Ile Ishara Je! Wewe Umeiona?
“KULE mbali chini ya uso wa bahari, sabmarini ndefu yenye pua ya mviringo inakaa ikiwa chonjo, bila kuyumbishwa-yumbishwa na yale mawimbi makubwa yanayopita haraka juu ya uso wa bahari ulio na dhoruba. Dirisha moja katika sitaha ya sabmarini linafunguka, na roketi moja yenye urefu wa meta 9 na unene wa meta 1.4 inafyatuka nje kama mshale na kuelekea juu kwenye uso wa bahari. Roketi hiyo inaanza safari kwa kusukumwa juu na hewa iliyojazanishwa mahali pamoja, lakini ikiisha kufika kwenye uso wa bahari, enjini yayo inawaka moto na roketi ile inajitupa nje ya maji yale kwa mngurumo.”
Uelezaji huo juu ya kombora la masafa marefu lenye kutupwa na sabmarini, ambao umetokana na kitabu Rockets, Missiles and Spacecraft, kilichotungwa na Martin Keen, unatia maana kwenye unabii mmoja wa kale unaotabiri wakati wa taabu kubwa ya ulimwengu yenye kusababishwa na “uvumi [mngurumo, NW] wa bahari.” (Luka 21:25) Tisho lenye kutokana na sabmarini zenye makombora ya masafa marefu ni kubwa kadiri gani?
Kulingana na kitabu Jane’s Fighting Ships 1986-87, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi, na United States zina sabmarini 131 zinazofanya utumishi wenye utendaji zikiwa na makombora ya masafara marefu. Hakuna jiji lolote lililo mahali pasipoweza kufikiwa na makombora hayo, na kwa kawaida vichwa vyenye baruti huanguka katika umbali usiozidi kilometa moja kutoka ilipo shabaha. Baadhi yavyo vinabeba vichwa vyenye baruti vya hesabu inayotosha “kufutilia mbali nchi yoyote iliyo katika umbali usiozidi maili 5,000 [kilometa 8,000],” kulingana na The Guinness Book of Records. Jambo baya zaidi ni kwamba, watu fulani wamedai kuwa vichwa vyenye baruti vilivyo katika sabmarini moja tu yenye makombora ya masafa marefu vingeweza kusababisha kipupwe cha nyukilia ambacho kingehatarisha uhai wote duniani! Udhibiti wa sabmarini za mbali ni tatizo pia. Inahofiwa kwamba kitendo kimoja cha haraka-haraka katika sabmarini moja kingeweza kufyatusha vita ya nyukilia yenye msiba wa kifo.
Wengi wameyahusianisha na ishara ya kiunabii ya Yesu matazamio hayo yenye kuogofisha. Je! ingeweza kuwa kwamba kizazi chetu kinapatwa na utimizo wa ishara hiyo? Mambo ya uhakika yanajibu: ndiyo. Na hiyo inamaanisha kwamba ukombozi wa kutolewa katika tisho la vita ya nyukilia uko karibu. (Luka 21:28,32) Likiwapo tazamio zuri kama hilo, sisi tunakualika wewe ufikirie ithibati ya utimizo wa ile ishara. Ndipo sasa sehemu fulani za kutokeza za ile ishara zimepangwa hapa chini pamoja na utimizo wazo wa ki-siku-hizi.
“Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme.”(Luka 21:10)
Tangu 1914 watu zaidi ya 100,000,000 wamekufa kutokana na vita. Vita ya Ulimwengu 1 ilianza katika 1914 na ilihusisha ndani nchi 28, bila kuhesabu makoloni kadhaa ya Ulaya ya siku hiyo. Ni nchi chache zilizobaki bila kuwamo. Iliua uhai wa watu zaidi ya 13,000,000 kukiwa na askari 21,000,000 wenye kujeruhiwa. Ndipo ikaja Vita ya Ulimwengu 2, iliyokuwa yenye uharibifu mwingi zaidi. Na tangu wakati huo je? Katika makala ile yenye kusema “Vita vya Ulimwengu,” karatasi-habari The Star ya Afrika Kusini ilinukuu Sunday Times ya London kuwa ikisema: “Robo moja ya mataifa ya ulimwengu kwa sasa yamenaswa katika mapigano.”
“Kutakuwa na matetemeko makubwa.”(Luka 21:11)
Katika kitabu chao Terra Non Firma, maprofesa Gere na Shah wa Chuo Kikuu cha Stanford wanaorodhesha maelezo marefu juu ya “matetemeko ya dunia [164] yaliyo ya umaana mkubwa ulimwenguni,” yenye kuhusu miaka zaidi ya elfu tatu kurudi nyuma katika wakati uliopita. Kati ya jumla hiyo, 89 yalitokea tangu 1914, yakichukua uhai wa watu wanaokadiriwa kuwa 1,047,944. Orodha hiyo ilitia ndani matetemeko ya dunia yaliyo makubwa-makubwa tu, na tangu Terra Non Firma kilipotangaza kuwa kimechapishwa katika 1984, matetemeko ya dunia yenye uharibifu yametukia katika Chile, Urusi, na Meksiko, yakitokeza maelfu ya vifo zaidi.
“Kutakuwa na... tauni [magonjwa ya kipuku, NW].” (Luka21:11)
Katika 1918 ugonjwa wa kipuku ulio wa kuua ulipiga aina ya wanadamu. Ukiwa unaitwa fluu ya Kihispania, huo ulienea kila mahali penye kukaliwa isipokuwa kisiwa cha St. Helena na uliua watu wengi kuliko wale waliouawa katika ile miaka minne ya vita. Sayansi ya kitiba imepiga hatua kubwa za kimaendeleo tangu wakati huo, na bado matokeo yanakuwa ya kinyumenyume. Inaeleza hivi The Lancet: “Uendelevu wa magonjwa yenye kuambukizwa kingono (STD) yakiwa ndicho kikundi kinachopatikana kwa wingi zaidi cha maambukizo yanayojulishwa kwa watabibu ni jambo linaloenda kinyume cha tiba ya ki-siku-hizi. . . . Ilionekana wakati mmoja kama kwamba tungeweza kuyadhibiti magonjwa yenye kuambukizwa kingono lakini jambo hilo limetuponyoka katika miaka ya hivi majuzi.”
Kuna magonjwa mengine ya kipuku ambayo tiba ya ki-siku-hizi imekuwa pia haiwezi kuyadhibiti, kama vile kansa na ugonjwa wa moyo unaoathiri mshipa-arteri. Huu wa pili, kulingana na S[outh] A[frica] Family Practice, “ni tukio jipya. . . . Ni tokeo la jamii ya baada ya vita ya ulimwengu ya kwanza.” Katika Uingereza, ugonjwa wa moyo na kuongezeka sana kwa msukumo wa damu “ndicho kisababishi kikuu cha kifo,” kulingana na kitabu Cardiovascular Update—Insight Into Heart Disease. Kinaongezea kwamba “mpaka sasa ni maendeleo kidogo sana yamefanywa kuelekea kuyadhibiti [magonjwa hayo].”
Katika nchi zinazositawi, mamilioni ya watu wanapatwa na maleria, ugonjwa wa malale, kichocho, na magonjwa mengineyo. Mmoja wa magonjwa yenye kuua zaidi ulimwenguni ni kuhara. Linaeleza hivi gazeti Medicine International: “Imekadiriwa kwamba [kwa] mwaka visa milioni 500 vya kuhara vitaelekea kutukia miongoni mwa vitoto vichanga na watoto wadogo wa Esia, Afrika na Latini Amerika, kukiwa na vifo kati ya milioni 5 na 18.”
“Kutakuwa na... njaa [ upungufu wa vyakula, NW].”
Kwa kawaida upungufu wa vyakula huandamana na vita. Vita ya Ulimwengu 1 haikuwa tofauti. Njaa mbaya sana zilifuata kumalizika kwa vita hiyo. Na tangu wakati huo je? Inaripoti hivi karatasi maalum The Challenge of Internationalism—Forty Years of the United Nations (1945-1985): “Ingawa katika 1950 walikuwako watu karibu milioni 1,650 wasiopata chakula cha kutosha kinachoufaa mwili walikuwako milioni 2,250 katika 1983; ndiyo kusema, ongezeko la milioni 600 au asilimia 36 zaidi.” Njaa yenye mkumbo mkubwa iliufuata ukavu wa Afrika hivi majuzi. “Katika mwaka mmoja,” linataarifu gazeti Newsweek, “wakulima-wadogo Waethiopia walio wengi kufikia milioni 1 na watoto Wasudani 500,000 walikufa.” Maelfu kutoka nchi nyinginezo walipotelea mbali pia.
“Kutakuwako maono yenye kutisha na kutoka mbinguni ishara kubwa. Pia, kutakuwako ishara katika jua na katika mwezi na katika nyota, na duniani huzuni kuu ya mataifa, yasijue njia ya kutokea kwa sababu ya mngurumo wa bahari na msukosuko wayo, huku watu wakizirai kwa sababu ya woga na taraja la vitu vinavyokuja juu ya dunia inayokaliwa.”(Luka 21:11, 25, 26, NW)
Vita ya Ulimwengu 1 ilianzisha utumizi wa silaha mpya zilizo mbaya sana. Kutoka kwenye mbingu, ndege na meli za angani zilimimina makombora na risasi kama mvua. Wenye kuogopesha hata zaidi ulikuwa ule uharibifu uliomiminika kama mvua juu ya raia walio hoi katika Vita ya Ulimwengu 2, kutia ndani ule wa makombora mawili ya atomi.
Bahari pia ikawa tamasha ya maogofyo mapya. Wakati Vita ya Ulimwengu 1 ilipoanza, sabmarini zilifikiriwa kuwa zisizo na matokeo mazito sana, lakini kufikia mwisho wa Vita ya Ulimwengu 2, zilikuwa zimezamisha vyombo elfu kumi vya baharini. “Kuzamisha meli za ubiashara, kutia ndani meli [za abiria], bila onyo kulionekana kuwa sehemu ya ule utendaji mpya wa kuogopesha wa ‘vita ya ujumla,’” anataarifu Norman Friedman katika kitabu chake Submarine Design and Development.
Leo watu wengi wanazifikiria sabmarini zenye makombora ya masafa marefu kuwa ndizo meli zilizo maarufu kupita nyinginezo ulimwenguni. Silaha zinazoweza kuua zinabebwa pia katika sabmarini zenye makombora ya masafa ya kadiri, katika meli zenye Kubeba ndege za kivita, na manowari nyinginezo. Kulingana na Kitabu Jane’s Fighting Ships 1986-87, sasa kuna sabmarini 929, meli 30 za kubebea ndege za kivita, meli 84 za kupeleleza bahari, meli 367 za uangamizi, meli 675 za aina ya frigeti na 276 za aina korveti zilizo za kukinza inashambulizi ya sabmarini, na meli 2,024 za ushambulizi wa Kasi, na maelfu ya vyombo-bahari vingine vya kijeshi vilivyo katika utumishi wenye utendaji kwa ajili ya mataifa 52. Ongezea hesabu hiyo makombora madogo lakini yanayoweza kuua ambayo yametegwa kwa kuchimbiwa chini. Mwanadamu hajapata kamwe kuleta “msukosuko” wa bahari ulio hatari kama huo.
Mwanadamu amefika pia ndani ya lile jimbo la ‘jua na mwezi na nyota.’ Makombora ya masafa marefu yanachapusha mwendo kuingia katika anga za juu kabla ya kuteremka mbio-mbio juu ya shabaha zayo. Vyombo vya anga za juu vimepenya mfumo wa sayari za jua na mbele zaidi. Mataifa yamekuwa yenye kutegemea sana setilaiti za kibinadamu ambazo zinaizunguka-zunguka dunia. Setilaiti za kuelekeza vyombo vya usafiri na za kuchunguza halianga zimeyawezesha kupanga makombora yaliyowekwa mahali panapowafaa sana yakiwa yamelenga shabaha kwa usahihi mkubwa kwa jinsi iliyo hatari. Utumizi mrefu unafanywa pia wa setilaiti za mawasiliano na za upelelezi. “Setilaiti,” anataarifu Michael Sheehan katika kitabu chake The Arms Race, “zimekuwa ndizo macho na masikio na sauti za kani zenye silaha za zile serikali [mbili] zenye nguvu nyingi mno.”
Kielelezo kimoja cha hivi majuzi kilikuwa ule ushambulizi wa angani uliofanywa juu ya Libya. Inaripoti hivi Aviation Week & Space Technology. “Picha [za United States] zilizopigwa na setilaiti zilitumiwa katika matayarisho ya kushambulia na kukadiria-kadiria matokeo ya baada ya ushambulizi. Ile Programu ya Ulinzi ya Setilaiti za Halianga iliandalia ushambulizi huo habari za hali ya hewa, na vyombo vya mawasiliano ya kijeshi katika anga za juu vilihusika katika kuelekeza na kudhibiti ushambulizi huo.” Kwa sababu ya fungu muhimu ambalo setilaiti za kijeshi zinatimiza, serikali zote mbili zilizo na nguvu nyingi mno zina silaha za kutatanisha ushambulizi wenye kuongozwa na setilaiti. Moja ya hizo serikali zenye nguvu nyingi mno ina madhumuni ya wazi ya kuweka silaha katika anga za juu katika programu ambayo watu wengi huiita Vita vya Nyotani. Muda wa baadaye tu ndio utaonyesha kama serikali hizo mbili zenye nguvu nyingi mno zitahusika au hazitahusika katika vita ya anga za juu.
Kwa sasa, kama ilivyotabiriwa, ‘watu wanazirai kwa sababu ya woga na taraja la vitu vinavyokuja juu ya dunia inayokaliwa.’ Uhalifu, uvamizi-haramu, angamio la hali ya uchumi, uchafuzi wenye kuletwa na kemikali, na sumu inayotokana na mnurisho wa mionzi ya viwanda vya nyukilia, pamoja na lile tisho linaloongezeka la vita ya nyukilia, yote hayo ni visababishi vya “woga.” Gazeti la Uingereza New Statesman linaripoti kwamba “zaidi ya nusu” ya vijana-matineja wa nchi hiyo “wanahisi kwamba vita ya nyukilia itatukia katika muda wa maisha zao, na asilimia 70 wanaitikadi kwamba itakuwa isiyoepukika siku moja.”
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Ile Ishara—Inamaanisha Nini?
Baada ya kuchunguza ile ishara kwa msaada wa historia ya karne ya 20, mamilioni ya watu wamekuja kusadiki kwamba inapata utimizo. (Ona pia Mathayo, sura 24 na Marko, sura 13.) Kile kizazi cha 1914 kimetiwa alama kweli kweli. Hicho ndicho kinachohusika katika ule utimizo wa pili wa maneno ya Yesu: “Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie.” (Luka 21:32) “Hayo yote” ni kutia ndani ukombozi wa aina ya wanadamu wa kutolewa katika matatizo yenye kufadhaisha sana.
Yesu aliwahakikishia wafuasi wake hivi: “Mambo hayo yaanzapo kutokea, jiinueni wima na kuinua vichwa vyenu juu, kwa sababu ukombozi wenu unakaribia. . . . Wakati ninyi mwonapo mambo hayo yakitukia, jueni kwamba ufalme wa Mungu uko karibu.” Ufalme wa Mungu, ambao ni serikali ya ulimwengu yenye nguvu kupita zile za kibinadamu, itageuza dunia hii iwe paradiso ya tufe lote. Kwa sababu hiyo, kama vile ilivyo hakika kwamba ile ishara imetimia kikweli ndivyo ilivyo hakika kwamba ukombozi pia utakuja.—Luka 21:28, 31, NW; Zaburi 72:1-8.
Labda wewe hujapata kufikiria ile ishara ya kiunabii hapo kwanza. Sisi tunakutia wewe moyo uendelee kuchunguza Neno la Mungu. Kufanya hivyo kutakuwezesha wewe uelewe mengi zaidi juu ya makusudi ya Mungu kwa aina ya wanadamu. Hivyo utajifunza mambo ambayo Yehova Mungu anataka kwa wale ambao yeye ‘atakomboa’ waingie katika Paradiso ya kidunia inayokuja.—Zaburi 37:10, 11; Sefania 2:2, 3; Ufunuo 21:3-5.
[Picha Credit Lines on page 5]
Courtesy of German Railroads Information Office, New York
Eric Schwab/WHO
[Picha Credit Lines katika ukurasa wa 6]
Jerry Frank/United Nations
U.S. Air Force photo