Neno la Mungu Li Hai
Alipokuwa Mtoto Aliteswa
UKIWA kijana, huenda ukawa unaona vigumu leo kuwa Mkristo wa kweli. Huenda ukawa unadhihakiwa kwa sababu ya kukataa kuvuta tumbako au kutumia dawa za kulevya. Au huenda ukateswa kwa sababu ya kukataa kushiriki sherehe zinazopingana na kanuni za Biblia. Jambo hilo linakumbusha namna alivyoteswa Isaka, mwana kijana wa Ibrahimu na mkewe mpendwa Sara.
Kwa Isaka taabu yake ilifikia upeo wake wakati wa karamu aliyofanya Ibrahimu katika siku ya Isaka kuachishwa kunyonya. Wakati huo, Isaka alikuwa na umri wapata miaka mitano. Siku zile akina mama waliwanyonyesha watoto wao kwa muda mrefu. Wakati wa karamu hiyo, Ishmaeli, mwana tineja (miaka 13-19) alianza kumdhihaki na kumchekelea nduguye mdogo. Hayo hayakuwa mabishano ya watoto tu. Biblia inasema kwamba kwa kweli Ishamaeli “alianza kumtesa” Isaka.—Gal. 4:29, NW.
Sara aliona yaliyokuwa yakitukia, naye hakuyafurahia hata kidogo. Kwa wazi kuteswa kwa Isaka kulihusiana na ulizo la kwamba ni nani ambaye angerithi aliyokuwa amejipatia Ibrahimu. Kwa hiyo Sara alimwendea Ibrahimu na kumwambia: ‘Mwambie Hajiri na mwanawe waondoke. Hatashiriki urithi wa mwanangu lsaka.’
Jambo hilo likamwudhi Ibrahimu. Yeye hakutaka kumfukuza Ishmaeli, kwa kuwa yeye pia alikuwa mwanawe. Lakini Mungu alimwamibia Ibrahimu amsikilize mkewe Sara. Kwa hiyo Ibrahimu akawapa Hajiri na mwanawe vitu walivyohitaji kwa safari yao akawaacha waende zao.—Mwa. 21:8-14.
Mtu anayeteswa aweza kupata kitia-moyo kutokana na habari hiyo ya Biblia juu ya Isaka. Sababu gani? Kwa sababu, baada ya wakati kupita, kudhihakiwa na Ishmaeli kulikomeshwa. Yehova Mungu alihakikisha kwamba Ibrahimu alichukua hatua ya kuondoa chanzo cha taabu katika nyumba yake. Vivyo hivyo leo, Mungu hataruhusu uteseke kuliko vile unavyoweza kuvumilia. Yeye atakupa nguvu ili uweze kuvumilia, au atahakikisha kwamba mwishowe chanzo cha tatizo hilo kimeondolewa.—1 Kor. 10:13.