Jirani Wema—Tunawahitaji
HIVI majuzi mwanamke mmoja katika Toronto, Kanada, alikwenda madukani akaacha nguo zake ambazo huziosha kila juma zikiwa zimeangikwa kwenye kamba zikauke. Alipokuwa ameondoka, nguo hizo zilianguka chini. Jirani yake kuona hivyo akaziokota akamwondolea uchafu uliozipata, akazifua tena kisha akaziangika zote tena zikauke.
Je! wewe una jirani wa namna hiyo?Jambo la kusikitisha ni kwamba siku hizi ni shida kuwapata. Siku hizi zinapatikana sana habari kama ile iliyotoka Toronto pia, juu ya mwanamke mzee ambaye mkono wake ulikwama kwenye stovu (jiko) lenye joto jingi. Alilia kuomba msaada, lakini jirani zake wakapuza vilio vyake, naye hakuokolewa mpaka siku mbili zikawa zimepita. Ikawa lazima mkono huo ukakatwe.
Kuishi katika mtaa ambako jirani wanajali kunaongeza usalama na uchangamshi kwenye maisha. Jirani wema wanatupikia vyakula tunapokuwa wagonjwa, wanarudisha watoto wetu nyumbani wanapotanga-tanga na kupotea, wanatusaidia tushinde matatizo makubwa sana na madogo, wanatununulia vitu vichache wanaponunua vyao wenyewe madukani, wanatulindia nyumba yetu tunapokuwa hatupo na kwa ujumla wanafanya maisha yapendeze zaidi wanapotuambia “Habari ya asubuhi?” kila siku. Nasi, bila shaka, tunawafanyia vivyo hivyo.
Zamani ilikuwa kawaida sana kuwa na jirani wa namna hiyo. Haikuwa shida kuwapata, kama ilivyo siku hizi. Hata siku hizi bado unaweza kuwapata sehemu za mashambani na katika miji midogo. Lakini katika miji mikubwa zaidi na sehemu zenye utajiri jirani wenye kujali wenzao wanaonekana kwa shida sana; na kwa kuwa watu walio wengi leo wanaishi katika miji mikubwa au kando za miji ya namna hiyo, watu wengi hawajaweza kuishi katika ujirani wa watu wenye kujali. Mchunguzi mmoja wa fikira za watu alisema: “Nikiishi katika nyumba ya kukodi kati ya nyumba nyingine nyingi huko Toronto, naweza kufa na nikae ndani ya nyumba hiyo miezi mingi kabla mtu ye yote hajajua nimekufa. Zamani mambo hayakuwa hivyo.” Ndivyo ilivyo kuhusu mingi ya miji mikubwa. Upande ule mwingine wa dunia mseja mwanamume kijana alikufa akiwa ndani ya nyumba ya kukodi katika mji mkubwa. Maiti yake ilipatikana baada ya kupita mwaka mmoja na nusu!
Yule mchunguzi wa fikira za watu alisema zamani haikuwa hivyo. Badiliko lililetwa na nini?