Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 3/15 kur. 5-12
  • “Funguo” za Serikali Kuu Zaidi Zatumiwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Funguo” za Serikali Kuu Zaidi Zatumiwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • WAKATI ZILIPOTOLEWA NA KUTUMIWA
  • UFUNGUO WA PILI ULITUMIWA KWA AJILI YA NANI
  • “Funguo za Ufalme” Ni Nini?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Kutangaza “Habari Njema Kumhusu Yesu”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Amfundisha Mwanamke Msamaria
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Mungu Si Mwenye Upendeleo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 3/15 kur. 5-12

“Funguo” za Serikali Kuu Zaidi Zatumiwa

“Mimi nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbingu, na lo lote ulifungalo duniani litakuwa jambo ambalo limekwisha kufungwa katika mbingu, na lo lote ulifungualo duniani litakuwa jambo ambalo limekwisha kufunguliwa katika mbingu”​—Mt. 16:19, NW.

1, 2. (a) Katika hadithi ya kale ya Kirumi, ni nani aliyekuwa bawabu mkuu zaidi mbinguni? (b) Kwa habari ya kuwa mtu aliyeishi kweli kweli, ni jambo gani linaloweza kusemwa juu ya Yesu akiwa mwenyeji wa ufunguo fulani?

JE! KUNAYE bawabu au mngojea mlango juu mbinguni? Katika hadithi ya kale ya Kirumi ya Yano, mungu wa miungu, ndiye aliyekuwa bawabu mkuu zaidi mbinguni na duniani. Hekalu la Yano lingali lasimama upande wa kaskazini mwa Baraza ya Rumi, karibu na Kuria, walakini yeye haabudiwi tena. Walakini namna gani juu ya mtu aliyeishi kweli kweli, Yesu Kristo, ambaye sasa ametukuzwa mbinguni kwenye mkono wa kuume wa “Mungu wa miungu” wa kweli, Yehova? (Kum. 10:17) Wapata mwaka 96 W.K., alipokuwa akiandikisha barua itumiwe kundi katika Filadelfia katika Asia Ndogo Yesu huyu aliyetukuzwa alimwambia mtume Yohana hivi:

2 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.”​—Ufu. 3:7, 8.

3. (a) Yesu Kristo alikuwa na uhusiano gani na Daudi? (b) Sababu gani Yehova alimpa Yesu Kristo “ufunguo wa Daudi,” naye anautumiaje?

3 Kwa kuhesabu kutoka Daudi, mfalme wa kwanza wa Kiyahudi wa Yerusalemu, Yesu Kristo ndiye wa 43 katika nasaba ya kifalme ya wazao wa mfalme huyo mwenye kujulikana sana. Nasaba hiyo ya kifalme inamalizikia katika Yesu Kristo, kwa sababu alipata kuwa mrithi wa kudumu wa ufalme wa Daudi. (Luka 3:23-31) Kwa sababu hiyo Yehova Mungu alimpa Mwanawe aliyetukuzwa “ufunguo wa Daudi.” Ufalme wa Daudi ulikuwa theokrasi ya mfano, ufalme wa Mungu wa mfano. (1 Nya. 29:23; 2 Nya. 13:5, 8) Mikononi mwa mzao aliyetukuzwa wa Daudi, Yesu Kristo, ufalme huu unakuwa ufalme wa Mungu uliofananishwa, ulio wa kweli. Akiwa mwenyeji mwenye haki wa “ufunguo wa Daudi,” yeye hufungua au kufunga mapendeleo na nafasi kwa watu duniani kuhusiana na ufalme wa Mungu.

4, 5. Karibu na Kaisaria Filipi, ni mapendeleo gani ambayo Yesu Kristo alisema angempa Petro aliyekuwa mwaminifu?

4 Akiwa anatazamia sana kumfungulia mtume wake mwaminifu Simoni Petro mapendeleo ya utumishi, Yesu alimwambia hivi katika pindi moja; “Wewe ndiwe Petro [Kigiriki: Petros; Latin, Petrus], na juu ya mwamba huu [Kigiriki: tautei tei petrai; Latin: hanc petram] nitajenga kundi langu, nayo milango ya Hadeze haitalishinda. Mimi nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbingu, na lo lote ulifungalo duniani litakuwa jambo ambalo limekwisha kufungwa katika mbingu, na lo lote ulifungualo duniani litakuwa jambo ambalo limekwisha kufunguliwa katika mbingu.”​—Mt. 16:18, 19, NW.

5 Yesu aliyasema maneno hayo ya kweli wakati fulani baada ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 32 W.K., katika ujirani wa Kaisaria Filipi, karibu na chemchemi ya Mto Yordani.​—Mt. 16:13-17.

WAKATI ZILIPOTOLEWA NA KUTUMIWA

6. Hizo “funguo za ufalme wa mbingu” zilikuwa za namna gani, nazo zilifananisha nini?

6 Kama vile “ufunguo wa Daudi,” “funguo za ufalme wa mbingu” hazikuwa halisi, funguo zilizofanyizwa kwa vitu vya kidunia. Zilikuwa funguo za kiroho, yaani, pendeleo, heshima, mgawo na mamlaka ya kuanzisha au kufungua programu ya maarifa, maagizo na kujitia kwa mtu binafsi kwa habari ya ufalme wa mbinguni. Kupitia kwa jambo hili, watu wale waliochagua kutafuta kwanza ufalme wa mbinguni wangeweza kutumia ifaavyo mpango aliotokeza Mungu kupitia kwa Yesu Kristo, Mrithi wa huo ufalme wa kimbinguni. Hivyo waliingia katika kitu kisichofunguliwa kwao hapo mbeleni.

7. Mapema, katika Yerusalemu, Yesu alikuwa amemfunulia Nikodemo masharti gani ya msingi kwa mtu yo yote kuingia kwenye ufalme wa kimbinguni wa Mungu?

7 Miaka miwili mapema, huko Yerusalemu, Yesu alikuwa amemfunulia mtawala wa Wayahudi, Farisayo aliyeitwa Nikodemo, masharti fulani ya msingi ambayo mwamini alipaswa kutimiza ili apate kuingia kwenye ufalme wa kimbinguni wa Mungu. Yesu alisema hivi: “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.” Ati nini, ‘kuzaliwa tena’ na mama yule yule wake wa kibinadamu? Sivyo, walakini Yesu alimwambia Nikodemo: “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa roho, hawezi kuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa roho ni roho.”‏​—Yohana 3:1-6.

8. Je! lingekuwa jambo la akili kwa mtu ye yote ambaye bado hajabatizwa na kuwa Mkristo aliyezaliwa kwa roho kuwa mwenyeji na kutumia “funguo” hizo, nasi tuna mfano gani kwa habari hii?

8 Kwa hiyo, je! mtu ambaye alikuwa bado ‘kuzaliwa kwa maji na kwa roho’, ambaye si Mkristo aliyezaliwa kwa roho na kubatizwa, angeweza kupokea na kutumia “funguo” hizo ili afungulie wengine njia kwenye ufalme wa Mungu wa kimbinguni? Hili lisingekuwa jambo la akili hata kidogo. Kwa hiyo “funguo za ufalme wa mbinguni” hazikupewa Yohana, hata ijapokuwa alimbatiza Yesu na ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhubiri: “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.”​—Mt. 3:1, 2.

9. Twajuaje kama Petro alikuwa amezaliwa kwa roho alipopewa wa kwanza wa hizo “funguo,” na namna gani juu ya mwogofu Mwethiopia aliyetahiriwa anayetajwa katika Matendo 8:27, 28?

9 Hivyo, basi, je! mtume Petro alikuwa amezaliwa kwa roho wakati Yesu alipompa ufunguo wa kwanza wa zile “funguo” apate kuutumia? Ndiyo, kwa kuwa, katika siku ya Pentekoste ya mwaka 33 W.K., Yehova Mungu alimtumia Yesu aliyetukuzwa abatize kwa roho takatifu wanafunzi wapatao 120, kutia ndani Petro ambao walikuwa wakingoja katika chumba cha orofani katika Yerusalemu. Kwanza baada ya Petro kuzaliwa kwa roho ya Mungu, alisimama azungumze na zaidi ya Wayahudi 3,000 na waamini waliotahiriwa ambao walikusanyika kushuhudia namna unabii wa Yoeli 2:28, 29 ulivyokuwa umeanza kutimizwa. Ikiwa mwamini aliyetahiriwa Mwethiopia anayetajwa katika Matendo 8:27, 28 alikuwa kati ya “watu watauwa” ambao wakati huo walikuwa wakikaa Yerusalemu wakati wa siku hiyo ya Pentekoste, hakutoka hekaluni kuja kumsikiliza Petro. (Matendo 2:1-12) Walakini alipata nafasi yake baadaye.

10. Petro alitumia wa kwanza za zile “funguo” wakati gani na jinsi gani?

10 Papo kwa hapo Petro aliwaambia hao maelfu ya waadhimishaji kwamba walikuwa wamefanya uhalifu kama jamii ya kidini kwa kumtundika Yesu Kristo siku 52 zilizotangulia. Kisha hao “watu watauwa” waliochomwa dhamiri wakauliza: “Tutendeje, ndugu zetu?” Petro ndiye aliyejibu: “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha [roho takatifu]. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na [Yehova] Mungu wetu wamjie.” Petro aliendelea kusema. “Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.” (Matendo 2:14-40) Hivyo Petro aliyezaliwa kwa roho alitumia wa kwanza wa zile “funguo.”

11. Maelfu waliokuwa wakimsikiliza Petro ‘walizaliwa tena’ au ‘kuzaliwa kwa maji na kwa roho’ namna gani?

11 Je! wo wote wa Waisraeli hao wa asili waliingia kupitia mlango uliofunguliwa sasa wakiwa Wayahudi ambao Yehova Mungu alikuwa amewapa babu zao ahadi ya Yoeli 2:28, 29? Matendo 2:41, 42 lajibu hivi: “Nao waliolipokea neno lake [neno la Petro] wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.” Kupitia kwa kubatizwa kwao katika maji katika jina la Yesu Kristo na baadaye kupata kipawa cha bure cha roho takatifu, ‘walizaliwa tena,’ ‘wakazaliwa kwa maji na roho.’​—Yohana 3:3, 5.

UFUNGUO WA PILI ULITUMIWA KWA AJILI YA NANI

12, 13. (a) Ikiwa Petro alihitaji kutumia ufunguo mmoja tu, hii ingemaanisha nini? (b) Hata hivyo, Yesu alisema nini juu ya hili kwa wanafunzi wake kabla tu ya kupaa kwake mbinguni?

12 Petro alikuwa ameahidiwa, si ufunguo mmoja, bali “funguo za ufalme wa mbingu.” Hii ilimaanisha angaa funguo mbili. Kwa hiyo ni wakati gani alipopewa ufunguo wa pili, na kwa ajili ya nani? Iwapo Petro alihitaji ufunguo mmoja tu, basi ni Wayahudi wa asili na waamini waliotahiriwa wa Kiyahudi peke yao ndio wangekuwa wale washirika 144,000 ambao Yesu Kristo anawajenga juu yake akiwa mwamba wawe kundi lake kamili lililozaliwa kwa roho. (Mt. 16:18; Ufu. 7:4-8; 14:1-3) Walakini je! wokovu wa kimbinguni ungekuwa kwa wale tu waliofunguliwa nafasi kwa ufunguo kutumiwa na Petro katika siku ya Pentekoste? Basi, Yesu alisema nini muda mfupi kabla hajapaa mbinguni katika siku ya 40 tangu kufufuliwa kwake? Katika siku hiyo, katika ujirani wa Yerusalemu, yeye aliwaambia wanafunzi wake hivi:

13 “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya. Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu [katika Yoeli 2:28, 29]; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”​—Luka 24:46-49.

14, 15. Kulingana na Matendo 1:8, Yesu alionyesha tofauti namna gani kwa habari ya kupanua kuhubiriwa kwa toba kwa “mataifa yote”?

14 Hata hivyo, kulingana na Matendo 1:8, Yesu alionyesha kwa urefu zaidi juu ya namna kuhubiriwa kwa toba juu ya msingi wa jina lake kungepanuliwa hatua kwa hatua kwa “mataifa yote.” Hapo alisema hivi: “Lakini mtapokea nguvu, [i]kiisha kuwajilia juu yenu [roho takatifu]; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho na nchi.”

15 Hapa Yesu alitenganisha Samaria na “Uyahudi wote.” Kwa sababu hiyo, wakati wote katika huduma yake ya kidunia alitofautisha kati ya Wayahudi wa asili waliotahiriwa na Wasamaria waliotahiriwa.

16. Ikawaje kwamba alipokuwa akirudi Galilaya Yesu alikaa siku mbili na wakaaji wa mji wa Samaria wa Sikari?

16 Baada ya sikukuu ya Kupitwa mwaka 30 W.K., wakati wa mwaka kwanza wa utendaji wake wa waziwazi, ilimpasa kupitia Samaria alipokuwa akitoka Yudea kwenda Galilaya. Kwa habari hiyo ilionekana kwamba ‘Wayahudi hawakuchangamana na Wasamaria.’ (Yohana 4:9) Hata hivyo, kwenye kisima cha Yakobo karibu na mji wa Sikari, Yesu aliamua kuzungumza na mwanamke Msamaria. Kwa kweli, alipata kuwa, mtu kwanza ambaye Yesu aliungamia kuwa ndiye Masihi au Kristo. Je! hii ilikuwa kwa sababu hakuwa Myahudi? (Mt. 16:20) Isitoshe, alipoalikwa na wakaaji Wasamaria wa Sikari, yeye na mitume wake walikaa na Wasamaria hao kwa siku mbili na kuzungumza nao. Hesabu fulani yao iliamini na kumwambia hivi mwanamke huyo Msamaria ambaye alikuwa amewatolea ushuhuda: “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.”​—Yohana 4:39-43.

17. Yesu alichukua msimamo gani kuelekea Wasamaria hao wenye kuamini na kuhusu ubatizo wa maji?

17 Hata baada ya hili, bado, Yesu aliendelea kutofautisha kati ya Wayahudi na Wasamaria, ijapokuwa Wasamaria wengine walimsadiki. Je! alitoa mwito kwa wo wote wa Wasamaria hao wenye kuamini wabatizwe katika maji kwa ubatizo wa Yohana? Hasha! Jambo hili lilikuwa lenye maana, kwa kuwa upesi kabla ya masimulizi ya ziara ya Yesu katika Sikari ya Kisamaria, imeandikwa hivi: “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake), aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya. Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo.”​—Yohana 4:1-6.

18. Miaka miwili baadaye, wakati Yesu alipokuwa akipitia Samaria akielekea Yerusalemu, wakaaji wa kijiji wa Samaria walionyesha mwendo gani?

18 Je! mambo yalimwendea Yesu vizuri miaka miwili baadaye? Yeye na wanafunzi wake walikuwa wakienda upande mwingine, ili wahudhurie sikukuu ya Kiyahudi ya vibanda huko Yerusalemu. Kisha wajumbe wa Yesu “wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake [wapi?] kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, Uwaangamize? Akawageukia, akawakanya. . . . Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine.” (Luka 9:51-56) Kama Yesu angeachilia hasira kali ya Yakobo na Yohana, huenda hili lingefanya Wasamaria wauchukie Ukristo.

19. (a) Wakati Yesu alipowatuma mitume 12 wakiwa wawili wawili, alitoa maagizo gani kuhusiana na Samaria? (b) Kulingana na Yohana 8:47, 48, maoni ya Wayahudi kwa ujumla yalikuwa nini kuwaelekea Wasamaria?

19 Hata mwaka mmoja kabla ya hapo, kabla ya Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 32 W.K., wakati Yesu alipowatuma mitume wakahubiri wawili wawili, yeye aliwaambia hivi: “Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mt. 10:5-7; Luka 9:1-6) Miezi mingi baadaye, baada ya sikukuu ya vibanda ya mwaka 32 W.K., Yesu aliwatuma wale wainjilisti 70 na kuwapa maagizo kama yale yaliyopewa wale mitume 12. Vijiji na miji ambayo katika hiyo walihubiri ufalme wa Mungu yawezekana ilikuwa katika Yudea, si katika Samaria. (Luka 10:1-24) Hawakuripoti kuzuru sehemu za Wasamaria. Waliwaendea “kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” Sababu gani hivyo? Kwa sababu wainjilisti hao hawakupewa mamlaka zaidi kuliko yale ya mitume. Maoni ya Wayahudi kwa ujumla kuwaelekea Wasamaria yalijionyesha wakati Yesu alipowaambia Wayahudi wasioamini kwamba hawakuwa wametoka kwa Mungu, nao wakajibu vikali: ‘Wewe u Msamaria, nawe una pepo.’​—Yohana 8:47, 48.

20. Sababu gani Wasamaria hawakupata faida yo yote kutokana na kutumiwa kwa wa kwanza wa “funguo za ufalme” na Petro wakati wa Pentekoste katika Yerusalemu, na kwa hiyo ni ulizo gani linalotokea?

20 Yesu alionyesha tofauti kati ya Wasamaria na Wayahudi alipomwambia mwanamke Msamaria: “Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka[na na] Wayahudi.” (Yohana 4:22) Yesu alimhesabu Msamaria kuwa ‘mtu wa taifa jingine’ au, kwa halisi zaidi, ‘wa kabila jingine.’ (Luka 17:16-18, NW; tazama tafsiri ya neno kwa neno ya Kingdom Interlinear Translation.)a Wasamaria, ambao waliabudu kwenye Mlima Gerizimu, hawakuhudhuria Pentekoste katika Yerusalemu katika mwaka 33 W.K. Kwa hiyo hawakufaidika hata kidogo kutokana na kutumiwa kwa wa kwanza wa “funguo za ufalme wa mbingu” na Petro. (Matendo 2:5-11) Basi, ni wakati gani, mitume 12 walipokazia Samaria fikira zao baada ya roho takatifu kumiminwa Yerusalemu kusudi wapate kushiriki katika yale aliyotabiri Yesu katika Matendo 1:8?

21. Ikawaje Filipo mwinjilisti akawa katika Samaria, na sababu gani furaha nyingi ilitokana na kuwapo kwake?

21 Baada ya Pentekoste mambo mengi yalilipata kundi la Kikristo katika Yerusalemu. Mateso yaliyofuata kuuawa kwa Stefano kwa ajili ya imani yalitawanya washiriki wote wa kundi hilo kutoka Yerusalemu isipokuwa wale mitume 12. (Matendo 8:1-5) Si kwa sababu ya maagizo na mashauri ya kimtume, walakini kwa sababu ya mateso, kwamba Filipo, mfanya kazi mwenzi wa karibu wa Stefano, na Wakristo wengine wa Kiyahudi walikimbilia kaskazini kwenye wilaya ya Samaria. (Matendo 6:1-6; 21:8) Huko Filipo, ambaye alikuwa amependelewa kwa karama za miujiza na roho ya Mungu, alihubiri habari njema juu ya Yesu Kristo aliyefufuliwa na kutukuzwa na kufanya ishara nyingi za kimwujiza kwa njia ya maponyo. “Ikawa furaha kubwa katika mji ule.”​—Matendo 8:8.

22. Kwa sababu ya ubatizo wa maji wa wanaume na wanawake wengi Wasamaria uliofanywa na Filipo, ni ulizo gani linalotokea?

22 Matokeo ya jambo hili yalikuwa nini? “Walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.” Hii ilitia ndani mchawi mmoja aliyeitwa Simoni ambaye ‘alikuwa akifanya uchawi na kushangaza taifa la Samaria.’ (Matendo 8:9, 12, 13) Kufikia hapa ulizo latokea, Je! Wasamaria hao wenye kuamini walizaliwa “kwa maji na kwa roho”? Basi, maji ya ubatizo yalihusika katika jambo hili, walakini namna gani juu ya roho? Iwapo walipata kuwa waliozaliwa kwa roho baada ya ubatizo wao wa maji, basi ni Filipo aliyefungulia njia kikundi hiki kipya, Wasamaria, kwenye “ufalme wa mbingu.” Walakini je! kweli kweli yeye alifanya hivyo, ijapokuwa yeye hakuwa mmoja wa wale mitume 12? Maandishi yaliyoandikwa yaonyesha nini?

23. Sababu gani hairipotiwi kwamba Filipo aliahidi Wasamaria wenye kubatizwa katika jina la Yesu roho takatifu?

23 Filipo huyu hakuwa mmojawapo wa mitume ambao Yesu aliambia hivi: “Yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.” (Mt. 18:18; 16:19, NW; 10:2-4; Yohana 1:43-48) Kwa hiyo hairipotiwi kuwa Filipo alitoa ahadi zo zote za karama ya roho takatifu kwa Wayahudi katika siku ya Pentekoste: “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha [roho takatifu].”​—Matendo 2:38.

24. (a) Je! kwa kutahiriwa na kuadhimisha sikukuu zilizoandikwa katika maandishi ya Musa, Wasamaria waliingia katika Agano la Torati ya Musa? (b) Baada ya ubatizo wa maji katika jina la Yesu, je! mara hiyo ‘walizaliwa kwa maji na kwa roho’?

24 Wasamaria hawakuwako katika agano la Torati ambalo Musa alikuwa mpatanishi kwa ajili ya Waisraeli kwenye Mlima Sinai, hata ijapokuwa Wasamaria waliviona vitabu vitano vya kwanza vya Musa, kuwa Neno la Mungu na kuadhimisha Sikukuu ya Kupitwa na Pentekoste kwenye Mlima Gerizimu katika wilaya ya Samaria. (2 Fal. 17:29, 30; Yohana 4:19, 20) Kwa hiyo kutahiriwa kwao kwa mwili kwenyewe hakukuwafanya waongofu Wayahudi. Wasamaria hawakuhusika na kutundikwa kwa Yesu na kwa hiyo hawakuhitaji kubatizwa katika maji kwa ajili ya kusamehewa na Mungu kwa dhambi nzito hiyo ambayo walihitajiwa kutubia. Walakini Wasamaria walibatizwa na Filipo katika jina la Yesu Kristo kuwa ndiye Masihi (Kristo) na “Mwokozi wa ulimwengu.” (Yohana 4:25, 26, 28, 29, 42) Kwa sababu hii, je! walipata kuwa ‘waliozaliwa kwa maji na kwa roho’? Hasha! Kwa sababu wakati huo hawakupata roho takatifu.

25. Matendo 8:14-17 laonyeshaje sababu ya Wasamaria waliobatizwa kutokuwa wamezaliwa kwa maji na kwa roho?

25 Sababu gani ikawa hivyo? Matendo 8:14-17 hutuambia hivi: ‘Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea waipokee roho takatifu; kwa maana bado haijashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu, Ndipo [Petro na Yohana wakiwa mitume] wakaweka mikono yao juu yao, nao [Wasamaria waliobatizwa] wakaipokea roho takatifu.’ Hii maana yake si karama za kimwujiza za kiroho tu.

26. Kwa hiyo Wasamaria waliobatizwa walistahili pendeleo gani, naye Petro, akiwapo Yohana, alitumia chombo gani?

26 Ni hapa kwanza Wasamaria waliobatizwa walipopata kuwa ‘waliozaliwa’ kwa roho na vilevile kwa maji na kustahili kuuingia ufalme wa kimbinguni wa Mungu. (Yohana 3:5) Utendaji wa roho hapa ulikuwa kama ule ulioripotiwa baadaye katika Matendo 10:44-46 na 11:15-17. Hivyo kwa ajili ya Wasamaria waamini waliobatizwa mtume Petro alitumia wa pili wa “funguo za ufalme wa mbingu.” Ni kweli, mtume Yohana alikuwako hapo pamoja na Petro, lakini, mapema, katika siku ya Pentekoste, mitume wengine 11 walikuwa pamoja na Petro mwenye kuwa na funguo.​—Tazama pia Mathayo 18:1, 18.

27. Matendo 8:18-23 laonyeshaje Petro akiongoza katika kushughulika na Simoni ambaye hapo kwanza alikuwa mchawi?

27 Kwamba Petro aliongoza katika habari hii Matendo 8:18-23 huonyesha kwa linavyosema kwa kufuata hayo: “Hata Simoni [mchawi] alipoona ya kuwa watu wanapewa [roho takatifu] kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee [roho takatifu]. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.” Jambo hili laonyesha kwamba Petro alikuwa akiongoza kama wakili mkuu wa Kristo wakati wa pindi hii. Yeye alizungumza, akiwa yule ambaye amepewa funguo za Ufalme.

28. Kisha nafasi ya Ufalme ilifunguliwa kwa nani wengine, nao Wasamaria waliozaliwa kwa roho walianza kuabudu wapi?

28 Kuanzia wakati huo na kuendelea nafasi iyo hiyo ingeweza kupewa wengine katika wilaya ya Samaria. Hivyo, Matendo 8:25 latuambia hivi: “Nao [Petro na Yohana] walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.” Sasa Wasamaria waliozaliwa kwa roho na kubatizwa, wakaanza kumwabudu Baba yao wa kimbinguni, Yehova, si juu ya Mlima Gerizimu wala huko Yerusalemu, walakini katika hekalu lake kuu zaidi la kiroho.​—Yohana 4:21.b

29. Baada ya kuongolewa kwa Paulo kwenye Ukristo, ni jambo gani lililopata kundi lililozaliwa kwa roho katika Yudea, Galilaya na Samaria, naye Filipo alichukua makao wapi?

29 Filipo na Wakristo wengine wa Kiyahudi walikuwa wamelazimishwa kukimbilia Samaria kwa sababu ya mateso yaliyoendelezwa na Farisayo Sauli wa Tarso. Walakini baada ya Sauli mwenyewe kugeuzwa kwenye Ukristo, mambo yalibadilika kwa kundi hilo katika Palestina. “Basi,” kulingana na Matendo 9:31, “kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha [Yehova], na faraja ya [roho takatifu].” Hata hivyo, Filipo, mwishowe alichukua makao katika mji wenye bandari wa Kaisaria, ambako liwali wa Rumi wa jimbo la Yudea alikuwa na makao yake na ambako kulikuwako na jeshi la askari wa Italia.​—Matendo 8:40; 21:8; 10:1; 23:23-25.

[Maelezo ya Chini]

a Tazama kitabu Theological Dictionary of the New Testament, Kit. 1, uku. 266, chini ya Allogenes’.

b Yote haya yalitukia wakati wa nusu ya mwisho ya juma la mwisho la “majuma sabini” ya miaka yaliyotabiriwa katika Danieli 9:24-27a. Wakati wa “juma” hilo la 70 Yehova Mungu alikuwa akitendesha kazi kuelekea Waisraeli wa asili agano la Ibrahimu ambalo katika hilo Waisraeli walijipata ndani yake kwa kuwa warithi wa asili wa Ibrahimu. (Mwa. 12:1-3; 22:18) Tofauti na Filipo ambaye alikimbia mateso na kwenda Samaria, Matendo 11:19 latuambia hivi: “Wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki ‘ iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na [kisiwa cha] Kipro na Antioka [katika Shamu], wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao.” “Juma” la 70 la kibali ya pekee kwa Wayahudi wa asili kwa sababu ya agano la Ibrahimu lilimalizika mapema katika vuli wa mwaka 36 W.K., likiwa lilianza na kubatizwa kwa Yesu na kutiwa mafuta katika mwaka 29 W.K. Kwa hiyo kufunguliwa nafasi kwa Wasamaria waliobatizwa hakukufungulia njia watu wote wasio Wayahudi katika ‘sehemu za mwisho wa dunia’ au kutanguliza kuingia kwa wingi kwa Mataifa hao wasiotahiriwa kwenye kundi la Kikristo lililozaliwa kwa roho.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Ufunguo wa Daudi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki