Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 5/15 kur. 17-24
  • Kukombolewa na Kuokoka Jumuiya ya Wakristo Iangukapo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kukombolewa na Kuokoka Jumuiya ya Wakristo Iangukapo
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • WAOKOKAJI WA KUHARIBIWA KWA JUMUIYA YA WAKRISTO WAFANANISHWA KIMBELE
  • KUEPUKA UHARIBIFU JUU YA DINI YOTE YA UONGO
  • Kuvumilia Kwa Uaminifu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1978
  • Mwelekeo Tofauti Juu ya Utii
    Kuokolewa Kuingia Katika Dunia Mpya
  • Kitabu Cha Biblia Namba 26—Yeremia
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • “Tafadhali, Itii Sauti ya Yehova”
    Mungu Asema Nasi Kupitia Yeremia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 5/15 kur. 17-24

Kukombolewa na Kuokoka Jumuiya ya Wakristo Iangukapo

1, 2. (a) Yubile ya mwisho kwa Wayahudi Ingetokea lini na katika wakati wa kazi ya kiunabii ya nani? (b) Sheria ya Yehova kupitia kwa Musa iliwaamuru Wayahudi jambo gani juu ya Yubile?

KATIKA siku za Yeremia mwaka wa sabato ulipaswa kuwa wakati wa kukombolewa kwa watumwa wa Kiyahudi. Mwaka wa sabato wa mwisho wa namna hiyo ulimalizika katika mwaka 609 K.W.K. katika Tishri 9, siku moja kabla ya Siku ya Upatanisho ya Kiyahudi. Watu wa Yeremia walikuwa wanatakiwa washerehekee miaka ya sabato tangu walipoingia nchi ya Kanaani katika mwaka 1473 K.W.K. Kila mwaka wa 50 tangu wakati huo ulipaswa kuadhimishwa kama mwaka wa Yubile, kila Yubile ikianza katika Siku ya Upatanisho. Yubile ya 17 ilipata kuwa ya mwisho. Ilimalizika katika mwaka 623 K.W.K., wakati wa utendaji wa kiunabii wa Yeremia. Akiwa kuhani katika hekalu Yeremia angeusikia mlio wa tarumbeta ukitangaza kuanza kwa Yubile hiyo, mwaka wa pekee wa kukombolewa. Sheria ya Yehova kama ilivyotolewa kwa nabii Musa iliamuru hivi:

2 “Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote waiketio; itakuwa ni [Y]ubile kwenu; nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake. Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni [Y]ubile kwenu.”​—Law. 25:10, 11.

3. Sheria ya Mungu ilikuwa nini kwa habari ya kila mwaka wa saba kati ya Yubile, nao wanunuzi Waebrania wangeendelea kuweka watumwa wao Waebrania kwa muda gani?

3 Kama vile sabato ya kila juma, kila mwaka wa saba kati ya Yubile ulipaswa kuwa mwaka wa sabato. (Law. 25:1-9) Kwa mpango kama uo huo, sheria ya Yehova ilisema hivi: “Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure.” (Kut. 21:2) “Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, alikuwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako.”​—Kum. 15:12.

4. Kwa hiyo, katika mwaka wa sabato wa 610-609 K.W.K., ingefaa kwa wenyeji wa watumwa Waebrania kufanya nini, walakini walimpaje Mungu sababu ya ziada ya kuwaadhibu?

4 Kwa hiyo, katika siku za Yeremia, katika mwaka huo wa sabato wa 610-609 K.W.K., ilikuwa vema machoni pa Yehova kwa Wayahudi wenye watumwa kufanya agano mbele yake katika hekalu katika Yerusalemu ili kuwaacha watumwa wao Waebrania wawe huru. Ijapokuwa hali ya mataifa yote yenye kutisha sana Yerusalemu, huu ulikuwa ndio mwendo wa utii kwa watu wa Yeremia kuchukua. Walakini, kabla ya mwaka huo wa kukombolewa kumalizika, wale wenyeji wa watumwa wa mbeleni walivunja agano lao zito na kuwalazimisha watumishi wao wanaume na wanawake kwenye utumwa tena. Jambo hilo lilimchukiza Yehova mwenye kushika agano na kumpa sababu nyingine zaidi ya kuwaadhibu.​—Yer. 34:8-16.

5. (a) Ni wageni gani katika Yerusalemu wakati huo ambao hawakuhusika na wakati ule ule walipokuwa katika hatari? (b) Mfano wa kisasa wa Yerusalemu umo hatarini namna gani, na kutokana na chanzo gani?

5 Kwa furaha kutoheshimu huko kwa agano lililofanywa kwa uzito mbele ya Yehova hakukutia ndani watu fulani ambao wakati huo walikuwa katika Yerusalemu waliojulikana kama Warekabi wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu. (Yer. 35:6-11) Hata hivyo, bado walikuwa hatarini kwa sababu ya adhabu ambayo kwa kustahili ilikuwa ikija juu ya wakaaji Wayahudi wa Yerusalemu. Walakini walikuwa katika hali ya kulindwa kutokana na yale ambayo Yehova Mungu aliendelea kutabiri kwa sababu ya kutokuaminika kwenye choyo kwa Wayahudi. Kama ambavyo ilikuwa kwa habari ya Yerusalemu wa siku za Yeremia, maneno yaliyofuata ya Yehova yanapaswa kuvutia zaidi Jumuiya ya Wakristo ya kisasa. Kama vile Yerusalemu wakati huo, Jumuiya ya Wakristo iko katika siku za mwisho za kuwapo kwake kwa muda mrefu. Mamlaka ya mwisho ya ulimwengu inayotabiriwa katika unabii wa Biblia, mamlaka ya ulimwengu ya nane, ipo pamoja nasi sasa. Ipo kwa namna ya Umoja wa Mataifa. Ina sehemu inayopaswa kutimiza kuiangamiza Jumuiya ya Wakristo, mfano wa kisasa wa Yerusalemu. Umoja wa Mataifa na mtangulizi wake, Ushirika wa Mataifa, sasa zimekuwa na maisha yaliyounganishwa ya miaka 60. (Ufu. 17:7-11) Kabla haujaangamia utafanya kitendo!

6. Jumuiya ya Wakristo, imewaletaje washiriki wake wa kanisa kwenye utumwa, ingawa inadai kutetea uhuru?

6 Kwa sababu ya kudai kuwa ya Kikristo, Jumuiya ya Wakristo, inapaswa kuleta uhuru kutokana na utumwa wa ulimwengu huu wenye kutumikishwa na dhambi. Ingawa hivyo, kwa hakika, imefanya washiriki wake wa kanisa kuwa watumwa wa ulimwengu huu, kwa ajili ya faida zake. Hii ni kwa sababu imejifanya rafiki ya ulimwengu huu na adui wa Mungu.​—Yak. 4:4.

7. (a) Waenda kanisani wa Jumuiya ya Wakristo wameongozwa kwenye utumwa gani na katika kupingana na nani? (b) Inaagizwa isikilize mambo gani zaidi katika unabii wa Yeremia?

7 Watumwa wa kiroho wa Jumuiya ya Wakristo wanatumikia, si ufalme wa Mungu kupitia kwa Kristo, bali ulimwengu uliohukumiwa maangamzi pamoja na mtawala na mungu wake, Shetani Ibilisi. (l Yohana 2:15-17; Efe. 2:2) Jumuiya ya Wakristo inawaongoza waenda-kanisani katika kupinga wale mashahidi Wakristo wa Yehova ambao walifananishwa na Yeremia. Basi acheni isikie yale aliyoendelea kusema:

“Basi [Yehova] asema hivi, Hamkunisikiliza kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake, na kila mtu jirani yake; tazama, mimi nawatangazieni uhuru, asema [Yehova], yaani, wa upanga, na njaa, na tauni; nami nitawatoa ninyi mtupwe huko na huko katika falme zote za dunia. Na watu waliolivunja agano langu, wasioyatimiza maneno ya agano lile, walilolifanya mbele zangu, wakati ule walipomkata ndama vipande viwili, wakapita katikati ya vipande vile; wakuu wa Yuda, na wakuu wa Yerusalemu, matowashi, na makuhani, na watu wote wa nchi, waliopita katikati ya vipande vile vya huyo ndama; mimi nitawatia katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta [nafsi] zao: na mizoga yao itakuwa ni chakula kwa ndege za mbinguni, na cha wanyama wakali wa nchi. Na Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake nitawatia katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta [nafsi] zao, na katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, waliokwenda zao na kuwaacheni. Tazama, nitawapa amri yangu, asema [Yehova], na kuwarejeza kwenye mji huu; nao watapigana nao, na kuutwaa, na kuuteketeza kwa moto; nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, isikaliwe na mtu.”​—Yer. 34:17-22; linganisha Mwanzo 15:10-18.

8. Kwa kusaidiwa na unabii huo wa Yeremia, ni jambo gani linalofananishwa kwa ajili ya Jumuiya ya Wakristo leo?

8 Je! unabii huo unaonya kimbele kuangushwa kwa Jumuiya ya Wakristo na majeshi ya kilimwengu ambayo Yehova anaruhusu yafanye mazingiwa juu yake? Ungeweza kufananisha nini zaidi kwa sababu ya yale yaliyoupata Yerusalemu? Kwa kutii, Yeremia alikuwa amemtabiria Mfalme Sedekia kukamatwa na kuhamishwa kwake mpaka Babeli, akafie huko. (Yer. 34:1-7) Basi, kwa hakika, katika utimizo mkubwa wa tukio hilo la kiunabii la Biblia, hakuna mema wanayongojea watawala wa Jumuiya ya Wakristo!

9. Yerusalemu ulianza kuzingirwa wakati gani baada ya mwaka wa sabato, nako kulikuwa kwa muda mrefu kadiri gani, nao mji’ huo ulipataje kuwa kitu cha kutetemesha kwa woga wa kupatwa na mwisho kama huo?

9 Katika mwaka 609 K.W.K. mwaka wa sabato ulimalizika katika siku ya 9 ya mwezi wa saba (Tishri), siku iliyotangulia Siku ya Upatanisho. Baada ya hapo, katika siku ya 10 ya mwezi wa kumi (Tebethi) wa mwaka uo huo, Mfalme Nebukadreza na majeshi yake ya Kibabeli walianza kuzingira Yerusalemu. (2 Fal. 25:1, 2) Miezi kumi na minane ikapita polepole mpaka Yerusalemu uliposhindwa, yaani, katika siku ya 9 ya mwezi wa 4 (Tamuzi), katika mwaka 607 K.W.K. Katika kujaribu kwake kutoroka na hivyo aushinde unabii wa Yehova, Mfalme Sedekia alifika kwenye mji wa Yeriko tu, na kisha wafuatiaji wake wa Kibabeli wakamkamata. Kisha wakamrudisha akutane uso kwa uso na Nebukadreza na kupelekwa uhamishoni usio na tumaini katika Babeli yenye kuabudu sanamu. (Yer. 34:2, 3) Katika mwezi uliofuata, au katika Abi 7, 607 K.W.K., Yerusalemu ulitekwa nyara na kuteketezwa. Hekalu lake lililonajisiwa (lililochafuliwa) la Yehova halikuuokoa. (2 Fal. 25:3-17) Kweli kweli uharibifu wenye kuogopesha sana wa Yerusalemu ulikuwa jambo la kufanya mataifa yale mengine yatetemeke kwa kuogopa kutendewa vivyo hivyo na Wababeli.

10. Je! Jumuiya ya Wakristo inaogopeshwa na tamasha hiyo ya kale, nao uharibifu wayo yenyewe utaanzisha nini?

10 Hata hivyo, karne nyingi baadaye uwezo wa tamasha ya Yerusalemu ukiwa magofu unaopaswa kutia woga mwingi hauonwi na Jumuiya ya Wakristo. Haitetemeki. Haioni katika tamasha hiyo ya zamani mfano wo wote wa kiunabii wa uharibifu wake unaokuja kwa haraka sana ulimwenguni pote. Huo utaanzisha uharibifu wa dini yote ya uongo katika dhiki iliyo kuu zaidi ambayo haijaupata ulimwengu huu unaompinga Yehova. Itakuwa kama vile ilivyotabiriwa katika Mathayo 24:15-22.

11. Nchi ya Yerusalemu iliachwa mahame pasipo mwanadamu au mnyama wa kufugwa wakati gani, na je! Yeremia na Baruku peke yao ndio waliookoka chini ya kibali ya Yehova?

11 Hivyo, basi, mwanadamu ye yote atawezaje kuokoka dhiki hiyo? Kwa njia ile ile Yeremia na mwandishi wake Baruku walivyookoka msiba wa Yerusalemu wa upanga, njaa, tauni na mteketeo mkubwa! Baadaye, katika mwezi wa saba wa mwaka huo wenye msiba, Yeremia alipelekwa Misri na watu hao wenye wasiwasi walioasi utawala wa Babeli. Hivyo nchi yote ya ufalme wa Yuda ikawa ukiwa bila mtu au mnyama wa kufugwa. (2 Fal. 25:22-26) Walakini, licha ya Yeremia na mwandishi wake Baruku, wengine vilevile waliokuwa na kibali ya Yehova waliokoka uharibifu wa Yerusalemu na kufanywa ukiwa kwa nchi ya Yuda. Walikuwa wamehakikishiwa hilo kupitia kwa Yeremia. Sisi leo twapaswa kupendezwa na habari ya waokokaji hao, iwapo tunataka kuiokoka dhiki inayokuja.

WAOKOKAJI WA KUHARIBIWA KWA JUMUIYA YA WAKRISTO WAFANANISHWA KIMBELE

12. Waokokaji hao wa dhiki inayokuja walifananishwa na watu gani waliokuwa wageni wenye kuhama-hama, naye Yeremia alipataje kuwakuta Yerusalemu?

12 Mhifadhi Mkuu wa uhai wa kibinadamu ataweka macho yake juu ya nani wakati wa ile dhiki inayokaribia ambayo katika hiyo taratibu hii ya mambo iliyohukumiwa maangamizi itaangamia? Juu ya wale Wakristo walio wakf, na kubatizwa ambao alifananisha kwa kutumia kikundi fulani cha wakimbizi wageni katika Yerusalemu. Rafiki hao wa Wayahudi walijiona kuwa na lazima ya kuacha maisha yao ya kuhama-hama na kuishi kwa muda katika Yerusalemu kwa sababu hawakutaka kujiunga na kambi ya adui ambao walikuwa wanasonga mbele ili wauzingire Yerusalemu chini ya amri ya mfalme wa Babeli, Nebukadreza. Baba yao alikuwa Yonadabu au Yehonadabu, mwana wa Rekabu. Hata hivyo, hawakuitwa Wayonadabu, kwa kuwa Mfalme Daudi alikuwa na mpwa aliyeitwa Yonadabu. Bali waliitwa Warekabi, jina hilo likiwaonyesha kuwa si Waisraeli. Yeremia alifahamiana nao vizuri sana.

13. Kuweka agano kwa Waisraeli kulilinganaje na kuweka ahadi ya kiapo kwa Warekabi?

13 Kwa zaidi ya miaka 250 walikuwa wamekuwa waaminifu kwa ahadi ya kiapo waliyowekwa chini yake na babu yao mwenye kujulikana sana Yonadabu. Waisraeli hawakuwa na kumbukumbu ambalo lingeweza kulingana na hilo kwa habari ya uaminifu wao kwa agano la Torati ambalo katika hilo babu zao walikuwa wameingia kupitia kwa Musa akiwa mpatanishi wao na Yehova Mungu, huko nyuma katika mwaka 1513 K.W.K. Kwa hiyo sasa Mungu yule ambaye agano lake walikuwa wamevunja alikusudia kuonyesha tofauti kati ya Waisraeli hawa na Warekabi wenye kuweka ahadi ya kiapo. Hivyo basi, sasa Warekabi hao wangejaribiwa katika mahali palipokuwa patakatifu kwa Yehova, hekalu lake katika Yerusalemu. Kwa hiyo yeye alimwambia Yeremia hivi: “Enenda nyumbani kwa Warekabi, ukanene nao, ukawalete nyumbani kwa [Yehova], katika chumba kimoja, ukawape divai wanywe.” (Yer. 35:1, 2) Jaribu hilo, ijapokuwa ilikuwa inafahamika vizuri kabisa kwamba Warekabi hawakuwa wanatumia vileo.

14. Warekabi walielezaje kukataa kwao kunywa divai waliyopewa na Yeremia, na vilevile kukaa kwao katika mji?

14 Yeremia alifanya kama alivyoamriwa. (Yer. 35:3-5) Hata kwa kupewa na nabii huyo Warekabi walikataa kunywa. Walieleza hivi:

“Hatutakunywa divai; kwa maana Yonadabu, mwana wa Eekabu, baba yetu, alituamuru, akisema, Msinywe divai, ninyi wala wana wenu, hata milele; wala msijenge nyumba, wala msipande mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo; bali siku zenu zote mtakaa katika hema; mpate kuishi siku nyingi katika nchi ambayo mtakaa ndani yake hali ya wageni. Nasi tumetii sauti ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, katika yote aliyotuamuru, kwamba tusinywe divai siku zetu zote, sisi, na wake zetu, na wana wetu, na binti zetu; wala tusijijengee nyumba za kukaa; wala hatuna shamba la mizabibu, wala konde, wala mbegu; bali tumekaa katika hema, nasi tumetii; tukafanya sawasawa na yote aliyotuamuru Yonadabu, baba yetu. Lakini ikawa, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alipopanda akaingia nchi hii, ndipo tukasema, Haya! twende Yerusalemu, tukiliogopa jeshi la Wakaldayo, na tukiliogopa jeshi la Washami; basi hivyo tunakaa Yerusalemu.”​—Yer. 35:6-11.

15. Ahadi ya kiapo waliyoweka Warekabi ilikuwa yenye kulinda namna gani, nalo agano la Torati ya Musa liliwahusuje?

15 Ahadi ya kiapo iliyopewa Warekabi ilikuwa ulinzi kwao. Iliwafanya waishi maisha mepesi wakiwa wageni katika nchi na bila kujitia katika upotovu wa miji. Kwa kuwa hawakuwa Waisraeli walio chini ya agano la Torati ya Musa, walikuwa kama wageni ndani ya malango ya Waisraeli na hawakuwapa matata wakaribishaji wao Waisraeli. Hawakuingiliana na Waisraeli katika kutimiza agano lao na Yehova, bali, mahali pake, walilifuata agano la Torati kwa kadiri lilivyowahusu. Hata hivyo, kwa habari ya kunywa vileo, walikuwa kama Wanaziri (watu waliojitoa kabisa kwa Mungu) Waisraeli. Kwa kuendelea bila kunywa vileo, waliendelea kuwa na kiasi. Kushambuliwa kwa nchi ya Yuda na majeshi ya Mfalme Nebukadreza kulikuwa kunakaribia kuyahusu maisha yao mepesi ya kuhama-hama. Ni jambo la akili kwamba, Wakaldayo wenye kushambulia waliposonga mbele, Warekabi walikimbilia Yerusalemu.

16. Warekabi hao wenye kushika ahadi yao ya.kiapo walimpaje Yehova mfano wa kutumia juu ya Waisraeli wenye kuvunja agano, naye aliona lazima ya kuleta nini juu yao?

16 Kushikamana kwa thabiti na ahadi ya kiapo ya kutokunywa divai, hata walipokaribishwa na nabii-kuhani Yeremia, kulimpa Yehova mfano wa kutumia kwa Waisraeli wenye kuvunja agano. Warekabi waliiweka ahadi yao ya kiapo, hata ingawa waliiweka pamoja na mwanadamu tu, babu yao. Waisraeli walivunja agano lao la Torati, hata ingawa liliwekwa, si pamoja na mwanadamu tu, bali na Mungu Aliye Juu Zaidi. Sasa kwa kufaa Yehova alimwambia Yeremia hivi:

“Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? asema [Yehova]. Maneno ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaamuru wanawe, kwamba wasinywe divai, yametimizwa, na hata leo hawanywi; maana waitii hiyo amri ya baba yao; lakini mimi nimesema nanyi, nikiamka mapema na kunena, bali ninyi hamkunisikiliza mimi. Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza. Basi, kwa kuwa wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wameitimiza amri ya baba yao aliyowaamuru, lakini watu hawa hawakunisikiliza mimi; kwa sababu hiyo, asema [Yehova], Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli; Tazama nitaleta juu ya Yuda, na juu ya wenyeji wote wa Yerusalemu, mabaya yote niliyoyatamka juu yao; kwa sababu nimesema nao, wasinisikilize nimewaita, wala hawakuniitikia.”​—Yer. 35:13-17.

17. Sababu gani uasi wa Waisraeli waweza kusemwa kuwa ulikuwa wa kukusudia, na kwa hiyo ni jambo gani wasingeweza kuokoka?

17 Ni wazi kutokana na ulinganishaji huu kati ya Warekabi na Waisraeli kwa-mba Waisraeli hao waliopendelewa wangeweza kwa msaada wa manabii wa Mungu, kuweka agano lao na Yehova Mungu wao. Yeye alikuwa ametoa hekalu na ukuhani wake utoe dhabihu za kuondoa dhambi za kutokusudia walizofanya kwa ajili ya udhaifu wa mwili. Hata hivyo, walichagua miungu ya ziada, sana sana Baali, na kuingiza katika ibada yao maovu ya namna zote yaliyokuwa yamekatazwa na sheria ya Mungu kupitia kwa Musa. Kwa hiyo kuasi kwao agano la Torati ya Mungu iliyodai ibada safi kulikuwa kwa kukusudia. Jambo hilo halikuonyesha heshima ama kwa Mungu wa kweli mmoja anayeishi au ahadi zao nzito za kiapo walizomtolea. Jambo hilo lilimaanisha si jambo jingine ila msiba kwa waasi hao. Kwa sababu izo hizo msiba usioepukika unaikaribia Jumuiya ya Wakristo yote!

KUEPUKA UHARIBIFU JUU YA DINI YOTE YA UONGO

18. “Mkutano mkubwa” unapata uhakikisho wa kuokoka kuharibiwa kwa Jumuiya ya Wakristo na rafiki yake, ulimwengu huu, kutokana na maneno gani ya Yeremia yaliyoelekezwa kwa Warekabi?

18 Ni nani leo anayetaka kuokoka kuharibiwa pamoja na Jumuiya ya Wakristo na rafiki yake wa karibu, taratibu hii ya mambo yenye kumvunjia Mungu heshima? “Twataka!” ndivyo wanavyosema wale wa “mkutano mkubwa” uliotabiriwa katika Ufunuo 7:9-17. Wanapata uhakikisho thabiti kutokana na ahadi ya Yehova waliyopewa Warekabi wale wenye kuweka ahadi ya kiapo, kama ilivyoandikwa katika Yeremia 35:18, 19, ambapo twasoma hivi: “Naye Yeremia akawaambia watu wa nyumba ya Warekabi, [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa sababu mmeitii amri ya Yonadabu, baba yenu, na kuyashika maagizo yake yote na kutenda sawasawa na yote aliyowaamuru; basi kwa sababu hiyo, [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.”

19. (a) Maoni ya Yonadabu juu ya ibada ya Baali yalikuwa maoni gani? (b) Majina Yonadabu (Yehonadabu) na Yaazania yanamtaja nani, nao walichukua msimamo gani kwa habari ya divai?

19 Hivyo Yonadabu mwana wa Rekabu, ijapokuwa hakuwa Mwisraeli, angeendelea kuwa na mzao mwenye kukubalika mbele za Yehova hapa duniani milele, Na tukumbuke kwamba Yonadabu alimwunga mkono Mfalme Yehu kwa moyo wake wote katika kuharibu ibada ya Baali katika Ufalme wa Israeli ulioasi. (2 Fal. 10:15-28) Jina la mwana huyo wa Rekabu, yaani, Yonadabu au Yehonadabu, linamtaja Mungu wa pekee wa kweli anayeishi, kwa kuwa linamaanisha “Yehova Ni Mkarimu.” Yeremia aliisema ahadi hii ya kimungu kwa Mrekabi aliyeitwa Yaazania, nalo jina lake lamaanisha “Yah [yaani, Yehova] Husikia.” (Yer. 35:3-5) Kwa kutimiza ahadi yao ya kiapo, Yaazania na ndugu zake walikataa kunywa divai waliyopewa na Yeremia katika hekalu la Yehova. Hapo mbele za Yehova walionyesha ukamilifu wao kuelekea ahadi yao ya kiapo.

20. Ijapokuwa hatuna ushuhuda wa moja kwa moja wa Biblia, twaweza kuwa na uhakika gani juu ya Warekabi wakati wa kuharibiwa kwa Yerusalemu, na baada ya hapo?

20 Yehova aliheshimu uaminifu wa Warekabi hao na akaahidi kwamba wasingefutiliwa mbali wakati wa uharibifu wenye kuja wa Yerusalemu katika mwaka 607 K.W.K. Twaweza kuwa na hakika kwamba wakati huo Warekabi hawakufutiliwa mbali kutoka mbele za Yehova, kwa kuwa yeye aliheshimu neno lake la ahadi kwa kadiri ile ile Warekabi walivyoheshimu ahadi yao ya kiapo kwa habari ya divai. Kwaweza kuwa ushuhuda wa kweli wa kuokoka kwao unaoonyeshwa kwa njia ya Malkiya mwana wa Rekabu, ambaye alijenga upya lango la Yerusalemu katika siku za Liwali Nehemia. (Neh. 3:14) Kama Warekabi wo wote waliokoka kufikia siku za Yesu Kristo na kuwa wanafunzi wake haijaandikwa katika Neno la Yehova. Lakini ingalifaa sana kuwa hivyo!

21. Warekabi waliokoka msiba gani wa taifa zima, na kwa hiyo ni jambo gani linalofaa waokoke wale waliofananishwa nao?

21 Warekabi wa asili hawatambuliki leo, ila kuna mfano wao wa kisasa. Ni wale wanaoshirikiana sana na Waisraeli wa kiroho, waliofananishwa na Yeremia. Warekabi wa kale waliokoka kuharibiwa kwa Yerusalemu wenye kuasi. Kwa kuwa walifananisha “mkutano mkubwa” wa “kondoo wengine” wa Kristo, inafaa kwamba hawa waliofananishwa na Warekabi waokoke “dhiki kubwa” ya ulimwengu, ambayo katika hiyo sehemu ya kwanza kuharibiwa itakuwa Jumuiya ya Wakristo, mfano wa Yerusalemu.

22. (a) Ni wakati gani kwa mara ya kwanza ilipoonyeshwa kwamba Yonadabu alifananisha jamii ya wenye mfano wa kondoo ambao wangeokoka “ile dhiki iliyo kuu”? (b) Toleo la Mnara wa Mlinzi la Aprili 15, 1935’ liliwaalika waje kwenye jambo gani?

22 Kitabu cha 3 cha Vindication (Kutetea), Kilichotolewa Jumatatu, Julai 18, 1932, katika Brooklyn, N.Y. (Amerika), ndicho kilichokuwa cha kwanza kuonyesha (katika kurasa 77-83) kwamba Yonadabu wa zamani alifananisha jamii ya watu wenye kumcha Mungu ambao, chini ya ulinzi wa Mungu, wangeipita “ile dhiki iliyo kuu” wakiwa hai na kuingia katika Taratibu Mpya chini ya ufalme wa Kristo. (Kur. 230-233 za toleo la Mnara wa Mlinzi [Kiingereza] la Agosti 1, 1932) Kichwa chenye kuvutia cha mazungumzo “Mamilioni Wanaoishi Sasa Hawatakufa Kamwe” kilidhaniwa kinawahusu. Basi, ni jambo la akili kwamba, toleo la Mnara wa Mlinzi (Kiingereza) la Aprili 15, 1935, lilitoa tangazo hili:

Kwa mara nyingine Mnara wa Mlinzi unawakumbusha wasomaji wake kwamba kusanyiko la Mashahidi wa Yehova na Wayonadabu litafanyiwa huko Washington, D.C., (Amerika), kuanzia Mei 30 na kumalizika Juni 3, 1935. Inatumainiwa kwamba wengi wa mabaki na wengi wa Wayonadabu wataona inafaa kuhudhuria kusanyiko hili. Kufikia wakati huu si wengi wa Wayonadabu waliopata pendeleo la kuhudhuria kusanyiko moja, nalo kusanyiko huko Washington laweza kuwa faraja na faida ya kweli kweli kwao.​—Uku. 114.

23. jambo gani walilofunuliwa Wayonadabu hao katika kusanyiko hilo la Washington (D.C.). na kwa hiyo ubatizo wa maji katika siku iliyofuata ulitia ndani wengi wa akina nani?

23 Lilipata kuwa hivyo, kwa kuwa huko katika siku ya Ijumaa, Mei 31, walifunuliwa kwamba jamii ya Yonadabu ndiyo ile ile ya “mkutano mkubwa” uliotabiriwa katika Ufunuo 7:9-17. Inaelekea kwamba wengi wa wahudhuriaji wa kusanyiko 840 waliobatizwa katika maji siku iliyofuata walikuwa Wayonadabu au Warekabi wa mfano.

24. Kwa kuokoka uharibifu wa Yerusalemu katika mwaka 607 K.W.K., wazao hao wa Yonadabu walifananisha nani vilevile leo?

24 Yonadabu mwenyewe aliishi katika karne ya 10 K.W.K. na hakuona kuharibiwa kwa Yerusalemu katika mwaka 607 K.W.K. Walakini wazao wake, Warekabi, aliowajaribu Yeremia juu ya kuweka ahadi ya kiapo, waliona kuanguka kwa Yerusalemu na wakakuokoka milele. Kwa sababu ya kuzaliwa na Yonadabu, wao pia walifananisha “mkutano mkubwa” uliokusudiwa kuokoka kuanguka kwa Jumuiya ya Wakristo.​—Tazama kitabu You May Survive Armageddon into God’s New World, kurasa 64-67.

25. Kwa sababu ya mambo yenye kutokeza juu ya Yonadabu na Warekabi, wale wa kisasa waliofananishwa nao wanasihiwaje?

25 Basi, enyi, Wakristo mliojiweka wakf na kubatizwa mliofananishwa na Warekabi hao wa kale! Nyie, kama vile wao, mwapaswa kujiepusha kuingilia anasa sana, ibada ya uongo na kuchangamana na ulimwengu huu,’ mkiufanya rafiki yenu. (Yak. 4:4; 1 Yohana 2:15-17) Endeleeni kumwiga Yonadabu mwana wa Rekabu katika kuonyesha juhudi kwa Yehova na katika kupinga ibada ya Baali ya kisasa, ili mpate kumwona Yehova kupitia kwa Yehu wake Mkuu Zaidi, Yesu Kristo, akiharibu Jumuiya ya Wakristo na dini nyingine zote za uongo. Kwa uaminifu kama wa Warekabi, timizeni wakf wenu kwa Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova na kufanya sehemu yenu katika kuendeleza faida za ufalme wenye utukufu wa Kristo. Jambo hilo litawasaidia mwendelee kushikilia ukombozi mlioupata kutokana na ulimwengu huu uliohukumiwa maangamizi, mpaka utakapotoweka. Kwa kutumia uhuru wenu uliobarikiwa kulingana na mapenzi ya Mungu, ‘hamtakatiliwa mbali’ wakati aletapo kisasi chake juu ya ulimwengu huu mwovu na rafiki zake wote, bali mtasimama mmekubalika mbele zake na kuthawabishwa na uzima juu ya dunia iliyo paradiso chini ya ufalme wa Mwanawe. Itakuwa furaha kubwa ambayo kwayo mabaki wa jamii ya Yeremia watawafurahia ninyi kweli kweli.

—Kutoka The Watchtower Des. 1, 1979. (Mazungumzo zaidi ya unabii wa Yeremia yataendelea katika Mnara wa Mlinzi wa Julai 15, 1980)

[Picha katika ukurasa wa 21]

Kuokoka Kuanguka Kwa Jumuiya ya Wakristo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki