Maswali Kutoka kwa Wasomaji
■ Ni kwa sababu gani Stefano, katika Matendo 7:14, alisema kwamba kulikuwako watu 75 katika jamaa ya Yakobo walipohamia Misri, na huku andiko la Mwanzo 46:26 linasema kwamba kulikuwako 66 na andiko la Mwanzo 46:27 linataja 70?
Kunaweza kukawa maelezo kadha wa kadha. Moja ni kwamba andiko la Matendo 7:14 linategemea Septuagint Version ya Kigiriki, na jingine ni kwamba Stefano alitia ndani wake tisa wa wana wa Yakobo.
Ebu kwanza tuangalie aliyosema Stefano, kama ilivyoandikwa katika Matendo 7:14: “Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano.” Tukiwa tunakumbuka hayo tunaweza kufikiria ambayo masimulizi ya Mwanzo yanasema juu ya jamaa ya Yakobo ikihamia Misri.
Andiko la Mwanzo 46:8 linaanza hivi: “Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe.” Halafu inafuata orodha ya wazao wa Yakobo, kutia ndani baadhi ya wajukuu wake. Masimulizi hayo yanamalizia hivi: “Nafsi zote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri waliotoka viunoni mwake, bila wake za wanawe Yakobo, nafsi zote walikuwa sitini na sita. Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa nafsi wawili. Nafsi zote za nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini.”—Mwanzo 46:26,27.
Orodha ya 66 kati ya wazao wa Yakobo imeongezwa kwa njia mbalimbali. Wataalamu wengine wametia ndani wana wa Yuda, Eri na Onani na pia wajukuu wake Hesroni na Hamuli. (Mwanzo 46:12) Wengine hawakuhesabu Eri na Onani, kwa maana tayari walikuwa wamekufa wakati wa kuhamia Misri. (Mwanzo 38:6-10) Wanafunzi wengine wa Biblia wamehesabu Dina, ambaye yaelekea hakuolewa kamwe, au labda Eliabu, mjukuu wa Reubeni anayetajwa katika Hesabu 26:8. Kwa wale wazao 66 aweza kuongezwa Yakobo na pia Yusufu na wanaye wawili (hawa wa mwisho watatu wakiwa si sehemu ya waliohamia Misri). Ndivyo jumla ya 70 inavyofikiwa.
Mwanafunzi Stefano kwa hakika angekuwa anajua kwamba andiko hilo la Kiebrania lilisema kwamba 66 kati ya wazao wa jamaa ya Yakobo walihamia Misri. Basi, ni kwa nini andiko la Matendo 7:14 linamwonyesha Stefano kuwa akitumia tarakimu 75?
Waelezaji wengine wa Biblia wanadai kwamba huenda Stefano akawa alitegemeza maelezo yake juu ya tafsiri ya Kigiriki ya Septuagint ya Mwanzo 46:27. Tafsiri hiyo inatoa tarakimu ya juu kwa sababu katika mstari wa 20 inaongeza majina matano (wana watatu wa Manase na Efraimu na wajukuu wawili) wasiotajwa katika maandishi hayo ya Kiebrania. Au, ikiwa Stefano mwenyewe alikuwa akifikiria tarakimu ya Kiebrania ya 66, Luka alipoandika kitabu cha Matendo katika Kigiriki huenda akawa alionyesha tarakimu ya Septuagint, kwa kuwa tafsiri hiyo ya Kigiriki ilitumiwa kwa ukawaida.
Lakini iwe Stefano mwenyewe alisema juu ya 75 au iwe kwamba tarakimu hiyo ilitokana na tafsiri ya Kigiriki ya Mwanzo 46:27, hesabu hiyo inaweza kupatanishwa na tarakimu ya Kiebrania ya 66 kwa kuongeza wake wa wana wa Yakobo, ambao andiko la Mwanzo 46:26 linataja waziwazi hawakutiwa ndani.
Ni kwa sababu gani wake tisa peke yao ndio wangehesabiwa? Kati ya wale wana 12, mke wa Yusufu hangetiwa ndani, kwa maana alikuwa Mmisri wala hakuitwa huko na Yusufu. (Matendo 7:13-15) Na wakati wa kuhamia mke wa Yuda alikuwa amekwisha kufa. (Mwanzo 38:12) Hiyo ingeacha wake 10 tukichukua hesabu ya juu zaidi. Inawezekana kwamba mke Mwebrania wa Simeoni alikuwa amesha kufa pia, kwa maana mwanaye wa mwisho, Shauli, anaelezwa kuwa “mwana wa mwanamke Mkanaani.” (Mwanzo 46:10) Au tarakimu tisa ingaliweza kuwa sahihi ikiwa Benyamini, mwana mchanga zaidi, alikuwa angali hajaoa jamaa hiyo ilipoanza kukaa Misri. Ikiwa ndivyo, wana wa Benyamini wanaotajwa katika Mwanzo 46:21 walizaliwa baada ya uhamiaji huo lakini wanaorodheshwa kwa sababu ya sehemu ambayo wangeshiriki katika kabila hilo na taifa. (Linganisha Waebrania 7:9,10.) Kwa hiyo, wake tisa wa wana wa Yakobo wakiongezwa kwenye jumla ndogo ya 66 inayotajwa katika Mwanzo 46:26 katika maandishi ya Kiebrania, tunakuwa na jumla ya 75, kama inavyosema Septuagint na kama tusomavyo katika Matendo 7:14.
Ni wazi kwamba hata ingawa kuna njia za akili za kufahamu Matendo 7:14, na pia tarakimu katika Mwanzo sura ya 46, hatuwezi kudhania-dhania tu mambo yote. Kwa hiyo tuna sababu ya ziada ya kutazamia wakati ambao Mungu atawafufua watumishi wake wa kale, kwa maana tutaweza kujua moja kwa moja kutoka kwao mambo yote hasa juu ya masimulizi mengi ya Kimaandiko.—Yohana 5:28, 29.