Maisha na Huduma ya Yesu
Apewa Mapokezi na Farisayo Mashuhuri
YESU ni mgeni katika maskani ya Farisayo mmoja mashuhuri, ambako ni sasa tu ametoka kuponya mwanamume mwenye ugonjwa wa kujazana maji mwilini. Sasa, Yesu anapoona wageni wenzake wakichagua mahali-mahali pa umashuhuri, yeye anafundisha somo la unyenyekevu.
“Ukialikwa na mtu arusini,” Yesu anashauri, “usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma [mahali pa chini zaidi, NW].”
Kwa hiyo Yesu anatoa ushauri huu: “Ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe.” Akikazia somo hilo, Yesu anamalizia hivi: “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
Halafu, Yesu anaelekeza maneno kwa Farisayo aliyemwalika na kueleza jinsi ya kuandaa mlo mkuu wenye ustahili halisi kwa Mungu. “Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri [mwenye furaha, NW], kwa kuwa hao hawana cha kukulipa.”
Kuandaa mlo wa jinsi hiyo kwa ajili ya wasiofanikiwa sana kutamletea furaha mwenye kuwaandalia kwa sababu kama vile Yesu anavyoeleza mkaribishaji wake: “Utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.” Uelezaji wa Yesu juu ya mlo huu wenye ustahili unakumbusha mgeni mwenzake juu ya aina nyingine ya mlo. “Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu,” mgeni huyo anasema. Hata hivyo, si wote wanaothamini tazamio hilo lenye furaha kwa njia inayofaa, kama vile Yesu anavyoendelea kuonyesha kwa kutumia kielezi.
“Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.”
Lo! ni udhuru bandia kama nini! Kwa kawaida shamba au mifugo huchunguzwa kabla haijanunuliwa, kwa hiyo hakuwi na uharaka wowote halisi wa kuitazama baadaye. Vivyo hivyo, ndoa ya mtu haipasi kumzuia asikubali mwaliko wa maana jinsi hiyo. Kwa hiyo anaposikia juu ya udhuru huo, bwana anakasirika na kumwamuru hivi mtumwa wake: “Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. . . .
Katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.”
Ni hali gani inayoelezwa na kielezi hicho? Basi, “bwana” mwenye kuandaa mlo ule anawakilisha Yehova Mungu; “mtumwa” mwenye kutoa mwaliko anawakilisha Yesu Kristo; na ile “karamu kubwa [ya jioni, NW]” inawakilisha fursa za kuwa katika mstari wa kupata Ufalme wa mbingu.
Zaidi ya watu wengine wote, wale waliokuwa wa kwanza kupokea mwaliko wa kuja katika mstari wa kupata Ufalme walikuwa viongozi wa kidini Wayahudi wa siku ya Yesu. Hata hivyo, wao walikataa mwaliko huo. Hivyo, kuanzia hasa Pentekoste 33 W.K., mwaliko wa pili ulitolewa kwa watu wenye kudharauliwa na walio dhalili wa taifa la Kiyahudi. Lakini walioitikia kujaza zile nafasi 144,000 katika Ufalme wa kimbingu wa Mungu hawakutosha. Kwa hiyo katika 36 W.K., miaka mitatu na nusu baadaye, mwaliko wa tatu ulio wa mwisho ulitolewa kwa watu wasiotahiriwa wasio Wayahudi, na kukusanywa kwao kukaendelea mpaka ndani ya karne ya 20. Luka 14:1-24.
◆ Ni somo gani la unyenyekevu ambalo Yesu anafundisha?
◆ Ni jinsi gani mkaribishaji anavyoweza kuandaa mlo wenye ustahili kwa Mungu, na kwa nini hiyo itamletea furaha?
◆ Kwa nini udhuru wa wageni walioalikwa ni bandia?
◆ Ni nini kinachowakilishwa na kielezi cha Yesu cha ile “karamu kubwa [ya jioni, NW]”?