Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
● Habari ya Biblia huonyesha makosa matatu mazito ambayo Daudi alifanya wakati wa ufalme wake. Ni jambo gani linaloonyesha kwamba Mungu hakushindwa kufanya sehemu yake katika kumlinda Daudi asijikwaze, kama vile alivyofanya akimtumia Abigaili?—1 Sam. 25:32-34.
Makosa hayo yalihusu (1) Daudi aliagiza Sanduku la Agano lichukuliwe juu ya gari badala ya kuchukuliwa mabegani mwa makuhani, jambo hilo likamletea kifo Uza; (2) dhambi yake pamoja na Bath-sheba, iliyoleta kifo juu ya Uria na mtoto aliyezaliwa kutokana na uzinzi wao; (3) alipohesabu jeshi la Israeli, jambo lililotokeza kifo juu ya watu 70,000.
Kwa habari ya kifo cha Uza: sheria ya Mungu ilitaka kwamba Daudi ajifanyie nakala ya Sheria hiyo akiwa kama mfalme na kuisoma kila siku. (Kum. 17:18) Kushindwa kwake kufanya kulingana na Sheria kuhusu kulihamisha Sanduku la Agano kulimletea Uza kifo. (Hes. 4:15; 7:6-9) Inapaswa kuangaliwa kwamba kwa unyenyekevu Daudi alikubali kulaumiwa kwa sababu ya jambo hilo lililokuwa limetukia katika kujaribu huko kwa kulihamisha Sanduku la Agano.—2 Sam. 6:2-10; 1 Nya. 15:12, 13.
Kwa habari ya uzinzi wake pamoja na Bath-sheba, Daudi alikuwa na sheria ya Mungu iliyoeleza waziwazi juu ya uzinzi, lakini yeye alichagua kutoijali.—Kut. 20:14.
Na kwa habari ya kosa lake la kuhesabu jeshi la Israeli: Bila shaka alifanya hivyo kwa kupenda kwake mwenyewe. Yehova alimtumia Yoabu ajaribu kumzuia Daudi, ili azuiwe asijikwaze, lakini Daudi alisisitiza ifanywe kulingana na mapenzi yake.—2 Sam. 24:1-17.
Kwa hiyo, katika kila mojawapo cha visa hivyo, Yehova hangeshtakiwa kwamba alishindwa kumzuia Daudi asijikwaze.
● Katika Habakuki 2:5, ni nani huyo ambaye “huongeza tamaa yake kama [kaburi],” nalo jambo hilo lamaanisha nini?
Andiko hilo lasomwa hivi: “Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama [kaburi], naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu.”
Yule ambaye “huongeza tamaa yake” ni yeye ambaye kupitia kwa ushindi wa kijeshi “hujiwekea kabila zote chungu chungu.” Habakuki sura ya 1 huonyesha kwamba huyo si mtu mmoja lakini ni jamii ya mtu, Wababeli au Wakaldayo kwa ujumla. Akiwa na jeshi lake la vita, Mkaldayo ‘aliyaua mataifa sikuzote.’ (Mst. 17) “Tamaa,” yake au njia yake ya maisha ambayo ilifuatilia ushindi haikuweza kutoshelezwa. Kama vile kunywa divai bila kiasi kunavyoweza kumdanganya mtu na kumrusha akili kukimfanya atende kama “mtu wa kiburi” au wa majivuno, ndivyo ilivyokuwa kwa Mkaldayo ambaye kufanikiwa kwake katika kutumia jeshi kulimrusha akili. Kama vile kaburi na mauti vinavyokuwa tayari sikuzote kupokea watu zaidi, yeye sikuzote alikuwa tayari kujitwalia taifa moja baada ya jingine. (Linganisha Mithali 30:15, 16.) Hata hivyo, Mkaldayo huyo hangefanikiwa kufikia mradi wake, jambo hilo likionyesha kwamba yeye pamoja na vita vyake vya ushindi angefikia kikomo chake.
Katika kuutimiza unabii wa Biblia, Babeli ilianguka katika usiku mmoja katika mwaka 539 K.W.K. Ndipo hiyo milki kubwa mno ya Kikaldayo ilipokuja chini ya utawala wa Koreshi Mwajemi na Dario Mmedi.—Dan. 5:28.