Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w79 9/15 kur. 8-13
  • Mwanamke Mwenye Akili Aonyesha Si Mchoyo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mwanamke Mwenye Akili Aonyesha Si Mchoyo
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • CHOYO CHALETA AIBU
  • MWANAMKE MTIIFU APATA KIBALI
  • MSHIKAMANIFU, LAKINI ASIYERIDHIANA NA ADUI
  • WAKATI WA UHODARI
  • Kitabu Cha Biblia Namba 17—Esta
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Aliwatetea Watu wa Mungu
    Igeni Imani Yao
  • Aliwatetea Watu wa Mungu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Esta
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1979
w79 9/15 kur. 8-13

Mwanamke Mwenye Akili Aonyesha Si Mchoyo

1, 2. (a) Ni matukio gani yenye kusisimua ya karne ya tano K.W.K. tunayotaka kufikiria, nayo yameandikwa wapi? (b) Ahasuero alikuwa nani? (c) Ni kwa sababu gani kufikiria mambo haya ya nyakati zilizopita kutatufaidi?

NDIPO iliposimama katika mji wa Shushani [Susa]. Jengo hilo lilikuwa nyumba ya kifalme nzuri sana! Walioijenga? Inaelekea walikuwa Mfalme Mwajemi Dario wa Kwanza na mwanawe Mfalme Artashasta wa Kwanza. Vifaa vya kupamba jengo hilo vilikuwa vimeletwa kutoka sehemu za mbali. Kwa mfano, maneno ya michoro ya Dario yanasema kwamba mbao zililetwa kutoka Lebanoni, dhahabu kutoka Sardi na Baktria, fedha na shaba kutoka Misri, nazo pembe kutoka nchi kama vile Ethiopia na Bara Hindi.

2 Leo, ni magofu madogo-madogo tu ya nyumba hiyo ya kifalme iliyokuwa nzuri sana yanayobaki. Lakini kupitia kwa kitabu cha Biblia cha Esta, kilichoandikwa bila shaka na Mwebrania mtawa Mordekai, tunaweza “kuzuru” makao hayo ya kifalme ya kipindi cha mwanzo-mwanzo wa karne ya tano Kabla ya Wakati wa Kawaida wetu. Tunaweza kuyaona tena matukio yenye kusisimua ya muda wa miaka kumi (kuanzia kama mwaka 484 mpaka 474 K.W.K.) kama yalivyokuwa wakati watu wa Mungu walipokabiliwa na maangamizi katika Milki yote ya Uajemi. Hizo zilikuwa zile siku za Ahasuero (kwa wazi Artashasta wa Kwanza). Tutafaidika kwa kuangalia mambo ya zamani zilizopita kwa kuwa habari kama hizo za Biblia ziliandikwa ili kufundisha watu wanaomwogopa Mungu, “ili kwa subira na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini.”​​—⁠Rum. 15:4.

CHOYO CHALETA AIBU

3-5. Shushani ngomeni ni nini, nao ni mkutano wa namna gani unaofanyiwa hapo katika mwaka wa tatu wa utawala wa Mfalme Ahasuero?

3 Mfalme Ahasuero Mwajemi, ambaye utawala wake watia ndani majimbo 127 toka Bara Hindi mpaka Ethiopia (kushi), anakalia kiti cha enzi katika Shushani makao yake ya muda, ambayo ni majengo yenye nyumba nyingi za kifalme katika eneo lililokuwa ngome. Sasa ni mwaka ya tatu wa utawala wake naye ameita mkutano wa wakuu wake, watumishi, wanaume wa jeshi na wengine wenye vyeo vikubwa. Mkutano huo waendelea kwa muda wa siku 180, yaelekea ili kuwapa nafasi wakuu ambao ni wengi ambao kazi zao haziwaruhusu kuwapo wote pamoja katika wakati ule ule. (Huenda kusudi la kijeshi linahusika, kwa kuwa mwanahistoria Mgiriki Herodoto aliripoti kwamba katika mwaka wa tatu wa utawala wake Mfalme Artashasta alifanya mkutano wa kupanga vita juu ya Ugiriki.)​​—⁠Esta 1:1-4.

4 Katika kumaliza mkutano huu wenye maana, mfalme afanya karamu ya siku saba kwa ajili ya watu wote waliokuwako Shushani ngomeni. Karamu hii inafanyiwa uani wa bustani ya nyumba ya kifalme. Ebu tazama kandokando yake! Kwani, vitu vya kupamba vyatia ndani mapazia ya bafta, nyeupe na samawi, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marimari.​​—⁠Esta 1:5, 6.

5 Katika karamu hii wanawanywesha divai katika vyombo vya dhahabu vya namna mbalimbali. Walakini desturi ya kumwekea mgeni sharti juu ya kiasi fulani cha kileo haifuatwi katika karamu hii.​​—⁠Esta 1:7, 8.

6. Vashti ni mwanamke wa namna gani, nalo hilo laonyeshwaje?

6 Mahali penginepo katika ngome hii ya kifalme, Malkia Vashti Mwajemi anawafanyia wanawake karamu. Sasa ni siku ya saba ya karamu ya mfalme nao moyo wake umechangamshwa na divai. Awaambia wasimamizi-wa-nyumba saba wamlete mrembo Vashti mbele yake na wageni wake. Lakini, nini hii? Yeye anaendelea kukataa neno la mfalme. Kwa kughadhibika, Ahasuero aomba shauri kutoka kwa wana wa kifalme saba waliokuwa wasiri wake, wakiwa baraza ya wanaume wenye hekima waliokuwa na elimu ya mambo ya kisheria. “Kwa sheria,” auliza mfalme, “tumfanyieje Vashti, malkia”? Mwanamke huyu mchoyo ana hatia ya kumkaidi mfalme!​​—⁠Esta 1:9-15.

7, 8. (a) Vashti amekosea nani, nao mwendo huo wake wamletea nini? (b) Wewe wadhani twaweza kujifunza nini kutokana na mwenendo wa Vashti?

7 Sikiliza! Memukeni mnenaji mkuu wa hawa wana saba wa kifalme anapoteta kwamba, Vashti amekosea, si mfalme peke yake, bali pia wana wa kifalme wote pamoja na watu wa milki yote. Mwenendo wake utajulikana, nao wake wote, hata binti za kifalme, watawadharau waume zao. Kwa hiyo, Memukani apendekeza hivi, mwache mfalme aamuru kwamba Vashti hatakuja mbele yake kamwe na kwamba heshima yake ya kifalme ichukuliwe na mwanamke aliye bora kumshinda. Ndipo wanawake wote walioolewa watawaheshimu waume zao.​​—⁠Esta 1:16-20.

8 Pendekezo hili lampendeza Ahasuero. Upesi zikapelekwa nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila taifa kwa lugha yake. Kwa kuandikwa sasa katika sheria za Wamedi na Waajemi zisizoweza kubadilishwa, amri ilitoa ruhusa “Kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake.” Choyo cha Vashti na ukaidi wake kimempotezea taji ya kifalme. Kimefanya aaibishwe.

MWANAMKE MTIIFU APATA KIBALI

9. Malkia wa kuchukua mahali pa Vashti atachaguliwaje?

9 Muda fulani wapita kabla ya ghadhabu ya Ahasuero kupoa. Halafu, kulingana na pendekezo la washauri wa mfalme, wasimamizi waliowekwa watafuta mabikira vijana wazuri katika majimbo yote ya ufalme. Wanawake hawa wanaletwa katika Shushani ngomeni na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai, msimamizi-wa-nyumba ya mfalme. Mabikira hao waliochaguliwa watapewa vifaa vya utakaso, na mwishowe, yule msichana atakayempendeza zaidi mfalme atafanywa malkia mahali pa Vashti. (Karibu miaka minne yapita tangu Vashti aondolewe umalikia wake mpaka kuchaguliwa kwa yule atakayechukua mahali pake, inaelekea kukawia huko kulisababishwa na kutokuwapo kwa mfalme alipokuwa amekwenda kupigana vita na Wagiriki.)​​—⁠Esta 2:1-4, 16, 17.

10. (a) Mordekai ni nani? (b) Esta ni nani?

10 Anayependezwa sana na kutafutwa huku kwa malkia mpya ni Mordekai, mtumishi wa mfalme. Myahudi huyu mtawa wa kabila la Benyamini ni wa wana wa mtu fulani aitwaye Kishi, aliyechukuliwa mateka huko Babeli na Mfalme Nebukadreza pamoja na Mfalme Yekonia na wengine (katika mwaka 617 K.W.K.) Muda fulani uliopita, Mordekai alipata kuwa mlezi wa msichana yatima Myahudi jina lake Hadasa, ambaye jina lake lamaanisha “mhadasi.” Jina jingine lake ni Esta (maana yake ‘mhadasi’), yeye ni binti ya Abihaili mjomba marehemu wa Mordekai. Naye amekuwa msichana mzuri ajabu! Kwani, yeye ana “umbo mzuri na uso mwema.” Si ajabu kwamba, anayechukua mahali pa Vashti alipokuwa akitafutwa, Esta alikuwa mmojawapo wa wanawake vijana waliokusanywa pamoja katika Shushani ngomeni na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai.​​—⁠Esta 2:5-8, 15.

11. Hegai amtendeaje Esta, na, kwa kutii maagizo ya Mordekai, ni uhakika gani ambao hakufunua?

11 Esta ampendeza Hegai, ambaye afanya haraka kumpa vifaa vya utakaso, pamoja na chakula kifaacho. Kwa kweli, wasichana saba wanachaguliwa wamtumikie katika sehemu iliyo nzuri zaidi ya nyumba ya wanawake. Esta hataji kwamba yeye ni Myahudi, hivyo akifuata maagizo ya Mordekai binamu yake mkubwa. Kwa muda wa miezi sita, hao mabikira waliochaguliwa wapata utakaso kwa mafuta ya manemane, ikifuatwa na miezi mingine sita kwa mafuta ya zeri. Kisha, kila moja wa wanawake hao waingia ndani kwa Ahasuero, na baadaye warudi katika “nyumba ya pili ya wanawake” mikononi mwa Shaashgazi, msimamizi wake mfalme, mwenye kuwalinda masuria.​​—⁠Esta 2:9-14.

12. Esta ana sifa gani, naye Ahasuero amwonaje, kukawa na matokeo gani?

12 Esta si mchoyo, yeye hategemei kujipamba kwa kujionyesha, na kwa hiyo yeye haombi cho chote asichotaja Hegai. Wakati huu wote, amekuwa akipata kibali machoni pa kila mtu amwonaye. Sasa ni mwezi wa Tebethi (Desemba-Januari), mwezi wa kumi wa mwaka wa saba wa Ahasuero. Wasiwasi waongezeka wakati Esta anapopelekwa mbele ya mfalme. Je! yeye anapendezwa naye? Sana! Mtawala huyo Mwajemi akaja kumpenda Esta zaidi ya hao wanawake wengine wote akamfanya kuwa malkia mahali pa Vashti. Mfalme huyo mwenye furaha awafanyia wakuu wake na watumishi wake karamu kuu, yaani, “karamu ya Esta.” Zaidi ya hayo, atoa msamaha katika majimbo yote ya ufalme wake (labda msamaha wa kulipa kodi, kufunguliwa kutoka katika utumishi wa kijeshi au gerezani, au yote hayo pamoja). Ahasuero aendelea kutoa zawadi ambazo utajiri wa mfalme peke yake ndio unaoweza kufanya iwezekane kutoa. Lo! ni wakati wa furaha namna gani!​​—⁠Esta 2:15-18.

13. (a) Kujipamba kwa maana zaidi kwa Esta kulikuwa kujipamba kupi? (b) Wanawake Wakristo wa karne ya 20 waweza kufaidikaje kwa kufikiria mwenendo wa Vashti na wa Esta?

13 Mwanamke mtiifu kweli kweli amepata kibali. Ijapokuwa sasa Esta ni malkia wa Uajemi, yeye anafuata maagizo ya Mordekai. (Esta 2:19, 20) Tunapoangalia nyuma, twaweza kumwona Esta akiwa mwanamke mwenye sura nzuri akiwa amejivika vazi la kifalme. Walakini ‘kujipamba kwake kwa maana zaidi kulikuwa utu usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.” (1 Pet. 3:3, 4) Wanawake Wakristo wa karne ya 20 wana sababu nzuri ya kujiepusha na choyo cha Vashti aliyeondolewa cheo na kuiga sifa za Esta mwenye kumwogopa Mungu na asiye mchoyo.

14. Ni kwa sababu gani sana sana Mordekai angefurahi sana kwa sababu ya Esta kuwa malkia?

14 Vilevile inastahili kuangaliwa kwamba Esta alipowekwa kuwa malkia, kulikuwako furaha kuu, ambayo, bila shaka Mordekai, binamu yake mkubwa alishiriki kwa moyo wote. Lazima awe aliona kwamba mwishowe hii ingewaletea faida Wayahudi wote waliokuwako katika mikoa ya Uajemi.

MSHIKAMANIFU, LAKINI ASIYERIDHIANA NA ADUI

15. Mordekai aripoti hila gani, nao wahaini hao wapatwa na jambo gani?

15 Esta amekuwa akipashana habari na Mordekai na kufuata maagizo yake. Alipokuwa akikaa langoni pa mfalme, Bigthana na Tereshi (ambao inaelekea ndio waliokuwa wakilinda mlango wa nyumba ya faragha ya mfalme) waghadhibika na kutaka kumtia mikononi mwao Mfalme Ahasuero. Akijua mpango huo wa uhaini, Mordekai amjulisha Esta mara moja, ambaye amwambia mfalme kwa jina la Mordekai. Maneno yatokeza uchunguzi. Upesi wahaini hao wawili wauawa na maiti zao kutundikwa juu ya mti machoni pa wote kwa kuwa uhalifu wao wa sheria ulihusu mfalme mwenyewe. Ijapokuwa Mordekai hapati zawadi yo yote wakati huo, tendo lake la ushikamanifu linaandikwa katika kitabu cha wakati huo cha kuandikwa mambo.​​—⁠Esta 2:21-23.

16, 17. (a) Hamani ni nani? (b) Mordekai anakataa kumsujudia Hamani kwa sababu gani?

16 Ijapokuwa Mordekai ni mshikamanifu na anaheshimu ifaavyo mamlaka ya kiserikali, yeye haridhiani na adui. Wakati wapita, na kwa sababu fulani Ahasuero amweka mtu fulani tajiri jina lake Hamani kuwa waziri mkuu. Vilevile, kwa amri ya kifalme watumishi wote walioko langoni pa nyumba ya kifalme wanainama na kumsujudia Hamani. Walakini, ebu mwangalie Mordekai! Yeye anaendelea kukataa kumsujudia waziri mkuu mpya aliyewekwa. Jambo hilo lamghadhibisha sana Hamani.​—⁠Esta 3:1-5.

17 Sababu gani Mordekai akachukua msimamo imara kama huo? Basi, Hamani ni Mwagagi, labda Mwamaleki wa nyumba ya kifalme. Yehova alikuwa ameamuru kwamba Waamaleki waangamizwe kabisa kwa sababu walionyesha chuki yao kwa Mungu kwa kuwashambulia watu wake kwa kuwashambulia Waisraeli jangwani. (Kut. 17:8, 14-16; Kum. 25:17-19; 1 Sam. 15:1-33) Kwa hiyo, Mordekai mwenye kumwogopa Mungu akataa kwa uthabiti kumsujudia Hamani. Kuinama kungeonyesha, si heshima tu, bali kumtakia amani Mwamaleki huyu. Mordekai anakataa kutii kwa sababu jambo hili linahusu kushika ukamilifu wake kwa Mungu.

18. Kwa kupatwa na hasira nyingi, Hamani apanga kumtendaje Mordekai pamoja na Wayahudi wote katika Milki yote ya Uajemi?

18 Kwa kupatwa na hasira nyingi Hamani aanza kutafuta njia ya kuangamiza Mordekai pamoja na watu wake Wayahudi katika milki yote. Kwa hiyo, katika mwezi wa Nisani, mwezi wa kwanza wa mwaka wa kumi na mbili wa Ahasuero, Mwagagi huyu mbaya anatumia unajimu. Awaomba wanajimu, “wakapiga Puri, yaani, kura.” Hili, lafanywa ili kuamua siku inayofaa zaidi kuwaangamiza watu wa Yehova.​​—⁠Esta 3:6, 7.

19, 20. Kwa uongo, Hamani amwambia nini Ahasuero juu ya Wayahudi, na kwa hiyo jambo gani lafanywa?

19 Akisema sasa na Mfalme Ahasuero, Hamani kwa uongo awaonyesha Wayahudi kuwa watu wasiotakikana, wavunjaji wa sheria. Akiongeza faida ya kiuchumi, Mwagagi huyo asema: “Na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha [zenye thamani ya shilingi au makuta milioni nyingi] mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme.”​​—⁠Esta 3:8, 9.

20 Je! Ahasuero anaamini mashtaka haya ya uongo? Ndiyo! Akiondoa pete yake, inayotumiwa kutia muhuri maandishi ya kiserikali, mfalme ampa Hamani. “Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema,” asema mtawala Mwajemi. Upesi, chini ya uongozi wa Hamani, waandishi wa kifalme waandika barua yenye amri ya kuangamiza Wayahudi. Kisha, Mwagagi huyo mwovu anatumia pete yenye ishafa ya pekee ya mfalme. Hamani ashindilia ile pete juu ya nta au kitu kingine kilicho laini juu ya barua hizi ili kuzihalalisha.​​—⁠Esta 3:10-12.

21. Kwa amri ya kifalme, ni jambo gani litakalowapata Wayahudi katika Adari 13 katika mwaka wa 12 wa utawala wa Ahasuero?

21 Upesi barua hizo zimewekwa mikononi mwa matarishi wanaowapanda farasi wenye mbio wa kupeleka barua. Amri hiyo ambayo imeandikwa katika lugha mbalimbali na kupelekwa katika kila jimbo la milki hiyo, inatoa ruhusa ya kuteka nyara mali na kuwaangamiza kabisa Wayahudi. Wakati gani? Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa majira ya baridi Adari (Februari-Machi). Kwa hiyo, kwa kufahamika, wakati Ahasuero na Hamani wanapokaa na kunywa, kuna mvurugo mwingi Shushani, ambapo kuna Wayahudi wengi.​​—⁠Esta 3:13-15; 9:18.

WAKATI WA UHODARI

22. Mordekai pamoja na Wayahudi wengine wanafanya nini wanapojua habari ya hila hiyo ya kuwaangamiza?

22 Mordekai ajifunzapo juu ya hila hii ya mauaji, anararua nguo zake, na kujivika magunia pamoja na majivu kama ishara ya kuomboleza kwake, alia kwa sauti kuu ya uchungu. Vivyo hivyo, hatari ya msiba huo yatokeza ombolezo kubwa kati ya Wayahudi katika majimbo yote ya ufalme huo. Hata hivyo, vilevile kunakuwa na kufunga kulana bila shaka sala nyingi zamwendea Yehova Mungu.​​—⁠Esta 4:1-3.

23. Mordekai amwamuru Esta afanye nini, lakini huenda jambo gani likatokea akienda mbele ya mfalme bila kualikwa?

23 Esta vilevile anahuzunika sana. Amepelekea Mordekai mavazi ajivike mahali pa magunia, walakini yeye hayapokei. Katika kujibu ulizo, ampelekea malkia nakala ya sheria ambayo imetolewa sasa hivi na kumwamuru aende mbele ya mfalme amwombe kibali kwa ajili ya watu wake. Jibu lake? ‘Kila mtu ajua kwamba mwanamume au mwanamke ye yote amwendeaye mfalme bila kuitwa naye lazima afe. Isipokuwa yeye ambaye mfalme amnyosheaye fimbo ya dhahabu ndiye anayeweza kuendelea kuishi. Kwa habari yangu mimi, hajaniita sasa mbele yake kwa siku 30.’ (Esta 4:4-11) Ndiyo, Esta angepoteza maisha yake isipokuwa Mfalme Ahasuero akubali kuwapo kwake mbele yake kwa njia ya kipekee kwa kunyosha mbele yake fimbo yake, fimbo anayochukua ikiwa ishara ya mamlaka yake ya kifalme. Bila shaka mtu angehitaji kuwa na uhodari na imani katika Yehova ili aende mbele ya mfalme bila kualikwa.

24. Mordekai anaamini nini kwa habari ya Esta kupata heshima ya kifalme?

24 Hata hivyo, Mordekai ajibu hivi: “Wewe usijidhanie ya kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote. Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?” (Esta 4:12-14) Mordekai anaamini kwamba Esta amepata heshima ya kifalme kwa wakati uu huu kwa kusudi la pekee​—⁠kuokoa watu wa Mungu. Lakini, je! yeye atajionyesha kuwa si mchoyo, ni hodari na mwenye imani?

25. Katika kufunga, Mordekai, Esta na Wayahudi walioko Shushani wanafanya nini?

25 Katika kujibu, Esta amsihi Mordekai awakusanye Wayahudi wote katika Shushani na kufunga kula kwa ajili yake. ‘Nami nitafunga vilevile,’ asema Esta, “kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.” Esta yu karibu kuhatirisha uhai wake mwenyewe, walakini mwanamke huyu mwenye akili ameazimia kutenda kwa uhodari na bila uchoyo kwa ajili ya watu wake. Ndivyo ilivyokuwa kwamba Esta, Mordekai pamoja na Wayahudi waliokuwako shushani wakachanganya sala na kufunga na kumtazamia Yehova Mungu kwa ajili ya wokovu wao.​​—⁠Esta 4:15-17.

26. Leo, adui za watu wa Mungu huenda wakaruhusiwa kufanya nini, lakini, kwa sababu hiyo, inawapaswa Wakristo watiwa mafuta pamoja na wanaoshirikiana nao walio wakf wafanye nini?

26 Vivyo hivyo, katika nyakati za kisasa, wafuasi watiwa mafuta wa Yesu Kristo, ambao ni Wayahudi wa kiroho, pamoja na wale wanaoshirikiana nao lazima wakabiliane na majaribu na adui zao kwa uhodari. (Rum. 2:28, 29) Mfalme anayetawala, Yesu Kristo, aweza kuwaruhusu adui za watu wa Mungu wajitahidi wawezavyo kuwaangamiza. Basi, ni jambo la maana kama nini, kwamba Wakristo watiwa mafuta pamoja na wale wanaoshirikiana nao walio wakf watende kwa uhodari, na kuomba hekima ya kimungu na kuonyesha imani ishindayo! Walakini je! Yehova ataendelea kuwategemeza watu wake? Hukumu mwenyewe, kama vile matukio yenye kusisimua ya siku za Esta yaendeleavyo kuwa wazi mbele yetu.

[Picha katika ukurasa wa 9]

“Nami nikiangamia, na niangamie.”​​—⁠Esta 4:16.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki