu abariki Israeli. Majaribio mengine mawili ya kuwalaani watu wa Mungu Israeli yalishindwa kabisa.​—Hes. 23:1–24:9.

Kwa hiyo, Balaki akamkasirikia sana Balaamu. “Nalikuleta ili unilaanie adui zangu,” akasema, “na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi. Basi sasa kimbilia mahali pako.” (Hes. 24:10, 11) Balaamu alijaribu kutoa sababu ya kushindwa kwake, akisema: “Je! sikuwaambia wajumbe wako ulionipelekea, nikisema, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la [Yehova], kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; [Yehova] atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi.”​—Hes. 24:12, 13.

Baada ya hapo, akisukumwa na roho ya Mungu, Balaamu alitoa unabii uliotia ndani ujumbe ulioonyesha kwamba Moabu angepatwa na mabaya. Kisha Balaki na Balaamu wakaachana. Biblia inaripoti kwamba Balaamu ‘alirudi mahali pake,’ ikimaanisha kwamba mwaguzi huyo alienda njia yake. Lakini je! mwishowe Balaamu alijifunza somo la kwamba kupinga mapenzi ya Mungu ni ubatili? Je! yeye alirudi Pethori? Hapana.​—Hes. 24:14-25.

BALAAMU APINGA MAPENZI YA MUNGU MPAKA MWISHO

Bado Balaamu alitaka ile zawadi na alijaribu kuipata kwa vyo vyote. Kwa kuwa hangeweza kulaani Israeli, alitokeza mpango ambao katika huo Waisraeli wangejiletea laana ya Mungu juu yao wenyewe. Alimweleza Balaki namna ya kutumia wanawake Wamoabi na Wamidiani wawafanye wanaume Waisraeli washiriki katika ibada ya sanamu na uasherati. (Hes. 31:16; Ufu. 2:14) Mpango huo ulifanikiwa kwa kadiri fulani, kwa sababu elfu nyingi walinaswa katika mtego huo wa ibada ya uasherati. Na kama matokeo, wanaume Waisraeli 24,000 waliangamia.​—Hes. 25:1-9.

Lakini je! kupinga mapenzi ya Mungu kwa Balaamu kulimfaidi? Hata kidogo. Yehova alipowaamuru Waisraeli walipize kisasi juu ya Wamidiani kwa kuwaingiza Waisraeli katika mtego, bado Balaamu alikuwa kati yao, kwa hiyo upanga wa kufisha ulimpata. (Hes. 31:7, 8) Ndiyo, kwa sababu ya tendo lake la ukaidi, Balaamu alipoteza uhai wake.

Kwa hiyo mwaguzi huyo kutoka Pethori ni mfano wa onyo kwa wale wote wanaoendelea kupinga mapenzi ya Mungu na kufuata tu faida za kichoyo. (2 Pet. 2:15, 16; Yuda 11) Hili lapaswa kututia moyo tujifunze Maandiko Matakatifu, ili tujue mapenzi ya Mungu kwetu ni nini kisha tuyafanye, bila kufuata hata kidogo mwendo wa upumbavu kama huo wa Balaamu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki