Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 12/1 kur. 14-17
  • Ufanisi Waja Tu kwa Kumtegemea Yehova

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ufanisi Waja Tu kwa Kumtegemea Yehova
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UFALME ULIOGAWANYIKA
  • MSAADA WA YEHOVA KWA ABIJA NA ASA
  • KUMBUKUMBU ZURI LAHARIBIWA NA MAPATANO MABAYA
  • TOKEA UTAWALA WA AMAZIA MPAKA YUDA KUACHWA UKIWA
  • 2 Mambo ya Nyakati—Yaliyomo
    Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya
  • Kitabu Cha Biblia Namba 14—2 Mambo Ya Nyakati
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Kitabu Cha Biblia Namba 12—2 Wafalme
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Mtumikie Yehova kwa Moyo Kamili!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2017
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 12/1 kur. 14-17

Ufanisi Waja Tu kwa Kumtegemea Yehova

KITABU cha Pili cha Mambo ya Nyakati kinaanza kwa kusimulia juu ya ufalme wa Sulemani, kisha kinaendelea kuzungumza juu ya utawala wa wafalme wa Yuda, kikitaja vivi hivi tu juu ya ufalme wa Israeli wa makabila 10, nacho kinamalizia kwa kutaja juu ya kuharibiwa kwa Yerusalemu na kuachwa kwake ukiwa mpaka Mfalme Koreshi akatoa amri hekalu la Yehova lijengwe upya huko. Habari hiyo inaonyesha waziwazi mara nyingi kwamba, wakati watawala pamoja na watu wengine walipomtumaini Yehova Mungu, matendo yao yote yalifanikiwa. Walakini kutoaminika kwao kuliwapotezea baraka pamoja na ulinzi wa kimungu.

Baada ya Sulemani kuimarisha ufalme wake, yeye pamoja na amiri jeshi wote, wakuu na waamuzi wa taifa hilo pamoja na wakuu wa nyumba za mababa, walikwenda katika hema la kukutanikia huko Gibeoni na kutoa dhabihu huko. Hivyo mfalme huyo kijana alimwomba Yehova abariki utawala wake. Wakati wa usiku, Aliye Juu Zaidi alimtokea Sulemani akamtolea nafasi aombe cho chote ambacho angetaka. Kwa unyenyekevu mfalme huyo aliomba apewe hekima iliyohitajiwa pamoja na maarifa ili aweze kuhukumu raia zake. Kwa sababu aliomba jambo bora hivyo, Sulemani alihakikishiwa kwamba, kutia na hekima, angepewa “mali na utajiri, na utukufu,” kupita ule aliofurahia Daudi na Sauli, na kwa kweli, mwingi kupita wo wote ambao ungefurakiwa na mtawala ye yote atakayekuja baadaye. (2 Nya. 1:12) Ahadi hii ilitimizwa kweli kweli, kwa kuwa masimulizi ya habari inatuambia hivi: “Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa kama nawe humo Yerusalemu.”​—⁠1:15.

Mojawapo la matendo makuu ya utawala wa Sulemani lilikuwa kujengwa kwa hekalu la Yehova katika Mlima Moria. Nyingi ya habari katika sura ya pili mpaka ya saba husimulia juu ya matayarisho yake ya ujenzi wa jengo lenyewe pamoja na vifaa vyake na kuzinduliwa kwa hekalu hilo.

Kwa mara nyingine tena, Sulemani alipokea kwa njozi usiku jibu la sala yake ya mzinduo. Jibu hilo lilionyesha kwamba kuendelea kufanikiwa kwa ufalme wake kulitegemea ushikamanifu wa uaminifu wa Israeli kwa sheria ya kimungu. Kwa upande mwingine, kutokuaminika kwa Israeli kungeleta msiba wa kitaifa. Hata hekalu hilo lenye utukufu sana lingefanywa kuwa magofu tu.​—⁠7:11-22.

Sura ya nane na ya tisa humalizia masimulizi juu ya utawala wa Sulemani. Tunaambiwa juu ya namna alivyojenga na kujenga tena miji, namna alivyotumia Wakanaani waliosalia kuwa shokoa, mipango aliyofanya kwa habari ya utumishi wa hekalu, matendo yake ya kujenga na kutumia merikebu, ziara yenye kujulikana sana ya malkia wa Sheba, utajiri wa Sulemani, kifo chake na juu ya mwanawe Rehoboamu alivyopata kuwa mfalme mahali pake.

UFALME ULIOGAWANYIKA

Akipendelea shauri la washauri vijana wasio na ujuzi kuliko shauri lenye kufaa la wazee, Rehoboamu aliwaambia wajumbe waliowakilisha taifa hilo kwamba angezidisha kongwa juu ya watu kuliko alivyofanya baba yake. Kwa kuwa watu hao walikuwa wamedhulumiwa vya kutosha baada ya Sulemani kuacha kufuata sheria ya Yehova karibu na mwisho wa utawala wake, makabila 10 yaliasi, yakitimiza neno la Yehova kupitia kwa Ahija.​—⁠10:1-19.

Akikusanya jeshi, Rehoboamu alitaka kurudisha chini ya utawala wake yale makabila 10 yaliyokuwa yameasi. Walakini, kwa amri ya Yehova kupitia kwa nabii Shemaia, aliachana na mpango huo. Makabila hayo yaliyoasi yaliungana yakawa ufalme wenye kujitawala wenyewe chini ya Yeroboamu, aliyeanzisha ibada ya ndama. Kama matokeo, Walawi waaminifu waliokuwa wakiishi katika miji iliyokuwa chini ya utawala wa Yeroboamu waliiacha wakaenda Yuda na Yerusalemu.​—⁠11:1-17.

Kwa sababu Rehoboamu pamoja na raia zake waliiacha sheria ya kimungu, Yehova aliondoa ulinzi wake. Shishaki aliuvamia utawala wa Yuda akitwaa miji yenye maboma mmoja baada ya mwingine. Walakini, kwa kusikia tangazo la kimungu kwamba wangeachwa washindwe na Shishaki kwa sababu ya kutoaminika kwao, Rehoboamu pamoja na wakuu walijinyenyekeza naye Yehova hakuruhusu huyo mtawala wa Misri auharibu Yerusalemu. Hata hivyo, hazina ya mji ilitwaliwa.​—⁠12:1-12.

MSAADA WA YEHOVA KWA ABIJA NA ASA

Baada ya kifo cha Rehoboamu, mwanawe Abija alianza kutawala. Ndipo ilipotokea vita kati ya Abija na Yeroboamu. Katika pindi moja, mashujaa wa ufalme wa Yuda walikuwa katika hali yenye hatari sana kwa sababu ya kushambuliwa na jeshi la Yeroboamu lililokuwa limejificha. Walakini, kwa kuwa walimlilia Yehova awasaidie, Aliye Juu Zaidi aliwapa ushindi.​—⁠12:16–13:20.

Vivyo hivyo, alipokabiliwa na jeshi la watu milioni moja la Waethiopia na Walubi chini ya Zera, Asa aliyechukua , mahali pa Abija, alimtegemea Yehova amsaidie. Yeye aliomba hivi: “[Yehova], hapana kuliko wewe aliye wa kusaidia, kati yake aliye hodari, na yeye asiye na nguvu; utusaidia, Ee [Yehova], Mungu wetu; kwa kuwa sisi twakutegemea wewe, na kwa jina lako tumekuja juu ya jamii kubwa hii. Ee [Yehova], wewe ndiwe Mungu wetu, asikushinde mwanadamu.” Kwa mara nyingine tena, Yehova aliwapatia ushindi watu wake.​—⁠14:9-15; 16:8.

Kwa kusifika, Asa alifuata maneno ya nabii wa Yehova Odedi akachukua tendo la haraka na kuharibu mahali pa ibada ya sanamu. Walakini, ajapokuwa alikuwa amepata msaada wa kimungu, baadaye Asa alifanya mapatano pamoja na Mfalme Ben-hadadi wa Shamu ili kuzuia Mfalme Baasha wa Israeli asifanye vita juu yake. Alipokaripiwa na Hanani mwonaji kwa sababu ya tendo hili la kutoaminika, Asa aliudhika. Alimfunga katika nyumba ya mkatale na vilevile akaanza kuwaonea baadhi ya wengine wa raia zake. Kwa hiyo Yehova akamwondolea mfalme huyo baraka yake. Aliposhikwa na ugonjwa miguuni yake, Asa alishindwa kumtegemea Yehova apate msaada bali alitafuta msaada kwa waganga.​—⁠15:1–16:13.

KUMBUKUMBU ZURI LAHARIBIWA NA MAPATANO MABAYA

Mwana wa Asa Yehoshafati alijionyesha kuwa mfalme mwema, na kwa hiyo, alipata msaada na ulinzi wa Yehova. Alijitahidi kumaliza ibada ya sanamu, akafanya mipango watu wafundishwe sheria ya Yehova na kuleta maendeleo katika taratibu za kuhukumu. Kwa sababu ya kumtegemea Yehova, alipata kuona wokovu mkubwa wakati jeshi la mwungano la Amoni, Moabu na mlima Seiri lilipoangamizana. Hata hivyo, kwa upumbavu Yehoshafati alifanya mapatano ya ndoa pamoja na Mfalme Ahabu wa Israeli mwabudu sanamu. Athalia, binti ya Ahabu na malkia Yezebeli mwabudu-Baali, akawa mke wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati. Jambo hili lilimfanya Yehoshafati ajiunge katika tendo la kijeshi pamoja na Mfalme Ahabu lenye kuleta msiba. Aliporudi Yerusalemu, Yehoshafati alipokelewa kwa karipio hili: “Je! imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao [Yehova]?” Walakini baadaye, Yehoshafati alishindwa tena na jambo lilo hilo kwa kushirikiana na Mfalme Ahazia aliyechukua mahali pa Ahabu,’katika mpango wa kujenga merikebu. Katika kutimiza unabii, merikebu hizo ziliharibiwa.​—⁠17:1–20:37.

Yehoramu, mfalme wa Yuda aliyefuata, alifuata mwendo mbaya wa nyumba ya Ahabu, kwa kuongozwa na mkewe Athalia. Ili aimarishe cheo chake cha kifalme, aliwaua ndugu zake zote pamoja na wakuu wengine. Pasipo baraka za Yehova, utawala wake ulishindwa. Alisumbuliwa mara nyingi na uasi wa Waedomu pamoja na mji wa Libna. Katika miaka miwili ya mwisho ya maisha yake, alipigwa kwa ugonjwa mkuu wa maradhi ya matumbo.​—⁠21:1-20.

Wakati Ahazia mwana aliye mdogo zaidi wa Yehoramu alipopata kuwa mfalme, utawala mbaya uliendelea, kwa kuwa yeye vilevile aliongozwa na Athalia. Alipokuwa akimtembelea Yehoramu mfalme wa Israeli aliyejeruhiwa, Ahazia aliingilia kitendo cha Yehu cha kuiadhibu nyumba ya Ahabu akauawa. Alipoona hivyo, Athalia alijitwalia kiti cha enzi kwa nguvu, baada ya kuwaua wana wa kifalme. Hata hivyo, Yoashi mwana wa Ahazia alikuwa amefichwa na mke wa kuhani Yehoyada. Baadaye Yehoyada alifanya Yoashi atangazwe kuwa mfalme na kuamuru kwamba Athalia auawe.

Chini ya uongozi wa Yehoyada, Yoashi alitawala vizuri hata akafanya mipango hekalu litengenezwe upya. Walakini, baada ya kifo cha Yehoyada, Yoashi aliiacha ibada ya kweli, na hata akaagiza kwamba Zekaria mwana wa Yehoyada apigwe mawe kwa sababu ya kumkaripia kwa sababu ya kutoaminika kwake. Ndipo Yehova alipowaruhusu Washami waushinde ufalme wa Yuda. Yoashi alipatwa na ugonjwa na mwishowe akauawa na watumishi wake mwenyewe.​—⁠22:1–24:27.

TOKEA UTAWALA WA AMAZIA MPAKA YUDA KUACHWA UKIWA

Amazia mwana wa Yoashi alianza vizuri walakini baadaye aligeuka akakosa kuwa mwaminifu. Bada ya miaka mingi ya kukaa pamoja kwa amani, falme mbili za Israeli ziliingiliana katika vita, nayo majeshi ya Amazia yakashindwa. Tangu Amazia aache kufuata sheria ya Mungu, hila ilipangwa juu yake. Alipolazimika kukimbilia Lakishi, aliuawa huko na wale waliopanga hila juu yake.​—⁠25:1-28.

Uzia, mfalme wa Yuda aliyefuata, alitawala vizuri naye alipendelewa akapata ushindi mwingi juu ya adui za ufalme wa Yuda. Walakini baadaye alijitanguliza kwa kiburi akaingia hekaluni na kufukiza uvumba kama kuhani. Kwa sababu ya tendo hili la kujitanguliza alipigwa kwa ukoma. Ndipo mwanawe Yothamu alipoanza kutawala. Kwa kuwa Yothamu aliifuata sheria ya Yehova, alifanikiwa, hata akawashinda Waamoni.​—⁠26:1–27:9.

Walakini, Ahazi, aliyechukua mahali pa Yothamu, akawa mwabudu-sanamu mwenye sifa mbaya sana, hata akafikia hatua ya kutoa [wa]nawe kuwa dhabihu. Kama matokeo, Yehova aliondoa baraka zake kwa Ahazi pamoja na raia zake wenye kuabudu sanamu. Ufalme wa Yuda ukapatwa na shida nyingi kwa kushambuliwa na Waedomu, Wafilisti, Waisraeli na Washami. Akiogopa kupoteza cheo chake cha kifalme, Ahazi aliwaomba Waashuru msaada wa kijeshi. Walakini tendo hilo lisilo la hekima halikumwondelea shida, lilimletea tu uonezi wa kigeni.​—⁠28:1-27.

Hezekia, mwana wa Ahazi alijitahidi kuondoa ibada ya sanamu katika utawala wake hata akawaasi Waashuru. Ijapokuwa Mfalme Senakeribu Mwashuru aliishambulia nchi ya Yuda, alishindwa kuuteka Yerusalemu. Hezekia alithawabishwa kwa kumtegemea Yehova, kwa kuwa malaika wa Yehova aliliangamiza jeshi la Ashuru katika usiku mmoja.​—⁠29:1–32:22.

Manase, mwana wa Hezekia aliianzisha tena ibada ya sanamu naye akawa na hatia ya kuwadhulumu vibaya sana raia zake. Walakini, alipopelekwa Babeli akiwa mateka, alirudiwa na fahamu zake akatubu. Yehova Mungu alimrehemu, akafungua njia Manase arudi Yerusalemu. Ndipo mfalme huyo alipojaribu kutengeneza mambo ya kidini, walakini wafu walikuwa wamezoea ibada ya sanamu sana hata jitihada za Manase hazikuweza kuleta mabadiliko ya kweli. Hata Amoni mwanawe alipokalia kiti cha enzi aliirudia ibada ya sanamu. Aliangamia mikononi mwa wenye kumfanyia hila.​—⁠33:1-25.

Yosia, mfalme mwema wa mwisho wa Yuda, alianzisha mpango mkubwa wa kuimaliza ibada ya sanamu. Walakini ilikuwa kuchelewa mno kuweza kuwaleta watu katika toba ya kweli. Vilevile, Yuda ilikuwa na hatia kubwa sana ya kumwaga damu. (2 Fal. 24:3, 4) Jambo la kuhuzunisha ni kwamba Yosia mwenyewe aliuawa alipokuwa akijaribu kuzuia majeshi ya Misri huko Megido yalipokuwa yakielekea Karkemishi kupigana vita na Wababeli. Wafalme wanne wa mwisho​—⁠Yehoahazi, Yehoyakimu, Yekonia na Zedekia walijionyesha wenyewe kuwa watawala wabaya. Yehova aliuacha kabisa ufalme wa Yuda, akiwaruhusu Wababeli chini ya Nebukadreza wauangamize Yerusalemu pamoja na hekalu lake kubwa. Wengi wa wale waliookoka walichukuliwa uhamishoni. Mwishowe, katika kutimiza neno la Yehova kupitia kwa nabii wake Yeremia, Koreshi alitoa amri iliyowawezesha wahamishwa hao wairudie nchi yao iliyokuwa imeachwa ukiwa.​—⁠2 Nya. 34:1–36:23.

Lo! namna maandishi haya yanavyoonyesha kwamba, hakuwezi kuwa na ufanisi wa kweli bila uaminifu kwa Yehova Mungu! Kama vile nabii Hanani alivyomwambia Mfalme Asa mwenye kuasi, matendo ya upumbavu yanayoonyesha kutokumwamini Mungu yanaleta msiba tu, hali, “Macho ya [Yehova] hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake.”​—⁠2 Nya. 16:9.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki