Sura 86
Hadithi ya Mwana Mpotevu
AKIWA ndipo tu amemaliza kusimulia vielezi kwa Mafarisayo kuhusu kupata tena kondoo alieyepotea na sarafu ya drakma, Yesu anaendelea sasa kusimulia kielezi kingine. Hiki ni juu ya Baba mwenye upendo na jinsi anavyotendea wanaye wawili, kila mmoja akiwa na dosari kubwa-kubwa.
Kwanza, kuna yule mwana mchanga zaidi, aliye mhusika mkuu wa kielezi hiki. Yeye anakusanya urithi wake, ambao baba yake amempa bila kusita-sita. Halafu yeye anaondoka kwenye nyumba yao na kuhusika katika njia ya maisha ya ukosefu mkubwa wa adili. Lakini sikiliza wakati Yesu anaposimulia hadithi hii, na uone kama unaweza kuwajua wahusika hao wamekusudiwa kuwakilisha nani.
“Mtu mmoja,” Yesu anaanza, “alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. [Baba huyo] anawagawia vitu vyake.” Huyu aliye mchanga zaidi anafanya nini na vile anavyopokea?
Yesu anaeleza, “Baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.” Kwa kweli, yeye anatumia pesa zake akiishi pamoja na malaya. Baadaye nyakati zenye magumu zinakuja, kama vile Yesu anavyoendelea kusimulia:
“Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.”
Lo, ni kushushwa cheo kama nini kulazimika kuanza kuchunga nguruwe, kwa maana wanyama hao walikuwa si safi kulingana na Sheria! Lakini kilichoumiza zaidi hisia za mwana huyo kilikuwa ile njaa yenye kumtafuna-tafuna ambayo hata ilisababisha atamani chakula walicholishwa nguruwe. Kwa sababu ya afa hilo baya sana, Yesu alisema, ‘akazingatia moyoni mwake [‘akili zake zikamrudia,’ NW].’
Akiendelea na hadithi yake, Yesu anaeleza hivi: “Alisema [akijiambia mwenyewe], Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye.”
Hapa pana jambo la kufikiria: Kama baba yake angalikuwa amemgombeza-gombeza na kumpigia makelele ya hasira wakati alipoondoka kwenye nyumba yao, haielekei kwamba mwana huyo angalikuwa na nia moja tu juu ya limpasalo kufanya. Huenda ikawa angaliamua kurudi na kutafuta kazi mahali pengine katika nchi ya kwao ili asilazimike kumkabili baba yake. Hata hivyo, hakuna fikira ya jinsi hiyo ilikuwa akilini mwake. Yeye alitaka kuwa huko huko kwenye nyumba yao!
Ni wazi kwamba, yule baba katika kielezi cha Yesu anawakilisha Baba yetu wa kimbingu mwenye upendo na rehema, Yehova Mungu. Na pia labda wewe unatambua kwamba yule mwana mpotevu anawakilisha watu wenye kujulikana kuwa watenda dhambi. Mafarisayo, ambao Yesu anena nao, hapo kwanza wamekuwa wakimchambua Yesu kwa kula pamoja na watu ao hao. Lakini mwana yule mwenye umri mkubwa zaidi anawakilisha nani?
Wakati Mwana Mpotevu Anapopatikana
Wakati mwana mpotevu katika kielezi cha Yesu anaporudia nyumba ya baba yake, anapata upokezi wa aina gani? Sikiliza Yesu anapoueleza:
“Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.” Lo, ni baba mwenye rehema na moyo mchangamfu kama nini, akiwakilisha vizuri sana Baba yetu wa kimbingu, Yehova!
Inaelekea kuwa baba huyo alikuwa amesikia kwamba mwanaye aliishi maisha ya ufasiki. Hata hivyo yeye anamkaribisha kwenye nyumba yao bila kungojea aelezwe mambo kirefu. Yesu pia ana roho hiyo ya ukaribishaji, akichukua hatua ya kwanza kukaribia watenda dhambi na wakusanya-kodi, ambao wanawakilishwa na mwana mpotevu katika kielezi hiki.
Ni kweli kwamba pasipo shaka baba mwenye utambuzi katika kielezi cha Yesu anajua kwa kiasi fulani kwamba mwanaye ana toba kwa kutazama sura yake yenye huzuni na kupondeka roho wakati wa kurudi. Lakini kule kuchukua kwa baba hatua ya kwanza yenye upendo kunafanya iwe rahisi zaidi mwana huyo kuungama dhambi zake, kama vile Yesu anavyosimulia: “Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. [Nifanye mmoja wa watu wako wa kukodishwa, NW].”
Hata hivyo, maneno hayo ya mwana yanakuwa hayajamalizika midomoni mwake wakati baba yake anapofanya kitendo, akiwaagiza hivi watumwa wake: “Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.” Kisha “wakaanza kushangilia.”
Kwa wakati ule ule, ‘mwana mkubwa wa baba alikuwako shambani.’ Ona kama unaweza kutambua yeye anawakilisha nani kwa kusikiliza sehemu iliyobaki ya hadithi. Yesu anasema hivi juu ya mwana huyo mkubwa zaidi: “Alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.”
Ni nani, akiwa kama yule mwana mkubwa, amekuwa akichambua-chambua rehema na fikira wanazopewa watenda dhambi? Je! si waandishi na Mafarisayo? Kwa kuwa kilichofanya kielezi hiki kitolewe ni uchambuzi wao juu ya Yesu kwa sababu ya yeye kukaribisha watenda dhambi, kwa wazi ni lazima iwe wao ndio waliowakilishwa na yule mwana mkubwa.
Yesu anamalizia hadithi yake kwa kusihi kwa baba kwa mwanaye mkubwa: “Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Hivyo Yesu anaacha bila kukata maneno ni jambo gani ambalo mwana mkubwa anafanya mwishowe. Kweli kweli, nyumaye, baada ya kufa na kufufuliwa kwa Yesu, ‘jamii kubwa ya makuhani waliitii ile Imani,’ yawezekana hiyo ni kutia ndani baadhi ya hawa wa jamii ya “mwana mkubwa” ambao Yesu ananena nao hapa.
Lakini ni nani katika nyakati za ki-siku-hizi wanaowakilishwa na wana hao wawili? Lazima iwe ni wale ambao wamepata kujua mambo ya kutosha juu ya makusudi ya Yehova hata wawe na msingi wa kuingia katika uhusiano pamoja naye. Mwana mkubwa anawakilisha washiriki fulani wa “kundi dogo,” au “kanisa [kundi, NW] la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni.” Hao walichagua kufuata mwelekeo unaofanana na ule wa mwana mkubwa. Hawakutaka kukaribisha jamii ya kidunia, “kondoo wengine,” wakihisi kwamba hao walikuwa wakifanya wao waache kujulikana kwa umashuhuri mwingi kama zamani.
Kwa upande mwingine, mwana mpotevu anawakilisha wale ambao kati ya watu wa Mungu wanaenda zao wakafurahie anasa ambazo ulimwengu unatoa. Hata hivyo, kwa wakati unaofaa wanarudi kwa kutubu na kuwa tena watumishi watendaji wa Mungu. Kweli kweli, Baba ni mwenye upendo na rehema sana kuelekea wale wanaotambua uhitaji wao wa kusamehewa na kumrudia! Luka 15:11-32; Walawi 11:7, 8; Matendo 6:7; Luka 12:32; Waebrania 12:23; Yohana 10:16.
▪ Yesu anasimulia kielezi, au hadithi hii kwa nani, na kwa nini?
▪ Ni nani mhusika mkuu katika hadithi hii, na ni jambo gani linalompata?
▪ Baba na mwana mchanga zaidi wa siku ya Yesu wanawakilisha nani?
▪ Yesu anaigaje kielelezo cha baba mwenye huruma katika kielezi chake?
▪ Mwana mkubwa zaidi ana oni gani juu ya kukaribishwa kwa ndugu yake, na Mafarisayo wanajiendeshaje kama huyo mwana mkubwa zaidi?
▪ Kielezi cha Yesu kina utumizi gani katika siku yetu?