Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w93 6/15 kur. 4-7
  • Jiografia ya Biblia Je! Ni Sahihi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jiografia ya Biblia Je! Ni Sahihi?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kule Kutoka
  • Jangwa la Sinai
  • Bara Lililoahidiwa
  • Bonde la Yezreeli
  • Wamegundua Nini Huko Yezreeli?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Funzo Namba 1—Ziara Kwenye Bara Lililoahidiwa
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Shekemu—Lile Jiji Katika Bonde
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Kutembelea Mahali Yalikotukia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
w93 6/15 kur. 4-7

Jiografia ya Biblia Je! Ni Sahihi?

JUA imeshuka katika Palestina. Ni mwaka wa 1799. Baada ya kupiga mguu katika siku yenye joto, Jeshi la Ufaransa limepiga kambi, na Napoléoni, mkuu wa jeshi, anapumzika katika hema lake. Kwa mwangaza wenye kuruka-ruka wa mshumaa, mmoja wa watumishi wake anasoma kwa sauti kutoka Biblia ya Kifaransa.

Yaonekana hilo lilitukia mara nyingi katika kampeni ya kijeshi ya Napoléoni katika Palestina. “Tulipokuwa tumepiga kambi kwenye mabomoko ya majiji hayo ya kale,” yeye akakumbuka baadaye katika maandishi yake ya kumbukumbu, “walisoma Maandiko kila jioni kwa sauti . . . Ulingano na ukweli wa masimulizi hayo ulistaajabisha; ungali wafaana na nchi hiyo baada ya karne nyingi na mabadiliko mengi.”

Kwa kweli, wasafiri wanaoenda Mashariki ya Kati huliona kuwa jambo rahisi kulinganisha matukio ya Biblia na mahali-mahali pa leo. Kabla ya Jeshi la Kifaransa kushinda Misri, machache yalijulikana na wageni kuhusu bara hilo la kale. Kisha wanasayansi na wasomi, ambao Napoléoni alikuwa amewaleta Misri, wakaanza kuufunulia ulimwengu mambo madogo-madogo juu ya utukufu wa Misri. Hilo limefanya iwe rahisi zaidi kuona akilini ile “kazi ngumu” ambayo Waisraeli walilazimishwa kufanya wakati mmoja.—Kutoka 1:13, 14.

Usiku wa kuachiliwa kwao kutoka Misri, Waisraeli walikusanyika huko Ramesesi wakapiga mguu hadi “kwenye mpaka wa ile jangwa.” (Kutoka 12:37; 13:20) Walipofikia hapo, Mungu aliwaamuru “warudi” na ‘kupiga kambi karibu na bahari.’ Hatua hiyo ya ajabu ilifasiriwa kuwa “wametatanisha katika nchi,” na mfalme wa Misri alisonga mbele pamoja na jeshi lake na magari ya vita 600 ili kuwateka tena wale waliokuwa watumwa wake.—Kutoka 14:1-9.

Kule Kutoka

Kulingana na Yosefo, mwanahistoria wa karne ya kwanza W.K., jeshi hilo liliwasukuma Waisraeli hadi “mahali pembamba” na kuwanasa “kati ya magenge isiyoweza kufikika na bahari.” Mahali barabara ambapo Waisraeli walivuka Bahari Nyekundu hapajulikani kwa hakika leo. Hata hivyo, ni rahisi kuona akilini tukio hilo kutoka mfululizo wa milima ambapo kutoka hapo upande wa kaskazini wa Bahari Nyekundu waweza kuonekana. Kwa kupendeza, mlima huo waitwa Jebel ʽAtaqah, linalomaanisha “Mlima wa Ukombozi.” Kati ya mfululizo huo wa milima na Bahari Nyekundu kuna uwanda mdogo unaozidi kuwa mwembamba hadi ncha ambapo vilima vya chini vinajitokeza vikiwa karibu kuingia baharini. Kwenye upande ule mwingine wa Bahari Nyekundu kuna oasisi (mahali penye maji jangwani), yenye chemchemi nyingi, ziitwazo ‘Ayun Musa,’ linalomaanisha “visima vya Musa.” Bonde la bahari kati ya mahali hapo pawili hushuka polepole, hali kwingineko linashuka kwa ghafula hadi kimo cha kati ya meta 9 na 18.

Wanatheolojia wa Jumuiya ya Wakristo wasio na imani wamejaribu kuondolea sifa muujiza huo ambao Mungu alifanya alipoyatenganisha maji ya Bahari Nyekundu na akawawezesha Waisraeli waponyoke kwenye nchi kavu. Wao wanaweka mahali pa tukio hilo kwenye bwawa lenye maji machache au mahali pa matope kaskazini mwa Bahari Nyekundu. Lakini hilo halipatani na rekodi ya Biblia, inayosema kwa kurudia-rudia kwamba kuvuka huko kulitukia katika Bahari Nyekundu palipokuwa na maji ya kutosha ya kuwazamisha Farao na jeshi lake lote, naam, ya kuwameza kabisa.—Kutoka 14:26-31; Zaburi 136:13-15; Waebrania 11:29.

Jangwa la Sinai

Hali mbaya sana zinazopatikana katika Peninsula ya Sinai zinaonyeshwa waziwazi katika usimulizi wa Biblia wa kutanga-tanga kwa Israeli. (Kumbukumbu la Torati 8:15) Kwa hiyo, je, taifa nzima lingeweza kukusanyika kwenye sehemu ya chini ya Mlima Sinai ili kupokea Sheria ya Mungu na baadaye kurudi nyuma “wakasimam[e] mbali”? (Kutoka 19:1, 2; 20:18) Je! pana mahali pakubwa pa kutosha kuruhusu hatua kama hiyo ya umati uliokadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni tatu?

Msafiri na msomi mmoja wa Biblia wa karne ya 19, Arthur Stanley, alitembelea eneo la Mlima Sinai na akasimulia mahali palipokabili kikundi chake baada ya kupanda Ras Safsafa: “Jinsi palivyotuvutia, ni jinsi panavyovutia kila mtu ambaye amepaona na kupasimulia, [palituvutia] mara moja. . . . Hapo palikuwa ule uwanda mpana wa kimanjano wenye kimo cha chini ukienea chini hadi msingi wenyewe wa magenge . . . Ikikumbukwa kwamba uunganisho wa uwanda na mlima haupatikani mara nyingi sana katika mkoa huo, huo ni uthibitisho wa maana wa ukweli wa usimulizi huo, kwamba uunganisho mmoja wa jinsi hiyo waweza kupatikana, na kwamba wapatikana katika ujirani wa Sinai ya kimapokeo.”

Bara Lililoahidiwa

Katika mwaka wa 40 wa kutanga-tanga kwa Israeli jangwani, Musa alitoa usimulizi huu wa sifa za bara ambalo walikuwa karibu kuingia: “BWANA [Yehova, NW] Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na vilima.”—Kumbukumbu la Torati 8:7.

Usahihi wa ahadi hiyo ulionwa upesi wakati taifa nzima lilipokusanyika pamoja—wanaume, wanawake, watoto, na wageni—katika bonde la Shekemu lenye maji mengi kati ya Mlima Ebali na Mlima Gerizimu. Makabila sita yalisimama chini ya Mlima Gerizimu. Yale makabila mengine sita yalikusanyika kwenye upande ule mwingine wa bonde chini ya Mlima Ebali ili kusikia zile baraka za kimungu ambazo taifa hilo lingefurahia ikiwa lingetii Sheria ya Yehova na laana ambazo zingelijia ikiwa lingeshindwa kutii Sheria ya Mungu. (Yoshua 8:33-35) Lakini je, kulikuwako nafasi ya kutosha kwa taifa hilo katika bonde hilo jembamba? Hao wote walisikiaje bila vifaa vya kisasa vya kukuza sauti?

Yehova Mungu angaliweza kukuza kimuujiza sauti za Walawi. Hata hivyo, yaonekana muujiza wa jinsi hiyo haukuwa wa lazima. Mtu aweza kusikia vizuri sana akiwa katika bonde hilo. “Wasafiri wote,” akaandika msomi mmoja wa Biblia wa karne ya 19 Alfred Edersheim, “hukubaliana na mambo haya mawili: 1. Kwamba kusingeweza kuwako ugumu wowote wa kusikia kwa wazi kutoka Ebali na Gerizimu, jambo lolote lililonenwa katika bonde hilo. 2. Kwamba milima hiyo miwili ilikuwa na nafasi ya kusimama ya kutoshea Israeli wote.”

Msomi mwingine wa Biblia wa karne ya 19, William Thomson, alisimulia ono lake katika bonde hilo katika kitabu chake The Land and the Book: “Nimepaza sauti ili kusikia mwangwi, kisha nimewazia jinsi ambavyo ni lazima iwe ilikuwa wakati wale Walawi wenye sauti kubwa walipopiga mbiu . . . ‘Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa BWANA [Yehova, NW].’ Na kisha ile AMINA! ya sauti ya juu sana mara kumi juu zaidi, kutoka kwa lile kundi kubwa sana, ikiinuka, na kufurika, na kurudisha mwangwi kutoka Ebali hadi Gerizimu, na kutoka Gerizimu hadi Ebali.”—Linganisha Kumbukumbu la Torati 27:11-15.

Bonde la Yezreeli

Kaskazini mwa Shekemu pana bonde jingine lenye rutuba, ambalo huanzia kwenye usawa wa bahari na kuenea likawa uwanda mpana sana. Mkoa huo wote huitwa Bonde la Yezreeli, kutokana na jina la jiji la Yezreeli. Kaskazini mwa bonde hilo pana vilima vya Galilaya palipokuwa mahali pa nyumbani kwa Yesu, Nazareti. “Nazareti,” aeleza George Smith katika kitabu chake The Historical Geography of the Holy Land, “lakaa katika bonde miongoni mwa vilima; lakini mara unapopanda hadi ukingoni mwa bonde hilo, . . . waona mandhari iliyoje! [Bonde la Yezreeli] liko mbele yako, pamoja na . . . wanja zalo za mapigano . . . ni ramani ya historia ya Agano la Kale.”

Katika uwanda wa bonde hilo, waakiolojia wamechimbua mabomoko ya majiji yaliyokuwa falme zilizoshindwa na Israeli katika siku za Yoshua, yaani, Taanaki, Megido, Yokneamu, na labda Kedeshi. (Yoshua 12:7, 21, 22) Katika mkoa uo huo, katika siku za Mwamuzi Baraka na Mwamuzi Gideoni, Yehova aliwakomboa kimuujiza watu wake kutoka kwa mataifa maadui yenye nguvu nyingi sana.—Waamuzi 5:1, 19-21; 6:33; 7:22.

Karne kadhaa baadaye, Mfalme Yehu alikwenda kwa farasi akikwea bonde hilo hadi kwenye jiji la Yezreeli ili kutekeleza hukumu ya Yehova juu ya nyumba ya Ahabu yenye kuasi-imani. Kutoka kwenye mnara wa mlinzi katika Yezreeli, ingalikuwa rahisi kuona kuelekea mashariki kukaribia kwa majeshi ya Yehu kwenye mwendo wa kilometa 19. Kwa hiyo, kungalikuwako wakati mwingi wa kutosha kwa Mfalme Yehoramu kutuma mjumbe wa kwanza na kisha wa pili juu ya farasi na, hatimaye, kwa wafalme Yehoramu wa Israeli na Ahazia wa Yuda kupanda magari yao ya vita na kwenda kukutana na Yehu kabla ya yeye kufika jiji la Yezreeli. Yehu alimwua Yehoramu upesi. Ahazia alikimbia lakini akajeruhiwa baadaye, na kufa huko Megido. (2 Wafalme 9:16-27) Kuhusu wanja za mapigano kama zile zilizo juu, George Smith aandika hivi: “Ni jambo la kutokeza kwamba hakuna usimulizi . . . usiowezekana kijiografia.”

Bila shaka Yesu mara nyingi alitazama chini kuelekea Bonde la Yezreeli na kutafakari juu ya ushindi mwingi wenye kusisismua uliokuwa umetukia hapo, akijua kwamba, Mesiya aliyeahidiwa, angetimiza daraka la Yoshua Mkuu Zaidi, Baraka Mkuu Zaidi, Gideoni Mkuu Zaidi, na Yehu Mkuu Zaidi katika kuitetea enzi kuu ya Yehova. Kwa kweli, Biblia hutumia Megido, jiji lililokuwa mahali pafaapo zaidi katika uwanda huo, likiwa ufananisho wa mahali pa vita ya Mungu ya Har–Magedoni (linalomaanisha “Mlima wa Megido”). Hilo litakuwa pigano la duniani pote ambamo Yesu Kristo, akiwa Mfalme wa wafalme, atawaharibu maadui wote wa Mungu na wa kundi la Kikristo, watu wa Mungu wa kweli.—Ufunuo 16:16; 17:14.

Biblia husimulia kwamba wakati mmoja Wayahudi wenye hasira wa Nazareti walijaribu kumtupa Yesu chini kutoka “ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake,” ili afe. (Luka 4:29) Kwa kupendeza, kuelekea kusini-magharibi mwa jiji la Nazareti la kisasa kuna genge la meta 12 ambako huenda ikawa jambo hilo lilitukia. Yesu aliwaponyoka maadui wake, na Biblia huongeza kwamba “akashuka mpaka Kapernaumu.” (Luka 4:30, 31) Kwa kweli, Kapernaumu, karibu na Bahari ya Galilaya, liko chini zaidi.

Hayo na mambo mengine mengi madogo-madogo yamewasababisha wengine zaidi ya Napoléoni kuonyesha mshangao juu ya usahihi wa jiografia ya Biblia. “Marejezo ya [Biblia] kwenye umbo la nchi ni mengi sana, na yafaa kabisa,” akaandika Thomson katika The Land and the Book. “Haiwezekani kutovutiwa na upatano wa daima kati ya historia iliyorekodiwa na jiografia ya asili ya Agano la Kale na Agano jipya pia,” aeleza Stanley katika Sinai and Palestine.

Usahihi wa ajabu wa Biblia kuhusu mambo ya kijiografia ni uthibitisho mmoja tu kwamba si kitabu chenye chanzo cha kibinadamu tu. Matoleo matatu ya Mnara wa Mlinzi yanayotangulia hili yana makala juu ya Biblia. Twakualika upate na ufurahie zile sehemu nyingine tatu katika mfululizo huu.

[Ramani page 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BONDE LA YEZREELI

Yezreeli

Nazareti

Taanaki

Megido

Yokneamu

Kedeshi

KASK

BAHARI YA GALILAYA

BAHARI KUU

maili

kilometa

5

10

10

20

[Habari kuhusu chanzo cha ramani]

Inategemea ramani iliyo haki ya Pictorial Archive (Near Eastern History) Est. na Survey of Israel.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Israeli walipokea Sheria kwenye Mlima Sinai

[Hisani]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki