Miujiza Ambayo Yesu Alifanya Katika Mji Alimokaa
JE! WEWE ungefurahia kuona wapendwa wagonjwa wakiponywa? Je! ungesisimuka kwa kuona masikio ya viziwi yakizibuliwa, kusikia ulimi wa babu ukiimba, kuona macho ya vipofu yakifunguliwa na hata kuona wafu wakifufuliwa? Ungefurahi? Lakini wasema hilo haliwezekani? Hata hivyo limepata kutokea wakati fulani uliopita!
Zaidi ya miaka 1,900 iliyopita alikuwako mwanamume mmoja aliyefanya miujiza kama hiyo katika nchi ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Israeli. Jina lake alikuwa Yesu. Biblia yatoa habari za kuonekana hadharani kwa Yesu katika jimbo hilo, ikisema: ‘“Akapanda chomboni, akavuka [Bahari ya Galilaya], akafika mjini kwao.”—Mt. 9:1.
Lakini ni mji upi ambamo Yesu alikaa?
JINSI MJI ALIMOKAA YESU UNAVYOWEZA KUJULIKANA
Mji huo ulikuwa karibu na bahari, kwa maana Yesu alipotoka mashuani aliuingia mji huo. Basi, je! Yesu alikaa Bethlehemu? Huko ndiko alikozaliwa. Lakini huo ungewezaje kuwa ndio mji alimokaa, na hali Bethlehemu hauko karibu na Bahari ya Galilaya? Uko karibu maili 60 (kilomita 96) kutoka bahari hiyo.
Basi, je! mji alimokaa Yesu ulikuwa Nazareti? Huko ndiko Yesu alikokulia akawa seremala. (Luka 4:16; Yohana 1:45; Marko 6:3) Lakini hata Nazareti hauko karibu na bahari. Ni wazi kwamba mji wa kisasa uitwao En Nasira ndio uliokuwa Nazareti ya kale, na ni karibu mwendo wa saa tano kutoka Bahari ya Galilaya.
Karibu na wakati Yesu alipoanza kuhubiri, alirudi Nazareti akatoa hotuba katika sinagogi la mji huo. Lakini, watu wa huko walikasirika, wakamtoa Yesu mjini kwa haraka wakajaribu kumwua. Lakini Yesu aliponyoka. (Luka 4:16-30) Biblia yaeleza kwamba Yesu ‘alikuja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani,’ baada ya kulazimishwa kuondoka Nazareti.—Mt. 4:13.
Naam, Kapernaumu, ambako Yesu alikaa kando ya bahari, ndiko kulikokuwa “mjini kwao.”
MAHALI ILIKOFANYIWA MIUJIZA MINGI
Yesu aliita wanafunzi wanne wake wa kwanza wamfuate alipokuwa akitembea kando ya bahari karibu na Kapernaumu. Walikuwa Simoni Petro na ndugu yake Andrea, na Yakobo na ndugu yake Yohana. Yesu aliwaambia hivi: “Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” Wote watano waliingia Kapernaumu.—Marko 1:16-21.
Wakiwa katika mji huo Yesu aliingia katika sinagogi akaponya mtu mwenye mashetani. Biblia inasema: “Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana.” (Marko 1:22-29) Kutokana na maelezo hayo twapata habari kwamba Petro na Andrea sasa walikuwa wakiishi Kapernaumu, walikohamia baada ya kutoka Bethsaida.—Yohana 1:44.
Mama-mkwe wa Petro, ambaye inaelekea alikuwa akiishi na Petro na Andrea, alikuwa mgonjwa homa. Kwa hiyo Yesu akamponya. Masimulizi ya Biblia yaendelea kusema hivi: “Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi.”—Marko 1:30-34.
Lo! huo ulikuwa ushuhuda mzuri namna gani kwa watu hao wote wa Kapernaumu! Waliona kwa macho yao wenyewe miujiza mingi iliyofanywa na Yesu.
Pengine Yesu alikaa nyumbani kwa Petro na Andrea alipokuwa akiishi Kapernaumu. Ikiwa ndivyo, Yesu alikuwa nyumbani kwao wakati unaotajwa na Biblia baadaye: “Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.”—Marko 2:1.
Watu waliposikia Yesu amerudi, walimiminika nyumbani hapo. Walisongamana sana hata wakaziba mlango na kujaa sehemu za nje. Mambo yakawa tayari kwa tukio la ajabu kweli kweli. Biblia yasema: “Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.”
Yesu alifanya nini? Alikasirika? Hata! Alishangazwa sana na imani yao, akamwambia mwenye kupooza: “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.” Ebu wazia hilo! Yesu angeweza kweli kusamehe watu dhambi zao?
Viongozi wa dini waliokuwako hawakudhani hivyo, naye Yesu alijua walivyokuwa wakifikiri. Kwa hiyo akasema: “Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote.”—Marko 2:2-12.
Kwa wazi mtu huyo aliponywa kwa uwezo wa Mungu. Lakini baadaye Yesu alifanya mwujiza wa kustaajabisha zaidi. Binti ya Yairo, afisa-msimamizi wa sinagogi la hapo Kapernaumu, aliugua akafa. Lakini Yesu alikubali kwenda nyumbani kwa mtu huyo alipoombwa asaidie. Biblia yasema: “[Yesu] akamshika mkono kijana, akamwambia . . . Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu.”—Marko 5:41, 42.
Bila shaka watu hao wa Kapernaumu walikuwa na sababu za kutosha ili waweze kukubali Yesu ni Mwana wa Mungu! Lakini ni wachache tu waliofanya hivyo. Wengi wao walifikiria faida ambazo wangeweza kujipatia wenyewe tu.
HIYO INA MAANA GANI KWETU LEO?
Mji wa Kapernaumu hauko tena. Magofu yake ni ya maili moja kando kando ya pwani ya kaskazini ya Bahari ya Galilaya. Linalopendeza ni kwamba, magofu ya sinagogi, yanayopendeza zaidi ya yote yaliyokwisha kugunduliwa yamechimbuliwa huko. Ingawa sinagogi hilo lilikuwako karne ya pili au ya tatu, inafikiriwa kwamba lilijengwa katika uwanja ambao sinagogi fulani ambamo Yesu mwenyewe alihubiri lilikuwa limejengwa. Kwa hiyo, magofu hayo ni kumbukumbu la miujiza mingi aliyofanya Yesu “mjini kwao.”
Ni kweli kwamba mapozo na ufufuo alioufanya Yesu katika Kapernaumu ulifaidi watu kwa muda tu, kwa maana watu hao waliugua tena na kufa mwishowe. Hata hivyo Yesu alihakikisha jambo moja—alihakikisha kwamba watu wanaweza kurudishiwa afya na hata uzima wenyewe. Kwa hiyo tuna msingi imara kuamini kwamba Yesu aweza kufanya katika dunia nzima mambo aliyoyafanya kidogo, kwa maana sasa amefufuliwa akatawazwa awe mfalme wa Mungu wa kimbinguni. Lakini kweli atatumia uwezo wake kwa njia hiyo?
Yesu mwenyewe ametuahidi. Alisema: “Saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka.” (Yohana 5:28, 29) Je! waamini hilo? Ikiwa waamini, usiwe kama wale wakaaji wa Kapernaumu walioona lakini wakakataa kuwa wafuasi wa Yesu. Badala yake, na uongozwe na moyo wenye kuthamini uwapende na kuwatumikia Yesu na Baba yake wa mbinguni.—Mt. 11:23, 24