Ripoti ya Watangazaji Ufalme
Kuungana Tena kwa Furaha Katika Brazili
WAMISIONARI 63 kati ya wale 67 waliozoezwa katika Gileadi ambao sasa wanatumikia katika Brazili walikutanika katika afisi ya tawi na wakapigwa picha hii ya kihistoria. Kuungana tena hivi kwa furaha kulitukia katika Novemba 18, 1986, wakati wa ziara ya A. D. Schroeder, mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York.
Miaka 41 iliyopita wakati wa tarehe inayokaribia sana kulingana na hiyo—Novemba 17, 1945—ndipo wanafunzi wawili waliohitimu katika darasa la kwanza la Shule ya Mnara wa Mlinzi na Biblia ya Gileadi walipokuja Brazili. Kwa mmoja wao, Charles Leathco (nyuma, kushoto kutoka katikati), huku kulikuwa kuungana tena kwa njia ya pekee kwa sababu yeye pamoja na mgeni Charlotte Schroeder walikuwa katika darasa moja katika Gileadi, na Ndugu Schroeder alikuwa mmoja wa walimu wao.
Tangu darasa hilo la kwanza, jumla ya wamisionari 258 wamekuja Brazili. Miongoni mwao walikuwako Wabrazili wenyeji 16. Mmoja wao, Augusto Machado (mbele kushoto), alikuwa amejifunza ukweli kutokana na mmisionari wa mapema, akaenda Gileadi, akarudi Brazili, akatumikia kwenye afisi ya tawi kwa miaka 30 iliyopita, na sasa ndiye mratibu wa halmashauri ya tawi. Hata ingawa wengi wa wamisionari hawa hawatumikii tena katika shamba hilo, kazi nzuri ambayo wamefanya imedumu. Katika 1945 kulikuwa wahubiri wa Ufalme 344 tu katika nchi hiyo, na sasa Brazili inasonga mbele kwenye hesabu ya 200,000, ikiripoti kilele cha wahubiri 196,948 katika mwaka wa utumishi wa 1986.
Ilikuwa furaha iliyoje kwa wamisionari wa Brazili, vijana kwa wazee, kukumbuka utendaji huo wa ajabu wa miaka 41 iliyopita kwenye pindi hii ya kuungana tena kwa furaha.