Neno la Mungu Li Hai
Jihadhari na Upendo Unaotegemea Tamaa za Ngono Tu
MUNGU MWEZA YOTE aliweka ndani ya mwanamume na mwanamke uvutano mzuri ajabu wa kumvuta mmoja kwa mwenzake. Walakini uvutano huo usipotumiwa vizuri, misiba mikubwa inatokea mara nyingi. Jambo hilo linaonyeshwa na kisa cha Amnoni, mwana wa Mfalme Daudi.
Amnoni alimpenda sana dada yake wa mzazi mmoja tofauti aliyekuwa mwenye umbo zuri, Tamari. Alimpenda sana hata akawa mwenye mapenzi mengi mno. Walakini alitaabika kwa sababu hakuweza kumkaribia Tamari. Wakati binamu wa Amnoni, Yonadabu alipojua namna Amnoni alivyokuwa na upendo mwingi kwa Tamari, yeye alimwambia hivi: ‘Jifanye mgonjwa. Na babako, Mfalme Daudi, atakapokuja kukutazama, umwambie, “Mwache [dada] yangu, Tamari, aje, nakusihi, anipe mkate nile. “’
Daudi alifanya kama ambavyo Amnoni alivyomwuliza. Tamari akaja, na kama unavyoweza kuona, akamtayarishia Amnoni chakula. Hata hivyo, alipompelekea, yeye alikataa kula. Yeye akasema: ‘Toeni watu wote kwangu.’ Pengine watu waliokuwa nyumbani walifikiri Amnoni alikuwa anajisikia mgonjwa sana hata kwamba hakutaka ushirika wa watu, na wote waliondoka isipokuwa Tamari.
Sasa Amnoni akasema: ‘Kilete chakula [kitandani], nipate kula mkononi mwako [kama mgonjwa].’ Alipofanya hivyo, Amnoni alimkamata na kusema: ‘Njoo ulale nami.’ Lakini Tamari akajaribu kutoroka. Hata hivyo, Amnoni alikuwa mwenye nguvu zaidi, naye akamwingilia kinguvu. Halafu ni nini yaliyotokea? Je! jambo hilo lilifanya Amnoni ampende zaidi Tarnari?
Hapana, matokeo yake yalikuwa tofauti kinyume cha hayo. Amnoni akaanza kumchukia Tamari hata zaidi ya alivyokuwa amempenda. Kwa hiyo akamwambia: ‘Ondoka.’ Alipokataa kuondoka, yeye alimwita mtumishi wake wa kibinafsi na kumwambia hivi: ‘Mtoe mwanamke huyu kwangu na ufunge mlango.’ Walakini jambo hilo halikuishia hapo.
Tamari alirarua kanzu yake, akaweka majivu kichwani mwake, na akaenda zake akilia. Ndugu yake wa baba na mama mmoja, Absalomu, alipomwona, yeye alijua yale ambayo Amnoni alikuwa amefanya. Hilo lilimfanya Absalomu amchukie Amnoni, na akangojea alipe kisasi kwa Amnoni kwa ajili ya kumnajisi Tamari.
Miaka miwili baadaye Absalomu aliwaalika wana wote wa Mfalme Daudi waje kwenye karamu. Walakini Absalomu akawaambia hivi watumishi wake: ‘Amnoni akiisha kunywa sana, mwueni.’ Na hivyo ndivyo walivyofanya kwa amri ya Absalomu. Baada ya jambo hilo Absalomu alitoroka nchi hiyo. Kwa hiyo, unaweza kuona namna taabu nyingi ilivyotokezwa kwa sababu Amnoni hakuzuia tamaa yake ya mahaba aliyokuwa nayo kwa Tamari?—2 Samweli 13:1-38.
Uvutano mzuri ajabu uliopo kati ya wanaume na wanawake ni baraka kweli kweli, yenye kutokeza uchumba na ndoa yenye furaha. Hata hivyo, wakati tamaa za ngono hazizuiliwi, kuzaa haramu, kutoa mimba na magonjwa ya kisonono na kaswende, na taabu nyingine nyingi, mara nyingi mambo hayo yanatokea. Je! utafaidika na masimulizi ya Biblia kama hayo kwa kutafuta msaada wa Mungu uongoze vizuri tamaa za ngono?—Wagalatia 5:22, 23, NW; Wakolosai 3:8; 1 Wathesalonike 4:3-7.