Maisha na Huduma ya Yesu
Wanafunzi Wanne Waitwa
BAADA ya lile jaribio la kumuua Yesu katika Nazareti mji wa kwao, yeye anahamia mji wa Kapernaumu karibu na Bahari ya Galilaya. Jambo hilo linatimiza unabii mwingine wa Isaya. Huo ndio uliotabiri kwamba watu wa Galilaya wenye kukaa karibu na bahari wangeona nuru kubwa.
Yesu anapoendesha kazi yake ya kuchukua nuru kwa kuhubiri Ufalme hapa, anakuta wanne wa wanafunzi wake. Hao walikuwa wamesafiri pamoja naye mapema kidogo lakini wakarudia biashara yao ya uvuvi wa samaki waliporejea na Yesu kutoka Yudea. Inaelekea kuwa Yesu sasa anawatafuta, kwa maana ni wakati wa kuwa na wasaidiaji wa kawaida wasioyumbayumba ambao anaweza kuzoeza waiendeshe huduma akiisha kwenda zake.
Kwa hiyo Yesu anapotembea kandokando na kumwona Simoni Petro na wenzi wake wakisafisha nyavu zao, anawaendea. Anapanda na kuingia katika mashua ya Petro na kumwomba asonge ndani zaidi kutoka nchi kavu. Wanapokuja nchi kavu umbali fulani kutoka hapo, Yesu anaketi mashuani na kuanza kuwafundisha makutano wakiwa ufuoni.
Baadaye, Yesu anamwambia Petro hivi: “Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.”
“Bwana mkubwa,” Petro anajibu, “tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.”
Nyavu zinaposhushwa, umati mkubwa sana wa samaki wananaswa hivi kwamba nyavu zinaanza kukatika. Wanaume hao wanafanya haraka kuwapungia mkono wenzao walio katika mashua ya karibu ili waje wawasaidie. Upesi mashua zote mbili zinajawa na samaki wengi sana hivi kwamba zinaanza kuzama, Kuona hivyo, Petro anajitupa chini mbele ya Yesu na kusema: “Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.”
“Usiogope,” Yesu anajibu. “Tangu sasa utakuwa ukivua watu.”
Yesu anamwalika pia Andrea ndugu ya Petro. “Njoni mnifuate,” anawahimiza, “nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” Wavuvi wenzao Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wanapewa mwaliko uo huo, nao pia wanaitikia bila kusitasita. Kwa hiyo hao wanne wanaacha biashara yao ya kuvua samaki na kuwa wafuasi wanne wa kwanza wenye kumfuata Yesu kwa ukawaida, bila kuyumbayumba. Luka 5:1-11; Mathayo 4:13-22; Marko 1:16-20; Isaya 9:1, 2.
◆ Kwa sababu gani Yesu anawaita wanafunzi wake wamfuate, nao ni akina nani?
◆ Ni muujiza gani unaomwogopesha sana Petro?
◆ Ni uvuvi wa namna gani ambao Yesu anaalika wanafunzi wake wafanye?