Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 4/15 kur. 3-11
  • Kutembelea Mahali Yalikotukia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutembelea Mahali Yalikotukia
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • KUSUDI LA KUTEMBELEA HUKO
  • MASHAHIDI WA KISASA
  • KUSINI MWA YERUSALEMU
  • KUSINI MWA TEL AVIV-YAFO
  • KATIKA SAMARIA
  • GALILAYA YENYE KUPENDEZA
  • YERIKO NA YERUSALEMU
  • Funzo Namba 1—Ziara Kwenye Bara Lililoahidiwa
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Jiografia ya Biblia Je! Ni Sahihi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • “Ondoka, Zunguka Katika Nchi”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Bonde la Ela—Mahali Ambapo Daudi Aliua Jitu!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 4/15 kur. 3-11

Kutembelea Mahali Yalikotukia

ASUBUHI ya Juni 12, 1978, vijana wawili Waarabu walikuwa wakisaidia kikundi chetu cha watu karibu 10 kutoka Norway kwenda Bethlehemu. Tulipokuwa tukingojea katika kituo cha gari la abiria katika kiunga (wilaya) cha Yerusalemu, kukatokea mshindo mkubwa. Uvumbi wake ulikuwa kama wa mlipuko wa kombora (mzifiga). Mara nyuso za vijana hao Waarabu zikaonyesha woga. Lakini wakati gari kubwa lilipokwenda kando ya njia, wasiwasi ulitulia, maana gurudumu moja lilikuwa limepasuka.

Mmoja wa vijana hao akasema: “Kama hilo lingekuwa kombora, bila shaka tungekuwa katika taabu.”‏ Alieleza kwamba Waarabu wote walio karibu na mlipuko wa kombora wanatiwa katika kizuizi, nao wanaweza kuzuiwa humo kwa muda usiojulikana. Kwa njia hiyo tukapashwa habari juu ya wasiwasi uliomo Israeli. Hata hivyo, tofauti na jinsi wengine walivyokuwa wametangulia kuogopa mwanzoni mwa mwaka, wasafiri wengi waliokuwa huko siku za karibuni wote walisema kwamba nchi hiyo ni salama kutembelewa na watalii.

Sisi tuliotoka Norway tulikuwa sehemu ya kikundi cha Mashahidi wa Yehova wa kutalii nchi. Mashahidi hao kutoka ulimwengu wote walikuwa wakifika katika Israeli tangu mwanzo wa masika. 2,400 walitoka Ufaransa, 1,500 walitoka Ujeremani, 1,200 walitoka nchi ya Netherlands, 750 walitoka United States, na vivyo hivyo. Karibu na mwezi Julai, watalii 9,000 walikuwa wamekwisha kufika, na jumla yao 15,000 walitazamiwa kufika mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Watalii wengi walivaa vitambulisho, nayo magari ya watalii yalitambulishwa na ishara hii iliyowekwa upande wa mbele wa dirisha la magari: MASHAHIDI WA YEHOVA WANATALII NCHI YA BIBLIA. Kwa kushangaa, mwanamke mmoja Myahudi aliyetoka California, akiisha kurudi huko kutoka kutembelea Israeli, alimwambia mtu wa jamaa yake hivi: “Kila tulipokwenda tuliwaona ninyi Mashahidi. Mimi sikudhani mnapendezwa sana na nchi ya Israeli.” Alitaka kujua sababu iliyotupeleka huko.

KUSUDI LA KUTEMBELEA HUKO

Sababu ya kwanza ni kwamba Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba Biblia ni Neno la Mungu nao wanatamani kuzijua sana habari zake. Kwa kuwa nchi ya Israeli ndiyo huko mambo mengi yanayotajwa katika Biblia yalitukia, tunapendezwa na nchi hiyo. Kuna faida ya kweli kutaka kujua sana mahali ambapo unasoma habari zake. Kwa mfano:

Tuseme unasoma katika gazeti habari ya jambo fulani lenye kujulikana sana karibu na mahali ulikozaliwa. Tuseme alama za nchi kama vile kilima, nyumba, mto, na mengineyo, zinatajwa kuambatana na hadithi hiyo. Basi sasa, je! hungesoma habari ya tukio hilo kwa furaha sana na kwa kufahamu kuliko kama hungekuwa umefika mahali hapo wakati wo wote? Ndiyo, maana sasa unaweza kuiona hali yake katika akili zako. Unaweza kuona katika akili zako jinsi nchi hiyo ilivyo, urefu wa kilima, upana wa mto na sura nyingine za nchi zinazokukumbusha ukweli wa tukio hilo.

Ndiyo, kuijua nchi kunamsaidia sana mtu awafahamu watu wanaotajwa katika Biblia na matukio yaliyowapata.

MASHAHIDI WA KISASA

Hata hivyo sisi hatupendezwi na watumishi wa kale wa Yehova peke yao. Tuliambiwa katika mkutano wa pekee waliofanyiwa Mashahidi waliotoka Norway katika Jumba la Ufalme katika Haifa, habari za makundi matano ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova katika Israeli, na habari za wahubiri wa Ufalme 260 wanaoshirikiana na makundi hayo. Tulielezwa kwamba kuna makundi katika Bethlehemu na Ramallah, na hesabu kubwa ya washiriki wake ni Mashahidi wanaosema Kiarabu. Katika yale makundi mawili yaliyomo Tel Aviv, washiriki wengi ni Wayahudi. Lakini kati ya Mashahidi 75 walio katika Haifa, karibu nusu yao ni Wayahudi na nusu nyingine ni wale wanaosema Kiarabu.

Kwa muda wa juma nyingi Mashahidi hawa wenyeji walikuwa wakishughulika sana ili wapange mikutano ya pekee, ambapo wangefurahia kutiana moyo kiroho pamoja na wageni. Vilevile, wakati kikundi chetu cha gari la abiria kutoka Norway kilipokuwa kikitalii Bethlehemu mwezi Juni 11, sisi tulikutana na Shahidi mmoja mwenyeji wa huko aliyetupeleka kwenye Jumba la Ufalme jipya, ambalo ni zuri sana. Tulipofika huko yeye na Shahidi mwingine walijibu maulizo yetu mengi.

Walituambia kwamba huko Yerusalemu, karibu mwendo wa kilomita 8 kuelekea kaskazini, walikuwako Mashahidi wanne lakini katika Hebroni mwendo wa kilomita 24 kuelekea kusini, hakuna Mashahidi. Walituambia kwamba “wahubiri wa Ufalme 25 walio Bethlehemu wana eneo kubwa sana la kuhubiria.” Kesho yake wengine kati ya kikundi chetu waliungana na Mashahidi waliotoka Bethlehemu katika kazi ya kuhubiri mlango kwa mlango katika Bethlehemu. Waliobaki kati yetu, pamoja na Mashahidi wenyeji wawili wakiwa viongozi wetu, tulipanda gari la abiria la Waarabu kutoka karibu na hoteli yetu katika Yerusalemu tukarudi Bethlehemu.

KUSINI MWA YERUSALEMU

Kwa muda wa dakika chache tukaingia Bethlehemu. Mahali hapo palionekana kwetu kuwa penye maana sana. Ndiyo, Yesu Kristo alizaliwa huko, nao malaika wakawatokea wachungaji wa kondoo katika mbuga (shamba) mojawapo ya karibu wawapashe habari za kuzaliwa huko.1 Sura ya nchi hiyo ni yenye vilima vilima, ni zaidi ya vile tulivyokuwa tumetazamia, nayo inaonekana kuwa kavu na kame sana. Tulishangaa kuona kwamba mwinuko wa Bethlehemu ulikuwa sawasawa na ule wa Yerusalemu. Sehemu za mashambani zinazozunguka zilitukumbusha matukio mengine mengi yanayotajwa katika Biblia.

Hilo ndilo lililokuwa eneo ambalo Yakobo alikuwa akipita karibu yake wakati mpendwa wake Raheli alipokufa akimzaa Benyamini.2 Yalikuwa mkao ya Boazi na Naomi. Naye Ruti Mmoabi alikuja huku akilivuka jangwa lenye mawe-mawe kuelekea mashariki na kuanza kuokota shayiri katika mashamba ya Boazi.3 Vilevile, hapa ndipo mchungaji kijana, Daudi, alipokulia na kuchunga kondoo za baba yake na, kwa wazi, vilevile hayo yalikuwa ndiyo makao ya wapwa wake wenye kujulikana sana, yaani, Yoabu na Abishai.4

Mara tukakodi motokaa, tukasafiri kusini kuelekea Hebroni. Mwinuko wa Hebroni ni wenye kipimo cha mita 137 kupita vipimo vya Yerusalemu na Bethlehemu, kwani kipimo chake ni mita 914 juu ya usawa wa bahari. Tulipoelekea kusini, nchi hiyo ilianza kubadilika. Ikawa na sura yenye rutuba zaidi. Eneo linalozunguka Hebroni limesifiwa muda mrefu kwa sababu ya mazao yake; ni kutoka bonde la Eshkoli lililokuwa karibu kwamba wapelelezi wa Israeli walirudi kwa Musa wakiwa na shada kubwa mno la zabibu hivi kwamba ikataka wanaume wawili kuibeba.5 Hata leo inaonekana kwamba nchi hiyo ni yenye rutuba.

Tulipokuwa tukitembea katika njia nyembamba za mji wa Hebroni, tuliona kama tumerudishwa kwenye wakati wa zamani. Hebroni ni mmojawapo wa miji ya kale sana kuliko yote katika ulimwengu, ambayo bado inakaliwa na watu. Ni karibu na Hebroni wa kale ambako Ibrahimu, Sara, Isaka, Rebeka, Yakobo na Lea walizikwa katika pango la Makpela.6 Tulitembelea mahali hapo pa kuzikia panaposifiwa sana; wakati huu muskiti wa Waislamu umejengwa juu ya pango hilo. Inaonekana kwamba makao makuu ya Ibrahimu yalikuwa karibu na Mamre, ambapo wakati mmoja ilimea miti mikubwa.7 Hapo ndipo alipokaribisha malaika kabla ya kuharibiwa kwa Sodoma na Gomora.8 Kutoka mahali fulani karibu na Hebroni, yeye alichungulia chini akiwa umbali wa kutoka juu wa kama mita 1,220 na mwendo wa kilomita nyingi ili auone moshi mnene wa uharibifu huo mkubwa.9

Tulipolifikiria eneo lenye milima tulilopita ili tufike Hebroni, ufahamu wetu wa habari nyingine ya Biblia uliongezeka. Alipokuwa akikaa Hebroni, Yakobo alimwambia Yusufu, mwanawe mwenye umri wa miaka 17 aende akaangalie ndugu zake 10 wa baba mmoja naye kama wa hali gani. Hao walikuwa wakilisha kondoo zao huko Shekemu (leo ni Nablus), yaliyokuwa makao ya jamaa hiyo zamani.10 Hiyo ilimaanisha, si mwendo wa kutembea tu kwa miguu kilomita 35 karibu na Yerusalemu, bali kilomita nyingi kwenda mbali kaskazini kupita katika nchi yenye taabu. Mwishowe Yusufu akawakuta ndugu zake ng’ambo ya Shekemu, katika Dothani (upande wa kusini wa Jenin ya siku hizi), kilomita 130 au zaidi ya hizo kutoka Hebroni!

Tulipokuwa tukitembea katika njia za kale za mji wa Hebroni, au tulipokuwa tukilitazama soko la kale, tulidhani kwamba bila shaka maisha hayakuwa tofauti na wakati Daudi alipoishi huko. Tukakumbuka kwamba ni katika Hebroni alikotiwa mafuta awe mfalme, naye alitawala toka huko miaka saba na nusu kabla ya kuhamia Yerusalemu, makao yake makuu huko kaskazini.11 Lakini, bila shaka, mambo yanayoshuhudia wakati wa sasa hayako mbali sana, mojawapo la hayo ni askari-jeshi wa Israeli ambao wako karibu wakati wote.

Hebroni ni mji ulio na watu wengi. Ni wa eneo lenye wakaaji Wapalestina karibu 700,000 na linalosimamiwa na majeshi. Eneo hilo, linaloitwa sasa “Ukingo wa Magharibi,” liko kati ya Bahari ya Chumvi na Mto Yordani upande wa mashariki na uwanda wa Kiyahudi wa pwani ya Bahari ya Kati upande wa magharibi. Eneo kubwa mno hilo, lenye kilomita za mraba 3,700 na lenye vilima na mabonde mapana, lilitekwa na Waisraeli kutoka Yordani mwaka wa 1967 wakati wa Vita ya Siku Sita.

Ilikuwa karibu na muda wa katikati ya alasiri kabla ya kuondoka Hebroni na kuanza safari ya kurudi Bethlehemu. Walakini, kabla ya kufika huko tuliacha barabara kuu tukafuata njia nyingine mahali ambapo ishara ilielekeza kwenye Vidimbwi vya Sulemani. Tulishangaa sana kuviona! Lo! vilikuwa vikubwa! Vilikuwako vitatu, kile kikubwa kushinda vyote kilikuwa chenye urefu wa mita 178, upana wake mita 54 na kina chake mita 15! Inaonekana kama vidimbwi hivyo vilijengwa upya katika nyakati za Warumi ili mji wa Yerusalemu upatiwe maji, lakini inaelekea kwamba vilikuwa vikitumiwa wakati wa Sulemani kwa kusudi lilo hilo.

Tulipofika tena Bethlehemu, tulitaka kuona jambo moja zaidi, yaani, boma la Herode. Hapa katika kilima kirefu na kinachojulikana sana, mwendo wa kilomita chache upande wa mashariki-kusini mwa Bethlehemu, ndipo yule Herode Mkuu, aliyekuwa ametaka kumwua mtoto Yesu akiwa mchanga,12 alijenga boma lililoitwa kwa jina lake. Siku iliyotangulia tulikuwa tumeona boma kubwa ajabu la makao ya kifalme ya Herode katika Masada kule upande wa mbali wa mashariki-kusini karibu na Bahari ya Chumvi. Huko ndiko Wayahudi walikopigana mara ya mwisho na Warumi katika mwaka 73 W.K. Lakini, lijapokuwa si kubwa, boma la Herode lilikuwa lenye maana kwetu hata zaidi katika njia fulani.

Hiyo ni kwa sababu ya sura ya nchi inayozunguka, ambayo, ijapokuwa haizai kitu, wakati wa kutua kwa jua ilikuwa na sura yenye kupendeza sana ya rangi ya mchanganyiko wo kahawa na dhahabu. Tukiwa upande wa mashariki, tuliweza kuona sehemu yote mpaka kuelekea Bahari ya Chumvi. Mbele yetu lilikuwako jangwa la Uyahudi ambako Daudi alimwepuka Sauli, aliyekuwa akimwinda.13 Tulipoona jinsi eneo hilo lilivyo na mawe, tukafahamu kwamba angeweza kufanya hivyo, sana sana kwa vile alivyokuwa amelijua sana tangu ujana wake. Tukafikiri, vilevile kwamba, alipokuwa akilisha kondoo zake, labda Daudi alikuwa akipanda mara nyingi kilima iki hiki ili apate kutazama sura nzuri ajabu tuliyokuwa tukifurahia.

KUSINI MWA TEL AVIV-YAFO

Wakati wa juma ya kwanza ya kuwa katika Israeli, tulikaa karibu na Tel Aviv katika hoteli inayokaribiana na Bahari ya Kati. Tel Aviv, ambao ni mji mkubwa sana wa Israeli, ni wa kisasa, lakini unapakana na Yafa, mji wa kale. Kwa hiyo miji hiyo inaitwa rasmi Tel Aviv-Yafo.

Ni katika Yafa ndimo mtume Petro alimfufua Dorkasi,14 na ndimo alimopokea maono fulani wakati alipokuwa akikaa nyumbani kwa Simoni mtengenezaji (fundi) wa ngozi karibu na bahari. Kwa sababu ya maono hayo, Petro alikuwa tayari kwenda pamoja na wajumbe waliotoka Kaisaria, waliokuwa wametumwa na Kornelio Mtaifa.15 Kwa vile tulivyokuwa na wakati wa kupita njia kuu inayotoka Tel Aviv kaskazini kwenda Kaisaria, tulikuwa tukiwazia jinsi gani safari hiyo ya muda wa kama saa nzima kwa motokaa ilivyomchukua Petro na wenzake siku mbili.

Siku ile tuliyoelekea kusini, tuliingia katika eneo la kale la Wafilisti. Kwa kuwa hakuna magari ya watalii yaliyokuwa yamepangwa juma hiyo ya kwanza, tulikodi motokaa ndogo ya kutuwezesha tutembelee sehemu zenye kupendeza zinazotajwa na Biblia. Tulipokuwa tukisafari kusini, kwanza tulifika Ashdodi, unakojengwa mji wa kisasa wa Kiisraeli kwenye Bahari ya Kati. Lakini tukakumbuka kwamba wakati mmoja kulikuwako na mji wenye sifa wa Wafilisti karibu na hapo, na kwamba sanduku la Yehova la agano lilipelekwa huko baada ya kutekwa vitani. Watu wa Ashdodi walipigwa kwa majipu makali, ikawalazimu walihamishe Sanduku hilo.16

Tukaendelea na safari yetu kuelekea kusini kwenye Ashkeloni, ambapo sasa panaanza kuwa mahali penye sifa pa watalii kutembelea, tena pana pwani zenye kupendeza. Lakini huo vilevile, ulikuwa mji mkuu wa Wafilisfi wakafi mmoja. Tulipotembelea magofu ya kale, tulipendezwa kuona kwamba katika ishara yake palikuwa na maneno haya ya wimbo wa Daudi juu ya kifo cha Sauli na Yonathani wakati wa kupigana na Wafilisti: “Msiyahubiri mambo haya kafika Gathi, msiyatangaze katika njia za Ashkeloni; wasije wakashangilia binti za Wafilisti, binti za wasiotahiriwa wakasimanga.17

Kisha tukaelekea Gaza na “Sehemu ya Gaza,’’ sehemu ya mji mkuu mwingine wa Wafilisti karibu na bahari. Katika safari yote tulivutwa na rutuba ya nchi; ni nchi yenye kilimo, na inaonekana kwamba ndicho kilicholetea Wafilisti wa kale ufanisi. Lakini Gaza wa siku hizi una alama za vita. Tulipokuwa tukisafiri kwa motokaa katika njia zake kuu, tuliona hali ya huzuni na isiyo na tumaini.

Mahali hapa palitukumbusha mwamuzi wa Israeli, Samsoni, aliyeujua Gaza sana. Usiku mmoja aling’oa milango ya lango kuu la mji, ‘akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.’’18 Basi, baada ya kutembelea sehemu hizi, tunafahamu zaidi sana nguvu za mwujiza alizokuwa nazo katika kupanda mlima wenye urefu wa karibu mita 914, akisafiri umbali wa kilomita 50 akiwa amebeba mzigo huo! Tena ni humu Gaza ambamo Samsoni aliua maelfu ya Wafilisti, kisha akajiua mwenyewe, wakati alipoziangusha nguzo zilizotegemeza paa ya nyumba ambamo Wafilisti walikuwa wakifurahia karamu yao.19

Kutoka Gaza tukageukia mashariki-kusini, kuelekea Beer-sheba, mwendo wa kilomita 50. Barabara nzuri ilitupitisha kuvuka nyanda pana sana, tulimoona ngamia, kondoo na mbuzi, pamoja na Mwarabu mchungaji wao. Tulipoona hema zao kwa umbali, tulidhani bila shaka maisha hayo si tofauti sana na wakati Ibrahimu na Isaka walipokuwa wakiishi katika eneo hilo. Katika Beer-sheba, ambao karibu wote ni mji wa kisasa, tulitembelea soko la Wabedui (linafunguliwa kila Alhamisi) tukastaajabia mazao bora​—⁠na jinsi hayana bei kubwa sana! Tukanunua kilo mbili za machungwa (karibu kumi na mawili) kwa bei kama ya shilingi 2.25 (kama makuta 45).

Walakini, kitu tulichokuwa tukitaka sana ni kilima cha kale, nje ya mji mdogo, unaokubaliwa na wengi kuwa ndio Beer-sheba unaotajwa katika Biblia. Kilima hicho kirefu kinaonekana katika eneo lote linalozunguka. Tulikipanda, tukaweza kuona sura nzuri sana ya nchi kubwa mno iliyo tambarare, ikipambwa vizuri kwa vivuli na nuru kwa sababu ya kutoweka kwa jua. Tulipoyachunguza mambo yaliyochimbuliwa ya magofu ya kale, tukawaza hivi: ‘Lo! mahali pazuri kama nini pa kuishi! ’ Bila shaka hata Ibrahimu aliwaza hivyo. Yeye alikuwa akiishi huko wakati Mungu alipomwagiza amchukue Isaka, apande Mlima Moria (ulio katika kuta za Yerusalemu leo) akamtoe kuwa dhabihu. Kisha Ibrahimu akarudi Beer-sheba.20

Tuliporejea kwenye hoteli usiku huo, tulijaa furaha nyingi. Kuziona sehemu hizo​—⁠nyingi zake hata zikiwa na majina yale yale ya Biblia​—⁠kulithibitisha na kutoa maana nyingi sana ya masimulizi ya Biblia tuliyokuwa tumesoma tangu utoto wetu.

KATIKA SAMARIA

Siku nyingine tulisafiri kwa motokaa kaskazini kando ya Bahari ya Kati, tukigeukia mashariki katika Netanya. Safari hiyo ilituvusha Uwanda wa Sharoni ulio na rutuba nyingi, na baada ya kusafiri mwendo wa kilomita chache, tukafika katika milima ya Samaria. Mara kando yetu tukakiona kilima ambapo zamani mji wa Samaria ulikuwa, mji mkuu wa ufalme wa Israeli wa makabila kumi. Tulipoelekea huko, tulifurahia sura nzuri ajabu ya milima iliyokuwa kando yake na mabonde yenye rutuba. Katika kilele chake tuliona masalio (mabaki) ya nyumba ya kifalme, inayotambulishwa kuwa ya Mfalme Ahabu wa Israeli. Vipande vya pembe za tembo vinavyopatikana huko, vikiwa vya wakati wa karne ya nane na ya tisa K.W.K., vinashuhudia makao hayo ya kifalme yalivyokuwa yenye kujengwa kwa anasa sana hapo mwanzoni.21

Tuliporudi kwenye barabara kuu, tulielekea kaskazini kwenye Bonde la Dothani, ambako kijana Yusufu alikowaona ndugu zake na mifugo yao. Wakulima waliokuwa katika mashamba wakivuna nafaka, na vilevile makundi ya kondoo na mbuzi, yalitoa tamasha yenye kupendeza ya jinsi maisha ya kuchunga mifugo yalivyokuwa hapo zamani. Karibu na Jenin (mji wa kale wa Walawi wa Engannim), tukageuka na kuchukua tena njia yetu, mpaka mwishowe tukafika Nablus. Hapa, katika sehemu ya Shekemu wa kale, Mlima Ebali ulikuwa juu yetu kuelekea kaskazini, nao Mlima Gerizimu ukiwa upande wa juu kuelekea kusini.22 Chini ya Mlima Gerizimu pana kisima cha Yakobo, labda ndicho kisima chenyewe ambapo Yesu alikutana na mwanamke Msamaria alipokuwa akirudi kutoka Yerusalemu. Bila shaka, maneno haya aliyomwambia mwanamke huyo, “Baba zetu waliabudu katika mlima huu,” yalimaanisha Mlima Gerizimu.23

Tukiisha kutelemka kutoka kilele cha Mlima Gerizimu wenye sifa, tukageukia tena kusini, tukisafiri labda katika njia ile ile ambayo Yesu alifuata alipokuwa akienda na kurudi Yerusalemu. Bila kutazamia tukaona ishara ya barabarani ikionyesha “Shilo.” Kwa furaha nyingi tukageukia mashariki tukifuafa barabara nyembamba sana, inayoelekea mahali lilipowekwa sanduku la agano la Yehova wakati wa waamuzi.24 Kijana mmoja ambaye ni askari-jeshi akatukagua, labda alishangaa kutuona tukija mahali hapa ambapo ni mbali sana, ambapo hajaonekana mtu mwingine. Lakini kwetu, hilo lilikuwa jambo lisilosahaulika tuliloona kuwaza kwamba, katika mahali hapa penye vilima na kimya, ndipo wakati mmoja binti Yefta na baadaye mtoto Samweli walipotumikia katika hekalu la Yehova.25

Wakati huu ukawa ni muda wa katikati ya alasiri na kulikuwako mambo mengi zaidi tuliyotaka kuona. Tukiendelea kusafiri mwendo wa kilomita kadha kusini kupita eneo lenye milima, tukageukia mashariki ambao ni mwendo mfupi kwenye vijiji vya Waarabu vya Beitin na Deir Dibwan. Karibu yake ndiko ilikokuwa miji ya Betheli na Ai, inayotajwa katika Biblia. Lakini kwa vile hatukuiona kwa vyepesi, tukauliza habari kutoka kwa wanaume wawili waliokuwa barabarani. Walikuwa wakisema Kiingereza, nao wakatuongoza kwa muda wa saa moja au mbili zilizofuata kwenda kutalii (kufembelea) magofu ya kale yaliyochimbuliwa.

Lo! lilikuwa jambo lenye kuvutia kama nini kusimama katika mwinuko huu, wenye vipimo vya mita 914 juu ya usawa wa bahari na kutazama sehemu ya mashambani inayozunguka, kulipokuwa jioni! Inaonekana kama ni hapa ndipo Ibrahimu alipomkaribisha Lutu achague upande ambao angetaka kwenda wakati wa kutengana na Ibrahimu kwa sababu ya ugomvi uliokuwa kati ya wachungaji wa mifugo yao. Na, kama Biblia inavyosema, “Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji.”26

Tulikuwa tayari kuondoka, lakini mmoja wa wanaume hao akasisitiza tufike nyumbani kwake tukanywe chai na kuonana na jamaa yake. Lo! tulifurahi tulipofika huko! Kulipoanza kuwa giza, tukaanza safari, tukifurahia ukaribishaji huo tulioonyeshwa na watu tusiowajua kabisa, hata pasipo kutazamia.

GALILAYA YENYE KUPENDEZA

Galilaya ilikuwa furaha yetu kuu. Sura zake peke yake zinapendeza sana​—⁠safu ya mlima wa Karmeli kando ya bahari, nchi yenye mawe-mawe upande wa kaskazini, Bahari ya Galilaya iliyo kama kito cha rangi samawati, na lile Bonde la Yezreeli lenye majani mabichi ya kupendeza (vilevile linaitwa Uwanda wa Esdra-eloni) linalotenga Samaria upande wa kusini na milima ya Galilaya upande wa kaskazini. Lakini, bila shaka, tulipendezwa sana na Galilaya kwa sababu huko ndiko Yesu aliishi karibu maisha yake yote ya kuwa hapa duniani, na mambo mengi yanayotajwa katika Biblia yalitukia huko.

Gari letu la watalii lilipoondoka Haifa na kufuata Bonde la Yezreeli, safu ya mlima wa Karmeli ikawa upande wetu wa kuume nao Mtu Kishoni, ukiwa na maua ya rangi zambarau bivu kando yake, ulikuwa upande wetu wa kushoto. Tulipotazama juu katika safu ya mlima, tulifikiria mwujiza wa Yehova uliofanyika huko, ukiteketeza dhabihu ya Eliya katika jaribio lile la moto lenye kujulikana sana. Kisha Eliya akaagiza wale manabii 450 wa Baali watelemshwe huko kwenye mto wa Kishoni, mwendo wa mita chache upande wetu wa kushoto, nao wakachinjwa wote. 27 Kuona mahali yalijotukia hayo kukaongeza maana na kuthamini tukio hilo.

Tuliposafiri umbali wa kilomita chache, tukafika penye magofu ya Megido wa zamani, mji uliokuwa mahali pa kufanyia mapigano kweli kweli. Lo! sura ya Bonde la Yezreeli inaonekana vizuri ajabu kutoka hapo! Ye yote aliyekaa mahali hapa penye kujengewa maboma, angeweza kuongoza njia ya kupita katika safu ya mlima Karmeli; kweli kweli, mapigano ya kukata maneno yalipiganwa hapa. Lo! jinsi jina ­Har–​Magedoni (maana yake “Mlima wa Megido”) linavyotumiwa kwa kufaa katika Biblia kuhusiana na vita ya ushindi ya Mungu juu ya wapinzani wote wa kisiasa!28

Kutoka Megido tukachagua sehemu za bonde hili lenye kujulikana sana, au uwanda. Kule, karibu na katikati ya bonde hilo, kuna kilima cha More. Wakati mmoja katika mitelemko au karibu yake palikuwa na miji midogo ya Naini, Shunemu na Endori. Ng’ambo ya kilima hiki, kilomita chache kuelekea mashariki-kaskazini, kuna Mlima Tabori wenye kujulikana sana, pamoja na kilele chake cha mviringo. Kutoka huko Mwamuzi Baraka akiwa pamoja na Debora, walishuka na kuwashinda Wakanaani wenye kushangaa.29 (Vilevile sura nzuri sana ya eneo hilo inaweza kutazamwa kutoka kilele cha Tabori, tulichokuwa tumepanda kwa motokaa pale mwanzoni.) Kile ambacho hafuwezi kuona kwa sababu kimefichwa na milima ya Galilaya, lakini kilicho karibu sana na bonde, ni Nazarethi, makao ya kwanza ya Yesu. Bila shaka Yesu alilijua sana eneo hili lililo mbele yetu, kwani Nazarethi ni mwendo mfupi sana wa kutembea kwa miguu kutoka mahali hapa pote.

Tukatazama upande mwirigine wa bonde, upande wa mbali wa mashariki-kusini, kuelekea Mlima Gilboa. Karibu na chini yake pana kisima, au chemchemi ya Harodi. Hapo ndipo Gideoni alipokutana na Wamidiani 135,000 waliokuwa wamepiga kambi upande mwingine katika kilima cha More. Tukakumbuka jinsi Yehova alivyomwongoza Gideoni apunguze majeshi yake yawe watu 300 tu, na kwa hao tu akampa Gideoni ushindi.30 Baadaye, katika mpambano kama huo, inaonekana kama Wafilisti walikuwa karibu na kilima cha More nao Waisraeli wakiwa tena penye kisima cha Harodi. Wakati huo Wafilisti waliwashinda Waisraeli, naye Sauli na Yonathani wakauawa.31 Kuona sehemu hizi kulitusaidia tuone vizuri sana katika akili zetu jinsi matukio hayo ya Biblia yalivyokuwa.

Lakini labda jambo lenye kupendeza kuliko yote tuliyoona ni ile Bahari ya Galilaya, kwani ndiyo mara ya kwanza kuiona. Wakati huo tulikuwa tukishuka milima kuelekea kaskazini ya bahari hiyo. Chini yetu, tukaona bahari yenye rangi samawati iliyoonekana kama kito kilindini. Urefu wake ulikuwa kilomita 21, na upana wake kilomita 12. Lakini ilionekana kidogo zaidi, kwa sababu tulikuwa tukitazama tukiwa juu. Inashangaza kujua kwamba ziwa hilo lina vipimo vya karibu mita 213 chini ya usama wa bahari, na karibu linazungukwa na vilima na milima yote.

Tulipokuwa tukistarehe kando ya ziwa hilo, tukilivuka kwa mashua au kulitazama kutoka sehemu zilizoinuka, tuliyafikiria mambo mengi yaliyotukia hapa. Yesu alitembea juu ya maji haya,32 kulipotokea tufani, akayatuliza,33 akala kiamshakinywa pamoja na wanafunzi wake katika pwani za Galilaya baada ya kufufuliwa kwake,34 akatoa hotuba bora kuliko zote kando ya mlima wa karibu,35 akalisha maelfu ya watu huko kwa mikate michache na samaki wawili tu,36 kisha akafanya Kapernaumu kuwa makao yake, mji ulio upande wa kaskazini wa pwani.37

Siku gari letu la watalii lilipoondoka Galilaya kwenda Yerusalemu, tulifika kwenye mji wa Beth-sheani, ulio mahali pa werevu sana kati ya mabonde ya Yezreeli na Yordani. Magofu ya mji huo wa kale yako katika kilima kinachoinuka kufika urefu wa mita 80. Lo! jinsi Bonde la Yezreeli kuelekea Mlima Gilboa na Megido linavyoonekana vizuri zaidi, ukitazama kutoka kileleni mpaka chini kwenye Bonde la Yordani kuelekea Yeriko! Huko Beth-sheani Wafilisti walifunga maiti (mzoga) wa Sauli katika ukuta wa mji alipokwisha kufa vitani katika Mlima Gilboa.38

YERIKO NA YERUSALEMU

Tukafuata Bonde la Yordani, tukitelemka karibu kilomita 80 kuelekea Yeriko. Eneo hilo lilikuwa lenye joto na kame sana, lakini tukakumbuka kwamba hali ingekuwa yenye baridi nzuri wakati wa masika ya mwaka. Basi tukawaza kwamba ijapokuwa ni ndefu zaidi, labda Yesu na jamaa yake walisafiri njia hii ambayo haina magumu, badala ya kupitia Samaria yenye milima mingi, kwenda kuhudhuria Sikukuu za Kupitwa za kila mwaka Yerusalemu.39

Lo! ilipendeza kama nini kufika Yeriko na kuona mitende yake mingi!40 Tukiacha gari lenye kutiwa hewa nzuri ya baridi, tukasikia joto kali la jua. Lilitusaidia tufahamu zaidi sana maneno ya Yesu ya kusifu wale ambao wangewapa wanafunzi wake “ngaa kikombe cha maji ya baridi.”41 Tukapanda kilima ambapo magofu ya Yeriko wa zamani yanachimbuliwa. Eneo hilo ni dogo sana, likitusaidia tufahamu jinsi ilivyowezekana kwa Yoshua na jeshi lake wauzunguke mji mara saba katika siku moja.42

Siku zetu za mwisho kuwa katika Israeli zilitumiwa katika Yerusalemu, mji mkuu unaotajwa katika Biblia. Lilikuwa jambo la maana sana kujionea wenyewe sehemu ambazo tulikuwa tumesoma sana habari zake. Tuliposimama katika Mlima wa Mizeituni, tulikumbuka kwamba Yuda alimsaliti Yesu kwa adui zake katika Bustani ya Gethsemane mahali fulani karibu na hapa.43 Tukitazama kuvuka Bonde la Kidroni, tukaona Kuba la Mwamba la Waislamu, lakini tukajua kwamba katika siku za Yesu, yeye aliona hekalu likiwa mahali hapo. Akiwa analitazama hekalu, alitoa unabii wake wenye kujulikana sana juu ya “mwisho wa taratibu ya mambo.”44

Toka tulipokuwa katika Mlima wa Mizeituni, tuliweza kupaona mahali halisi pa “mji wa Daudi,” na jinsi unavyohusiana na Yerusalemu uliopanuliwa miaka ya baadaye, ulioenea kuelekea kaskazini na magharibi. “Mji wa Daudi,”‏ au “Mlima Sayuni” wa kwanza, ulitekwa kutoka kwa Wayebusi.45 Uko nje ya kuta za kisasa za Yerusalemu, upande wa kusini ya Kuba la Mwamba. Siku nyingine tukafahamu zaidi kwa nini mahali halisi palipokuwa pa mji huo wa kwanza ni maalumu sana.

Tukatelemkia Bonde la Kidroni kwenye chemchemi ya Gihoni, chini ya kilima ulipojengwa “mji wa Daudi.” Chemchemi hiyo iliyofichwa katika pango, ni ya maana sana ili kujua ulipokuwa mji huo, kwani chemchemi ya maji iliyolindwa ilikuwa ya lazima nyakati hizo za kale. Inaonekana kwamba Yoabu na watu wake walitelemka ili waifikie sehemu ya ndani ya mji, wakipita katika tundu ambalo Wayebusi walikuwa wamechimba likafika kwenye chemchemi hii nje ya kuta za mji. Kwa njia hiyo, walifanya shambulio wakiwa ndani na kuuteka mji kuwa mji wa Daudi na Waisraeli.46 Miaka iliyofuata, Mfalme Hezekia aliamuru lichimbwe tundu lenye urefu wa mita 533 kutoka Gihoni mpaka kwenye kidimbwi cha Siloami, kilichokuwa ndani ya mji wakati wa Hezekia. Kweli kweli hiyo ilikuwa kazi ya ufundi sana.47 Jambo hilo liliupatia Yerusalemu akiba ya maji wakati wo wote kukitokea mazingiwa ya mji.

Maji yangali yakitiririka katika tundu la Hezekia. Tulipotembea ndani yake, maji yalifika magotini. Tulipokwisha kutoka mpaka kwenye chemchemi ya En-rogeli. Tukakumbuka kwamba ni hapa En-rogeli ndipo Adoniya, mwana mwasi wa Daudi, alipofanyia karamu ili kuomba watu wamwunge mkono katika kunyakua kiti cha enzi.48 Mfalme Daudi aliyekuwa akifa alipopashwa habari hizo, akaagiza Sulemani mwanawe apakwe mafuta awe mfaIme katika chemchemi hiyo ya Gihoni, ni mwendo wa mita chache upande wa juu wa bonde.49

Basi, kutembelea sehemu hizo kulitupa maoni gani? Hatukuhitaji kuziona kusudi tusadiki kwamba ziko. Hata hivyo, kuzitembelea kulikuwa uhakikisho wa kwamba bila shaka ziko. Lakini, sana sana kufika huko na kuzijua sana hali za matukio ya Biblia kumeongeza maana nyingi na ufahamu wa mambo hayo yaliyotukia.

[Box on page 11]

MITAJO YA BIBLIA

1 Luka 2:​4-16.

2 Mwanzo 35:​16-20.

3 Ruthu 1:​16-19; 2:​2-4.

4 Yohana 7:42; 2 Samweli 2:​18, 32.

5 Hesabu 13:23.

6 Mwanzo 23:​14-19; 25:9; 49: 30, 31; 50:13.

7 Mwanzo 13:18; 35:27.

8 Mwanzo 18:​1-8.

9 Mwanzo 19:​27-29.

10 Mwanzo 37:​12-14.

11 2 Samweli 5:1 -5.

12 Mathayo 2:​7-18.

13 1 Samweli 24:​1-3.

14 Matendo 9:​36-43.

15 Matendo 10:​1-25.

16 1 Samweli 5:​1-9.

17 2 Samweli 1:20.

18 Waamuzi 16:3.

19 Waamuzi 16:​21, 25-30.

20 Mwanzo 21:​30-34; 22:​1-19.

21 1 Wafalme 22:​37-39; Amosi 6: 1, 4. 

22 Kumbukumbu la Torati 11:​29, 30; Yoshua 8:​30-35.

23 Yohana 4:​5-7, 19, 20.

24 Yoshua 18:1.

25 Waamuzi 11:40; 1 Samweli 3: 21.

26 Mwanzo 13:​1-11.

27 1 Wafalme 18:​18-40.

28 Ufunuo 16:​14, 16.

29 Waamuzi 4:​4-16.

30 Waamuzi 7:​1-22; 8:10.

31 1 Samweli 28:4; 31:​1-4.

32 Mathayo 14:​23-32.

33 Marko 4:​35-41.

34 Yohana 21:​9-14.

35 Mathayo 5:​1,2.

36 Mathayo 14:​14-22.

37 Marko 2:1.

38 1 Samweli 31:10.

39 Luka 2:​41,42.

40 Kumbukumbu la Torati 34:3.

41 Mathayo 10:42.

42 Yoshua 6:15.

43 Mathayo 26:​30, 36-47.

44 Marko 13:​3, 4; Mathayo 24: 3, NW.

45 2 Samweli 5:​7, 9; 6:12.

46 2 Samweli 5:​6-9; 1 Mambo ya Nyakati 11:​4-7.

47 2 Wafalme 20:20; 2 Mambo ya Nyakati 32:30.

48 1 Wafalme 1:​9, 10.

49 1 Wafalme 1:​33-41.

[Map on page 4]

(For fully formatted text, see publication)

ISRAELI

BAHARI YA KATI

Kapernaumu

BAHARI ya GALILAYA

Nazarethi

Mto Kishoni

MLIMA KARMELI

MLIMA TABORI

Kilima cha More

Bonde la Yezreeli

Megido

Kaisaria

En-ganimu (Jenin)

MILMA GILBOA

Beth-sheani

Uwanda wa Sharoni

Netanya

Samaria

MLIMA EBAL

MLIMA GERIZIMU

Shekemi (Nablus)

Mto Yordani

UKINGO WA MAGHARIBI

Shilo

Yafa (Tel Aviv)

Betheli

Ai

Yeriko

YORDANI

Yerusalemu

Ashdodi

Bethlehemu

Ashkeloni

Vidimbwi vya Sulemani

Boma la Herode

Bonde la Eshcol

Mamre

Gaza

Hebroni

DEAD SEA

Masada

Beer-sheba

Sodoma na Gomora?

[Picture on page 7]

Tulimwona kijana huyu mchungaji wa kike, akichunga kondoo na mbuzi karibu na Tell Beer-sheba

[Picture on page 9]

Bahari nzuri ya Galilaya kama inavyoonekana leo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki