Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w85 1/15 kur. 3-6
  • Mianzo ya Wafalme Katika Israeli—Vitabu Viwili vya Samweli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mianzo ya Wafalme Katika Israeli—Vitabu Viwili vya Samweli
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mfalme Aliyeshindwa na Wajibu Wake
  • Mafanikio ya Kifalme
  • “Mwana wa Daudi”
  • Matendo Yaliyobadili Historia
  • Kitabu Cha Biblia Namba 9—1 Samueli
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Mfalme wa Kwanza wa Israeli
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Waisraeli Wataka Mfalme
    Biblia—Ina Ujumbe Gani?
  • 1 Samweli—Yaliyomo
    Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
w85 1/15 kur. 3-6

Mianzo ya Wafalme Katika Israeli​—Vitabu Viwili vya Samweli

“KUMBE hamjasoma alilofanya Daudi wakati yeye na watu wake walipokuwa na njaa? Aliingia ndani ya Nyumba ya Mungu akauchukua mkate mtakatifu ale kisha akawapa watu wake, ingawa makuhani peke yao ndio wanaoruhusiwa kuula, na si mtu mwingineye yote.” (Luka 6:3, 4, The New English Bible) Kwa maneno hayo, Yesu alinyamazisha Wafarisayo fulani waliokuwa wameshitaki wanafunzi wake juu ya kuvunja Sabato kwa sababu walikuwa wamechuma nafaka chache wazile wakati wa siku ya Sabato.

Alionyesha jambo jingine pia. Masimulizi ya kihistoria juu ya Daudi na “mkate mtakatifu” yameandikwa katika kitabu cha kwanza cha Samweli. (1 Samweli 21:1-6, NEB) Kwa kuwa Yesu alitaja kitabu hicho kukanusha kipingamizi, hiyo inaonyesha alikifahamu vizuri kitabu hicho na inapendekeza kwamba hata sisi ingefaa tukifahamu vizuri. Pamoja na kitabu chenzake, yaani Samweli wa Pili, kina habari zilizokuwa za thamani kwa Yesu nazo ni zenye thamani kwetu leo.​—Warumi 15:4.

Vitabu viwili vya Samweli ni vya namna gani? Ni vitabu vya kihistoria vinavyopatikana katika Maandiko ya Kiebrania ambavyo vinaeleza kipindi cha mabadiliko katika historia ya watu wa Mungu. Kabla ya hapo, Waisraeli walikuwa wametawalwa na mfuatano wa waamuzi. Vitabu viwili hivi vinaeleza mwisho wa kipindi hicho na mwanzo wa kutawalwa na wafalme Waisraeli. Vimejawa na matukio ya kuvutia na watu wa kusisimua. Tunamkuta Samweli mwenyewe, aliyekuwa mwamuzi wa mwisho, na wale wafalme wawili wa kwanza, Sauli na Daudi. Pia tunakuta watu kadha wenye tabia zisizosahaulika: Eli mwenye huzuni, Abigaili mwenye hekima na busara, Yonathani aliye hodari lakini mwenye fadhili, vilevile Abishai na Yoabu ambao ni ndugu, wenye matendo hodari kwa ajili ya Yehova lakini wakatili katika mambo yao ya kijamaa. (Waebrania 11:32) Vitabu hivyo viwili vinafundisha kanuni ambazo zingali na maana na vinasimulia matukio yaliyoleta matokeo yenye kudumu muda mrefu juu ya watu wa Mungu, hata juu ya wanadamu wote.

Mfalme Aliyeshindwa na Wajibu Wake

Mtu wa kwanza kupakwa mafuta na Yehova awe mfalme juu ya Israeli alikuwa Sauli. Alianza vizuri lakini baadaye akashindwa kuonyesha tegemeo linalofaa juu ya Yehova alipoelekeana na shambulio lililokaribia kufanywa na Wafilisti. Kwa hiyo, Samweli alimwambia kwamba wanaye hawangerithi uufalme. Badala yake, akasema Samweli, “Yehova kwa uhakika atajitafutia mwanamume anayekubalika kwa moyo wake; na Yehova atamwagiza kuwa kiongozi juu ya watu wake.” (1 Samweli 13:13, 14, NW) Lakini, Sauli aliendelea kuwa mfalme muda wote uliobaki wa maisha yake.

Baadaye, mfalme huyo wa kwanza aliamriwa akafanye vita ya kuadhibu Waamaleki. Sauli hakutimiza kabisa maagizo ya Yehova na hivyo akajiletea hasira zaidi. Samweli anajisikia akichochewa kusema: “Je! [Yehova] huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawasawa na kuitii sauti ya [Yehova]? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu.” (1 Samweli 15:22) Hiyo ni kanuni ambayo ingali ya maana kwa wale wanaotumikia Yehova katika vyeo vya uongozi. Kwa sababu Sauli hakuwa mtiifu, Samweli nabii aliendelea kusema: “Kwa kuwa umelikataa neno la [Yehova], yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.” (1 Samweli 15:23) Baadaye, Sauli alionyesha ni kwa kadiri gani alikuwa ameiacha ibada safi wakati alipoendea mtu mwenye kupashana habari na roho waovu.​—1 Samweli 28:8-25.

Mafanikio ya Kifalme

Yule aliyerithi Mfalme Sauli alikuwa Daudi, mwana wa Yese. Daudi alikuwa tofauti na Sauli. Katika ujana wake, alikuwa ameonyesha kumtegemea Yehova alipoua Goliathi, jitu la Kifilisti. Halafu, alipolazimika kukimbia aokoe uhai wake kwa sababu ya wivu wa Sauli, bado aliendelea kutii Yehova katika mambo yote. Zaidi ya mara moja, Daudi angaliweza kuua Sauli. Lakini alijizuia, akangojea wakati wa Yehova aliomwekea awe mfalme. Ni wakati wa kipindi hicho chenye magumu Ahimeleki kuhani alimpa mkate wa wonyesho aule katika kisa walichotajiwa Wafarisayo na Yesu.

Baada ya muda fulani Sauli akafa na Daudi akaanza kutawala. Lakini kwa mara ya kwanza ni kabila lake mwenyewe tu, Yuda, lililomkubali. Makabila yale mengine yaliendelea kufuata mwana wa Sauli aliyebaki akiwa hai, Ishboshethi. Hata hivyo, Daudi hakuonyesha hali ya kutaka kujilipa kisasi kuelekea mshindani wake. Wakati Ishboshethi alipouawa mwishowe, Daudi aliua waliomwua. Na wakati Abneri, jemadari mkuu wa Ishboshethi, alipouawa, yeye aliagiza kuwe na maombolezo ya watu wote. (2 Samweli 3:31-34; 4:9-12) Unyenyekevu huo, subira, ustahimilivu na kumtegemea Yehova ni mambo yanayohitajiwa na watumishi wa Yehova katika kipindi cho chote.

“Mwana wa Daudi”

Daudi alipokuja mwishowe kuwa mfalme juu ya taifa lililounganishwa tena, moja la mawazo yake ya kwanza lilikuwa kujenga makao ya kudumu kwa ajili ya sanduku la agano, ambalo lilikuwa mfano wa kuwapo kwa Yehova katika Israeli. Yehova hakukubali jambo hilo, lakini kwa kutambua uaminifu mwingi ajabu wa Daudi alifanya agano zuri sana pamoja naye: “Nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.”​—2 Samweli 7:16.

Hivyo Daudi akawa kiunganishi katika ukoo mrefu, usiovunjika ambao ulianzia Adamu, ukapita kwa Abrahamu, Isaka, Yakobo na Yuda mpaka kwa Masihi aliyeahidiwa. (Mwanzo 3:15; 22:18; 26:4; 49:10) Wakati Masihi angefika mwishowe, angekuwa mzao wa Daudi. Yesu alikuwa mzao huyo, kwa upande wa baba yake mlezi na hata kwa upande wa mama yake. (Mathayo 1:1-16; Luka 3:23-38) Katika masimulizi ya Injili, anaitwa mara kwa mara “Mwana wa Daudi.”​—Marko 10:47, 48.

Akiwa ndiye “Mwana wa Daudi” aliye rasmi, Yesu alikuwa mrithi wa Daudi. Yeye alirithi nini? Malaika Gabrieli alimwambia Mariamu: “Huyo [Yesu] atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:32, 33) Daudi aliunganisha tena watu wote wa Mungu wakawa ufalme mmoja, kama kinavyoeleza kitabu cha Samweli wa Pili. Kwa hiyo Yesu alirithi utawala juu ya Israeli wote.

Angalia, pia, uhakika mwingine juu ya Daudi kama unavyoripotiwa na kitabu cha kwanza cha Samweli: “Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese.” (1 Samweli 17:12) Maneno hayo si maelezo ya historia ya kupendeza tu isiyo na maana. Masihi, pia, akiwa “Mwana wa Daudi,” alipaswa kuzaliwa Bethlehemu: “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” (Mika 5:2) Bila shaka, Yesu alitimiza takwa hilo la Umasihi.​—Mathayo 2:1, 5, 6.

Matendo Yaliyobadili Historia

Mengi ya matendo ya ujasiri ya Daudi yalikuwa na matokeo ya kudumu. Kwa mfano, Daudi alikulia mahali palipokuwa maili chache tu kutoka Yerusalemu. Alipokuwa mvulana mji huo wa Yerusalemu ulikuwa mikononi mwa Wayebusi, na bila shaka Daudi alivutiwa mara nyingi na mahali ulipokuwa. Palikuwa mahali palipoelekea kutoweza kushindwa na mashambulio yo yote, juu ya sehemu iliyochongoka yenye mwinamo wa miamba, iliyoitwa Mlima Sayuni. Sasa, yeye akiwa mfalme, alikuwa katika cheo cha kuchukua hatua badala ya kuvutiwa macho tu. Kitabu cha pili cha Samweli kinaeleza wazi sana namna “Daudi akachukua hatua ya kuteka ngome ya Sayuni, yaani, Mji wa Daudi,” ijapokuwa wakaaji Wayebusi walifanya madharau. (2 Samweli 5:7, NW) Hivyo ndivyo Yerusalemu ulivyoanza kujulikana sana katika historia ya ulimwengu kama vile umekuwa​—ukikaziwa-kaziwa fikira na kuacha-acha kukaziwa​—tangu wakati huo.

Mji huo ukawa ndio mji wa kifalme wa Daudi na ukaendelea kuwa mji mkuu wa wafalme wa Mungu wa kidunia kwa mamia ya miaka. Katika karne ya kwanza, “Mwana wa Daudi,” Yesu, alihubiri huko. Ni katika Yerusalemu Yesu aliingia akiwa amepanda punda ili ajitokeze akiwa Mfalme kwa Wayahudi. (Mathayo 21:1-11, Mt 21:42–22:13; Yohana 7:14) Na ni nje ya malango ya Yerusalemu alipotolea uhai wake kwa ajili ya wanadamu, kisha akafufuliwa na kupaa akaingia mbinguni, akangoje kwa subira​—kama Daudi alivyofanya kabla yake​—ili Yehova aseme ni wakati gani anapopaswa kuanza kutawala akiwa Mfalme.​—Zaburi 110:1; Matendo 2:23, 24, 32, 33; Waebrania 13:12.

Kutawala kwa Daudi katika Yerusalemu kunatukumbusha pia kwamba mzao wake, Yesu, anatawala sasa pia katika Yerusalemu, “Yerusalemu wa mbinguni.” (Waebrania 12:22) Na mahali ulipo Yerusalemu wa mbinguni huo panaitwa “Mlima Sayuni.” Hiyo inatukumbusha ile sehemu iliyochongoka yenye miamba ambapo ndipo mji ule wa kwanza ulikuwa.​—Ufunuo 14:1.

Kuelekea mwisho wa utawala wake, Daudi aliendesha mpango haramu wa kuhesabu watu wa taifa. Yehova alitoa adhabu kwa kulipiga taifa, na yule malaika mwenye kuleta pigo akasimama mwishowe kwenye sakafu ya kupuria ya Myebusi mwenye shamba jina lake Arauna. Daudi alinunua shamba hilo kutoka kwa Arauna kisha akamjengea Yehova madhabahu hapo. (2 Samweli 24:17-25) Tendo hilo, pia, lilileta matokeo ya muda mrefu. Kipande hicho cha ardhi kikawa ndipo mahali pa hekalu la Sulemani, na mwishowe, pa hekalu lililojengwa upya. Hivyo, kwa karne nyingi palikuwa ndipo mahali pakuu ulimwenguni pa ibada ya kweli. Yesu mwenyewe alihubiri katika hekalu la Herode, lililojengwa karibu pia na mahali ambapo zamani palikuwa sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.​—Yohana 7:14.

Ndiyo, vitabu viwili vya Samweli vinatujulisha kwa watu halisi na kueleza kanuni za maana. Vinaonyesha sababu gani mfalme wa kwanza wa Israeli alishindwa kutimiza wajibu wake na kwa sababu gani mfalme wa pili wa taifa hilo alipata mafanikio makubwa sana. Vinatueleza mambo ya kipindi cha maana katika historia, mianzo ya utawala wa kifalme wa mwanadamu kati ya watu wa Mungu. Tunaona Yerusalemu ukiwa mji mkuu wa wafalme hao na kuona ununuzi wa mahali ambapo kwa muda wa karne kadha pangekuwa mahali pakuu ulimwenguni pa ibada ya kweli. Na tunajifunza kiishara cha maana cha kusaidia kumtambua Masihi aliyekuwa anakuja. Angepaswa kuwa “Mwana wa Daudi.”

Hivyo ni vitabu vya maana kweli kweli. Inampasa kila Mkristo ajisomee vitabu hivyo yeye mwenyewe.

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

“Kujiendesha Kama Nabii”

Biblia ina maana gani inaposema. “Roho ya Mungu ikaja kuwa juu [ya Sauli], ndiyo, yeye, naye akazidi kutembea na kuendelea kujiendesha kama nabii.”—1 Samweli 19:23, NW.

Wakati manabii wa Yehova walipokuwa wakitangaza ujumbe wa Mungu, walisema kwa uongozi wa roho takatifu ambayo ‘iliwajaza uwezo’ na bila shaka ikawaongoza kusema kwa juhudi na hali ya kujisikia isiyokuwa ya kawaida. (Mika 3:8; Yeremia 20:9) Labda njia yao ya kujiendesha ilionekana ya ajabu​—pengine hata ya kipumbavu​—machoni pa watu. Hata hivyo, ilipokwisha kuthibitishwa kwamba walikuwa wakinena yaliyotoka kwa Yehova, ujumbe wao ulichukuliwa kwa uzito na watu wenye kumwogopa Mungu.​—Linganisha 2 Wafalme 9:1-13.

Hivyo, katika pindi hii Sauli alianza kutenda kwa njia isiyo ya kawaida, ikakumbusha watazamaji juu ya mtetemeko ambao nabii alikuwa nao akiwa karibu kutangaza ujumbe kutoka kwa Yehova. Alipokuwa angali akitenda kwa njia hiyo, alivua mavazi yake akalala uchi usiku mzima. (1 Samweli 19:23, 24) Huenda kusudi likawa alitaka kuonyesha alikuwa mtu tu asiye na uwezo au mamlaka ya kifalme wakati alipotenda kinyume cha makusudi ya Yehova Mungu. Katika pindi moja iliyotangulia, wakati Mfalme Sauli ‘alipojiendesha kama nabii’ alijaribu kuua Daudi kwa mkuki.​—1 Samweli 18.10, 11.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

‘Roho Mbaya Kutoka kwa Yehova’

“Basi, roho ya [Yehova] ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa [Yehova] ikamsumbua.” (1 Samweli 16:14) Wewe unajua maana ya hilo?

Haitupasi kuelewa kwamba Yehova alituma kwa uhalisi roho mbovu ikasumbue Sauli. Bali, wakati Yehova alipoondoa roho takatifu yake, Sauli alipagawa na roho mbaya, au tamaa ya ndani yenye kumhimiza afanye ubaya. (Linganisha Mathayo 12:43-45.) Kwa sababu gani Yehova anatajwa kuwa chanzo cha hiyo roho mbaya? Kwa sababu alifanya iwezekane Sauli aingiwe na tamaa au vichocheo vyenye kumhimiza afanye mabaya wakati alipoondoa roho takatifu yake. Hiyo “roho mbaya” iliondoa amani ya akili ya Sauli na, pindi kwa pindi, ikamfanya atende kipumbavu.

[Picha katika ukurasa wa 4]

GOLIATHI

DAUDI

SAULI

SAMUELI

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki