Maisha na Huduma ya Yesu
Bidii kwa Ajili ya Ibada ya Yehova
BAADA ya kuhudhuria arusi katika Kana, Yesu anasafiri kwenda Kapernaumu, mji ulio karibu na Bahari ya Galilaya. Yuko pamoja na wanafunzi wake, mama yake na ndugu zake, ambao ni Yakobo, Yusufu, Simoni, na Yuda. Lakini, kabla ya kufunga safari hiyo huenda wakawa kwanza wamesimama kidogo nyumbani kwa Yesu katika Nazareti ili jamaa hiyo ichukue vitu ambavyo wangehitaji.
Lakini sababu gani Yesu anaenda Kapernaumu, badala ya kuendelea na huduma yake Kana, katika Nazareti, au mahali pengine katika vilima vya Galilaya? Kwanza, Kapernaumu ni mji ulio mahali panapojulikana na watu wengi zaidi na kwa wazi ni mkubwa zaidi. Pia, wengi wa wanafunzi ambao Yesu amejipatia karibuni wanaishi ndani au karibu ya Kapernaumu, kwa hiyo hawatalazimika kuondoka makwao wapokee mazoezi kutoka kwake.
Wakati wa kukaa Kapernaumu, Yesu anafanya mambo mazuri ajabu, kama vile yeye mwenyewe anavyoshuhudia miezi kadha baadaye. Lakini baada ya muda mfupi Yesu na wenzake wanaanza safari tena. Ni wakati wa masika, nao wanaelekea Yerusalemu wakahudhurie Sikukuu ya Kupitwa ya mwaka 30 W.K. Wakiwa huko, wanafunzi wake wanaona jambo fulani kuhusu Yesu ambalo labda hawajapata kuliona hapo kwanza.
Kulingana na Sheria ya Mungu, Waisraeli wanatakwa watoe dhabihu za wanyama. Kwa hiyo, ili kuwasaidia Waisraeli hao wasiende mbali, wafanya biashara katika Yerusalemu wanauza wanyama au ndege kwa kusudi hilo la kutolewa wawe dhabihu. Lakini wao wanawauza ndani kabisa ya hekalu, nao wanawapunja watu kwa kuwauzia kwa bei ya juu mno.
Kwa kujawa na ghadhabu, Yesu anafanya kikoto cha kamba na kuwafukuzia nje wauzaji hao. Anazimwaga sarafu za wavunja-fedha na kuzipindua meza zao. “Viondoeni vitu hivi hapa!” anawapaazia sauti wale wanaowauza njiwa. “Acheni kuifanya nyumba ya Baba yangu nyumba ya biashara ya bidhaa!”
Wanafunzi wa Yesu wanapoona hilo, wanaukumbuka unabii unaomhusu Mwana wa Mungu: “Bidii kwa ajili ya nyumba yako itanila mimi kabisa.” Lakini Wayahudi wanauliza: “Wewe una ishara gani ya kutuonyesha, kwa kuwa unatenda mambo haya?” Yesu anajibu: “Bomoeni hekalu hili, na katika muda wa siku tatu nitaliinua.”
Wayahudi wanadhani Yesu anasema juu ya lile hekalu halisi, lakini yeye anasema juu ya hekalu la mwili wake. Halafu miaka mitatu baadaye wanafunzi wake wanakumbuka usemi huo wake anapofufuliwa kwa wafu. Yohana 2:12-22; Mathayo 13:55; Luka 4:23.
◆ Baada ya arusi katika Kana, Yesu anasafiri kwenda wapi na wapi?
◆ Kwa sababu gani Yesu ana ghadhabu, naye anafanya nini?
◆ Wanafunzi wa Yesu wanakumbuka nini wanapoona vitendo vyake?
◆ Yesu alisema nini juu ya “hekalu hili,” naye alimaanisha nini?