Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w89 10/15 kur. 30-31
  • Johari Kutokana na Gospeli ya Marko

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Johari Kutokana na Gospeli ya Marko
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Iliandikwa kwa Ajili ya Nani?
  • Mwana wa Mungu Ni Mfanya Miujiza
  • Huduma Katika Dekapoli
  • Yesu na Pokeo
  • Huduma ya Peupe Ambayo Yesu Aliifanya Mwishoni
  • Kitabu Cha Biblia 41—Marko
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Marko, Mwandikaji wa Injili ya Vitendo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Mambo Makuu Katika Kitabu cha Marko
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Kitabu Cha Biblia Namba 43—Yohana
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
w89 10/15 kur. 30-31

Johari Kutokana na Gospeli ya Marko

ROHO ya Yehova ilivuvia Marko aandike usimulizi wenye kujawa na vituko kuhusu maisha na huduma ya kidunia ya Yesu. Ingawa Gospeli hii haisemi kwamba Marko ndiye aliyeiandika, kuna ushuhuda wa jambo hilo katika maandishi ya Papias, Justin Martyr, Tertullian, Origen, Eusebius, Jerome, na wengine ambao maandishi yao yalihusika kipindi cha karne nne za kwanza za Wakati wa Kawaida wetu.

Kulingana na pokeo, mtume Petro aliandaa habari za msingi kwa Gospeli hii. Kwa kielelezo, Origen alisema kwamba Marko aliiandika “kwa kupatana na maagizo ya Petro.” Lakini yaonekana Marko aliweza kupata habari kutokana na vyanzo vingine pia, kwa maana wanafunzi walikutana katika makao ya mama yake. Kwa uhakika, kwa kuwa labda Marko alikuwa ndiye yule “kijana” aliyewaponyoka wenye kumkamata Yesu, huenda ikawa alikuwa na mwonano wa kibinafsi pamoja na Kristo.—Marko 14:51, 52; Matendo 12:12.

Iliandikwa kwa Ajili ya Nani?

Yaonekana Marko aliandika hasa kwa kuwafikiria wasomaji Wasio Wayahudi. Mathalani, mtindo wake wa kuandika mambo kwa ufupi lakini kwa maelezo thabiti uliifaa hali ya Waroma. Yeye alifafanua “korbani” kuwa ni “zawadi iliyowekwa wakfu kwa Mungu” (7:11, NW) na akaonyesha kwamba hekalu lingeweza kuonwa kutoka Mlima wa Mizeituni. (13:3) Pia Marko alieleza kwamba Mafarisayo ‘walizoea kufunga’ na kwamba Masadukayo “husema hakuna ufufuo.” (2:18; 12:18, NW) Maelezo hayo yangekuwa hayana uhitaji wa lazima kwa wasomaji Wayahudi.

Bila shaka, kusoma Gospeli ya Marko kwaweza kunufaisha mtu yeyote. Lakini ni mambo gani ya mandhari-nyuma ambayo yaweza kutusaidia tuthamini baadhi ya johari zayo?

Mwana wa Mungu Ni Mfanya Miujiza

Marko asimulia miujiza ambayo Kristo alifanya kwa nguvu ya Mungu. Mathalani, katika pindi moja kulikuwa na halaiki kubwa ya watu katika nyumba fulani hivi kwamba ili mtu aliyepooza apate kuponywa, ilikuwa lazima ashushwe karibu na Yesu kupitia nafasi wazi iliyotobolewa katika dari. (2:4) Kwa sababu nyumba hiyo ilisongamana watu, huenda ikawa mwanamume huyo alipandishwa kwa ngazi iliyoletwa pale au kwa vidato vya ngazi iliyojengwa kwa nje. Lakini kwa nini kuwe na uhitaji wa kutoboa dari? Ni kwamba, dari nyingi zilikuwa tambarare na ziliegemea maboriti yaliyopita kutoka ukuta mmoja hadi ukuta mwingine. Maboriti hayo yalikingamwa na pao zilizofunikwa na matawi, matete, na vitu kama hivyo. Juu yayo ilikuwapo tabaka ya ardhi iliyopakwa mkandiko laini wa udongo-mfinyango au udongo-mfinyango na chokaa. Kwa hiyo, ili kumwingiza mpoozi huyo ndani ya kuwapo kwa Yesu, wanaume walilazimika kutoboa dari ile yenye ardhi. Lakini ilikuwa baraka iliyoje baada ya wao kufanya hivyo! Kristo aliponya mwanamume huyo, na wote wale waliokuwapo wakamtukuza Mungu. (2:1-12) Ni uhakikishio ulioje kwamba Mwana wa Yehova atafanya maponyo mazuri sana katika ulimwengu mpya!

Yesu alifanya mmoja wa miujiza yake akiwa amepanda mashua wakati alipoambia dhoruba ya upepo ikae kimya kabisa katika Bahari ya Galilaya baada ya kuamshwa alipokuwa amelalia “mto.” (4:35-41, NW) Yaonekana kwamba mto huo haukuwa wa aina ile nyororo ambayo sasa hutumiwa kama kilalio cha kichwa kitandani. Huenda ukawa ulikuwa manyoya tu ya kondoo ambayo wapiga makasia walikuwa wakikalia au kiegemeo cha mgongoni au mto wenye kutumika kama kiti kwenye usukani. Kwa vyovyote vile, Yesu alipoiambia bahari, “Kaa kimya kabisa! Nyamaza!” wale waliokuwapo waliona ushuhuda wa imani katika kitendo, kwa maana “upepo ule ulishuka chini, na utulivu mkubwa ukaingia.”

Huduma Katika Dekapoli

Alipovuka Bahari ya Galilaya, Yesu aliingia Dekapoli, au jimbo la majiji kumi. Ingawa bila shaka majiji haya yalikuwa ya wakaaji wengi Wayahudi, yalikuwa vitovu vya utamaduni wa Kigiriki au Kihelleni. Humo, katika nchi ya Wagerasene, Yesu alifungua mwanamume mmoja aache kupagawa na roho waovu, ambaye “makao yake yalikuwa pale makaburini.”—5:1-20.

Nyakati fulani, makaburi yaliyochongwa kutokana na mwamba yalikuwa makao yenye kutumiwa sana kuwa mahali pa wasio timamu akilini, kuwa maficho ya wahalifu, au makao ya maskini. (Linganisha Isaya 22:16; 65:2-4.) Kulingana na maandishi mamoja ya karne ya 19, mgeni mmoja aliyezuru eneo ambapo Yesu alikabiliana na mpagawa huyu alisema hivi juu ya kao la jinsi hiyo: “Kaburi lenyewe lilikuwa na urefu wa karibu futi nane upande wa ndani, kwa maana kulikuwako na mshuko wa kidato kilichoinama sana kutoka kwenye kizingiti cha jiwe hadi sakafuni. Ukubwa walo ulikuwa karibu hatua kumi na mbili za mraba; lakini, kwa kuwa hakuna nuru iliyopokewa ndani isipokuwa karibu na mlango, hatukuweza kuona kama mlikuwamo chumba cha ndani zaidi kama kilivyokuwamo katika baadhi ya mengine. Jeneza kamili lililofanyizwa kwa jiwe la chokaa bado lilibaki humo, nalo sasa lilitumiwa na jamaa kama sanduku la kuwekea mahindi na maandalizi mengine, hivi kwamba haya malalo ya mwisho kwa wafu yalikuwa yamechafuliwa utumizi wayo yakawa mahali salama, penye ubaridi, na pafaapo kuendewa na walio hai.”

Yesu na Pokeo

Katika pindi moja, Mafarisayo na waandishi fulani walilalamika kwamba wanafunzi wa Yesu walikula bila kunawa mikono. Kwa manufaa ya wasomaji Wasio Wayahudi, Marko alieleza kwamba Mafarisayo na Wayahudi wengine ‘hawakula wasiponawa mikono yao mpaka kwenye kiko cha mkono.’ Waliporudi kutoka sokoni, walikula baada tu ya kujisafisha sana kwa kujinyunyizia, na mapokeo yao yalitia ndani “mabatizo ya vikombe na midumu na vyombo vya shaba.”—7:1-4, NW.

Zaidi ya kujinyunyizia kisherehe kwa njia ya kujionyesha utakatifu kabla ya kula, Wayahudi hawa walibatiza, au walizamisha katika maji, vikombe, midumu, na vyombo vya shaba walivyovitumia kwenye milo. Kadiri ambavyo walishikwa sana na mapokeo ilitolewa kielezi na mwana-chuo John Lightfoot. Akitumia maneno ya maandishi ya kirabi, yeye alionyesha kwamba uangalifu mwingi ulielekezwa kwenye mambo madogo sana kama vile ni kiasi gani cha maji kingetumiwa, ni njia gani ingetumiwa, na ni wakati gani ungetosha kwa kuosha. Lightfoot alinukuu chanzo kimoja kinachoonyesha kwamba Wayahudi fulani walioga kwa uangalifu kabla ya milo ili kuepuka kutiwa jeraha na Shibta, “roho mmoja mwovu ambaye huketi juu ya mikono ya wanadamu usiku: na ikiwa mtu yeyote agusa chakula chake kwa mikono isiyonawishwa, roho huyo huketi juu ya chakula hicho, na kuna hatari kutokana nacho.” Si ajabu Yesu aliwashutumu waandishi na Mafarisayo kwa ‘kuacha amri ya Mungu iwaponyoke huku wakishika sana pokeo la wanadamu’!—7:5-8, NW.

Huduma ya Peupe Ambayo Yesu Aliifanya Mwishoni

Baada ya kuripoti kuhusu huduma ya Yesu ya baadaye katika Galilaya na kazi Yake katika Perea, Marko alikaza uangalifu juu ya matukio yaliyofanyika katika Yerusalemu na sehemu za kandokando. Mathalani, yeye alisimulia juu ya pindi moja ambapo Kristo alikuwa akiona watu wakitumbukiza pesa ndani ya masanduku ya hazina ya hekalu. Yesu aliona kwamba mjane mmoja maskini alichanga ‘sarafu ndogo mbili tu za thamani kidogo sana.’ Hata hivyo, yeye alisema kwamba mwanamke huyo alitoa zaidi ya wengine wote, kwa maana wao walichanga kutokana na mazidio yao, hali ‘kutokana na upungukiwa wake, yeye alitumbukiza humo maishilio yake mazima.’ (12:41-44, NW) Kulingana na maandishi-awali ya Kigiriki, mwanamke huyo alichanga lepta mbili. Leptoni ilikuwa ndiyo sarafu ndogo zaidi ya Kiyahudi ya shaba au bronzi (shaba-nyeusi), na thamani yayo ya pesa ni kama upuuzi tu leo. Lakini mwanamke maskini huyu alifanya kile ambacho angeweza, akitoa kielelezo kizuri sana cha kutokuwa na ubinafsi katika kuunga mkono ibada ya kweli.—2 Wakorintho 9:6, 7.

Huduma ya Yesu ilipokaribia mwisho, yeye aliulizwa maswali na Pontio Pilato, ambaye jina na mtajo wake wa cheo cha “prifekti” waonekana juu ya maandishi ya kuchongelewa yaliyopatikana Kaisaria katika 1961. Katika mikoa ya nje-nje kama Yudea, gavana (prifekti) mmoja alikuwa na udhibiti juu ya jeshi, alikuwa ndiye mwenye daraka la usimamizi wa fedha, na alitumikia akiwa hakimu wa kujaribu kesi. Pilato alikuwa na mamlaka ya kumfungua Kristo, lakini alijiacha akazwe na adui za Yesu na akatafuta kuridhisha umati huo kwa kumpokeza atundikwe na kumweka huru Baraba muuaji mwenye kufitini serikali.—15:1-15,

Kuna mapokeo mbalimbali kuhusu maisha ya baadaye na kifo cha Pilato. Mathalani, mwanahistoria Eusebio aliandika hivi: “Pilato mwenyewe, gavana wa siku ya Mwokozi wetu, alihusika katika maafa makubwa sana hivi kwamba akalazimika kuwa mwenye kujiua yeye mwenyewe na kujiadhibu kwa mkono wake mwenyewe: yaonekana kwamba haki ya kimungu haikufanya polepole kumfikilia.” Ingawa hivyo, hata kama kuna uwezekano huo, kifo chenye umaana mkubwa kuliko vyote kilikuwa kile cha Yesu. Ofisa wa jeshi la Kiroma (msimamizi wa askari mia) ambaye alishuhudia kifo cha Kristo na matukio yenye ajabu isiyo ya kikawaida ambayo yalihusiana nacho alinena ukweli halisi aliposema hivi: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”—15:33-39.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]

Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

Idara ya Israeli ya Hifadhi ya Vitu vya Kikale na ya Majumba ya Makumbusho; foto ni kutoka Jumba la Israeli la Makumbusho, Yerusalemu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki