Maisha na Huduma ya Yesu
Yesu Afundisha Katika Yeriko
UPESI Yesu na makutano wanaosafiri pamoja naye wanafika Yeriko, ambalo ni jiji lililo umbali wa mwendo wa siku moja toka Yerusalemu. Yaelekea Yeriko ni jiji maradufu, jiji la kale la Kiyahudi likiwa lapata kilometa moja na nusu toka jiji jipya la Kiroma. Makutano wanapoondoka katika jiji la kale na kukaribia jiji jipya zaidi, vipofu wawili waombaji wanasikia makelele yale. Mmoja wao anaitwa Bartimayo.
Wanapopata kujua kwamba Yesu ndiye anayepita, Bartimayo na mwandamani wake wanaanza kupaaza sauti: “Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi!” Mkutano wanapowakaripia wanyamaze, wanazidi kupaaza sauti hata zaidi wakisema: “Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi!”
Akisikia msukosuko huo, Yesu anasimama. Anawaomba wale walio pamoja naye wawaite wale wanaopaaza sauti. Wanawaendea wale waombaji vipofu na kumwambia mmoja wao: “Jipe moyo; inuka, anakuita.” Kwa msisimuko mwingi sana, yule kipofu anatupa mavazi yake ya nje, anaruka-ruka kwa miguu yake, na kumwendea Yesu.
“Mwataka niwafanyie nini?” Yesu awauliza wale wanaume wawili.
“Bwana, twataka macho yetu yafumbuliwe,” wanasihi.
Akisukumwa na huruma, Yesu agusa macho yao. Kulingana na usimulizi wa Marko, Yesu amwambia mmoja wao: “Enenda zako, imani yako imekuponya.” Mara moja wale waombaji vipofu wanapata kuona, na bila shaka wote wawili wanaanza kumtukuza Mungu. Wakati watu wote wanapoona jambo ambalo limetukia, wao pia wanaanza kumsifu Mungu. Bila kukawia, Bartimayo na mwandamani wake wanaanza kumfuata Yesu.
Yesu anapopita Yeriko, makutano ni wengi ajabu. Kila mtu anataka kumwona yule ambaye ameponya wale wanaume vipofu Watu wanamsonga Yesu kutoka kila upande, na kama tokeo, watu fulani hawawezi hata kumtazama mara moja tu. Miongoni mwao ni Zakayo, mkuu wa watoza ushuru katika Yeriko na sehemu zinazouzunguka. Yeye ni mfupi sana hivi kwamba hawezi kuona kinachoendelea.
Kwa hiyo Zakayo anatangulia mbele na kupanda mti wa mtini-mforsadi ulio katika njia ambayo Yesu anafuata. Kutoka mahali hapa panapofaa, yeye anaweza kuona kila kitu vizuri. Makutano wanapokaribia, Yesu anaita juu kuelekea mti ule: “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.”
Zakayo anashuka chini akishangilia na kuharakisha kwenda nyumbani ili atayarishe mambo kwa ajili ya mgeni wake mashuhuri. Lakini watu wanapoona kinachotendeka, wote wanaanza kunung’unika. Wanaliona kuwa jambo lisilofaa Yesu awe mgeni wa mtu wa namna ile. Wajua, Zakayo alitajirika kwa kunyang’anya watu pesa kwa kutofuata haki katika biashara yake ya kukusanya kodi.
Watu wengi wanafuata, na Yesu anapoingia nyumbani mwa Zakayo wanalalamika wakisema: “Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” Hata hivyo Yesu anaona katika Zakayo uwezekano wa kutubu. Naye Yesu hatamaushwi, kwa kuwa Zakayo asimama na kutangaza: “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.”
Zakayo anathibitisha kwamba toba yake ni halisi kwa kutoa nusu ya mali zake na. kuwapa maskini na kwa kutumia nusu ile nyingine kuwarudishia wale aliowadanganya. Inaonekana anaweza kukadiria kiasi anachowiwa na watu wale kutokana na maandishi yake ya kodi. Kwa hiyo yeye anaweka nadhiri ya kurudisha mara nne, kwa kulingana na sheria ya Mungu inayosema: ‘Mtu akiiba kondoo, atalipa kondoo wanne badala ya kondoo huyo mmoja.’
Yesu anapendezwa na njia ambayo Zakayo anaahidi kugawanya mali zake, kwa kuwa Yeye anapaaza sauti hivi: “Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Hivi karibuni, Yesu alikuwa ametoa kielezi kuhusu hali ya ‘waliopotea’ kwa hadithi yake kuhusu mwana mpotevu. Sasa tuna kielelezo cha maisha halisi cha mtu aliyepotea ambaye amepatikana. Ingawa viongozi wa kidini na wale wanaowafuata wanasema-sema maneno na kulalamika kwamba Yesu amewaelekezea fikira watu kama Zakayo, Yesu anaendelea kuwatafuta na kuwarudisha wana hawa waliopotea wa Abrahamu. Mathayo 20:29-34; Marko 10:46-52; Luka 18:35–19:10; Kutoka 22:1.
◆ Yaelekea Yesu anawakuta wapi wale waombaji vipofu, naye anawafanyia nini?
◆ Zakayo ni nani, na kwa nini anapanda mti?
◆ Zakayo anathibitishaje toba yake?
◆ Tunaweza kujifunza somo gani kutokana na Yesu alivyomtendea Zakayo?