Maswali Kutoka kwa Wasomaji
● Mwanzo 11:1 linasema kwamba kabla ya kuchafuliwa lugha katika Babeli, dunia yote ilisema lugha moja; lakini, mapema, Mwanzo 10:5 linaelekea kutoa wazo la kwamba lugha mbalimbali zilikwisha kuwapo. Hili linaweza kuelewekaje?
Kikisema juu ya wazao wa Nuhu kupitia kwa mjukuu wake Yavani, Mwanzo 10:5 husema hivi: “Kwa hao nchi za pwani za mataifa ziligawanyika . . . , kila moja kwa lugha yake, kwa jamaa zao, kufuata mataifa yao.”
Sura ya 10 ya Mwanzo huonyesha kile kinachoitwa kwa kawaida “Orodha ya Mataifa.” Inatoa orodha ya jamaa 70 au mataifa yaliyo uzao wa wana wa Nuhu, ikitoa habari fulani kuhusu sehemu ambazo mataifa haya yalikotawanyikia na kukaa. Kwa wazi, Musa aliandika habari hii karne nyingi baada ya Gharika na kuchafuliwa lugha katika Babeli. Kwa hiyo aliweza kuandika katika ile ambayo sasa ni sura ya 10 ya Mwanzo habari nyingi zaidi juu ya namna mambo yalivyoendelea baada ya kupita karne nyingi.
Baada ya Mwanzo sura ya 10 kutoa habari nyingi kuhusu “Orodha ya Mataifa,” sura ya 11 inachukua habari hiyo au mfuatano wa historia ikianzia na Babeli ikionyesha namna lugha nyingi zilivyotokea na sababu watu walivyotawanyika duniani.—Mwa, 11:1-9.
Kwa hiyo, mitajo ya lugha mbalimbali katika sura ya 10 haipaswi kueleweka kwamba lugha hizi zilitokea kabla ya kuchafuliwa kwa lugha katika Babeli. (Mwa. 10:5, 20, 31, 32) Walakini lugha hizo zilipatikana baadaye kati ya wazao wa Nuhu, ambao nasaba zao zatolewa katika sura hiyo.