Maisha na Huduma ya Yesu
Wakati Mwana Mpotevu Anapopatwa
WAKATI mwana mpotevu katika kielezi cha Yesu anaporudia nyumba ya baba yake, anapokewaje? Sikiliza Yesu akisimulia:
“Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.” Lo, ni baba mwenye rehema na moyo mchangamfu kama nini, akiwakilisha vizuri sana Baba yetu wa kimbingu, Yehova!
Inaelekea kuwa baba huyo alikuwa amesikia kwamba mwanaye aliishi maisha ya ufasiki. Hata hivyo yeye anamkaribisha kwenye maskani yao bila kungojea aelezwe mambo kirefu. Yesu pia ana roho hiyo ya ukaribishaji, akiwa ndiye mwenye kuchukua hatua ya kwanza kukaribia watenda dhambi na wakusanya-kodi, ambao wanawakilishwa na mwana mpotevu katika kielezi hiki.
Ni kweli kwamba pasipo shaka baba mwenye utambuzi katika kielezi cha Yesu anajua kwa kiasi fulani kwamba mwanaye ana toba kwa kutazama sura yake ya kuhuzunika na kupondeka roho wakati wa kurudi. Lakini kule kuchukua kwa baba hatua ya kwanza yenye upendo kunafanya iwe rahisi zaidi mwana huyo kuungama dhambi zake, kama vile Yesu anavyosimulia: “Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. [Nifanye mmoja wa watu wako wa kukodishwa, NW].”
Hata hivyo, maneno hayo ya mwana yanakuwa hayajamalizika midomoni mwake wakati baba yake anapofanya kitendo, akiwaagiza hivi watumwa wake: “Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.”
Kwa wakati huo, ‘mwana mkubwa wa baba alikuwako shambani.’ Ona kama unaweza kutambua yeye anawakilisha nani kwa kusikiliza sehemu iliyobaki ya hadithi. Yesu anasema hivi juu ya mwana huyo mkubwa: “Alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani.
“Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.”
Ni nani, akiwa kama yule mwana mkubwa, amekuwa akichambua-chambua rehema na fikira wanazopewa watenda dhambi? Je! si waandishi na Mafarisayo? Kwa kuwa kilichofanya kielezi hiki kitolewe ni uchambuzi wao juu ya Yesu kwa sababu ya yeye kukaribisha watenda dhambi, kwa uwazi ni lazima iwe wao ndio waliowakilishwa na yule mwana mkubwa.
Yesu anamalizia hadithi yake kwa usihi wa baba kwa mwanaye mkubwa: “Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Hivyo Yesu anaacha bila kukata maneno ni jambo gani ambalo mwana mkubwa anafanya mwishowe. Kweli kweli, nyumaye, baada ya kufa na kufufuliwa kwa Yesu, “jamii kubwa ya makuhani waliitii ile Imani,” yawezekana hiyo ikiwa ni kutia ndani baadhi ya hawa wa jamii ya “mwana mkubwa” ambao Yesu ananena nao hapa.
Lakini katika nyakati za ki-siku-hizi wana hao wawili wanawakilisha nani? Lazima iwe ni wale ambao wamepata kujua mambo ya kutosha juu ya makusudi ya Yehova hata wawe na msingi wa kuingia katika uhusiano pamoja naye. Mwana mkubwa anawakilisha washiriki fulani wa “kundi dogo,” au “kanisa [kundi, NW] la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni.” Hao walichagua kufuata mwelekeo unaofanana na ule wa mwana mkubwa. Hawakutaka kukaribisha jamii ya kidunia, “kondoo wengine,” wakihisi kwamba hao walikuwa wakifanya wao waache kujulikana kwa umashuhuri mwingi kama zamani.
Kwa upande ule mwingine, mwana mpotevu anawakilisha wale ambao kati ya watu wa Mungu wanaenda zao wakafurahie anasa ambazo ulimwengu unatoa. Hata hivyo, kwa wakati unaofaa wanarudi kwa kutubu na kuwa tena watumishi watendaji wa Mungu. Kweli kweli, Baba ni mwenye upendo na rehema sana kuelekea wale wanaotambua uhitaji wao wa kusamehewa na kumrudia! Luka 15:20-32; Matendo 6:7; Luka 12:32; Waebrania 12:23; Yohana 10:16.
◆ Yesu anaigaje kielelezo cha baba mwenye huruma katika kielezi chake?
◆ Mwana mkubwa ana oni gani juu ya kukaribishwa kwa ndugu yake, na Mafarisayo wanajiendeshaje kama huyo mwana mkubwa?
◆ Kielezi cha Yesu kina utumizi gani katika siku yetu?