Maisha na Huduma ya Yesu
Mtoto wa Ahadi
BADALA ya kurudi Nazareti, Yusufu na Mariamu wanabaki Bethlehemu. Na Yesu anapokuwa na siku nane wanamtahiri, kulingana na amri ya Sheria ya Mungu. Ni wazi pia ni desturi kumpa mtoto mvulana jina lake siku ya nane. Kwa hiyo wanamwita mtoto wao Yesu, sawa na malaika Gabrieli alivyokuwa ameelekeza mapema.
Zaidi ya mwezi mmoja unapita, na Yesu ana umri wa siku 40. Sasa wazazi wake wanampeleka wapi? Kwenye hekalu katika Yerusalemu, ambalo liko maili chache tu kutoka mahali wanapoishi. Kulingana na Sheria ya Mungu aliyompa Musa, siku 40 baada ya kuzaa mwana, mama anapaswa kutoa sadaka ya utakaso hekaluni.
Ndivyo anavyofanya Mariamu. Lakini analeta ndege wawili kuwa sadaka yake. Jambo hilo linatuonyesha hali ya kiuchumi ya Yusufu na Mariamu. Sheria ya Musa inaonyesha kwamba kondoo-mume mchanga, ambaye ni mwenye thamani zaidi ya ndege, anapaswa kutolewa sadaka. Lakini ikiwa mama hangeweza, njiwa au ua wawili wangetosha.
Huko hekaluni mwanamume mmoja mzee anamchukua Yesu mikononi mwake. Jina lake ni Simeoni. Mungu amekwisha kumfunulia kwamba hatakufa kabla hajamwona Kristo, au Masihi wa Yehova aliyeahidiwa. Simeoni anapokuja hekaluni siku hiyo, anaelekezwa na roho takatifu kwenda kwenye mtoto huyu aliyeshikwa na Yusufu na Mariamu.
Simeoni akiwa amemchukua Yesu mikononi anamshukuru Mungu, akisema: ‘Umetimiza ahadi yako, kwa maana nimeona kwa macho yangu njia ya wokovu uliyotayarisha.’ Yusufu na Mariamu wanastaajabu kusikia hayo. Halafu Simeoni anawabariki na kumwambia Mariamu kwamba mwanaye “amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli” na kwamba huzuni, kama upanga mkali, itachoma nafsi yake.
Katika pindi hiyo yupo nabii wa kike mwenye miaka 84 anayeitwa Ana. Kwa kweli, hakosi kamwe hekaluni. Saa iyo hiyo anakaribia na kuanza kumtolea Mungu shukrani na kusema juu ya Yesu kwa wote watakaosikiliza.
Matukio hayo hekaluni yamefanya Yusufu na Mariamu wafurahi kama nini! Hakika, jambo hilo linawathibitishia kwamba mtoto huyo ndiye Mwahidiwa wa Mungu. Luka 2:21-38; Mambo ya Walawi 12:1-8.
◆ Kwa wazi ni wakati gani ilikuwa desturi kumpa mtoto mvulana Mwisraeli jina lake?
◆ Mama Mwisraeli alipaswa kufanya nini mwanaye alipokuwa na umri wa siku 40, na kutimizwa kwa takwa hilo kulionyeshaje ilivyokuwa hali ya kiuchumi ya Mariamu?
◆ Ni nani aliyetambua cheo cha Yesu katika pindi hiyo, na jinsi gani?