Sura 99
Yesu Afundisha Katika Yeriko
UPESI Yesu na umati unaosafiri pamoja naye wafika Yeriko, ambalo ni jiji lililo umbali wa mwendo wa siku moja kutoka Yerusalemu. Yaelekea Yeriko ni jiji maradufu, jiji la kale la Kiyahudi likiwa yapata kilometa moja na nusu toka jiji jipya la Kiroma. Umati unapoondoka katika jiji la kale na kukaribia jiji jipya zaidi, vipofu wawili waombaji wanasikia makelele yale mmoja wao anaitwa Bartimayo.
Wanapopata kujua kwamba Yesu ndiye anayepita, Bartimayo na mwandamani wake waanza kupaaza sauti: “Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi!” Umati unapowakaripia wanyamaze, wapaaza sauti hata zaidi wakisema: “Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi!”
Akisikia msukosuko huo, Yesu asimama. Awaomba wale walio pamoja naye wawaite wale wanaopaaza sauti. Wawaendea waombaji vipofu na kumwambia mmoja wao: “Jipe moyo; inuka, anakuita.” Kwa msisimuko mwingi sana, yule kipofu atupa mavazi yake ya nje, aruka kwenye miguu yake, na kumwendea Yesu.
“Mwataka niwafanyie nini?” Yesu auliza.
“Bwana, twataka macho yetu yafumbuliwe,” wale vipofu wawili wasihi.
Akisukumwa na huruma, Yesu agusa macho yao. Kulingana na usimulizi wa Marko, Yesu amwambia mmoja wao: “Enenda zako, imani yako imekuponya.” Mara moja wale waombaji vipofu wapata kuona, na bila shaka wote wawili waanza kumtukuza Mungu. Wakati watu wote wanapoona jambo ambalo limetukia, wao pia waanza kumsifu Mungu. Bila kukawia, Bartimayo na mwandamani wake waanza kumfuata Yesu.
Yesu anapopita Yeriko, umati ni mkubwa ajabu. Kila mtu ataka kumwona yule ambaye ameponya wale wanaume vipofu. Watu wanamsonga Yesu kutoka kila upande, na kama tokeo, watu fulani hawawezi hata kumtazama hata mara moja. Miongoni mwao ni Zakayo, mkuu wa wakusanya kodi katika Yeriko na sehemu zinazozunguka. Yeye ni mfupi sana hivi kwamba hawezi kuona kinachoendelea.
Kwa hiyo Zakayo akimbia mbele na kupanda mti wa mtini-mforsadi ulio katika njia ambayo Yesu anafuata. Kutoka mahali hapo panapofaa, yeye aweza kuona kila kitu vizuri. Umati unapokaribia, Yesu aita juu kuelekea mti ule: “Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.” Zakayo ashuka chini akishangilia na kuharakisha kwenda nyumbani ili atayarishe mambo kwa ajili ya mgeni wake mashuhuri.
Lakini watu wanapoona kinachotendeka, wote waanza kunung’unika. Wanaliona kuwa jambo lisilofaa Yesu kuwa mgeni wa mtu wa namna ile. Wajua, Zakayo alitajirika kwa kunyang’anya watu pesa kwa kutofuata haki katika shughuli yake ya kukusanya kodi.
Watu wengi wafuata, na Yesu anapoingia nyumbani mwa Zakayo walalamika wakisema: “Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” Hata hivyo Yesu anaona katika Zakayo uwezekano wa kutubu. Na Yesu hatamaushwi, kwa kuwa Zakayo asimama na kutangaza: “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.”
Zakayo athibitisha kwamba toba yake ni halisi kwa kutoa nusu ya mali zake na kuwapa maskini na kwa kutumia nusu ile nyingine kuwarudishia wale aliowadanganya. Inaonekana anaweza kukadiria kiasi anachowiwa na watu wale kutokana na maandishi yake ya kodi. Kwa hiyo yeye anaweka nadhiri ya kurudisha mara nne, kulingana na sheria ya Mungu inayosema: ‘Mtu akiiba kondoo, atalipa kondoo wanne badala ya kondoo huyo mmoja.’
Yesu apendezwa na njia ambayo Zakayo aahidi kugawanya mali zake, kwa kuwa Yeye apaaza sauti hivi: “Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Hivi majuzi, Yesu alikuwa ametoa kielezi kuhusu hali ya ‘waliopotea’ kwa hadithi yake kuhusu mwana mpotevu. Sasa tuna kielelezo cha maisha halisi cha mtu aliyepotea ambaye amepatikana. Ingawa viongozi wa kidini na wale wanaowafuata wasema-sema maneno na kulalamika kwamba Yesu amewaelekezea fikira watu kama Zakayo, Yesu aendelea kuwatafuta na kuwarudisha wana hawa wa Abrahamu. Mathayo 20:29-34; Marko 10:46-52; Luka 18:35-19:10; Kutoka 22:1.
▪ Yaelekea Yesu awakuta wapi wale waombaji vipofu, naye awafanyia nini?
▪ Zakayo ni nani, na kwa nini apanda mti?
▪ Zakayo athibitishaje toba yake?
▪ Tunaweza kujifunza somo gani kutokana na jinsi Yesu alivyomtendea Zakayo?