Sura 16
Bidii kwa Ajili ya Ibada ya Yehova
NDUGU wenye mzazi mmoja na Yesu—wale wana wengine wa Mariamu—ni Yakobo, Yusufu, Simoni, na Yuda. Kabla ya hawa wote kufunga safari pamoja na Yesu na wanafunzi wake kwenda Kapernaumu, jiji moja lililoko karibu na Bahari ya Galilaya, labda watua katika kao lao katika Nazareti ili familia hiyo ichukue vitu watakavyohitaji.
Lakini sababu gani Yesu aenda Kapernaumu badala ya kuendelea na huduma yake katika Kana, katika Nazareti, au mahali penginepo katika vilima vya Galilaya? Kwanza, Kapernaumu ni jiji lililoko mahali panapojulikana na watu wengi zaidi na kwa wazi ni kubwa zaidi. Pia, wengi wa wanafunzi ambao Yesu amejipatia karibuni wanaishi katika au karibu na Kapernaumu, kwa hiyo hawatalazimika kuondoka kwao ili wapokee mazoezi kutoka kwake.
Wakati wa kukaa kwake Kapernaumu, Yesu afanya kazi za ajabu, kama vile yeye ashuhudiavyo miezi kadhaa baadaye. Lakini upesi Yesu na waandamani wake wako mwendoni tena. Ni masika, nao waenda Yerusalemu wakahudhurie Sikukuu ya Kupitwa ya 30 W.K. Wakiwa huko, wanafunzi wake waona jambo fulani kuhusu Yesu ambalo labda hawajapata kuliona hapo kwanza.
Kulingana na Sheria ya Mungu, Waisraeli watakwa watoe dhabihu za wanyama. Kwa hiyo, ili kuwasaidia, wafanya biashara katika Yerusalemu wauza wanyama au ndege kwa kusudi hilo. Lakini wao wawauzia ndani kabisa ya hekalu, nao wawapunja watu kwa kuwauzia kwa bei ya juu mno.
Kwa kujawa na ghadhabu, Yesu afanya kikoto cha kamba na kuwafukuzia nje wauzaji hao. Azimwaga sarafu za wavunja-fedha na kuzipindua meza zao. “Viondoeni vitu hivi hapa!” awapaazia sauti wale wanaouza njiwa. “Acheni kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara ya bidhaa!”
Wanafunzi wa Yesu waonapo hilo, waukumbuka unabii unaomhusu Mwana wa Mungu: “Bidii kwa ajili ya nyumba yako itanila mimi kabisa.” Lakini Wayahudi wauliza: “Wewe una ishara gani ya kutuonyesha, kwa kuwa watenda mambo haya?” Yesu ajibu: “Bomoeni hekalu hili, na katika muda wa siku tatu mimi nitaliinua.”
Wayahudi wadhani Yesu asema juu ya lile hekalu halisi, na hivyo wauliza: “Hekalu hili lilijengwa kwa miaka arobaini na sita, nawe utaliinua kwa siku tatu?” Lakini Yesu asema juu ya hekalu la mwili wake. Na miaka mitatu baadaye, wanafunzi wake wakumbuka usemi huo wake afufuliwapo kutoka kwa wafu. Yohana 2:12-22; Mathayo 13:55; Luka 4:23, NW.
▪ Baada ya arusi katika Kana, Yesu asafiri kwenda mahali gani?
▪ Kwa nini Yesu ana ghadhabu, naye afanya nini?
▪ Wanafunzi wa Yesu wakumbuka nini waonapo vitendo vyake?
▪ Yesu asema nini juu ya “hekalu hili,” naye amaanisha nini?