Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w74 4/1 kur. 147-153
  • Yehova Anawabariki Walio Waaminifu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yehova Anawabariki Walio Waaminifu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MFALME WA ISRAELI
  • BALAKI AWAFANYIA ISRAELI HILA
  • JARIBU LA UAMINIFU
  • WALIO WAAMINIFU WABARIKIWA
  • Mwanamume Aliyepinga Mapenzi ya Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Punda wa Balaamu Anazungumza
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Punda Anasema
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Uaminifu Katika Wakati wa Mwisho
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
w74 4/1 kur. 147-153

Yehova Anawabariki Walio Waaminifu

“Enyi wapenda Yehova, yachukieni yaliyo mabaya. Yeye anazilinda nafsi za waaminifu wake.”​—Zab. 97:10, NW.

1. Kwa sababu gani Yehova anayo haki ya kutazamia uaminifu kwetu, na ni matendo gani aliyo na haki ya kuchukua?

KWA nguvu za kuwa Muumba wa vyote vilivyo hai mbinguni na duniani, Yehova ndiye Mfalme aliye mkuu zaidi sana na Mungu aliye wa pekee wa kweli. Biblia inamzungumza kama “Mfalme wa milele.” (Yer. 10:10) Basi, je! yeye hana haki ya kutaka uaminifu kwa raia zake aliowaumba? (Efe. 4:24) Je! si inafaa kwake si kuwaadhibu tu wasio waaminifu lakini kuwabariki wale walio waaminifu? Je! watawala wa kibinadamu hawafanyi lile lile?

2. Watu wengi wanafikiri uaminifu wao wa kwanza wapaswa uwaendee akina nani? Kwa sababu gani hili ni kosa?

2 Kati ya watu zaidi ya bilioni tatu (milioni elfu tatu) duniani leo, ni wachache kwa kulinganisha wanaoufikiria wajibu wao wa kuwa waaminifu kwa Mwenye Enzi Yote Aliye Mkuu, Yehova Mungu. Kwa kutokuona vema wanaiona serikali ya kibinadamu yenye utukuzo wa taifa peke yake inayowatawala mara hiyo. Wao wanafikiri kwamba uaminifu kwa serikali hiyo lazima uyatangulie mambo mengine yote. Wao wana nia ya kuzivunja sheria za Mungu inapotaka hivyo, wakifanya yaliyo mabaya machoni pake. Lakini je! huu si ufahamu uliopotoka wa wakuu? Ni kama vile waajiriwa katika kazi fulani kuiona mamlaka ya wasimamizi kana kwamba iko juu ya ile ya mwenyeji. Mamlaka ya watawala wa kibinadamu si kubwa zaidi ya ile ya Yeye aliye Mfalme juu ya vyote.

3. Wanaume fulani katika karne ya kwanza waliuonyeshaje uaminifu wao kwa Mungu?

3 Nyuma katika karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida kikundi fulani cha wanaume kilionyesha ufahamu ufaao wakati baraza ya watawala wa kibinadamu ilipofanya madai ya nguvu yaliyotia ndani kutokumtii Mwenye Enzi Yote Aliye Mkuu Zaidi Sana. Wao walionyesha uaminifu wao kwake kwa jibu lao, wakisema: “Inatupasa kumtii Mungu kama mtawala kuliko wanadamu.” (Matendo 5:29, NW) Katika ulizo kubwa kama hili huenda isiwe vigumu kwa mtu kuwa mwaminifu kwa Mungu, lakini namna gani juu ya mambo yanayoelekea kuwa madogo? Namna gani juu ya mambo yanayoweza kuelekea kuwa safi lakini yawezayo kumwelekeza mtu kwenye matendo mazito hata zaidi yasiyo ya uaminifu?

4. Neno “uaminifu” linachukua maana gani?

4 Neno “uaminifu” linachukua maana ya kushikamana kwa unyofu na kujitoa kwa mtawala au kiongozi. Vile vile linachukua maana ya kujitoa kwa kitu fulani au mtu fulani na vile vile unyofu kwa mtu ye yote au watu wo wote ambao wanamwia mtu uaminifu. Katika sehemu ya Kiebrania ya Biblia neno la Kiebrania kwa “uaminifu” lina maana ya fadhili. Lakini lina maana zaidi ya kupendezwa kwa huruma au fadhili inayotokana na upendo, ijapokuwa linatia mambo haya ndani hivi kwamba neno la Kiebrania linatafsiriwa mara nyingi kama “fadhili za upendo” au “upendo mwaminifu.” Fadhili ndiyo inayojishikamanisha na kitu fulani kwa upendo mpaka kusudi lake na kitu hicho limetimizwa, nayo ni kama ile ambayo Mungu anaionyesha kwa watumishi wake na wanayoionyesha kwake yeye. Kwa hiyo yaweza kuonwa kwamba uaminifu waweza kuwa wa njia mbili. Waweza kuonyeshwa na raia kwa ajili ya mtawala na mtawala kwa ajili ya raia zake. Juu ya Yehova, imeandikwa hivi katika 2 Samweli 22:26, NW; “Kwa mtu mwaminifu kwako utatenda kwa uaminifu.” Hii imeonekana kuwa kweli, kwa maana hajashindwa hata kidogo kutimiza ahadi kwa watumishi waaminifu.

MFALME WA ISRAELI

5. Yehova alionyeshaje wazi uaminifu kwa Waisraeli?

5 Kwa kutazama nyuma kwenye taifa la Israeli la kale twaweza kuona namna Mungu alivyotenda kwa uaminifu kwa habari yake. Taifa hilo lilikuwa nao ujamaa wa ajabu pamoja naye. Kwa mkono wenye nguvu alikuwa amewakomboa watu katika utumwa Misri naye akawaleta wakiwa salama chini ya Mlima Sinai katika Arabia. Huko alifanya agano au mapatano pamoja nao, jambo ambalo hakuwa amelifanya na kikundi cho chote kingine cha kitaifa. Yeye aliwapa orodha ya sheria na kuwatawala kama Mfalme wao asiyeonekana. Juu ya ujamaa huu usio wa kawaida, Musa aliwaambia: “[Yehova], Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.” (Kum. 7:6) Hivyo yeye alikuwa ndiye Mfalme wa Israeli mwenyewe. Vile vile Yehova aliwaonyesha uaminifu wake wazi kwa kuwapa ushindi mbalimbali juu ya mataifa maadui yaliyojulikana sana na yenye nguvu kuwapita.​—Kum. 9:1-3.

6. Yeye alitazamia nini kwao, naye aliwafahamisha hili waziwazi kwa njia gani?

6 Kwa kufaa Yehova aliwatazamia waonyeshe uaminifu kwake kwa kutoifuatia miungu mingine. Hii ilionyeshwa waziwazi katika sheria alizowapa. Ya kwanza ya Amri Kumi zijulikanazo sana yasema: “Mimi ni [Yehova], Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi.” (Kut. 20:2, 3) Lingekuwa tendo zito lisilo la uaminifu kwake, Mungu wao na Mfalme, kwa ye yote katika taifa kuigeukia ibada ya miungu ya kigeni.

7. Uaminifu ulikaziwaje kwenye fikira za Waisraeli katika nyanda za Moabu?

7 Miaka mingi nyumaye walipokuwa katika nyanda za Moabu wakijitayarisha kuingia katika nchi ambayo Mungu alikuwa amewaahidi, Musa alionya juu ya adhabu ambazo Mfalme wao asiyeonekana angewapa wakitenda katika njia isiyo ya uaminifu. Kati ya mambo mengine, yeye alisema: “Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.” (Kum. 28:16) Vile vile alizitaja baraka ambazo zingewajia kwa kuwa waaminifu.​—Kum. 28:1-14.

8. Waisraeli walikuwa na kichocheo gani cha kuwa watiifu na waaminifu?

8 Waisraeli walikuwa na kichocheo cha kweli cha kuendelea katika njia ya utiifu na uaminifu kwa Mungu katika yale ambayo yeye alikuwa amewafanyia. Yeye alikuwa amewakomboa katika utumwa wa Kimisri na alikuwa amewapa kila walichohitaji mnamo miaka yao 40 jangwani. Aliwapa mana ya mwujiza kwa chakula, akawapa maji, akawapa orodha ya mambo ya usafi iliyoilinda afya yao, na hata akafanya viatu vyao na mavazi visichakae mnamo kipindi hicho.​—Kum. 29:5.

9. Wamoabu na Wamidiani walitendaje juu ya kuwapo kwa Waisraeli katika nyanda za Moabu?

9 Kuelekea mwisho wa miaka yao 40 jangwani walishambuliwa na Waamori wakiwa chini ya uongozi wa wafalme Sihoni na Ogu. Yehova aliwasaidia Israeli katika kuwashinda maadui hawa. (Kum. 2:32-36; 3:1-13) Wamoabu waliuona ushindi huu nao wakaogopa sana, zaidi walipoona kambi kubwa ya Waisraeli ikienea pote katika nyanda za Moabu. Wao ‘walifadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.’ (Hes. 22:1-3) Wamidiani wenye kutanga-tanga vile vile walipatwa na wasiwasi, na kwa hiyo wanaume wao wazee wakashauriana na wanaume wazee wa Wamoabu. Hawa wa pili wakasema: “Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng’ombe arambavyo majani ya mashamba.” (Hes. 22:4) Hivyo matukio yaliendelea ambayo yangefanya jambo lililoelekea kuwa dogo liwe jaribu zito la uaminifu wa Israeli kwa Yehova, Mfalme wao.

BALAKI AWAFANYIA ISRAELI HILA

10. Kwa sababu gani Balaki aliutafuta msaada wa Balaamu, nalo ombi lake lilikuwa nini?

10 Akijua kwamba wasingeweza kupata ushindi wa kijeshi juu ya Waisraeli bila ya msaada wa kimungu, Balaki, mfalme wa Wamoabu, aliutafuta msaada wa Balaamu, mwanamume aliyeishi katika mji wa mbali wa Pethori, kwa wazi katika bonde la juu la Frati karibu na Harani. Ajapokuwa si Mwisraeli, Balaamu alimjua Yehova Mungu wa kweli kwa kadiri fulani. Balaki na rafiki zake za Kimidiani wakapeleka ujumbe kwa Balaamu wakimwuliza aje na kuwalaani Waisraeli. Wakalipitisha ombi la Balaki: “Basi, njoo wewe, nakusihi, unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.” (Hes. 22:6) Balaamu alilikataa ombi hili nyuma ya kumwuliza Yehova, akisema: “Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana [Yehova] amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi.”​—Hes. 22:13.

11. Balaamu alilifunuaje wazi kusudi la moyo wake?

11 Ujumbe wa pili wa wajumbe wenye kuheshimiwa zaidi ukapelekwa na Balaki. Walimtolea Balaamu zawadi nyingi kama angekuja na kuwalaani Israeli. Ijapokuwa Mungu alikuwa amemwambia Balaamu asiende nyuma ya ziara ya ujumbe wa kwanza, tena Balaamu alitafuta ruhusa ya kwenda, akivutwa na pupa yake ya zawadi nyingi. Yehova aliruhusu Balaamu ajifanyie uamuzi wake mwenyewe akafanye yaliyomo moyoni mwake, lakini Balaamu alipochagua kuambatana na wajumbe hao, Yeye alichukizwa na kumtuma malaika Wake akaweke kizuizi. Malaika huyu alisema: “Tazama, mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu.” (Hes. 22:22-32) Akiudharau ushuhuda huu wa kuchukizwa kwa Yehova. Balaamu akaendelea kufanya yaliyokuwamo moyoni mwake malaika aliposema angeweza kwenda na wanaume hao.​—2 Pet. 2:15, 16, Yuda 11.

12. (a) Simulia matokeo ya jitihada za Balaamu kuwalaani Waisraeli. (b) Ni mpango gani tofauti aliomtolea Balaki na wazee wa Kimidiani?

12 Alipofika Moabu, Balaamu alifanya majaribio matatu ya kuwalaani Israeli, lakini kila mara Yehova alimfanya Balaamu kusema baraka. Akifahamu hili Mfalme Balaki alighadhibika. “Nalikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi.” (Hes. 24:10) Ushuhuda huu zaidi wa kuchukizwa kwa Mungu juu ya tamaa ya Balaamu ya kuwalaani Israeli haukuipunguza pupa ya Balaamu ya zawadi. Sasa akashauriana na Balaki na vile vile na watawala wa Kimidiani kwamba kama wangeweza kuwafanya Waisraeli kuwa wasio waaminifu kwa Yehova, basi Yehova mwenyewe angewalaani. Balaamu alishauri kwamba wawashawishi Waisraeli wajitie katika ibada ya utukuzo wa nguvu za uzazi ya Baali wa Peori. (Hes. 31:16) Juu ya hili, Ufunuo 2:1-14 unasema kwamba Balaamu ‘alimfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.’ Ilikuwa hila.

JARIBU LA UAMINIFU

13. (a) Balaamu alikusudia kupiga mahali gani palipo dhaifu? (b) Udhaifu huu ulikuwa umekwisha kufanya uaminifu wao kwa Mungu ujaribiwe na mambo yaliyoelekea kuwa madogo kwa njia gani?

13 Kwa kuufuata mpango wa Balaamu, Wamoabu na Wamidiani wangekuwa wakipiga mahali palipo dhaifu pa Waisraeli, tamaa zao za kimwili. Udhaifu huu tayari ulikuwa umewalelea taabu. Wakali mmoja walipokuwa safarini kupita jangwa walitaka sana vyakula vya namna fulani walivvokuwa wamefurahia walipokuwa Misri. Halikuwa shauri la kuona njaa, bali la kushindwa kwao na tamaa yao ya kimwili ya namna za chakula walizozitaka. Hawakuridhishwa na kile ambacho Mungu alikuwa amewapa, na kwa hiyo wakalalamika: “N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa [nafsi] zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.” (Hes. 11:4-6) Maneno haya yasiyo ya shukrani yaliwaletea hasira ya Yehova kwa maana kulikuwa ni kuikataa mipango yake. Wakati mwingine waliiita mana kwa dharau “chakula hiki dhaifu.” (Hes. 21:5) Kitu kidogo kama chakula kiliweza kuwafanya wamlalamikie Mfalme wao asiyeonekana. Balaamu alipanga kuutumia udhaifu huu wa kimwili, ambao ungeelekea kuwa jambo dogo, awaelekeze kwenye tendo zito lisilo la uaminifu kwa Mungu.

14. Simulia namna ambavyo huenda Balaamu aliwatolea Wamoabu na Wamidiani mpango wake.

14 Alipokuwa akimtolea Balaki na rafiki zake mpango wake, labda Balaamu alisema jambo kama hili: ‘Tazameni, tafadhali, namna wanawake wa Moabu na wa Midiani walivyo warembo. Nao ni wenye kuvuta na kushawishi zaidi sana katika dansi zao. Na, je! si kweli kwamba Waisraeli wamekuwako jangwani kwa miaka 40 na je! Mungu wao hakuwapa mana peke yake wale? Je! haiwezekani kwamba watayatazama mazao ya nchi kwa macho yenye kutaka kula? Sasa, kama wanawake wa Moabu na Midiani wangetoa ukaribishaji wao, je! watu hawa wenye kutanga-tanga wasingeweza kuwa tayari kwa ajili ya karamu iliyo kweli kweli ya chakula kilicho bora na divai ya Moabu? Na waketi wakale na kunywa. Na wavionje vyakula vyenye kushawishi vya Moabu, na mioyo yao iburudishwe na divai yenye kulevya ya Midiani. Wakiisha kuyazoelea haya, kisha wanawake watajua njia ya kuwavutia kwenye ngono nao, na Israeli waiinamie miungu ya Moabu.’

15, 16. (a) Pengine wengine wa wanaume wa Kiisraeli waliwaza kwa njia gani walipopokea ukaribishaji uliotolewa na wanawake wa Kimoabu na wa Kimidiani? (b) Kwa sababu gani kuwaza kwao kulikuwa hatari?

15 Wanawake warembo wa Moabu na Midiani walipowakaribisha wanaume wa Kiisraeli waje kwenye karamu yao, bila shaka ulielekea kwa wanaume hawa kuwa wonyesho safi wa ukaribishaji. Huenda waliwaza kwa njia hii: ‘Kuna dhara gani katika kuukubali ukaribishaji wenye fadhili wa Wamoabu na Wamidiani? Kusingekuwako dhara lo lote katika kushiriki chakula na divai. Dansi zitakuwa kiburudisho. Bila shaka, nyuma ya pigano kali tulilokuwa nalo na Waamori, tumestahilishwa kiburudisho.’ Kuwaza huko kungekuwa kukadiri kwenye hatari kwa matendo ambako kungewatia katika hali yenye mashaka sana.

16 Lingeelekea kuwa jambo dogo kuukubali ukaribishaji wa Wamoabu na Wamidiani na kula vyakula vyao vitamu vyenye kushawishi. Lakini lilikuwapo shauri la mashirika mabaya. Watu hawa walikuwa waabudu wapagani wenye kutukuza nguvu za uzazi waliojitia katika desturi za ufisadi kama sehemu ya ibada yao ya Baali, kutia na umalaya wa wakati wa sherehe. Ushirika wa mara kwa mara na watu hao, zaidi katika hali ya kuburudika ya karamu, haukuwa salama. Chakula kizuri na wingi wa divai ungetokeza roho yenye uchangamfu na kupunguza kizuizi cha yaliyo mabaya machoni pa Mungu. Chini ya hali hizi, je! wanaume wa Kiisraeli wasingeshawishiwa kwa kuwaona wanawake waliovalia mavazi mafupi walio warembo sana wakicheza dansi kwa kuchochea nyege mbele ya meza zao za karamu? Je! wasingeshindwa na ukaribishaji wenye kushawishi wa wanawake hawa washiriki nao katika desturi za ufisadi za ibada ya Baali? Hivyo mashirika mabaya yangewaelekeza kwenye matendo mazito yasiyo ya uaminifu kwa Mungu wao na Mfalme.​—Kut. 34:12-15; Hos. 4:11.

17. (a) Nini kilichofanya karamu ziwe na mengi zaidi kuliko kula tu na kunywa? (b) Ziliwategaje Waisraeli waliozihudhuria?

17 Karamu za watu hao wapagani zilikuwa za kidini katika kila upande. Muziki wao, dansi na desturi za ufisadi vyote vilikuwa sehemu ya ibada yao ya Baali. Dansi ambazo wanawake wao walicheza kwa kuiheshimu miungu yao zilikusudiwa kuchochea nyege za wale waliokuwako. Wale wanaume wa Kiisraeli walioshiriki katika karamu hii walishindwa kweli kweli na vishawishi vilivyowekwa mbele yao. Kama fahali anayeelekezwa akachinjwe wao walielekezwa na tamaa zao za kimwili kwanza kwenye karamu iliyoelekea kuwa safi kisha kwenye mwenendo wa ufisadi na wa ibada ya sanamu, yote yakiwa ni dhambi juu ya Mungu. (Mit. 7:22) “Watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.”​—Hes. 25:1, 2.

18. Jambo lililoelekea kuwa dogo la kuukubali ukaribishaji mwishowe lilielekeza kwenye nini wakati wafanya karamu wa Kiisraeli walipoirudia kambi yao?

18 Kama ilivyotangulia kusemwa na Balaamu, hasira ya Yehova ilipanda kwa sababu ya ubaya huu na kutokuaminika kwa upande wao. Alileta pigo lenye kufisha likapite katika kambi ya Kiisraeli, likiwaua watu 23,000. (1 Kor. 10:8) Hesabu, sura ya 25, haisemi waziwazi ni waabudu sanamu wangapi waliouawa na waamuzi wa Israeli, lakini yaelekea hawa walikuwamo katika hesabu ya jumla ya watu 24,000 waliopatwa na pigo, yaelekea wakiuawa 1,000. Hivyo kuukubali ukaribishaji kuhudhuria karamu iliyoelekea kuwa safi kulielekeza kwenye msiba huu kwa Waisraeli hao.

19. Pigo katika kambi ya Kiisraeli lililetwaje kwenye kikomo chake, naye Hosea aliwakumbusha Waisraeli juu ya kutokuaminika kulikotukia huko karne nyingi nyumaye kwa maneno gani?

19 Mwishowe pigo lililetwa kwenye kikomo wakati Finehasi, mwana wake Eleazari kuhani mkuu, alipomchoma Zimri mkuki na mwanamke wa Kimidiani Kozbi, ambaye alikuwa amemleta ndani ya hema yake kwa ajili ya ngono ya ufisadi. Yaelekea sana kuwa Zimri alikuwa kiongozi mkubwa kati ya wasiokuwa waaminifu. Kwa kuwa umalaya wa wakati wa sherehe ulikuwa sehemu ya ibada ya Baali, Zimri angeweza kuonwa kana kwamba alikuwa akileta ibada ya Baali katika kambi ya Israeli alipomleta Kozbi hemani mwake na kufanya ngono naye humo. (Hes. 25:6-8) Karne nyingi nyumaye Yehova aliwakumbusha Waisraeli juu ya kutokuaminika huku juu yake alipomfanya nabii wake Hosea aandike: “Walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda.”​—Hos. 9:10.

20. Kwa sababu gani hila ya Balaamu haikushinda, nayo ilirudia ilikotoka namna gani?

20 Hila ya Balaamu, ingawa iliwadhuru sana Waisraeli, haikushinda, kwa maana Waisraeli waaminifu walivizuia vishawishi vya kimwili vya kufanya yaliyo mabaya machoni pa Mungu. Hila hiyo kwa kweli iliwarudia Wamidiani, kwa maana Mungu aliwaamuru Waisraeli waaminifu wawapige. “[Yehova] akanena na Musa, na kumwambia, Wasumbue Wamidiani, na kuwapiga; kwa sababu wao wawasumbua ninyi kwa hila zao, ambazo kwa hizo wamewadanganya ninyi katika jambo la Peori, na katika jambo la huyo Kozbi, binti wa mkuu wa Midiani, umbu lao, huyo aliyeuawa siku hiyo ya pigo katika jambo la Peori.” (Hes. 25:16-18) Miji ya Kimidiani na kambi zenye kuta katika eneo iliteketezwa kwa moto. Wafalme watano wa Midiani, wanaume wote, na kila mwanamke ambaye alikuwa amefanya ngono, na vile vile Balaamu, waliuawa. (Hes. 31:1-20) Wamoabu, waliokuwa wazao wa mpwa wake Ibrahimu Lutu, hawakuuawa, lakini kwa kuwa walishiriki katika hila Mungu aliwazuia wasiingie katika kundi la Yehova, “hata kizazi cha kumi . . . milele.”​—Kum. 23:3, 4.

WALIO WAAMINIFU WABARIKIWA

21, 22. Finehasi alikuwaje mfano wa uaminifu kwa Yehova, nasi twaweza kujifunza nini kutokana na kilichotukia kwa wasio waaminifu?

21 Kuhani Finehasi alionekana kuwa mmojawapo wa walio waaminifu, naye alisifiwa kwa ajili ya tendo lake la haraka juu ya Zimri na Kozbi. Yeye hakuachilia “ushindani wo wote” kuelekea ibada ya Yehova, nalo hili “alihesabiwa kuwa haki.” Kwa sababu hii alipewa agano la amani na Yehova ambalo “lazima litumikie kama agano la ukuhani kwa wakati usiojulikana kwake na uzao wake baada yake.”​—Hes. 25:11-13, NW; Zab. 106:30, 31.

22 Ni mfano mwema wa Finehasi mwaminifu tunaopaswa kufuata leo, si ule wa wale walioshindwa na tamaa za kimwili. Kilichotukia kwa hao wasio waaminifu ni mfano wa kutuonya sisi. (1 Kor. 10:11) Ni mfano wa namna kuwaza tamaa mbaya, hata zinapoelekea kuwa ndogo sana, kuwezavyo kuelekeza kwenye msiba.​—⁠Yak. 1:14, 15.

23. Hali ya Wakristo waaminifu leo inalinganaje na ile ya Waisraeli waaminifu katika nyanda za Moabu, nazo zinafanyiza baraka gani?

23 Kama vile ambavyo wale Waisraeli waliobaki waaminifu kwa Yehova walivyobarikiwa na pendeleo la kuingia katika Nchi ya Ahadi, kama Finehasi, ndivyo na Wakristo leo wanaoshika uaminifu kwa Yehova wanavyoweza kutazamia kupokea baraka za ajabu ambazo Mungu amewawekea wale wampendao. Wao wataingia katika wakati mpya ulio mzuri ajabu ulioahidiwa kuja chini ya utawala wa Mfalme wake aliyetiwa mafuta, Yesu Kristo. “Juu ya ongezeko la serikali yake, na la amani, hakutakuwako kikomo.” Yeye atatawala “katika haki na katika uadilifu, tangu wakati huo, hata milele.” (Isa. 9:7, An American Translation) Lo! kutokushindwa wakati wo wote na vishawishi vya kimwili wala kujitia katika matendo yasiyo ya uaminifu kwa Mungu ni kichocheo kama nini!

24. Lazima tujue nini juu ya tamaa za kimwili, na kwa sababu gani hali yetu inafanana na ile ya Waisraeli walipokuwa katika nyanda za Moabu?

24 Tukiwa na tumaini la wakati mpya huo ulioko mbele yetu, tunayo sababu yenye nguvu kushinda vishawishi vya kufanya yaliyo mabaya machoni pa Yehova. Lakini inatupasa tujue kwamba tamaa za kimwili ni sehemu iliyo dhaifu leo ya kibinadamu sawa na zilivyokuwa siku za Waisraeli hao waliopiga kambi katika nyanda za Moabu. Vishawishi vya kujitoa kwa tamaa hizo ni vyenye nguvu sana kwa maana tumezungukwa na watu wa kilimwengu waliojitoa kwa ajili ya mwenendo mpotovu na ufisadi. Kwa njia fulani wanajitia katika ibada ya utukuzo wa nguvu za uzazi kama vile walivyofanya Wamoabu na Wamidiani. Vitabu vyao, maonyesho yao jukwaani, sinema na programu za televisheni vinaonyesha kila tamaa iliyopotoka ya mwili inayoweza kufikiriwa na akili yenye upotovu. Lazima tuuzuie uvutano huo mbaya. Kushindwa nao na kuelekezwa nao kwenye kufanya yaliyo mabaya machoni pa Mungu kwaweza kuwa kwenye maangamizi kwetu, kama vile ilivyokuwa kwa wale Waisraeli 24,000 waliotoweka kwa sababu ya kutokuaminika kwao.

25. Tunapokutana na vishawishi vya kimwili, imetupasa tukumbuke nini?

25 Basi, unapokutana na vishawishi vinavyoweza kuelekea kuwa mambo madogo lakini ambavyo vyaweza kweli kuelekeza kwenye kufanya yaliyo mabaya machoni pa Mungu, itakupasa kulikumbuka jaribu hili la uaminifu lililotukia katika nyanda za Moabu. Uchague mwendo wa walio waaminifu, na ukumbuke yaliyoandikwa katika Zaburi 97:10, NW: “Enyi wapenda Yehova, yachukieni yaliyo mabaya. Yeye anazilinda nafsi za waaminifu wake.”

[Picha katika ukurasa wa 150]

Kwa kukubali ambacho huenda kilielekea kuwa wonyesho wa ukaribishaji wa Kimidiani, Waisraeli walivutwa kwenye matendo ya dhambi nzito juu ya Mungu wa kweli

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki