Maisha na Huduma ya Yesu
Imani Kuu ya Afisa wa Jeshi
WAKATI Yesu anapomaliza Mahubiri ya Mlimani yake, anafikia karibu nusu ya kituo cha huduma yake ya peupe. Hiyo inamaanisha yeye ana mwaka mmoja na miezi tisa tu hivi inayobaki amalize kazi yake duniani.
Sasa Yesu anaingia mji wa Kapernaumu, ambapo ni kama makao ya kuendeshea utendaji wake. Akiwa kule wanaume wazee Wayahudi wanamfikia wakiwa na ombi fulani. Wao wametumwa na afisa mmoja katika jeshi la Roma ambaye ni Mtaifa.
Mtumishi mpendwa wa afisa huyo wa jeshi yuko karibu kufa kutokana na ugonjwa mzito, naye anataka Yesu aponye mtumishi wake. Wayahudi wanamsihi kwa bidii kwa ajili ya afisa yule: “Amestahili huyo umtendee neno hili,” wao wanasema, “maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.”
Bila kusita, Yesu anaondoka pamoja na wanaume hao. Lakini, wanapofika karibu, yule afisa wa jeshi anatuma rafiki wakaseme: “Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako.”
Hayo ni maneno ya unyenyekevu kama nini kwa afisa ambaye amekuwa na desturi ya kutolea wengine maagizo! Lakini labda yeye anafikiria Yesu pia, akitambua kwamba desturi inamkataza Myahudi kuwa na uhusiano wa kirafiki pamoja na watu wasio Wayahudi. Hata Petro alisema: “Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lile lingine wala kumwendea.”
Labda kwa sababu hataki Yesu apatwe na matokeo mabaya ya kuvunja desturi hiyo, afisa yule anamwagiza rafiki zake wakamwombe hivi: “Sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivyo, hufanya.”
Basi, wakati Yesu anaposikia hilo anastaajabu. “Nawaambia,” yeye anasema, “hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii.” Baada ya kuponya mtumishi wa afisa huyo, Yesu anatumia pindi hiyo kusimulia jinsi watu wasio Wayahudi wenye imani watakavyopendelewa kupewa baraka zinazokataliwa na Wayahudi wasio na imani.
“Wengi,” Yesu anasema, “watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”
“Wana wa Ufalme . . . [wanaotupwa] katika giza la nje,” ni Wayahudi wa asili wasioikubali nafasi iliyotolewa kwao kwanza ya kuwa watawala pamoja na Kristo. Ibrahimu, Isaka, na Yakobo wanafananisha mpango wa Mungu wa Ufalme. Hivyo Yesu anasimulia jinsi watu wa Mataifa watakavyokaribishwa waegemee kana kwamba ingekuwa penye meza ya kimbingu, “katika ufalme wa mbinguni.” Luka 7:1-10; Mathayo 8:5-13; Matendo 10:28.
◆ Kwa sababu gani Wayahudi walisihi kwa ajili ya afisa wa kijeshi Mtaifa?
◆ Huenda ikawa ni kwa sababu gani afisa yule alimwomba Kristo asiingie nyumbani mwake?
◆ Yesu alimaanisha nini kwa maneno yake ya kumalizia?