Maswali Kutoka kwa Wasomaji
■ kwa kuwa Danieli alikuwa amesema kwamba hangekubali zawadi kutoka kwa Mfalme Belshaza kwa ajili ya kufasiri ule mwandiko ukutani, kwa nini yeye alipatwa akivaa nguo zile na mkufu ule baadaye?
Kabla tu ya Wamedi na Waajemi kupindua Babuloni, Mfalme BeIshaza na baraza lake walikuwa katikati ya karamu. Wakati karamu ilipokuwa ikiendelea, yeye alichukua vyombo ambavyo vilikuwa vimetoka kwenye hekalu la Yehova na akavitumia kunywea divai, akisifu miungu ya Kibabuloni. Lakini karamu hiyo ilikatizwa kwa ghafula sana wakati mkono wenye nguvu kuliko zile za kibinadamu ulipoandika mambo ya kigeni juu ya ukuta.—Danieli 5:1-5.
Wanaume wenye hekima na wanajimu wa Babuloni hakuweza kufasiri mwandiko ule, hata ingawa Belshaza aliahidi kumpa mtu ye yote mkufu wa dhahabu na umashuhuri wa kiserikali mtu yeyote ambaye angeweza kusoma na kueleza maana ya mwandiko huo wa kigeni.—Danieli 5:7-9.
Wakati yule Mwebrania mwenye kuitwa Danieli alipoletwa ndani hatimaye, mfalme alirudia kutaja toleo lake—kumvika Danieli kwa rangi ya zambarau, kumvalisha mkufu wa dhahabu, na kumfanya awe mtawala wa tatu katika ufalme ule. Nabii alijibu hivi kiheshima: “Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.”—Danieli 5:17.
Kwa hiyo Danieli hakuhitaji kuhongwa au kulipwa ndipo aandae fasiri ile. Mfalme angeweza kuweka zawadi zake au kumpa mtu mwingineye. Danieli angeandaa elezo, si ili apate thawabu, bali kwa sababu yeye alitiwa nguvu za kufanya hivyo na Yehova, yule Mungu wa kweli, ambaye hukumu yake ilikuwa ikining’inia juu ya Babuloni.
Kama vile sisi tunavyosoma kwenye Danieli 5:29, baada ya Danieli kuwa amesoma na kufasiri maneno yale kama alivyosema angefanya, mfalme aliagiza kwamba thawabu zile zipewe kwa Danieli ingawaje. Danieli hakujivalisha nguo zile na mkufu ule. Alivalishwa kwa agizo la yule mtawala mwenye mamlaka kamili, Mfalme Belshaza. Lakini hiyo haihitilafiani na Danieli 5:17, ambapo nabii alielewesha wazi kwamba kusudio lake halikuwa la ubinafsi.
Baadaye Yesu alisema kwamba “ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii.” (Mathayo 10:41) Ni shida kuwa kwamba jambo hilo lilitumika kwa Belshaza, kwa maana yeye hakuwa akimtendea Danieli kwa fadhili au kwa staha kwa sababu ya kumstahi mwanamume huyo mwaminifu kuwa ni nabii wa yule Mungu wa kweli. Mfalme Belshaza alikuwa na nia ya kutoa zawadi hizo hizo kwa yeyote ambaye angeweza kutatua lile fumbo la mwandiko, hata kwa mnajimu fulani wa kipagani. Mfalme alipata thawabu iliyofaa, ile iliyopatana na mwandiko wa kiunabii uliokuwa ukutani: “Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa. Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme.”—Danieli 5:30, 31.