Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 2/15 kur. 3-11
  • Njia ya Uzima au Njia ya Mauti—Njia Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Njia ya Uzima au Njia ya Mauti—Njia Gani?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MATESO YA KIDINI NA MATOKEO YAKE
  • KUKIMBILIA KWENYE UPANDE WA MAJESHI YA MUNGU YENYE KUANGAMIZA
  • Kitabu Cha Biblia Namba 26—Yeremia
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Yeremia Nabii wa Hukumu za Mungu Asiyependwa na Wengi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Kutumikia Katika “Siku za Mwisho”
    Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
  • “Siwezi Kunyamaza Kimya”
    Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 2/15 kur. 3-11

Njia ya Uzima au Njia ya Mauti​—Njia Gani?

“Nawe waambie watu hawa, [Yehova] asema hivi, Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.”​—Yer. 21:8.

1. Ni maulizo gani yanayotokea kwa habari ya kuelekeana kwetu sasa na uchaguzi kati ya “njia ya uzima na njia ya mauti”?

JE! KWELI KWELI limekuwa jambo zito namna hiyo? Je! sote tunaelekeana nalo? Je! ulimwengu wote sasa unakabiliwa na uchaguzi kati ya “njia ya uzima, na njia ya mauti”? Je! kweli hili laweza kuwa hivyo? Je! si kifo ndilo jambo la kawaida? Ikiwa ndivyo, sababu gani mambo ya wanadamu yanatofautiana na yalivyokuwa mbeleni? Kwa maelfu ya miaka yaliyopita wanaume, wanawake, watoto na vitoto hawakuepuka kifo. Hawakuwa na uchaguzi wa “njia ya uzima” au “njia ya mauti”? Tuna nafasi gani ya kuepuka adui wa muda mrefu MAUTI?

2, 3. (a) Kulingana na historia ya zamani, ni wakati gani ulimwengu mzima ulipoelekeana na kifo cha ghafula, kwa wakati mmoja, na wote pamoja? (b) Ni nini kilichowezesha wakati huo kuwepo uchaguzi kati ya kuishi na kufa?

2 Basi, huu siyo wakati wa kwanza ambapo ulimwengu mzima wa watu umeelekeana na kifo, kifo cha ghafula, wote pamoja. Wanahistoria wanataja wakati uliopita kwenye pindi moja ya mapema ya namna hii. Mwanahistoria mmoja asema hivi: “Zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu; kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.”​—2 Pet. 3:5, 6.

3 Mwanahistoria huyo, mtume Mkristo Petro, alikuwa akiandika juu ya gharika ya duniani pote ya siku za Nuhu. Je! njia ya uzima na njia ya mauti zilikuwa zimewekwa mbele ya ulimwengu wa wakati huo? Bila shaka, Ndiyo! Ilikuwa habari ya kwamba ama kwa kutosadiki mtu akae nje ya safina ambayo Nuhu na jamaa yake walikuwa wametengeza na hivyo asiishi kupita gharika ama mtu aingie ndani ya safina pamoja na Nuhu na jamaa yake na hivyo aepuke kifo cha jeuri pamoja na ulimwengu usiomcha Mungu.

4, 5. (a) Sababu gani sote tungali hai ijapokuwa gharika ya siku za Nuhu? (b) Sababu gani sisi leo hatupaswi tukose maana ya somo lililotolewa na Nuhu na jamaa yake?

4 Mapema katika barua iyo hiyo mtume Petro aliandika hivi: “Wala [Mungu] hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu.”​—2 Pet. 2:5.

5 Kwa sababu Nuhu na jamaa yake walichagua njia ya uzima kabla ya gharika kutokea, sisi twajipata hapa leo, zaidi ya miaka elfu nne na mia tatu baadaye. Somo linalotolewa na Nuhu na jamaa yake haipasi tukose kulifahamu leo. Sababu gani hivyo? Kwa sababu Maandiko Matakatifu yanatabiri mwisho wa namna hiyo kwa ulimwengu wa watu wasiomcha Mungu ambao umekua na kujaza dunia mpaka sasa.

6. Sababu gani sasa mkazo u juu yetu ili tuchague njia ya uzima” na kukataa “njia ya mauti”?

6 Kwa akili basi, uchaguzi kama ule ulioelekea Nuhu na jamaa yake lazima uwe unatuelekea wakati fulani kadiri ule mwisho uliotabiriwa ukaribiavyo. Kutokana na njia ambayo unabii wa Biblia umekuwa ukitimizwa tangu Vita ya Kwanza ya Ulimwengu, iliyoonyesha kwamba miaka 2,520 ya Nyakati za Mataifa ingemalizika katika mwaka 1914, wanafunzi wa Biblia wasiofungamana na madhehebu yo yote wamekuwa wakijua kwamba tunaishi katika wakati wa “mwisho wa taratibu ya mambo.” (Mt. 24:3, NW) Kufikia mwaka huu, 1980, tunajipata tukiwa tumeingia sana katika kipindi cha kumalizia cha hii taratibu ya mambo. Kwa hiyo, sasa, kupita wakati mwingine wo wote uliopata kuwako, mkazo upo juu yetu tuchague “njia ya uzima” na kuikataa “njia ya mauti.” Kwa rehema, uchaguzi huu umewekwa mbele yetu na Mpaji-Uzima wa wale wote wenye kupumua.

7, 8. Mfano wa hali kama iyo hiyo katika historia ulitolewa katika siku za mtu gani wa zamani? (b)Yehova alimtaka nabii huyo awe mtu mwenye kujulikana na watu wote kwa kadiri gani?

7 Licha ya gharika ya siku za Nuhu kunao mfano mwingine katika historia ya kibinadamu ambapo uchaguzi ulikuwa kati ya maisha yenye kuendelea na kumalizwa kwa ghafula kwa mapendeleo yote ya maisha. Hii ilikuwa kwa habari ya taifa la Israeli wakati wa siku za kuhani-nabii Yeremia, mwana wa Hilkia. (Yer. 1:1-5) Yehova Mungu alimfanya “nabii wa mataifa.” Kwa hiyo hata ingawa huenda tusiwe watu wa Yeremia mwenyewe, yale ambayo nabii huyu wa mataifa yote alisema na kufanya yanatuhusu sisi.

8 Mungu yule aliyemweka Yeremia kuwa mnenaji wake alimtaka awe mtu mwenye kujulikana na wote, mtu mwenye kuvuta fikira za wafalme, za wakuu, za makuhani, za raia, ndiyo, za mtawala, Nebukadreza mfalme wa Babeli. Vilevile Yeremia anavute fikira za ulimwengu leo kupitia kwa unabii wake ulioandikwa ambao umehifadhiwa ili sisi sote tuufikirie kwa wakati wenye kufaa katika hizi siku zenye hatari.​—Yer. 1:18, 19; 39:11-14; linganisha Warumi 15:4.

9. Kwa habari ya mabadiliko ya kisiasa duniani, wakati wa Yeremia ulifananaje na kipindi chetu tangu mwaka 1914?

9 Kizazi kinachozeeka kilichoyashuhudia matukio ya ulimwengu tangu mwaka 1914 W.K. kimeona mabadiliko mengi kati ya watawala wa mataifa. Vilevile Yeremia aliona mabadiliko ya kisiasa. Baada ya mfalme mwema Yosia kufa katika mwaka 628 K.W.K., Yeremia aliona wana watatu wa Yosia na mjukuu wake mmoja wakiketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa Yuda. Baada ya mwana wa Yosia, Yehoahazi kutawala kwa miezi mitatu tu huko Yerusalemu, aliondolewa, na ndugu yake Yehoyakimu akamrithi. Baada ya mwana huyu wa Yosia kufa kwa ghafula katika mwaka 618 K.W.K., mwana wake mchanga Yehoyakini alitawala kwa miezi mitatu na kisha alikubali kushindwa na Nebukadreza, mfalme wa Babeli. Ndipo Nebukadreza alipomfanya mwana aliyesalia wa Yosia, yaani, Sedekia, mfalme mpya wa Yuda. Katika mwaka wa 11 wa utawala mbaya wa Sedekia Yerusalemu ulianguka kwa Wababeli naye Sedekia akahamishwa mpaka Babeli, akiuacha Yerusalemu na hekalu lake zikiwa magofu.​—2 Nya. 35:23–36:21.

10. Ni nini kilichofanya ujumbe wa Yehova usiwe mgawo mwepesi kwa Yeremia kuutoa, naye ni mfano wenye kutia moyo kwa nani leo?

10 Yeremia aliona kuharibika kwenye kuendelea kwa adili na kwa kidini kati ya wafalme hao wa mwisho wanne wa Yuda. Je! tumeona kitu cho chote chenye kuhuzunisha namna iyo hiyo kikitukia kati ya watawala wa kisiasa wa mataifa yanayojidai kuwa ya Kikristo? Mgawo uliomtaka Yeremia adumu katika kutangaza kuhukumiwa maangamizi Yerusalemu na kupinduliwa kwa ufalme wa ukoo wa Daudi haukuwa mwepesi kwake. Leo haikuwa kazi rahisi kwa jamii ya Yeremia Kutangaza unabii wa Yehova unaotabiri uharibifu wenye kuleta msiba wa Jumuiya ya Wakristo pamoja na majengo yake yote ya makanisa, cathedrals na basilicas (namna ya majengo ya makanisa) ambayo sasa ni yenye kuvutia watalii. Hii inaifanya jamii ya Yeremia kutofautiana sana na viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo. Walakini Yeremia wa zamani amekuwa mfano wenye kuchochea sana wa huu mfano wake wa kisasa.

11. Kusudi alionyeshe kitamasha tangazo la Yeremia la kuhukumiwa maangamizi, Yehova alimwambia afanye na kusema nini?

11 Pindi moja, ili kufanya tangazo la Yeremia la kuhukumiwa maangamizi liwe tamasha Mungu alisema hivi:

“Enenda ukanunue gudulia [nyungu] la mfinyanzi, ukachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa watu, na baadhi ya wazee wa makuhani [wawe mashahidi]; ukatoke uende mpaka bonde la mwana wa Hinomu, lililo karibu na mahali pa kuingia kwa lango la vigae, ukahubiri huko maneno nitakayokuambia, ukisema, Lisikieni neno la [Yehova], enyi wafalme wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalieni, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, ambayo mtu ye yote akisikia habari yake, masikio yake yatawaka. Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia; nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu.”​—Yer. 19:l-5.

12. Baada ya Yeremia kuivunja nyungu vipande vipande, alisema nini juu ya Tofethi katika Bonde la Hinomu?

12 Ni “mabaya” gani ambayo ripoti yake itafanya masikio yawake? “Mahali” palipofanywa kuwa patakatifu kwa miungu wa uongo pangechafuliwa kwa waabudu hao wa sanamu ‘kuchinjiwa’ hapo. (Yer. 19:6) Kisha, baada ya Yeremia kutangaza haya, huku wazee wa watu na wazee wa kikuhani wakitazama, aliivunja-vunja juu ya ardhi nyungu hii akasema hivi:

“[Yehova] wa majeshi asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyowavunja watu hawa, na mji huu, kama mtu avunjavyo chombo cha mfinyanzi, kisichoweza kutengenezwa tena na kuwa kizima; nao watazika watu katika Tofethi hata hapatabaki mahali pa kuzikia.”​—Yer. 19:10, 11.

13. Baada ya hayo, Yeremia alitangaza nini kwenye ua wa hekalu la Yerusalemu?

13 Baada ya tendo hilo la kitamasha mbele ya wazee, ilifaa ujumbe wa namna iyo hiyo utangaziwe watu wa Yerusalemu. Kwa hiyo Yeremia aliacha vigae vya nyungu iliyovunjika karibu na Lango la Vigae akaenda kaskazini kupitia mjini kwenye ua wa hekalu. Kisha, wasikilizaji wote wakisikia, akasema hivi:

“[Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaleta juu ya mji huu na juu ya vijiji vyake [vilivyo kandokando ya mji] vyote, mabaya yote niliyoyanena juu yake; kwa sababu wamefanya shingo zao kuwa ngumu, kusudi wasiyasikie maneno yangu.”​—Yer. 19:14, 15.

MATESO YA KIDINI NA MATOKEO YAKE

14. Pashuri alimtendeaje Yeremia, na kwa sababu gani?

14 Wazee waliomwona Yeremia akivunja nyungu kwenye Bonde la Hinomu na ambao walisikia maneno yake ya kuhukumiwa maangamizi hawakujiona kuwa na mamlaka ya kumfanya jambo lo lote. Walakini mkuu wa hekalu, yaani, Pashuri mwana wa kuhani Imeri, alijiona kuwa mwenye mamlaka kuchukua hatua fulani. Uongo aliotabiri haukuungwa mkono na Yeremia. Kwa ghadhabu Pashuri alimpiga kofi usoni na kumweka katika mikatale ya watu wote katika Lango la Benyamini la hekalu, katika ukuta wa kaskazini. Lo! namna anavyolitukuza taifa! huenda watazamaji wengi wangefikiri hivyo kwa kuwa Pashuri alikuwa akiunga mkono Misri, akitegemea msaada wa kijeshi wa Misri ulizuie neno la Yehova kupitia kwa Yeremia lisilete msiba juu ya ufalme wa Yuda kupitia kwa Wababeli. Walakini kutukuza taifa kwa Pashuri hakukumletea sifa ya Yehova. Alikuwa akipigana na Mungu!

15. Yehova alibadili jina la Pashuri kuwa nini, nalo likiwa na maana gani ya kiunabii?

15 Siku iliyofuata, baada ya Pashuri kumwachilia Yeremia, Yehova alikuwa na ujumbe kwa Pashuri. Jina lake ni mwunganisho wa maneno mawili ya Kiebrania Pash na Hhur. Maneno haya yakiwa pamoja yanafahamika kuwa yanamaanisha “Yale Yaliyosalia Pande Zote.” Kwa hiyo, akitumia wazo la jina Pashuri, Yehova alimwongoza Yeremia kwa roho abadili jina hilo:

“[Yehova] hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu [Kiebrania, Hofu iko Pande Zote]. Maana [Yehova] asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki [wapenzi] zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga. Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli. Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe na rafiki, zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo.”​—Yer. 20:3-6.

16. Pashuri alikuwa akiongoza wengine katika njia gani, na ni nini linalofanana na jambo hilo leo?

16 Kutokana na maneno haya ya Yehova ni wazi kwamba Pashuri alikuwa amejichagulia “njia ya mauti.” Vilevile, kupitia kwa matabiri yake ya uongo, alikuwa akiongoza rafiki au wapenzi wake wa kidini kwenye njia iyo hiyo. Kwa kufanana, katika Jumuiya ya Wakristo mamia ya mamilioni ya waenda-kanisani wanaongozwa kwenye hiyo “njia ya mauti.” Hata hivyo, jamii ya Yeremia haiwezi kulaumiwa kwa ajili ya hilo.

17. Tamasha iliyoonyeshwa kule Cedar Point, Ohio, katika mwaka 1919, iliizidije ile ya Yeremia ya kuvunja nyungu kwenye Bonde la Hinomu?

17 Kwa njia ya tamasha Yeremia alionyesha kwa mfano unabii wa Yehova kwa kuivunja ile nyungu kwenye Bonde la Hinomu. Kwa maonyesho ya waziwazi yaliyo makubwa zaidi sana ya hayo, jamii ya Yeremia imeiarifu Jumuiya ya Wakristo juu ya maangamizi yake yanayokaribia. Chukua, kwa mfano, kusanyiko lile katika Cedar Point, Ohio, katika Septemba wa mwaka 1919. Pale, mbele ya wasikilizaji 10,000 msimamizi wa Sosaiti alitoa hotuba ambayo katika hiyo alitaja kwamba baraka za viongozi wa kidini juu ya Ushirika wa Mataifa uliokuwa ukikusudiwa kusimamishwa zingekuwa kazi bure. Tengenezo hilo la mataifa yote kwa ajili ya amani na usalama wa ulimwengu lisingefanikiwa. Bila shaka liliiaibisha Jumuiya ya Wakristo katika mwaka 1939, wakati mtawala mmoja mwenye mamlaka peke yake Adolf Hitler alipoitumbukiza Jumuiya ya Wakristo kwenye Vita ya Pili ya Ulimwengu.

18. Tamasha nyingine ilifanywaje na jamii ya Yeremia katika mwaka 1933?

18 Kama mfano mwingine, chukua mwaka 1933. Mwaka huu ulitangazwa kuwa Mwaka Mtakatifu kwa sababu ulikuwa mwaka wa 1900 wa kifo cha dhabihu cha Yesu Kristo. Katika tangazo la papa la sherehe hii, faida ziliahidiwa kwa habari ya amani na fanaka ya Jumuiya ya Wakristo sana sana na vilevile ya ulimwengu wote, ajapokuwapo Hitler mtawala mwenye mamlaka peke yake wa Jamuhuri ya Ujeremani. Walakini kwa ujasiri jamii ya Yeremia ilizipinga ahadi hizo za kipapa. Jumapili, Aprili 23, kwa njia ya kuunganisha vituo vya radio pamoja na kituo cha radio cha WBBR cha mji wa New York kikiwa kituo kikuu cha kutangazia, msimamizi wa Sosaiti alitoa hotuba ya saa moja juu ya “Matokeo ya Mwaka Mtakatifu juu ya Amani na Fanaka.” Mwenezo wa ulimwenguni pote ulitolewa kwa ujumbe huu wenye kuwasha masikio kwa kuchapisha katika toleo la Mei 10, 1933, la gazeti lenye kutoka baada ya kila juma mbili liitwalo The Golden Age. Mara moja viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo waliinua juu vilio vya kupinga, na kutumia mikazo ya kisiasa na kuwatesa walio wa jamii ya Yeremia. Walakini hili halikuhifadhi amani na fanaka ya ulimwengu kama vile ilivyoshindwa Miaka Mitakatifu iliyofuata ya 1950 na 1975. Jumuiya ya Wakristo ingali inaelekeana na uharibifu katika “dhiki kubwa” inayokuja.

19. Kubadilishwa kwa jina la Pashuri na unabii wa kuhukumiwa maangamizi uliofuatana nako vilipataje kuwa na mfano wavyo katika viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo leo?

19 Hivyo kofi la usoni ambalo mkuu wa hekalu Pashuri alimpiga Yeremia limepata kuwa na mfano wa kisasa katika karne hii ya 20. Kama vile kiongozi huyo wa kidini mwenye kutukuza taifa wa zamani, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo wameitia jamii ya Yeremia kwenye mikatale. Sababu gani? Kusudi wawaaibishe mbele ya watu wote na wazuie kuhubiriwa kwa kusudi la Yehova juu ya Ukristo ya jina, tena wa kinafiki, ndiyo juu ya dini yote ya uongo na walinzi na vidalali (watu wenye kuunga mkono kwa uaminifu) wake wa kisiasa. Mwenendo wa namna hiyo haukuwa na matokeo mazuri juu ya Pashuri wa zamani au juu ya viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo. Yehova alibadili jina la Pashuri kuwa Magori-misabibu, linalomaanisha ‘Hofu Iko Pande Zote.’ “Hofu” hiyo ingehusiana na uharibifu wenye kuogopesha katika mwaka 607 K.W.K. Vilevile, Pashuri alikuwa amehukumiwa maangamizi afie Babeli akiwa mtumwa. Kwa habari ya waigaji wa leo wa Pashuri, jamii hii ya viongozi wa kidini ilifunuliwa na kuhukumiwa maangamizi ya uharibifu wa milele.

20. Katika mwaka 1951, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo walifunuliwaje kuwa jamii iliyohukumiwa maangamizi?

20 Tangu kame ya kwanza kufahamu kile ambacho mtume Paulo aliita “mwana wa kupotea milele” au “mwana wa uharibifu” kulikuwa kumewatatiza Wakristo. Walakini kwa wakati wake Yehova hii “siri ya uovu” au “siri ya kuasi” ilikuwa imepangwa ifunuliwe. (2 The. 2:3, 7, Authorized Version; UV) Kwa hiyo, katika mwaka 1951, jamii ya Yeremia ilichapa kitabu kiitwacho What Has Religion Done for Mankind? (Dini Imefanyia Wanadamu Nini?) Katika mwaka huo kitabu hicho kilitolewa kwenye kusanyiko la mataifa yote la Mashahidi wa Yehova katika London, Uingereza. Sura yacho ya 25 ilieleza juu ya “Dini Nyekundu na ‘Mtu wa Kuasi.’ ” Katika kurasa za 320 na 321 twasoma juu ya “ukengeufu” au “kuasi imani” hivi:

Kwa hiyo kukengeuka kwa viongozi wa Kikristo kutoka kwa Ukristo wa kweli ili kufanyiza jamii au taratibu ya “mtu wa kuasi” kulianza muda mfupi baada ya mitume kumi na wawili kufa. Kwa jinsi hiyo mitume wakiwa hawazuii, jamii ya mtu wa kuasi ilijitokeza waziwazi na ikafuata mwenendo wa mwendo wake wa kujikweza, tena wa kuasi. Ilijikweza kama viongozi wa kidini wenye kuasi wenye uweza juu ya faida za kidini za Wakristo wa kujidai. Neno la viongozi wa kidini lilikuwa lenye nguvu zaidi ya Neno la Mungu lililoandikwa. Viongozi wa kidini waliweka mapokeo na amri za wanadamu juu ya sheria za Mungu na kuzifanya kuwa bure. Wakijitanguliza kwa vyeo vya “Reverend,” “Right Reverend,” “Most Reverend,” “Divine” (Mungu), na hata “vice-god” (mungu-mdogo) kwa upande wa papa, walijikweza wenyewe katika mahekalu, cathedrals na katika majengo yao ya kanisa wakawa vitu vya kuheshimiwa wakitwaa heshima na hofu anayostahili Yehova Mungu na Mwanawe Yesu Kristo. Walidai kuwa ni wana wa Mungu, walakini walijifanya kuwa miungu au watu wenye nguvu kiroho kwa wakaaji wa mitaa yao na kondoo zao.

21. Wakati “mwana wa uharibifu” wa Jumuiya ya Wakristo atakapotoweka, ni nini kitakachotoweka pamoja naye, katikati ya hali gani kwa Wakristo wa jina wa kujidai?

21 Kitabu hicho kilichotajwa hapo juu kilionyesha waziwazi kwamba “mtu wa kuasi” mwenye kukengeuka atapatwa na uharibifu uliotabiriwa katika “dhiki kubwa” inayokaribia, pamoja na dini nyingine zote za uongo za Kibabeli. Wakati “mtu wa kuasi,” “mwana wa uharibifu,” wa Jumuiya ya Wakristo atakapotoweka, vilevile nayo Jumuiya ya Wakristo yenyewe itatoweka. Kwa ajili ya tukio hilo lenye kushtua watu wenye kuchukua dini kwa wepesi, kutakuwako ‘hofu kila upande’ kwa Wakristo wa jina wenye kujidai, vilevile na kwa wengine wote wenye kutangaza dini zisizo za kibiblia, tena zisizo za kimaandiko.—2 The. 2:8-12; tazama pia kitabu “Babylon the Great Has Fallen!”​—God’s Kingdom Rules!, kilichochapwa katika mwaka 1963, sura 26, inayoeleza Ufunuo, sura ya 17.

KUKIMBILIA KWENYE UPANDE WA MAJESHI YA MUNGU YENYE KUANGAMIZA

22. Twaweza kuepukaje kuharibiwa pamoja na “mwana wa uharibifu” wa Jumuiya ya Wakristo, kama Inavyoonyeshwa kwa mfano katika wakati wa Yeremia?

22 Mwendo wa Jumuiya ya Wakristo ni mwendo wa “njia ya mauti.” Tusiendelee kuenenda zaidi katika hiyo. Wakati ungali unaruhusu mtu aepuke kuangamizwa pamoja na “mwana wa uharibifu” wake. Mtazame Yeremia kama kielelezo. Ijapokuwa alikuwa amefungwa katika Ua wa Mlinzi wa Mfalme Sedekia huku njaa, tauni na vita vikifisha watu kumzunguka, aliokoka uharibifu wa Yerusalemu na hakuhamishwa kupelekwa Babeli. Wachaji wa Yehova ambao walifanya urafiki na Yeremia waliokoka pamoja naye. Sisi leo vilevile tunayo nafasi ya kuokoka.

23. Sababu gani wakati huo hakukuwa na msingi wa ujumbe wenye kibali kutoka kwa Yehova kupitia kwa Yeremia kwa Mfalme Sedekia?

23 Kule nyuma katika mwaka 609 K.W.K., Watekaji Wababeli walikuwa wakijibidiisha kufika Yerusalemu. (Yer. 21:13) Akifahamu kilichokuwa kikikaribia, Mfalme Sedekia alituma watu wawili wenye kuomba habari kwa Yeremia ili kwamba, ikiwezekana, apate ujumbe wenye kibali ya Yehova. Walakini kulikuwa sababu gani ya Sedekia kutazamia neno lo lote lenye kibali kupitia kwa Yeremia? Katika Yerusalemu na kote kote katika ufalme wa Yuda kulikuwa kumeenea mambo haya ambayo Yehova alivuta fikira kwayo: kuvunja kwa agano Lake na Israeli, kuabudu miungu wengine, kuhukumiwa mahakmani isivyo haki, wapunjaji (wadanganyaji) wenye kunyang’anya watu wasiojiweza, kuwatumia vibaya wajane na watoto yatima ili kujifaidi, kuwanyima wafanya kazi ngumu malipo yao ya haki, kumwaga damu isiyo na hatia, kutabiri uongo. (Yer. 21:12; 22:3, 3-16; 23:14, 16) Ilimlazimu Yeremia kujipa ujasiri na kutangaza kwa ujasiri ujumbe wa Yehova usiobadilika wa msiba kwa wavunjaji wa agano la Mungu.​—Yer. 21:1-7; 1:7, 8, 17.

24. Yeremia ni mfano mzuri namna gani kwa habari ya kutangaza ujumbe wa Yehova kwa Jumuiya ya Wakristo leo?

24 Lo! namna Yeremia alivyowekea Mashahidi wa Yehova wa leo mfano mzuri! Katika Jumuiya yote ya Wakristo leo hali ni mbaya kidini, kiadili, kijamii, kisheria, pasipo tumaini la faraja. Kama vile kwa habari ya Yeremia, leo Yehova hajapunguza ukali wa maneno katika kuusema uamuzi wake wa kisheria juu ya Jumuiya ya Wakristo. Ameipa jamii ya Yeremia mgawo wa kutangaza ujumbe kama ule wa moja kwa moja wa msiba kwa mfano wa kisasa wa Yerusalemu na Yuda wa kale. Bila kuacha jambo lo lote, tena bila kusita, jamii ya Yeremia yapaswa kushikamana na yote yale Anayowaamuru katika Neno Lake.

25. Mataifa ya ulimwengu yanapiga hatua kwenye nini, nacho kitabu Deliverance! cha mwaka 1926 kilielezaje jambo linalotukia hapo?

25 Mataifa yote, kutia na yale ya Jumuiya ya Wakristo, wanapiga hatua kuelekea Har–Magedoni. Jina hilo halimaanishi tu vita vya kifahari kati ya matajiri na wafanya kazi wenye kuajiriwa, vyenye kutokeza kutokuwa na serikali ulimwenguni pote. Si vita kati ya mwanadamu na mwanadamu, bali ni jambo lenye uzito mwingi zaidi na msiba mwingi zaidi. Kule nyuma katika mwaka 1926 jambo hili la hakika lilianza kufanywa kuwa wazi. Kilisema hivi kitabu Deliverance! (Ukombozi!), kilichotolewa kwa watu wote kwenye kusanyiko kuu la International Bible Students Association kule London, Uingereza, katika Mei wa mwaka 1926:

Watakatifu hawashiriki katika vita vyenyewe hasa. Hivi ni vita vya Mungu Mwenyezi; na vita vyenyewe vinaongozwa na Mwanawe mpendwa, Kuhani ambaye Melkizedeki alikuwa wa namna yake. Zamani sana nabii wa Yehova aliandika kuhusu kipindi hiki:“Bwana [Yehova] yu mkono wako wa kuume; Ataseta wafalme, Siku ya ghadhabu yake. Atahukumu kati ya mataifa, Ataijaza nchi mizoga; Ataseta kichwa katika nchi nyingi.” (Zaburi 110:5, 6) Vilevile yeye anapigana kwa ajili ya wokovu wa watu hao, kusudi wapate kuokolewa kutokana na mwonezi; naye anapigana kwa ajili ya watiwa mafuta wa Mungu, kusudi wapate kutukuzwa kwa ajili ya ushuhuda wao wa uaminifu wa jina la Yehova. . . .

Ndivyo utawala wa Shetani unavyofutiliwa mbali kutoka duniani na kusahuliwa kabisa. Jina la Yehova Mungu linatukuzwa. Walakini maneno yote ya kibinadamu yenye kujaribu kueleza siku kuu na yenye kutisha ya Bwana hayatoshi hata kidogo.​—Ukurasa 280, chapa ya kwanza.

Mtu ye yote na asijidanganye na kufikiri kwamba vita ya Har–Magedoni ni vita tu kati ya wanadamu, au ni picha tu. Maandiko yanaonyesha wazi kwamba ni vita halisi. Ni vita vya Mungu Mwenyezi, ambavyo katika hivyo ataondoa duniani taratibu mbovu ambayo Shetani ametumia kupofusha watu kwa karne hizi zote.​—Ukurasa 282, 283; tazama pia ukurasa 261, fungu 2.

26. Kama vile Yeremia, jamii ya Yeremia haipaswi kufanya nini kusudi tu ipendeze watawala wa ulimwengu?

26 “Vita ya Har–Magedoni” italeta mwisho wa “dhiki iliyo kuu” ambayo katika hiyo milki ya ulimwengu ya dini ya uongo, kutia na Jumuiya ya Wakristo, itafutiliwa mbali. (Ufu. 16:13-16; 17:1-18) Jamii ya Yeremia haiwezi kupunguza uhakika wa jambo hili la hakika ili tu ipendeze watawala wa kisiasa wa namna ya Sedekia wa Jumuiya ya Wakristo au hata wale wa ulimwengu mzima. Wanapaswa ‘kushikamana na agizo lao,’ kama vile alivyofanya Yeremia kwa Mfalme Sedekia katika kutii mgawo wake kutoka kwa Yehova.

27. Ni majeshi gani ya kuangamiza ambayo watu wataelekeana nayo katika vita vitakavyopiganwa katika Har–Magedoni?

27 Katika “vita ya siku ile kuu” katika Har–Magedoni, watawala wa taratibu hii ya mambo watalazimika kupambana na Mungu Mwenyezi, si wanadamu wenzao tu. Kwa habari ya watu wenye kutukuza taifa wanaounga mkono uongozi wa kisiasa wa taratibu hii ya mambo, watakabiliana na majeshi ya kuangamiza chini ya amri ya Yehova. Katika siku za Yeremia majeshi yenye kuleta maangamizi yalikuwa majeshi ya Babeli chini ya Mfalme Nebukadreza. Katika vita inayokuja kwenye Har–Magedoni watakuwa malaika watakatifu wa Yehova wakiongozwa na Mwanawe Yesu Kristo.​—Ufu. 16:12; 19:11-21.

28, 29. Sisi watu wa kawaida twapaswa kufanya uchaguzi gani, hivyo tutii maneno ya Yehova katika Yeremia 21:8-10?

28 Watawala wa Jumuiya ya Wakristo wamemwiga Mfalme Sedekia wa Yerusalemu na wamekataa kugeuka wapatanishwe na Mungu. Kwa hiyo twapaswa kufanya nini sisi watu wa kawaida tunaoelekeana na uharibifu wa ulimwengu unaokaribia sana? (Yer. 21:11, 12; 22:3-5) Twapaswa kuchukua hatua ya kibinafsi. Twapaswa kufanya uchaguzi wa kibinafsi wa “njia ya uzima.” Kila mmoja wetu apaswa kutii maneno ya Mungu kupitia kwa Yeremia:

29 “Nawe waambie watu hawa, [Yehova] asema hivi, Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti. Yeye atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atakayetoka, na kujitia pamoja na Wakaldayo wanaowahusuru, yeye ataishi, na maisha yake yatakuwa nyara kwake. Maana nimeweka uso wangu juu ya mji huu niuletee mabaya, wala nisiuletee mema, asema [Yehova]; utatiwa katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza.”​—Yer. 21:8-10.

30. Sababu gani Myahudi ‘aliyejiweka upende wa Wakaldayo’ hakuwa akikosa kutukuza taifa au kuwa msaliti?

30 Myahudi ‘anayejiweka upande wa Wakaldayo’ waliokuwa wakiuzingira ufalme wa Yuda hangekuwa akikosa kutukuza taifa au kuwa msaliti. Ndio uliokuwa mwendo wa kumtii Yehova Mungu, mfalme asiyeonekana wa kimbinguni wa Israeli. Hii ndiyo iliyokuwa “njia ya uzima,” hali “njia ya mauti” ilikuwa mwendo wa kutokutii uliochaguliwa na watukuzaji wa taifa wa Kiyahudi.

31. Jambo hilo lilifanana na lile la nani katika karne ya kwanza W.K.?

31 Hali hii ilikuwa sawa na ile ya Wayahudi waliofanywa kuwa Wakristo wa karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu. Yesu Kristo alitabiri kuharibiwa kwa mji uliojengwa upya wa Yerusalemu na majeshi ya Warumi, ambao aliwataja kama “chukizo la uharibifu.”​—Mt. 24:15.

32. Kwa hiyo, ni maagizo gani ambayo Yesu aliwapa wafuasi wake waliojiweka wakf?

32 Hivyo, Yesu aliwaagiza wafuasi waliojiweka wakf hivi: “Ndipo ule mwisho utakapokuja. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu) ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. . . . Kwa kuwa wakati huo kutakuwa dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo, kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; walakini kwa ajili ya wateule zitafujizwa siku hizo.”​—Mt. 24:14-22.

33. Katika kipindi kilichokuwa katikati ya mwaka 66 na mwaka 70 W.K., kutii au kutokutii agizo la Yesu kulitokeza nini?

33 Wayahudi waliofanywa kuwa Wakristo wenye kuamini walitii agizo hili kutoka kwa Bwana wao. Majeshi ya Rumi yaliporudi nyuma baada ya shambulio lao lisilofaulu juu ya Yerusalemu na hekalu lake katika mwaka 66 W.K., Wakristo waliokuwa hatarini walitoroka wakatoka jimbo lote la Yudea. Hawakuliacha kusudi la Kiyahudi. Walikuwa watiifu kwa Kiongozi wao Yesu Kristo, na kwa hiyo mwendo waliochagua ulikuwa “njia ya uzima.” Wayahudi wenye kutukuza taifa walichagua “njia ya mauti” nao kaangamia hesabu ipatayo 1,100,000 kati majeshi ya Kirumi chini ya Jemadari Tito yalipouharibu Yerusalemu katika mwaka 70 W.K.

34. Wanaopenda uzima katika taratibu mpya wanapaswa kukimbilia wapi bila kuchelewa?

34 Tukiwa na mifano ya kihistoria namna hiyo mbele yetu, sisi watu tutafanya nini leo? Tunaishi katika kile ambacho wanafunzi wa Yesu walikiita “mwisho wa taratibu hii mbovu ya mambo.” “Dhiki kubwa” juu ya ulimwengu isiyo na kifani iliyofananishwa kimbele na uharibifu wa Yerusalemu sasa inaelekeana na “kizazi hiki.” Sasa ni jambo la kuchagua “njia ya uzima” au “njia ya mauti.” Jamii ya Yeremia imechagua “njia ya uzima.” Jamii hii inaonyesha kwamba wengine waweza kufanya vivyo hivyo. Pasipo kukawia wote wapenda uzima wa milele katika taratibu mpya yenye haki watatumia kwa kufaa nafasi iliyotolewa na Mungu kusudi wachague “njia ya uzima.” Watakimbilia kwenye upande wa majeshi ya Yehova yenye kuangamiza.​—Mt. 24:3, 34, NW.

[Picha katika ukurasa wa 8]

WBBR, Staten Island, N.Y.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki